Tanzania yafanya vibaya katika mitaji ya uwekezaji

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
804
Tanzania yafanya vibaya katika mitaji ya uwekezaji

Mwandishi Wetu

TANZANIA imetajwa kufanya vibaya katika mitaji ya uwekezaji moja kwa moja (FDI) huku ikiacha maswali baada ya sekta ya madini kudhihirika haijatoa mchango mkubwa wa kuinua uchumi na kuvutia uwekezaji katika sekta nyinginezo.

Ripoti ya mwaka huu ya dunia kuhusu uwekezaji, imeeleza kuwa tofauti na mwaka jana ambako ilikuwa ndani ya 10 bora katika Afrika, mwaka huu Tanzania haikupata nafasi yoyote katika Afrika na dunia kwa ujumla. Badala yake, imeshika namba moja katika ukanda wa Afrika Mashariki, lakini ikitajwa kuwa hadi sasa haijafaidika ipasavyo na madini yanayochimbwa.

“Swali kubwa tunalotakiwa kujiuliza, ni kwamba kwa nini sekta ya madini haichangii uwekezaji zaidi? Ilitarajiwa kwamba sekta hii ingekuwa chachu kwa shughuli zaidi za kiuchumi kwa kupanua shughuli za kiuchumi katika sekta nyinginezo,” alisema Mkurugenzi wa Utafiti na Mifumo ya Mawasiliano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Joel Kyaruzi wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Dar es Salaam.

Kyaruzi alisisitiza kuwa ipo haja ya kubadilika katika kuvutia FDI katika sekta nyingine za uchumi. “Tunahitaji kubadilika katika udhibiti. Tunahitaji kubadilika katika namna ambavyo tunaingia mikataba na kampuni kubwa na pia tunahitaji kufanya mabadiliko namna tunavyoshirikisha jamii,” alisisitiza.

Katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa, Kyaruzi aliyemwakilisha Mkurugenzi wa TIC, Emanuel ole Naiko alisema ripoti ya mwaka huu ililenga zaidi kampuni kubwa na shughuli zao hususan katika madini.

Akirejea yaliyomo katika ripoti hiyo, Kyaruzi alishauri serikali kuwa makini na wawekezaji katika sekta ya madini kwa kuitaka iwe makini na ajenda za kampuni zinazowekeza kwa kutozisikiliza kwa kiwango kikubwa kwa kuwa malengo yao siyo kuendeleza jamii, bali wamelenga kuwekeza mitaji yao katika faida.

Huku akiwashauri watunga sera kuzingatia maoni ya ripoti hiyo, alisema miongoni mwa mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele ni kuhakikisha kwamba uchumi wa madini unatumika kuibua uchumi mwingine kwa ajili ya Watanzania.

Alitahadharisha kuwa uchumi wa madini unahitaji mifumo bora ya uongozi itakayohakikisha kwamba mapato yake hayaathiri uwajibikaji wa serikali kwa watu wake na matokeo yake, ikajikita katika kujali maslahi ya tabaka la wenye uwezo.

Wakati ripoti hiyo imeainisha kuwa ushiriki wa kampuni kubwa za nje zinaweza kuwa na athari za mazingira, jamii na siasa, TIC imesema hilo linawezekana kukabiliwa kulingana na uwezo wa nchi wa kutunga na kutekeleza sheria za kulinda mazingira.

Awali, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Patricia Scott alisema serikali mbalimbali zinahitaji kuwa na maono na mikakati thabiti katika kuhakikisha kwamba mafuta na rasilimali nyingine za madini zinatumika katika uwazi kuchangia maendeleo endelevu katika nchi zao.

Alizitaja nchi zilizofanya vizuri katika ripoti ya mwaka huu kuwa ni Misri, Nigeria, Sudan na Tunisia zilizoingiza mitaji ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3. Morocco imeingiza mitaji ya moja kwa moja ya thamani ya dola bilioni 2 hadi 2.9. Kwa upande wa Algeria, Libya, Guinea, Chad na Ghana, mitaji yake ni kati ya dola bilioni moja hadi 1.9.

Source: HabariLeo
 
Back
Top Bottom