Baada ya Tanzania na Uganda kukubaliana mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta utekelezwe kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, matumaini mengine mapya yameonekana kutokana na Uganda kuweka wazi azma yake ya kujenga bomba jingine la gesi katika njia hiyohiyo kwa ajili ya biashara na Tanzania.
Licha ya kutofafanua kwa kina juu ya mpango huo, Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Serikali ya Uganda na Tanzania bado ziko kwenye majadiliano ya kuanzisha mradi mwingine wa bomba hilo la gesi.
“Ni mpango mpya bado tunajadiliana, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga bomba hilo lakini utekelezaji wake utaanza baada ya mradi huo wa bomba la mafuta wa sasa kukamilika,” alisema.
Waziri Muloni aliyekuwa ameongozana na mwenyeji wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kwanza wa jopo la watalaamu wa sekta mbalimbali waliokutana kwa mara ya kwanza kuandaa mpango wa utekelezaji wa mradi huo.
Mkutano huo unafanyika ikiwa ni siku sita tangu azungumze na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili nchini akitokea Kampala ambako Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alitangaza kuwa bomba hilo la mafuta ghafi kutoka Hoima, Ziwa Albert litapita katika ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga.
Waziri Muhongo alisema mbali na bomba hilo, nchi nyingine za Afrika Mashariki pia zimekubali kununua gesi ya Tanzania.
Kuhusu mradi wa bomba, Profesa Muhongo alisema nchi hizo zimekubaliana kukamilisha Kazi hiyo kabla ya makubaliano ya awali ya 2020.
Makubaliano mengine ya nchi hizo ni kuchangia ujenzi wa mtambo wa kuchakata mafuta ghafi utakaojengwa Uganda ambao alisema utasaidia kuweka akiba ya mafuta kwa ajili ya biashara kwa nchi wanachama.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea uzoefu wa Tanzania kwenye ujenzi wa miradi ya mabomba ya gesi na mafuta katika mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Dk. Fred Kaliisa (kushoto) akifafanua jambo katika kikao hicho. Kulia ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni
Balozi wa Uganda Nchini Tanzania, Dorothy Hyuha akifafanua jambo katika mkutano huo.
Chanzo: Mpekuzi
Kwa maoni yangu naona Tanzania tunazidi kulamba karata dume na hapa ndipo utajiri wetu wetu utaanza kutusaidia na hii ni nyota njema pia kwa Rais Magufuli.