Tanzania ya Ujamaa ndani ya Ubepari uchwara(petty bourgeoisie)

Anna Mghwira

R I P
Mar 9, 2012
206
362
Kuna utata katika uhalisia, mchanganuo, na matumizi ya sera za kijamaa na kibepari. Wakati miaka ya 60 mwishoni na 70 katikati, sera ya ujamaa ilionekana kuwa kimbilio la watu wanyonge, miaka ya kuanzia 80 hadi sasa tumejikuta katika mtanzuka bila maelezo ya kina juu ya msimamo wetu kisera katika medani za siasa na uchumi.

Mwaka 2015 chama cha ACT WAZALENDO kilinadi sera za kijamaa, kwa mtazamo wa ujamaa wa kidemokrasia. Awali tangazo la sera hii lilipotoka, umma ulijibu kwa njia tofauti. Majibu ya baadhi ya watu katika jamii yetu yalionesha kuwa ujamaa umeshindwa, ukomunist umeporomoka Urusi na udikteta wa China chini ya serikali ya Kikomunist ni dalili za kushindwa kwa ujamaa.

Licha ya maoni haya, hakukuwa na majibu halisi ya mafanikio ya ubepari. Zaidi sana hakukuwa na mjadala wa kina juu ya tabia za ubepari uchwara naoendeshwa katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Tanzania. Kwa kawaida wanaopinga ujamaa huwa hawaji na hoja za kutosha za ubepari na faida zake kwa raia wa kawaida, wafanya kazi na wachuuzi wadogo.

Kwa hiyo tunapojadili kushindwa ama kushinda kwa ujamaa na ubepari ni lazima tuweke bayana faida na hasara za kila mmoja. Aidha ni jukumu la msingi la vyama vya siasa kujitanabaisha na mojawapo ya sera hizi, na zingine na kuzitumia katika kunadi vyama vyao na mifumo vinavyoisimamia.Bila aina hii ya siasa tunajikuta na ombwe la hoja juu ya ubora ama upungufu wa itikadi zote mbili, ama zingine.

Hoja za jumla hazitoshi na hazikidhi mahitaji ya kisiasa na kiuchumi. Kwa hitimisho mwaka 2015 tulisema kila wakati turudi kwenye misingi.

Tunapotafuta misingi katika jamii za sasa za Kiafrika na Tanzania, tunakutana na mlolongo wa matukio yanayomkimbiza mtu kutoka katika asili yake. Ni fedheha kwa Waafrika kudai chochote katika dhana hizi mbili: ujamaa na ubepari. Kwa sababu ukiacha ujamaa kama dhana ya udugu na ushirikiano, hakuna juhudi za kuuendeleza kama sehemu muhimu ya kuwa mwafrika / mtanzania. Ubepari kwa upande mwingine, haukuwa na mizizi ya kukomaa afrika mpaka ujio wa wageni walowezi katika bara hili.

Historia ya dunia mpaka sasa haioneshi mapambano ya mtu mweusi kama jamii iliyotafuta kujitambulisha duniani. Mapambano ya mtu mweusi yanaanza kuonekana kama sehemu ya mapambano na wageni waliofika kupora bara hili. Kwa msingi huu, Waafrika hawaonekani kuwa na mchango wa kihistoria katika mifumo ya dunia.

Wamechukuliwa na mawimbi ya utumwa, ukoloni, ubepari na ubepari uchwara na ubepari mambo leo. Hatujaandika kilicho chetu bado. Mpaka sasa sisi tunaandika maisha yetu kulingana na watu waliokuja katika maisha yetu na si jinsi sisi wenyewe tulivyo.

Hii ni changamoto kubwa katika kujadili dhana hizi za ujamaa ama ubepari katika muktadha huu. Kwa hiyo ninapenda kujikita katika kuangalia namna ambavyo Mwafrika wa asili angetaka kujulikana kama angeamua hivyo. La kwanza Mwafrika wa asili angekuja kuzungumza nasi kwa lugha yake ya utoto: Kinyakyusa, Kimakonde, Kihaya nk.

Kiswahili bado ni lugha ya matokeo na si lugha ya asili. Ni lugha ya pili ama ya tatu kwa wengi wetu. Pili mwafrika huyu ama Mtanganyika (nalo si jina la asili ) au Mzanzibari, angelielezea anakotoka kama taifa lake: Wamasai ni taifa, Wabarbaig ni taifa, Warimi nao ni taifa. Mataifa haya yalikuwa nchi kamili zenye muundo wa utawala ulioheshimu watu wake, lugha na taratibu zingine.

Mapambano halisi ya maisha ya mwafrika yangejengwa katika msingi huu kwanza, kasha msingi wa umoja baadae. Lakini tumekwama mahali Fulani. Moja tumekwama kuendeleza misingi ya asili yetu, yaani misingi ya tulivyo hasa: Tunakotoka na tunakotaka kwenda kama watu, si kama viambatanishi vya utu wa watu wengine. Si kama matokeo ya utumwa, ukoloni na utandawazi sasa.

Kuna kitu zaidi ya majira tu. Kuna mtu na utu wake wenye asili yake. Kuna jamii za makabila nchi ndogo ndogo zilizounganishwa na mfumo wa ukoloni hasa kama mfumo wa uzalishaji wa kinyonyaji. Mwafrika anaanza kuonekana wakati wa utumwa na wakati wa ukoloni mpaka anapokataa mifumo hii na kuanza kujisemea, alikuwa amekwisha poteza asili yake halisi.

Kuna hali ya kudanganyana kuwa makabila ni uasi. Kwa vipi asili yangu iwe uasi? Kwa nini nchi ya Uingereza ni ya Waingereza yaani kabila lao, lakini wasukuma na Wamasai wenye eneo kubwa kijiografia hawawezi kuwa taifa? Hata ndani ya Uingerezakulikuwa na mataifa yaani makabila madogo mawili ya Uskoti yaani nchi ya Wa-Scotish na Ireland- nchi ya Wa-Irish. Haya ni makabila, si mataifa tu.

Huko nyuma wakati Uingereza ikiwa taifa kubwa duniani, iliwatawala hawa pamoja na sisi wengine na kuanzisha ilichokiita, jumuiya ya madola ( The common wealth).

Wakati sisi tumepigania uhuru kutoka himaya ya Malkia wa Uingereza, Wa-Irish nao wamedai uhuru wao kutoka himaya ya kabila la Mwingiereza na kujitoa kwenye muungano wa umoja wa Uingereza na kufanikiwa.

