Tanzania yakubali kuipatia Kenya madaktari 500 kusaidia upungufu wa Madaktari

Mar 5, 2017
44
62
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania imekubali ombi la kuipatia Kenya madaktari 500 watakaoisaidia nchi hiyo kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba hasa baada ya kutokea kwa mgomo wa madaktari nchini humo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekubali kutoa madaktari hao leo tarehe 18 Machi, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta.

Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Waziri wa Afya wa Kenya Mhe. Dkt. Cleopa Mailu amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa baada ya kutokea mgomo wa madaktari pamoja na uamuzi wa nchi hiyo kugatua madaraka katika sekta ya afya, imebainika kuwa nchi hiyo ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea madaktari wanaosomeshwa nchini humo bali kupata madaktari kutoka nje ya nchi.

Mhe. Dkt. Cleopa Mailu aliyeongozana na Gavana wa Kisumu Mhe. Jack Ranguma amesema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 watakaopatiwa kutoka Tanzania ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.

Nae Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara yake ipo tayari kutoa madaktari hao haraka iwezekanavyo kwa kuwa Tanzania inao madaktari wengi wazuri ambao wamemaliza masomo yao na hawajapata ajira, na wengine wamemaliza mikataba yao ya kazi na bado wana uwezo wa kufanya kazi.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa madaktari wote Tanzania ambao hawapo katika utumishi wa umma, hawapo katika hospitali teule na ambao hawapo katika hospitali za mashirika yasiyo ya kiserikali wanaolipwa na Serikali, waombe nafasi hizi.

Vigezo vikubwa ambavyo tutaviangalia ni kwanza awe amemaliza mafunzo ya vitendo (Internship) na pili awe amesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika, kwa hiyo leo hii tutatoa tangazo na tumefurahi sana kwa sababu tunao madaktari wa kutosha ndani ya nchi na tunaweza kuwapeleka Kenya” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania imekubali ombi hilo kwa kuwa Kenya ni ndugu, jirani na rafiki wa kweli wa Tanzania na amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mhe. Ummy Mwalimu kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda Kenya kutekeleza jukumu hilo.

“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri” amesema Mhe. Rais Magufuli.


Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

18 Machi, 2017
 
Yaani wameshindwa kumaliza mgomo wa madaktari wao, wamekimbilia kuazima madaktari bongo?

How sustainable is that?

Wamesema kuna madaktari wa ziada ambao HAWAJAPATA AJIRA, siyo WASIOHITAJIKA. Kuwaajiri serikali haitaki wanawagawa nje. Natumaini ni mwisho wa kusikia kwenye changamoto za sekta ya afya kuwa tuna uhaba wa madaktari.
 
"...Tanzania ina madaktari wa kutosha..."
Ummy Mwalimu

Hizi hospitali za wilaya zinazokosa madaktari zipo nchi gani?
Hii nchi ina vituko sana.

Usishangae kauli kama hizi. Ni sawa na zie za vyeti vya kuzaliwa kuwa absolute legal requirement ya kufunga ndoa
 
11 Reactions
Reply
Back
Top Bottom