Tanzania yaongoza rekodi ya kuwa na wazalendo mafisadi baran afrika

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,779
TANZANIA imeweka rekodi ya aina yake barani Afrika kwa kuibuka nchi pekee yenye wananchi wenye mapenzi makubwa kwa taifa lao kuliko jambo au mfumo wowote wa kitamaduni, kiuchumi au kijamii unaowagawa katika makundi mbalimbali na matabaka.

Rekodi hiyo ambayo ni moja ya kigezo cha nchi iliyo na ulinzi imara, imepatikana baada ya wananchi wa nchi za Afrika, wakiwemo Watanzania, kufanyiwa mahojiano maalumu kuhusu jambo la fahari wanalodhani ni muhimu kujitambulisha nalo kati ya mambo kadha wa kadha yanayotumika kumtambulisha mwanadamu.

Vigezo vingine vinavyoifanya nchi kuwa na ulinzi imara na madhubuti licha ya uzalendo wa wananchi wake kulipenda taifa lao ni teknolojia ya vita, ushirikiano mzuri na nchi marafiki zikiwemo nchi jirani, wingi wa wanajeshi, bajeti inayotumika kwa ajili ya ulinzi na usalama na idadi ya watu.

Katika mahojiano hayo yaliyohusisha wananchi kati ya 1,200 na 2,400 katika kila nchi kati ya nchi 16 zilizochaguliwa kufanya utafiti kuhusu ujenzi wa taifa katika nchi za Afrika, wananchi waliulizwa maswali ili kubaini iwapo wanajisikia fahari zaidi kutambulishwa kwa jina la taifa lao kwa mfano Mtanzania, au kwa jina la kitu kingine haswa kabila.

Kwa mujibu wa maoni ya utafiti huo uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya utafiti ya Afro Barometer yenye makao makuu nchini Ghana na kuongozwa na Amanda Lea Robinson wa Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani ulionesha kuwa waliojisikia fahari kutambuliwa kwa mataifa yao zaidi ya kitu kingine ilikuwa asilimia 42 ya wahojiwa wote wanaofikia 22,765.

Robinson ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Stanford University anasema katika utafiti huo uliotolewa Septemba mwaka huu kwamba wakati wastani wa wanaopenda mataifa yao katika nchi hizo ni asilimia 42 ya wahojiwa, kwa Tanzania wanaolipenda taifa lao ni asilimia 88 ya wahojiwa wote.

Nchi ya pili kwa kuwa na wananchi wanaopenda taifa lao kuliko kabila ilikuwa Afrika Kusini ambayo asilimia 63 ya wananchi wake wanalipenda taifa lao kuliko kabila, ya tatu Namibia ambayo wiki hii ilikuwa katika mchakato wa uchaguzi wa Rais.

Namibia wao ni asilimia 57. Nchi ya nne ni Senegal asilimia 51 na ya tano Madagascar, asilimia 50. Nigeria imekuwa ya mwisho kwa kuwa na asilimia 17 tu ya wananchi wake wanaolipenda taifa lao kuliko kabila.

Katika nchi za Afrika Mashariki zilizoteuliwa katika utafiti huo, Kenya ilishika nafasi ya nane kwa kuwa na asilimia 40 ya wananchi ambao wanalipenda zaidi taifa kuliko kabila lao na Uganda ilishika nafasi ya 12 ikiwa na asilimia 31 tu ya wananchi wake wanaopenda taifa lao zaidi ya kabila lao.

Msomi huyo anasema kabla ya kuanza kwa utafiti huo ambao ni wa kwanza kufanya uchunguzi wa harakati za ujenzi wa taifa katika nchi za Afrika, alitumia nadharia kadhaa za ujenzi wa taifa zikiwemo zinazoelezea ujenzi wa mataifa ya Ulaya na zilizokuwa zikionesha kuwa mataifa ya Afrika ni dhaifu kutokana na wananchi wake kupenda zaidi makabila yao kuliko taifa lao.

Moja ya nadharia hizo ilikuwa ikijaribu kuoanisha ujenzi wa taifa katika nchi za Ulaya ambazo wananchi wake wanajitambua zaidi kwa utaifa wao na ujenzi wa taifa katika nchi za Afrika ambazo zimekuwa zikitazamwa kuwa hazijafanikiwa kujenga utaifa kwa wananchi wao kama zilivyo za Ulaya.

Kutokana na nadharia hizo alifanya utafiti wa makabila na kuandaa orodha ya makabila zaidi ya 200 aliyodhani kuwa yangewakilisha taarifa za makabila mengine katika nchi husika ili kufanikisha utafiti wake.

Robinson anabainisha kuwa katika nchi zote 16 ambazo utafiti huo ulifanyika, asilimia 95 ya wahojiwa walitambua kabila lao lililokuwa katika orodha yake na hivyo alifanikiwa kupata taarifa za tabia ya kabila husika ikiwemo ukubwa na uwezo wa kiuchumi wa kabila ili kuhusisha mchango wa kabila husika na mapenzi ya wananchi fulani katika taifa lao.