Na kwa sasa Uingereza ilipoamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya, U-skoti nao unadai kujitoa katika umoja huu kwa sababu yenyewe inaona faida ya kuwa sehemu ya umoja wa ulaya. Tunaona jinsi mataifa haya madogo yalivyo imara katika kutetea utambulisho wao kama watu. Hata lafudhi yao ya Kiingereza ni tofauti na ya Waingereza wa ndani. Huu ndio ubinadamu wa kawaida wenye kujitambua.

Kwa nini sisi tumekimbia makabila yetu? Kwa nini hata sasa tunapotaka kujenga Kiswahili kama lugha ya kutuunganisha, tunajaribu kufanya hivyo nje ya uasili wetu. Kwangu mimi ukabila ni utajiri. Ni utajiri wa mila na desturi. Ni utajiri wa maneno ambayo tungeweza kuyatumia kukuza falsafa ya Kiswahili ili ikidhi mahitaji mapana ya bara la afrika, kwa sababu licha ya ugeni wake, Kiswahili kina mashiko maeneo mengi ya Kibantu.

Tukijikumbusha makabila yetu yalivyoishi enzi hizo, tunaambiwa kulikuwa na mahusiano mazuri na mabaya kati ya makabila, kama mataifa. Kulikuwa na vita pia za kikabila na kitaifa cha wakati ule. Mahusiano kati ya makabila mataifa yalifanana tu na makabila mataifa ya leo. Kulipiganwa vita na kuchukuliwa mateka wa vita.

Mahusiano kati ya Wabarbaig na Wairaq kwa mfano yalifikia hatua ambayo wanawake wa Kiiraq walichukuliwa mateka na Wabarbaig kwa mfano, wakaolewa huko na wakawa sababu ya kupunguza vita baada ya kuwazalia wabarbaig watoto. Mtemi Sarwat wa Wairaq alipigana na Wabarbaig na mpaka leo kuna semi zinazoashiria utamaduni huu. Hii ndio asili yetu.

Tukiichunguza vizuri inafanana na jamii zingine duniani. Si ya kubeza na kutupa, hasa wakati huu tunapotaka kujenga Kiswahili kama lugha ya taifa la Tanzania na kama lugha pekee mpaka sasa inayoweza kuunganisha bara hili lote.

Kiswahili halisi chenye mashiko kitajengwa na falsafa inayotokana na lugha na makabila ya Kiafrika. Kwa hiyo watafiti waanze kazi ya kuongeza maneno, mila na desturi muhimu zinazohitajika katika kukikuza kwa haraka zaidi Kiswahili.

Maandalizi ya vitabu na waalimu wa Kiswahili duniani kote iwe moja wa mkakati wa Tanzania kujenga na kuimarisha mahusiano kupitia lugha. Umoja wa Afrika unaozungumza Kiswahili unawezekana, unahitaji nguvu kidogo ya mataifa yote haya na mengine yanayounga mkono juhudi za afrika kufikiwa.

Kwa hiyo makabila licha ya kuwa utajiri wa mila na desturi, pia ni utajiri wa utambulisho wa utu. Tabia iliyoingia ya mataifa ya mbali kuja kwetu na kujipa ukuu, wa kiuchumi, kisiasa na kijamii si kigezo cha kutuzuia sisi kurudi kwenye misingi ya asili yetu na kuitawala.

Wajerumani ndio walioanza kutuunganisha kwa kupitia lugha ya Kiswahili, si kwa sababu ya kutaka tuungane bali kwa sababu ya kutaka kuwa na kundi la kazi ( working class) linaloshabihiana na ambalo ingekuwa rahisi kulitawala. Kiswahili kikashika kasi wakati ule pia kwa uwepo wa lugha za mwambao zilizoshabihiana na Kiswahili.

Waingereza hawakujali umoja huu. Wao walitumia mbinu za kuwagawa watu ili iwe rahisi kuwatawala. Na kwa hiyo lugha za makabila na ukabila zilirudi tena, bila unafuu katika kujiunda kama mataifa na kama taifa moja ndani ya nchi na ndani ya bara zima.

Ubepari uchwara ni matunda ya mfumo huu wa ukoloni. Leo ni kipenzi cha nchi nyingi za afrika bila falsafa na siasa zinazoujenga mfumo huu.

Maana ya ubepari uchwara ni nini hasa: Maana yake halisi ni utambulisho wa kundi la jamii katika mfumo wa kibaguzi linaloundwa na wakulima wadogo (peasants), na kwa kiwango kikubwa wafanya biashara / wachuuzi wadogo.

Historia ya maendeleo ya Ulaya inawaelezea hawa kama chimbuko la siasa zinazopingana na kundi la mabepari halisi wanaomiliki njia kuu za uchumi, ambazo mabepari uchwara wadogo kiuchumi wanalitegemea kwa kuuza nguvu kazi yao kujipatia maisha.

Kiutamaduni mabepari uchwara hawaupendi ubepari halisi kwa ababu unawanyonya lakini huiga kwa kila namna na kutaka sana kuwa kama kundi hilo. Kwa mantiki hii, dhana ya ubepari uchwara inahusisha maendeleo ya vitu katika mfumo wa kisiasa unaowanyima fursa ya kumiliki njia kuu za kiuchumi.

Kundi hili ndilo pia baadae lilibadilika na kuwa daraja la kati katika mfumo wa ubaguzi wa kiuchumi na kisiasa. Wanafalsafa kina Marx na Lenin waliuelezea vizuri mfumo huu. Mahusiano kati ya kundi hili la raia na kundi la mabepari ndilo lililozaa aina ya siasa za ujamaa na ubepari barani ulaya na hata Marekani ambayo raia wake wa sasa wengi ni wahamiaji kutoka mataifa ya Ulaya.

Katika mfumo wa ubaguzi, mabepari uchwara walidharauliwa na mabepari halisi. Mfumo wa dini nao ulionekana kupendelea ubepari halisi na kwa hiyo mafundisho ya dini yalielekeza laana kwa kundi hili kama kundi lililoachwa na Mungu.

Ilidaiwa kuwa tabia ya ubepari uchwara haibadiliki hata mtu akiwa na cheo kikubwa kama cha uwaziri mkuu. Katika nchi za ufalme kama Uingereza na Uholanzi, waziri mkuu ndiye Kiongozi wa serikali na mwenye nafasi ya juu. Hata hivyo ikitokea alitokana na kundi la mabepari uchwara, alidharaulika vile vile kwa asili yake.

Mabepari uchwara walionekana kama watu wasio na malengo, wasio na mipango ya muda mrefu na wategemezi. Kundi hili ndilo pia lililozalisha siasa za kijamaa likitafuta usawa na kundi la ubepari halisi.

