Tanzania yapaa viwango vya FIFA

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MATUNDA ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kutwaa Kombe la Chalenji yameanza kuonekana baada ya Tanzania kupanda kwenye ubora wa viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa nafasi tisa.

Kwa mujibu wa orodha mpya ya Fifa iliyotolewa jana, Tanzania imekuwa katika nafasi ya 116 kutoka nafasi ya 124 iliyokuwepo mwezi uliopita.

Kilimanjaro Stars ilitwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji baada ya kuifunga Ivory Coast kwa bao 1-0 katika fainali zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Aliyekuwa bingwa mara mbili mfululizo wa Kombe la Chalenji, Uganda imeporomoka kutoka nafasi ya 69 mwezi uliopita mpaka nafasi ya 80 wakati Kenya imeshuka kutoka nafasi ya 116 mpaka nafasi ya 120.

Misri bado inaongoza kwa upande wa Afrika ambapo imepanda kwa nafasi moja, kutoka nafasi ya kumi mwezi uliopita mpaka ya tisa.

Aidha, mabingwa wa dunia Hispania watamaliza mwaka wakiwa kileleni mwa orodha hiyo kwani bado wanashika namba moja ikiwa ni kwa mara ya kwanza kuongoza tatu bora Ulaya ndani ya miezi 18.

Uholanzi, iliyofungwa na Hispania kwenye fainali za Kombe la Dunia Julai mwaka huu iko kwenye nafasi ya pili ikifuatiwa na Ujerumani inayoshika nafasi ya tatu.

Brazil imeporomoka hadi nafasi ya nne kutoka ya tatu kutokana na kufungwa na Argentina katika mechi ya kimataifa ya kirafiki mwezi uliopita, Argentina na England ziko katika nafasi ya tano na sita.

Urusi iliyoshinda kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 mapema mwezi huu imebaki nafasi ya 13, wakati waandaaji wa fainali hizo kwa mwaka 2022 Qatar wameporomoka hadi nafasi ya 114.

Wakati huohuo, Tanzania imealikwa kwenye michuano ya nchi zinazotoka kwenye bonde la mto Nile inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Cairo, Misri.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, Tanzania imepata mwaliko kutoka Misri ambao ndio waandaaji wa michuano hiyo. Timu nyingine zinazoshiriki mbali ya Tanzania na Misri ni Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo, Eritrea, Ethiopia na Sudan.

Alipoulizwa suala hilo Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Sunday Kayuni alikiri kuwa na taarifa za michuano hiyo lakini akasema hana maelezo zaidi.

“Tunafahamu kama kuna suala hilo, lakini hatujapewa maelezo zaidi, tukiyapata tutawambia,”alisema.
 
Back
Top Bottom