Anasema japo katika utafiti huo asilimia 95 ya wahojiwa katika nchi hizo 16 walitambua makabila yao katika orodha ya makabila iliyokuwa imeandaliwa kabla ya kuanza kwa utafiti huo, walipofika Tanzania walishangazwa kukuta asilimia 60 ya wahojiwa wakisema kuwa kabila lao halipo katika orodha hiyo.

Kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wahojiwa Watanzania ambao walisema kuwa kabila lao halipo katika orodha yake ya makabila, msomi huyo anaeleza kuwa alishindwa kufanya uchambuzi wa mchango wa kabila katika mapenzi ya wananchi kwa taifa lao.

Hata hivyo anabainisha kuwa Watanzania ambao makabila yao yalikuwepo katika orodha na ambao makabila yao hayakuwepo katika orodha wote walipoulizwa iwapo kati ya taifa lao na kabila lao nini wanaona fahari kutambulishwa nacho, asilimia 88 walisema wanaona fahari kutambulishwa na Taifa lao.

"Tanzania ni ya pekee, ambapo asilimia 88 wanaelezea kulipenda zaidi taifa lao, hata wale ambao kabila lao lilikuwepo katika orodha asilimia 87 walisema wanajisikia fahari kutambulishwa kwa taifa lao,” alieleza msomi huyo katika utafiti wake huo.

Utafiti huo ambao ulihoji watu wenye umri wa kupiga kura tu, pia ulibainisha kuwa wakati mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza na ambayo yalipata uhuru kwa njia ya amani, wananchi wake walionekana kuwa na fahari sana na makabila yao, bado Tanzania ambayo iliwahi kuwa chini ya uangalizi wa Uingereza kwa kipindi kirefu na ilipata uhuru kwa njia ya amani ilionekana kuwa taifa linapendwa kuliko kabila.

Kutokana na matokeo hayo, msomi huyo ameitaja Tanzania kama nchi yenye wananchi wanaolipenda zaidi taifa lao na ameshauri kuwa nadharia zilizopo za ujenzi wa taifa katika nchi za Afrika hazifanyi kazi kwa Tanzania labda kama kutakuwa na nadharia nyingine.

Alifafanua kuwa mapenzi hayo kwa taifa yanaweka mazingira mazuri ya kukua kwa demokrasia kwa kuwa mtu hatazuiwa haki yake ya kuchaguliwa kwa kigezo cha kuwepo katika kikundi fulani ambayo pia itachangia kukua kwa uchumi na maendeleo ya watu.
 
kwani hii inahusiana nini na ufisadi sasa,kwani toka lini kupenda nchi yako imekuwa ufisadi?wewe kwako kila anayependa nchi yake(mzalendo) basi ni mfisadi?mi nadhani kama hii research inatuonesha kitu chochote basi ni kuwa prouds kwa kutokungángánia ukabila kama zilivyo sehemu nyingine.unapoweka habari weka habari kama ilivyo na tuache wenyewe tuichambue na kutoa maonni yetu na sio kutulazimisha tuione uionavyo wewe............
 
asilimia 12 hawaipendi tanzania. Hiyo asilimia siyo ndogo. Bila shaka humo ndo wamejaa mafisadi.
 
Hawa asilimia kumi na mbili ambao ni mafisadi ndio wanaoipenda Tanzania kuliko sisi wote,hawa ndio wanaoiita Tanzania 'a land of opportunity.'
 
huu ni moja ya tafiti za ovyo kabisa nilizowahi kusikia. hata waliompa jukwaa nadhani walikuwa na malengo maalum sio kwamba walikunwa na uvumbuzi wake.

kama unataka kutafuta asilimia ya wanaopenda nchi yao nadhani moja ya methodologies ingekuwa hivi: ondoa hitaji la viza, fungua milango yote ya viwanja vya ndege na uweke ndege nyingi kubwa tayari kuchukua watu kwenda kokote nje ya tazania kwa gharama nafuu au bure, halafu uone wangapi watakataa kwenda nje, andika asilimia yako. basi hayo ndo matokeo halisi si haya ya kutafutia fedha za wafadhiri wa propaganda za utawala bora.
 
Tanzania yaongoza rekodi ya kuwa na wazalendo mafisadi baran afrika
TANZANIA imeweka rekodi ya aina yake barani Afrika kwa kuibuka nchi pekee yenye wananchi wenye mapenzi makubwa kwa taifa lao kuliko jambo au mfumo wowote wa kitamaduni, kiuchumi au kijamii unaowagawa katika makundi mbalimbali na matabaka.
Sijaelewa ufisadi ndio kuwa na mapenzi makubwa kwa taifa au la! Sijakupata Pdiddy
 
Back
Top Bottom