Licha ya kudharaulika kwake, mabepari uchwara ndio waliojenga hoja za kujenga mfumo wa huduma za kijamii. Kwa mfano inafahamika kama kundi lililohudumia wajane, na masikini wa chini yao. Ndio pia waliokuwa wabunifu wa mifumo ya kijamii, maeneo ya starehe, upashanaji habari na umbeya ulioambatana nao, na kuunda makundi ya kijamii ya kusaidiana.

Huu ndio ubepari uchwara: ubepari unaotamaniwa na watu wasiomiliki njia kuu za uchumi. Aina hii ya ubepari unafanana sana na kiwango cha maendeleo tulipo leo Tanzania. Tofauti ya ubepari uchwara wa Ulaya na wa hapa kwetu ni kuwa wa wenzetu una mzizi ya historia ya mataifa yao, na historia ya maendeleo yao kiuchumi na kisiasa.

Ubepari uchwara wa Tanzania na Afrika, hauna mizizi. Unaelea katikati ya wimbi la umasikini wa fikra mbadala na hali halisi. Kwa sehemu ni kama tuna bahati kuundiwa mifumo na watu wengine na sisi kupata fursa ya kuchagua mfumo wa kufuata ama kuacha. Kwa sehemu ni hasara kwa sababu asili ya utu inataka uzoefu wako uzae matokeo yake.

Kwa sababu hii wengi wetu hapa ni hawa mabepari uchwara wanaotamani ubepari halisi. Azimio la Arusha la kuweka mipango ya maendeleo na maisha yetu haina maana tena. Dhana rahisi za kuletewa zilizofanyiwa kazi na watu wengine ndizo tumezipenda.

Kwa sababu hii hatuwezi kudai kuwa na uzoefu wa kutosha kuzitangaza sera hizi. Hata hivyo mwaka 2015 tulijaribu kuzitangaza tena na matokeo yake tuliyaona. Watu wengi walipenda kiwango cha uchambuzi na ufafanuzi. Inawezekana watu walipenda kwa kukosa mbadala. Inawezekana pia kuwa walipenda kwa uhalisia wake.

Hata hivyo, msingi wa ubepari ni uchumi na siasa inayotetea uchumi huo. Wakati wa kampeni za marekani tuliona jinsi ambavyo mfumo wa kibepari ulivyoshabihiana hata miongoni mwa wagombea wa itikadi tofuati. Mama Clinton hakuwa tofuati na Trump katika msimamo wao juu ya ubepari na misingi yake. Walitofautiana katika uwezo wa uwasilishaji. Hii iliacha ombwe la hoja kama ilivyotokea kwetu mwaka 2015.

Hapa niseme hivi kuwa siasa ni muhimu sana katika kujenga uchumi. Kila mrengo wa kiuchumi una siasa zinazoujenga ama kuubomoa. Hiki kitu kinakosekana kabisa hapa kwetu. Nyakati za uchaguzi ndizo pia ni nyakati za kuwaambia raia sisi ni nani na tunataka nini kwa maisha ya raia wetu.

Katika kuuza sera zetu pia msingi mkuu wa hoja zetu ulikuwa uchumi. Tulitaka na bado tunataka uchumi wetu umilikiwe na wananchi kupitia mfumo shirikishi wa utawala.

Tulitaka na bado tunataka kuona serikali ikisimamia njia za uchumi.
Tulitaka sana mabadiliko makubwa katika kukuza uchumi wa viwanda utakaotokana na kilimo. Kwa hiyo mkazo wetu ungekuwa kuimarisha kilimo cha wakulima wetu wadogo, Nyerere aliwaita peasants…aina ya mabepari uchwara masikini kabisa, wasio na kitu isipokuwa nguvu zao dhaifu.

Udhaifu wa masikini wa Tanzania na afrika unaongezwa na kukosekana kwa siasa zinazolenga kujijenga katika maisha halisi ya watu. Hakuna ushindani wa kisiasa katika hili. Kuna ushindani wa majina, wa vyama na hali ya hewa chafu wakati wa uchaguzi. Hakuna dhamira ya kweli ya kujenga nchi na kuitoa katika makucha ya ubepari halisi na ubepari uchwara unaotafuta kuiga ubepari halisi.

Kwa hiyo kwa mfano sasa tunaposikia uchumi wa viwanda bila kilimo, tunajiuliza utawezekanaje? Tunaposikia uchumi wa viwanda bila siasa inayoelezea malengo haya, tunajiuliza itakuwaje? Maswali ni mengi kuliko majibu lakini mwisho wa siku ni huyu mkulima mdogo anayeumia na kwa kuwa hawa ni wengi maumivu yake ni makubwa pia.

Kwa hiyo uzoefu tu wa kunadi sera hizi hautoshi, hautoi jawabu na haujibu maswali ya watu juu ya hali zao kiuchumi, kijamii na kisiasa. Tunahitaji kwenda mbali zaidi ya kunadi sera. Tungependa kuona mijadala ya bunge ikilenga mambo haya pia. Tungependa kuona mikutano ya kisiasa ikizungumzia hoja hizi na kuzioanisha na itikadi zinazotetea ama kupinga hoja hizi.

Kukosekana kwa aina hii ya mifumo katika siasa zetu inatulazimishia ufukara wa kisiasa na kuzuia ubunifu ambao ungetokana na mijadala na mipango mbadala. Kwa upande wetu tumetoa mchango wetu katika eneo hili. Tumethibitisha kuwa ubepari uchwara upo Tanzania na unafanya kazi. Ubepari halisi umeimarika kwa mkono wa utandawazi na uwekezaji.

Sasa tuna mabepari halisi na mabepari uchwara kwa pamoja. Kinachopungua kwetu ni siasa za kila mrengo na za kujipambanua hivyo. Kuna haja ya mabepari uchwara kuja na siasa zinazogusa maisha yao kupinga ubepari halisi na kulea tabia ya kuhoji mifumo hii inavyofanya kazi.

Ina tija kuendesha siasa za namna hii na kuleta ushindani wenye masilahi kwa taifa. Kwa hiyo ni wajibu wetu kuendelea kuonesha kwa vitendo jinsi mfumo wa ujamaa wa kidemokrasia unavyoweza kuleta unafuu kwenye maisha ya watu.
Kuna mambo ya msingi ya kufanya ili kufikia lengo hili. Kwa mfano umiliki wa ardhi. Wananchi wanaoishi vijijini kwenye maeneo ambayo yamemilikishwa wageni ni lazima wajue hatima yao.

Haiwezekani sheria inayotungwa Tanzania impe unafuu mgeni anayekuja kuwekeza kwa muda na kumnyima kabisa haki mwenyeji mmiliki halisi wa ardhi hiyo kwa kigezo cha hati. Wananchi wetu hawana mbadala wa uraia na umiliki wa asili. Tuwape nguvu kuijua na kuisimamia haki yao hii ya msingi.

