Tanzania yachaguliwa kuwa katika Bodi ya Shirikisho la Wahasibu Afrika

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,007
9,873

Shirikisho la Wahasibu la Afrika (PAFA) lilifanya Mkutano Mkuu wa Mwaka huko Catonou, Benin Ijumaa tarehe 18 Juni 2021. Kati ya dondoo zilizojadiliwa ilikuwa ni kuteua Bodi mpya ya PAFA. Tanzania ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA. Pius Maneno, iliteuliwa katika Bodi ya PAFA kwa miaka miwili kuwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki. Kanda ya Afrika Mashariki inajumuisha nchi zifuatazo: Burundi, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Kusini mwa Sudan na Uganda.


Bwana Cosme Goundété (Benin) na Bi Keto Kayemba (Uganda) waliteuliwa kushika nafasi za Urais na Makamu wa Rais, mtawaliwa.

Hii ni mara ya pili NBAA kuhudumu katika Bodi ya PAFA kwa nafasi tofauti. Mnamo mwaka 2011, Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA, CPA Prof.Mussa Assad, aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa PAFA kwa miaka miwili na kisha kuwa Rais wa PAFA mnamo 2013 kwa miaka miwili, kabla ya kuachia nafasi yake baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kufuatia uteuzi huu Tanzania itanufaika kushiriki katika uundaji wa miongozo ya kawaida ya kiufundi, kimaadili na kielimu kwa taaluma ya uhasibu Afrika. Pia, kushiriki na kubadilishana taarifa na maboresho katika masuala ya kiufundi, mifumo ya udhibiti na kanuni za utawala bora wa Shirikisho. Kwa kuongezea, Tanzania itakuwa na jukwaa la kubadilishana habari muhimu juu ya taaluma ya uhasibu.

Shirikisho la Wahasibu la Afrika (PAFA) linawakilisha Wahasibu Wanataaluma wa Afrika lilianzishwa tarehe 5 Mei 2011 huko Dakar, Senegal. PAFA inajumuisha Taasisi 55 za Uhasibu (PAOs) kutoka nchi 44 za Afrika. Ujumbe wa PAFA ni kuharakisha na kuimarisha sauti na uwezo wa taaluma ya Uhasibu katika kufanya kazi kwa maslahi ya umma, kuwezesha biashara, uchumi na kuongeza faida na huduma bora kwa raia wa Afrika
 
Back
Top Bottom