Pili mfumo wa uzalishaji kiuchumi unaotegemea kilimo na ufugaji uwekewe mazingira rafiki ya uzalishaji wa ndani kwa mauzo ya ndani na nje. Katika ubepari halisi wakulima na wafugaji wanaendesha shughuli zao kwa ushindani bila bughdha, lakini sisi tumeshindwa kuweka utaratibu wa kuwawezesha hawa kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Matokeo yake imesababisha migogoro na uhasama mkubwa miongoni mwa makundi haya.
Tatu ni kuhakikisha sekta zote za uchumi zinalenga na zinaleta athari chanya za moja kwa moja kwa mwananchi. Hizi ni pamoja na utalii, misitu, uvuvi, na usafirishaji.

Kwa ujumla mjadala wa azimio la arusha / tabora baadae na muktadha wa maendeleo ya Tanzania umekuwa kama dhima iliyokosa wachezaji.[1] Sisi tunafikiri dhima hii ina tija na inahitaji kuendelezwa.

Tuweke mikakati ya kuushawishi umma kuwa inawezekana kulihuisha azimio la arusha na kuendana na Azimio la Tabora / ama lingine lolote linaloweza kuimarisha hoja hizi.
Kwa hili tulipanga kutoa heshima zetu Arusha kwa historia yake na mchango kwa siasa za Tanzania na Afrika Mashariki. Arusha imekuwa mlezi wa mabadiliko ya aina mbalimbali tangu wakati wa ukoloni hadi leo na wenyeji asili wa mji na mkoa huu. Hongera kwa watanzania wote kwa kuunga mkono mabadiliko ya aina mbalimbali yaliyoasisi taifa letu.

Mungu Ibariki Arusha, Ibariki Tanzania na Afrika.


AMINA!


[1] Barani afrika mjadala huu umelipooza bara lote. Juhudi za kikomboa afrika ilikuwa na lengo la kuiunganisha kwanza kuwa jamii moja, kwa sababu kimsingi pia afrika ni moja, kama ambavyo Korea ni moja. Iwe kusini ama magharibi, afrika ni moja. Kuna wanaofikiri kwa mfano kuwa ukiita sehemu moja ya afrika kwa jina tofuati unaiondoa kutoka bara hili na unaipeleka kwingine.
 
Uchumi wa kibepari umeshakita mizizi mama Anna mghwira. Whether ni ubepari uchwara au ubeberu.

Tanzania kwa sasa kuturudisha kwenye Sera za ujamaa ni kutuvuruga tu na kutugombanisha wananchi. Lazima na nyie ACT mtambue kwamba ujamaa una gharama zake na si rahisi kuusimika. Yalimshinda Mwalimu Nyerere akaamua kukaa pembeni. Hii na namna ulimwengu unavyoendeshwa. Leo ukisikia Marekani anaweka vikwazo kwa Iran au kwa Zimbabwe utambue kuwa ni mfumo unapigwa vita.

Nawatakia kila la kheri katika azma yenu lakini naona mbele mkigonga mwamba.
 
Lazima na nyie ACT mtambue kwamba ujamaa una gharama zake na si rahisi kuusimika. Yalimshinda Mwalimu Nyerere akaamua kukaa pembeni.[/QUOTE]
 
Waterloo


Ninafikiri Tanzania inahitaji kujitafakari upya. hatuna mfumo unaoeleweka. Katiba inasema tunafuata sera ya ujamaa na kujitegemea.

Uhalisia unaonesha ubepari usio na mizizi. Ujamaa umebaki kama sera ya kijamii tena inayoishia. Hatupo popote. Ni vema tuamue sasa kabla hatujachelewa zaidi, kwa maoni yangu.
 
Ninafikiri Tanzania inahitaji kujitafakari upya. hatuna mfumo unaoeleweka. Katiba inasema tunafuata sera ya ujamaa na kujitegemea. Uhalisia unaonesha ubepari usio na mizizi. Ujamaa umebaki kama sera ya kijamii tena inayoishia. Hatupo popote. Ni vema tuamue sasa kablahatujachelewa zaidi, kwa maoni yangu.
Hilo ndio la msingi .ujamaa umebaki kwenye ilani ya CCM na kwenye katiba kiuhalisia ni tofauti kabisa.na pia nadhani kwa kukosa katiba maradufu inatuchelewesha sana kupiga hatua kwenda mbele japo si mwarobaini wa matatizo ya watanzania lakini itatupa mwelekeo wa taifa gani tunataka nchi yetu iweze kufikia.
Ubinafsi na chuki vinaliangamiza taifa badala ya kushughulika na masuala ya msingi wanasiasa wamebaki kukwamishana. Sijui kama tutafika.
 
Ujamaa na ubepari. Mwandishi kuacha ujamaa hivyo hivyo lakini ubepari kauongezea neno 'uchwara'. Naona hata ujamaa pia angeongezea na neno hilo.

Binafsi si mwana historia zaidi ya kuwa mpekenyuzi (jf kukiwa ni reference yangu kubwa). Ujamaa hapa kwetu ulishindwa kwa sabau nyingi tu - kubwa ikiwa kuhubiri yasiyowezekana kwenye uhalisia. Binadamu wote ni sawa wakati hayo yalikuwa kinyume, nikiwa na maana kwamba enzi zile ikiwa ni lazima kila amalizae kidato cha sita lazima ajiunge na jeshi la kujenga taifa. Kipindi hicho tulisoma na vijana wengi wa kihindi lakini kila walipokuwa wanamaliza karibia wote hawakujiunga na jeshi (ukiachilia mbali isolated cases ambazo ni chache sana kwa wahindi waliojiunga na jeshi). Tunakutana nao tena ukubwani wakiwa ni matajiri wenye ukwasi mkubwa tu. Enzi za ujamaa waswahili tulizuiwa kufungua maduka yetu hadi yawe ya ujamaa, yalifika wapi? Lakini wahindi waliendelea kuwa na makampuni yao yakifanya kazi na serikali, kama KJ Motors, Lonrho n.k.

Upande mwingine elimu. Iwe ubepari au ujamaa ni kiasi gani tulielimishwa kuhusu ujamaa? Au kuna tafiti zipi zilifanyika kuhusu hilo?

Kujitambua. Hatukuwa tunajua kusoma au kuandika hadi walipokuja wazungu (waarabu walikazania madrasa tu). Nasikia huko elimu ilikotoka watu walishaanza kusoma magazeti enzi za miaka 1670! Africa ilikuwaje kipindi hicho?

Ukitafakari utaona bado Africa hatujakuwa nauelewa wa kutosha ni nini tufuate kama mfumo wa maisha yetu. ILA kwa wingi tutaunga mkono ubepari kwa sababu hapa demokrasia imetafsiriwa vizuri zaidi tofauti na kwenye ujamaa. mfano mzuri ni huu ujamaa wa kitanzania ambao mwanzilishi alitengeneza mazingira ya kwamba yeye na chama chake ndo wa kuongoza nchi hii. Kupoteza, kuwekwa kizuizini wapinzani wa fikra za mwenyekiti hakujaanza leo na ndiyo maana hata wakati wa kupiga kura kipindi fulani serikali ilinunua magari mia saba kwa ajili ya kujihami na nguvu ya wananchi. Na sasa serikali iliyoko madarakani inakusanya kwa nguvu pesa kwa minajili kama hiyo kwa sababu kwenye bajeti hailekezwi.

Ubepari ni uchwara kama ulivyokuwa ujamaa.
 
Ni fikra pevu Sana na zinafaa Kuweka changamoto kwa wanazuoni Wetu na wanasiasa wengine na wapika sera wote serikalini.

Nakubaliana na hoja kwamba ccm imechanganyikiwa na kitu gani ikifuate.
Leo Dr magufuli anendesha Vita baridi na vuguvugu na wafanyabiashara haswa pale linapokuja suala la kodi na ushiriki wa hii sekta katika uchumi wetu haswa pale tofauti za kiuchumi na kipato zimeongezeka Sana sambamba na ufisadi wa Hali ya juu na kuporomoka kwa maadili kwa wafanyakazi na viongozi serikalini wanaoshirikiana na sekta binafsi (mabepari halisi wa ndani na nje wanaowatumia mabepari uchwara Wetu ambao ni viongozi Wetu wa serikali na umma kuendeleza huu ubepari uchwara usio na tija kwa taifa zaidi ya sectoral development na kupanua mianya ya mgawanyiko wa kitaifa).

Maamuzi ya Rais yanaendeshwa na sera rasmi iliyo kwenye makatarasi ya ujamaa huku tayari tumeshaweka misingi ya ubepari kiutendaji na hapa hata wawekezaji wa ndani na nje wanakua wqnachanganyikiwa na inawalazimu "kupiga dili" zaidi ya uwekezaji halisia kwa sababu taifa halieleweki na serikali haiaminiki huku wingu la utaifishaji kama wa 1967 likiwepo muda wote.

Kinachoendelea hapa na watawala Wetu ni kwamba wanakua reactionary na survivalists ya kwamba kila siku wanakuja na sera za kiuchumi za muda mfupi zisizoambatana na marekebisho halisia ya mfumo uliopo na kila mtu anataka kumaliza mihula yake miwili salama "survival" and doing the minimum basi na hamna jitihada madhubuti za Kuweka mipango ya sera ya muda mrefu ya ukuaji uchumi ndani ya mfumo husika au hata Kuukubali rasmi mfumo wa ubepari ndani ya CCM na kuvunja huu unafiki wa kuongea ujamaa na kujidai kutetea wafanyakazi na wakulima huku wanakula na mabepari na kuwasaidia kunyonya wananchi wa chini. Matokeo yake kila mtawala anakuja na yake na kuondoka kaache hajafanya kitu huku mwingine anakuja na nguvu kubwa na hamasa ya wananchi kwamba atarekebisha hiki au kile naye kuishia pale pale kama aliyemtangulia.

Tanzania ili kukua kiuchumi, kijamii, na kisiasa inahitaji itikadi na mfumo utakaofuatwa rasmi na watawala na viongozi wake huku sera zikitekelezeka kirahisi na kuvutia uwekezaji wa mitaji ya ndani na ya nje ambayo kwa sasa haina uhakika wa kurudi kama ikiwekezwa. Mwekezaji aliyevutiwa na kilimo kwanza sasa muda mfupi baadae inakuja viwanda huku kilimo kwanza serikali haikujikita kisawa sawa kuwaandaa wananchi, wakulima wadogo, kurekebisha sheria ya polisi ardhi, kutenga maeneo, Kuweka a multi ministerial platform ikishirkiana na taasisi muhimu za ndani na nje katika kuhakikisha utekelezaji wa sera sasa Nani atakuja kuwekeza katika viwanda? Haswa mawaziri wanapotiahiwa bastola, wawekezaji wanaponyang'anywa ardhi bila ya taratibu wala sheria, Rais anapoagiza passport zikamatwe za wakandarasi.

Serikali inapoamka tu na kupiga marufuku sehemu ya sekta ya vinywaji vyenye kilevi, n.K, n.K haya yote ni ishara za kachanganyikiwa kwa serikali na chama kisichojua itikadi yake haswa
 
Mama, kwanza nikupe pongezi kwa uwezo wako mkubwa kifikra na ujasiri wa kuleta hoja kwa hadhira tata kama hii ya JF - yenye mchanganyiko wa wajinga kama mimi, wapambafu, na werevu. Contribution yangu ni kwamba kiukweli ujamaa ni mfumo mfu. Kwa ACT kujinadi kwa kutumia ujamaa ni kupoteza muda na rasilimali. Socialism is good in theory, but practically it is very flawed. Na hiyo ndiyo sababu pekee inaufanya ubepari kuwa juu kwa sasa.

Ubepari unaendana na selfish nature ya binadamu na uhalisia mwingi tu wa maisha ya kawaida. Nashangaa hulioni hilo. Mfano (kwa mimi Mkristo, hata Biblia imenena) binadamu ni selfish by nature - since the fall of Adam and Eve. Ubepari unakiri hilo. Ujamaa unajifanya binadamu wote ni wakarimu. Ubepari unaamini ktk matabaka kwasababu binadamu siyo wote sawa kiuwezo hata ndani ya familia moja, lakini ujamaa unajifanya wote tupo sawa. I could go on and on ... but naomba niiishie hapa: mwisho nakusifu Mama, upo juu kifikra japo fikra zako kisiasa ni sawa na za mama yangu: ziilifaa zamani siyo sasa.
 
Ninafikiri Tanzania inahitaji kujitafakari upya. hatuna mfumo unaoeleweka. Katiba inasema tunafuata sera ya ujamaa na kujitegemea. Uhalisia unaonesha ubepari usio na mizizi. Ujamaa umebaki kama sera ya kijamii tena inayoishia. Hatupo popote. Ni vema tuamue sasa kablahatujachelewa zaidi, kwa maoni yangu.
Nafikiri mama kuliweka hili sawa ni lazima kwanza tuchambue misingi mikuu na tabia zinazounda ubepari ambayo kwayo imekuwa ikibadilika nayo kadiri mabadiliko ya teknolojia na ya kijamii yanapotokea. Pia twapaswa kuifahamu misingi na tabia za ujamaa wa kisayansi na ule wa kiafrika wa kina Mwl Nyerere na Nhrumah na namna unavyobadilika kadiri ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Nafikiri tukitumia huu mpangilio tutakuwa tuna kwenda vizuri kwa kupima misingi na tabia za kila mfumo katika jamii tunayoijenga. Je ni ya kijamaa au ya kibebari.

Ubepari umejikita zaidikatika upataji wa faida kubwa kupita kiasi kupitia mitaji yao kama njia ya uzalishaji. Mwanafalsafa wa ubepari Adam Smith katika kitabu chake The Wealth of Nattions aliiasa serikali isiingilie uzalishaji wa mali. Alisema biashara na uzalishaji ukiwahuru,mkono usioonekana utaidhibiti. Kwa kutekeleza haya ubepari ukawa na tabia ya uunyonyaji wa wafanyakazi kwa kufanya kazi muda mrefu, mazingira mabaya ya kazi, mshahara usiokidhi. Ubepari umekuwa ukibadilika mpaka kufikia ubepari wa utandawazi tulionao msingi wake mkubwa ni kupata faida kubwa na tabia zake ni unyonnyaji.

Ujamaa ni mfumo wa uzalishaji mali unaoamini katika kujenga taifa lenye usawa ambapo kila mtu anaishi kwa kufanya kazi. Tabia yake huwa hakuna fursa pana ya unyonyaji wa mtu dhidi ya mwenzie. Mfumo huu ulikuja kupinga ubepari. Uliasisiwa na Karl Max. Ulisaidia kuweka mazingira ya usawa kati ya mwenye mtaji na mwenye nguvu kazi kuwa watu sawa katika uzalishaji. Kipindi hicho ujamaa uliwezesha kupunguza saa za kazi kurekebisha mishahara, kuunda vyama vya wafanyakazi.Maneno niliyokoleza ndio misingi mikuu na tabia ya kila mfumo ambayo ndio tutakayo iangalia katika jamii tuliyonayo na kujijua sisi wajamaa au bepari. Tukumbuke na ujamaa uumekuwa ukitekelezwa kwa namna tofauti lakini lengo ni moja. Namna hizo ni usoshalisti,ukomunisti na usoshalisti wa Kiafrika.

Mfumo wa uzalishaji mali umekuwa ukiwasumbua sana watekeleza ujamaa. Kuna walioamini kuwa serikali ikimiliki njia kuu za uchumi itasaidia kupunguza unyonyaji wa mtu kwa mtu. Wengine walikataza kabisa kuwa na mali binafsi kila kitu kuwa cha umma. Nionavyo mimi hapa ndipo tunapojichanganya kuona ujamaa ni namna ya kuzalisha mali badala ya kujenga taifa lenye usawa lisilokuwa na unyonyaji.Mwl Nyerere katika moja ya andiko lake aliwahi sema ujamaa ni imani kwani tajiri anaweza kuwa mjamaa na masikini asiwe mjamaa. Huwezi kumwaga chakula wakati jirani yako anakufa njaa.
Katika mazingira ya sasa inaaminika kuwa sekta binafsi inaufanisi katika uzalishaji mali. Ilibainika kuwa watu walikuwa hawana uchungu na mali ya umma. Hivyo sekta binafsi ikapewa nguvu kuwa injini ya uzalishaji mali ikishiikiana na sekta ya umma. Hapa msingi wa ujamaa unailindwaje hapa? Maana ukiacha bila udhibiti ndio kurudi kwa Adam Smith.

Katika mfumo wa kijamaa tumekuja na mamlaka za kudhibiti wazalishaji wasiwanyonye wananchi kwa kuwapandishia bei na hata kusimamia mishahara. Hapa Tanzania kuna mamlaka mbalimbali za udhibiti zinazomlinda mlaji. Hiki ni kielelezo cha Taifa kuendeshwa kijamaa.

Andiko hili laweza kuhitimisha kwa kusema Tanzania ni nchi ya kijamaa kwa asilimia 90 kwa kuangalia namna umma mkubwa wa watanzania wanavyofaidika na mamlaka hizi za udhibiti. Mwamvuli huu umehifadhi watanzania wote wanafaidika nazo na kukingwa dhidi ya unyonyaji ambao ni tabia ya kibepari inayopingwa na ujamaa. Kuingia katika ujamaa si kama kuvuka mto kwamba ukipiga filimbi wote mnakuwa upande wa pili. Jamii ndogo zitakuwa na maisha ya kibepari na nyingine ya wakusanya matunda na uwindaji. Hata zana za mwisho za mawe bado zipo. Kuwepo kwao hakuondoi ukweli kuwa Tanzania ni nchi ya kijamaa.
 
Kipengele cha ujamaa na kujitegemea ni cha ccm, kitolewe kwenye katiba, kiwe tu sera ya ccm. Kikibaki ina maana vyama vyote (pamoja na ccm) vitalazimika kuhubiri misingi ya kijamaa vinaposhika dola, wakati matendo yatakuwa ya ubepari uchwara. Tukubali ujamaa hauna nafasi katika karne ya 21, na ukilazimishwa kwa mtutu wa bunduki hautakuwa na tija.
 
Ujamaa,uwe wa kidemokrasia au kidikteta,ni mfumo usiofaa kabisa

Ujamaa ndio umetufikisha hapa,nchi imekuwa masikini ya kutupwa,wananchi hawana ubunifu na matajiri wamekuwa chukizo kwa taifa bila sababu.

Ujamaa ulichochea uvivu,watu hawakufanya kazi ili wapate mali, waliokuwa na ubunifu wa kupata mali waliitwa wanyonyaji,wahujumu uchumi,hivyo basi serikali na vyombo vya dola viliwa-harass usiku na mchana na wengine kufikia kufungwa jela,hii iliua ubunifu katika nyanja zote,watu wakaona wakiwa wabunifu,wanatenda kosa la jinai,serikali ikaona ni yenyewe pekee ndio ilikuwa na jukumu la kubuni kwa niaba ya kila mtu,


Wazee waliokuwa na vipaji vyao wakaamua kuanzia kunywa pombe tu na kuongeza idadi ya wake.

Madhara ya ujamaa unaweza kuyaona hata katika utawala wa sasa,matajiri ni maadui! Nchi gani ya kijamaa ina vipaji vikubwa kama vya Mark Zuckerberg aliyeleta mitandao wa Facebook?

Watoto,hata nyumbani hawawezi kuwa sawa,lazima mmoja atamzidi mwenzake,ujamaa unalazimisha watu wawe sawa,mvivu awe sawa na mchapa kazi,tajiri awe sawa na masikini,huh ni upuuzi na ndio umetufikisha hapa,China waliuacha na baada ya kuutupa wamepiga hatua kimaendeleo
 
Pia mtoa mada,hujatupa tofauti ya ujamaa ulioshindwa kufanya kazi Tanzania enzi ya Nyerere kulinganisha na Ujamaa unaosema wa kidemokrasia

-je, ujamaa wa enzi ya Nyerere haukuwa wa kidemokrasia?

-Misingi halisi ya kijamaa haina demokrasia mpaka sasa tunataka tuiwekee kipengele cha demokrasia?

-misingi ya kijamaa haiheshimu private ownership of property,na ndio ilituletea nationalisation,watu walinyanganywa majumba yao ikapewa National Housing Coorporation,watu walinyanganywa viwanda,mashamba,ndio huh ujamaa unaohamasisha Umma kumiliki njia za uzalishaji?

-Shida kubwa ya ujamaa iliyofanya ukaanguka duniani kote ni ukosefu wa demokrasia?


-Tanzania inatakiwa ibadili vitu gani katika Sera na sheria ili iufikie ujamaa wa kidemokrasia?

-pia ni vigumu sana ujamaa ku-survive bila kuwa na element ya udikteta,ili umma upate kumiliki njia za uzalishaji,maana yake lazima uminye haki ya mtu mmoja mmoja kumiliki mali,kumfungia mipango ya mahakama kupigania haki ya kumiliki mali, na pia kumyima jukwaa la kisiasa la kusema,ukifuatilia duniani note,utekelezaji wa ujamaa uliambatana na udikteta mkubwa,misingi ya kidemokrasia ilistawi na imestawi katika mataifa ya kibepari
 
Ujamaa na ubepari. Mwandishi kuacha ujamaa hivyo hivyo lakini ubepari kauongezea neno 'uchwara'. Naona hata ujamaa pia angeongezea na neno hilo.

Binafsi si mwana historia zaidi ya kuwa mpekenyuzi (jf kukiwa ni reference yangu kubwa). Ujamaa hapa kwetu ulishindwa kwa sabau nyingi tu - kubwa ikiwa kuhubiri yasiyowezekana kwenye uhalisia. Binadamu wote ni sawa wakati hayo yalikuwa kinyume, nikiwa na maana kwamba enzi zile ikiwa ni lazima kila amalizae kidato cha sita lazima ajiunge na jeshi la kujenga taifa. Kipindi hicho tulisoma na vijana wengi wa kihindi lakini kila walipokuwa wanamaliza karibia wote hawakujiunga na jeshi (ukiachilia mbali isolated cases ambazo ni chache sana kwa wahindi waliojiunga na jeshi). Tunakutana nao tena ukubwani wakiwa ni matajiri wenye ukwasi mkubwa tu. Enzi za ujamaa waswahili tulizuiwa kufungua maduka yetu hadi yawe ya ujamaa, yalifika wapi? Lakini wahindi waliendelea kuwa na makampuni yao yakifanya kazi na serikali, kama KJ Motors, Lonrho n.k.

Upande mwingine elimu. Iwe ubepari au ujamaa ni kiasi gani tulielimishwa kuhusu ujamaa? Au kuna tafiti zipi zilifanyika kuhusu hilo?

Kujitambua. Hatukuwa tunajua kusoma au kuandika hadi walipokuja wazungu (waarabu walikazania madrasa tu). Nasikia huko elimu ilikotoka watu walishaanza kusoma magazeti enzi za miaka 1670! Africa ilikuwaje kipindi hicho?

Ukitafakari utaona bado Africa hatujakuwa nauelewa wa kutosha ni nini tufuate kama mfumo wa maisha yetu. ILA kwa wingi tutaunga mkono ubepari kwa sababu hapa demokrasia imetafsiriwa vizuri zaidi tofauti na kwenye ujamaa. mfano mzuri ni huu ujamaa wa kitanzania ambao mwanzilishi alitengeneza mazingira ya kwamba yeye na chama chake ndo wa kuongoza nchi hii. Kupoteza, kuwekwa kizuizini wapinzani wa fikra za mwenyekiti hakujaanza leo na ndiyo maana hata wakati wa kupiga kura kipindi fulani serikali ilinunua magari mia saba kwa ajili ya kujihami na nguvu ya wananchi. Na sasa serikali iliyoko madarakani inakusanya kwa nguvu pesa kwa minajili kama hiyo kwa sababu kwenye bajeti hailekezwi.

Ubepari ni uchwara kama ulivyokuwa ujamaa.
Ndio maana kuna haja ya kutafakari upya! Kuchagua tunayoweza kufuata na kuacha. Kila uchwara uachwe na kila chenye thamani kifuatwe.
 
Pia mtoa mada,hujatupa tofauti ya ujamaa ulioshindwa kufanya kazi Tanzania enzi ya Nyerere kulinganisha na Ujamaa unaosema wa kidemokrasia

-je, ujamaa wa enzi ya Nyerere haukuwa wa kidemokrasia?

-Misingi halisi ya kijamaa haina demokrasia mpaka sasa tunataka tuiwekee kipengele cha demokrasia?

-misingi ya kijamaa haiheshimu private ownership of property,na ndio ilituletea nationalisation,watu walinyanganywa majumba yao ikapewa National Housing Coorporation,watu walinyanganywa viwanda,mashamba,ndio huh ujamaa unaohamasisha Umma kumiliki njia za uzalishaji?

-Shida kubwa ya ujamaa iliyofanya ukaanguka duniani kote ni ukosefu wa demokrasia?


-Tanzania inatakiwa ibadili vitu gani katika Sera na sheria ili iufikie ujamaa wa kidemokrasia?
Ninafikiri tunahitaji kujitazama upya na kuamua tuende vipi mbele. Si hoja ujamaa ama ubepari ama ukijani ama chochote. Ni muhimu sana tuamue kwa pamoja mrengo tunaoutaka na sababu zake.
 
Ujamaa,uwe wa kidemokrasia au kidikteta,ni mfumo usiofaa kabisa

Ujamaa ndio umetufikisha hapa,nchi imekuwa masikini ya kutupwa,wananchi hawana ubunifu na matajiri wamekuwa chukizo kwa taifa bila sababu.

Ujamaa ulichochea uvivu,watu hawakufanya kazi ili wapate mali, waliokuwa na ubunifu wa kupata mali waliitwa wanyonyaji,wahujumu uchumi,hivyo basi serikali na vyombo vya dola viliwa-harass usiku na mchana na wengine kufikia kufungwa jela,hii iliua ubunifu katika nyanja zote,watu wakaona wakiwa wabunifu,wanatenda kosa la jinai,serikali ikaona ni yenyewe pekee ndio ilikuwa na jukumu la kubuni kwa niaba ya kila mtu,


Wazee waliokuwa na vipaji vyao wakaamua kuanzia kunywa pombe tu na kuongeza idadi ya wake.

Madhara ya ujamaa unaweza kuyaona hata katika utawala wa sasa,matajiri ni maadui! Nchi gani ya kijamaa ina vipaji vikubwa kama vya Mark Zuckerberg aliyeleta mitandao wa Facebook?

Watoto,hata nyumbani hawawezi kuwa sawa,lazima mmoja atamzidi mwenzake,ujamaa unalazimisha watu wawe sawa,mvivu awe sawa na mchapa kazi,tajiri awe sawa na masikini,huh ni upuuzi na ndio umetufikisha hapa,China waliuacha na baada ya kuutupa wamepiga hatua kimaendeleo
Ni vizri kufikiri na kutoa maoni. Ninafikiri tumefikia masikini huu kwa sababu nyingi tofuati ikiwa ni pamoja na ujamaa wa aina iliyoendeshwa na Mwl Nyerere. Kiuhalisia mfumounaotoa fursa sawa kwa wote ni mfumo sahihi bila kuupa jina. Tukiuta ujamaa ni lazima tueleze aina yake na mifano yake, vivyo ubepari. Kiini cha kuchelewa kwetu kimaendeleo kinaweza kuwa elimu zaidi kuliko siasa.
 
Mama, kwanza nikupe pongezi kwa uwezo wako mkubwa kifikra na ujasiri wa kuleta hoja kwa hadhira tata kama hii ya JF - yenye mchanganyiko wa wajinga kama mimi, wapambafu, na werevu. Contribution yangu ni kwamba kiukweli ujamaa ni mfumo mfu. Kwa ACT kujinadi kwa kutumia ujamaa ni kupoteza muda na rasilimali. Socialism is good in theory, but practically it is very flawed. Na hiyo ndiyo sababu pekee inaufanya ubepari kuwa juu kwa sasa.

Ubepari unaendana na selfish nature ya binadamu na uhalisia mwingi tu wa maisha ya kawaida. Nashangaa hulioni hilo. Mfano (kwa mimi Mkristo, hata Biblia imenena) binadamu ni selfish by nature - since the fall of Adam and Eve. Ubepari unakiri hilo. Ujamaa unajifanya binadamu wote ni wakarimu. Ubepari unaamini ktk matabaka kwasababu binadamu siyo wote sawa kiuwezo hata ndani ya familia moja, lakini ujamaa unajifanya wote tupo sawa. I could go on and on ... but naomba niiishie hapa: mwisho nakusifu Mama, upo juu kifikra japo fikra zako kisiasa ni sawa na za mama yangu: ziilifaa zamani siyo sasa.
Ninaishi sasa na ninafikiri sasa. Kuleta hoja ijadiliwe ni kutoa fursa ya kujifunza kujua wengine wanafikiri nini na nini kifanyike kuboresha maisha, sera, sheria nk. Nafikiri hili si la zamani kama mimi eti? Tujadili kujifunza na kuchukua hatua. Asante kwa mchango wako.
 
Ni vizri kufikiri na kutoa maoni. Ninafikiri tumefikia masikini huu kwa sababu nyingi tofuati ikiwa ni pamoja na ujamaa wa aina iliyoendeshwa na Mwl Nyerere. Kiuhalisia mfumounaotoa fursa sawa kwa wote ni mfumo sahihi bila kuupa jina. Tukiuta ujamaa ni lazima tueleze aina yake na mifano yake, vivyo ubepari. Kiini cha kuchelewa kwetu kimaendeleo kinaweza kuwa elimu zaidi kuliko siasa.
Mtu aliyeelimika kipindi cha ujamaa wa Nyerere asingeweza kufanya chochote kwa kutumia elimu yake,na nina imani pia hawezi kufanya chochote chini ya ujamaa.

Ujamaa ni mfumo hodhi usiojali vipaji wala elimu,vijana wa nchi za kibepari,wasomi,wanaumiza vichwa kufanya uvumbuzi wa mambo mbalimbali ya kiteknolojia na kuyauzia makampuni makubwa ambayo huwapa pesa nyingi,hii ndio ilichochea mapinduzi katika nyanja nyingi.

Nadhani ujamaa,kwa maana serikali kumiliki njia za uzalishaji ni impractical,ni mfumo ambao serikali(sio jamii) inachukua jukumu la kufikiria kwa niaba ya kila mtu, kama ni ubunifu wa teknolojia,basi serikali itafikiri kwa niaba yetu,

na kama serikali ikiwa zigzag,inaacha kufikiri,matokeo yake,viwanda vya URAFIKI,MWATEX,SUNGURATEX vilizalisha khanga miaka nenda rudi,havikujua kama kuna wanaume wanahitaji masharti na suruali,na viongozi walijua kuna teknolojia za kuzalisha masharti na suruali duniani.

Ujamaa hauchochei ushindani,ushindani ndio mama wa ubunifu duniani kote, katika ujamaa,mali zote ni za umma,unashindana umshinde nani wakati mali ni zetu sote?

Katika muktadha wa kiuchumi,japo mimi si mchumi,ujamaa ulifeli asilimia mia
 
I hate the so called ujamaa,,:mad::mad:

Ni kudumizana akili tu, kubweteka, na kurudishana nyuma kimaendeleo. Mataifa makubwa kama china, Urusi yaliyokuwa mama na waanzilishi wa Ujamaa wenyewe wameshindwa kuukumbatia na kuingia kwenye ubepari siye kataifa kachanga bado bado hata kamasi tunashindwa kufuta ndo ntuende tena kwenye Ujamaa,, Mama hebu acheni mambo yenu ya kuturudisha kwenye ujima.

Wakati mataifa mengine yanakimbia sisi ambao tulikuwa tumelala angalau sasa tumejinyoosha tunataka hata kutambaa tujipigie tena misumari ya kujivunja tuwe vulnerable kabisa. Hata North Korea wenyewe wamekumbatia kaujamaa wakaona hawatoboi wakaanzisha "JUCHE", tuachani kujidanganya.

Tukitaka kusonga mbele kama Taifa na tuwe na uchumi tishio Afrika ni tuwe mabepari kweli kweli. Yaani Taifa bepari kweli kweli.


Hakunaga kitu usawa duniani tusidanganyane. Kwamba watu walingane kwa kila kitu, hiyo kitu haipo na wala haitakaa iwepo. Tung'ang'ane watu wapate kwa haki lakini si kwa usawa. Ndo maana kuna wanene, wembamba, warefu, wafupi, weusi, weupe n.k. hatuwezi kuwa sawa.

Nawashauri badilisheni sera. Mabepari hoyeeeo_Oo_O
 
Back
Top Bottom