Tanzania ya ndoto zangu

JMP Mchungu

Member
Jun 30, 2015
49
125
Hotuba inayoitwa I Have a Dream (Nina Ndoto) ya mwanaharakati na nembo ya haki za mtu mweusi Marekani, Martin Luther King Jr, ilipambanua ni nchi ya aina gani ambayo
mwanaharakati huyo aliitaka na aliyotamani watoto wake waishi. Hotuba hiyo ya Agosti 28, 1963, aliyoitoa kwenye kilele cha Maandamano ya Washington kwa ajili ya Kazi na Uhuru, Martin Luther alisema: “Nina ndoto kwamba watoto wangu wanne wadogo ipo siku wataishi kwenye taifa ambalo hawatahukumiwa kwa rangi ya ngozi yao, bali kwa maudhui ya uhusika wao.”

Hotuba hiyo imebaki kuwa bora zaidi kwa Martin Luther na maudhui yake yalikuwa ni kuchagiza hamasa na kuchochea uhuru na usawa kwa Wamarekani rangi zote kuwa na haki linganifu mbele ya huduma za kijamii, ajira, shughuli za uzalishaji mali na uchumi kwa jumla. Nyakati ambazo Marekani ilikithiri vitendo vya ubaguzi wa rangi,
Wamarekani weusi wakinyanyaswa hasa kwa kunyimwa haki za kiraia kama wananchi na wanajamii, King anaumia lakini kwa sababu kiu yake ni usawa ndiyo maana alisema alikuwa na ndoto. Nami pia kama Mtanzania, nina ndoto. Ipo Tanzania ambayo naitamani.

Niishi katika maisha yangu yaliyosalia au ndugu zangu, Watanzania wenzangu na mtoto wangu aishi kwenye Taifa ambalo utu linakuwa jambo la kwanza kwa kila mmoja. Kama ambavyo mataifa makubwa Ulaya yalipoketi Ujerumani mwaka 1884-1885 ili kuligawa
Bara Afrika, lakini kwa umuhimu zaidi wakatiliana saini ya kulinda raia wa nchi zao popote walipokuwapo, ndiyo hamu yangu kuona Mtanzania anakuwa mwenye thamani
kubwa. Mantiki inayosimama hapo ni kuwa watawala wa Ulaya pamoja na makubaliano mengine muhimu lakini waliweka mkazo wa kumlinda raia wa nchi yoyote ya Ulaya hasa miongoni mwa mataifa yaliyokubaliana biashara ya kugawana mkate wa kuitawala Afrika.

Ni kwa mkazo huo ndiyo maana Wajerumani walikataa kuelewana na Chifu wa Wahehe, Mtwa Mkwawa, kosa lake likiwa kuwaua raia 40 wa Ujerumani, akiwamo aliyekuwa kiongozi wao, Emil von Zelewski. Mwaka 1891, Ujerumani ikiwa inajieneza Tanganyika kiutawala, ilikutana na kipigo kikali kutoka kwa Mkwawa. Hata baadaye Mkwawa alipotaka mazungumzo na Wajerumani kupitia kwa aliyekuwa msaidizi wake, Mtaki Myayenza, suluhu haikupatikana. Wajerumani walimwambia Mtaki kuwa wasingeweza kuelewana na Mkwawa, kwani alifanya kosa kubwa kuwaua raia wenzao 40.

Baada ya hapo, walimrubuni Mtaki aliyeuza ramani ya vita ya Mkwawa ambaye baada ya kuzingirwa na Wajerumani alijiua kwa kujipiga risasi. Wajerumani hawakuishia hapo, baada ya kumtambua Mkwawa na kuthibitishiwa na Mtaki kwamba ndiye, walimkata kichwa na fuvu lake kulipeleka Ujerumani. Kwao ilikuwa ushindi kwenda kutangaza kifo cha Mkwawa angalau kufidia machungu ya vifo vya wenzo 40. Chuki na elimu Nina kumbukumbu za Wajerumani kwa sababu ya kuwa chanzo cha kifo cha Mkwawa na Watanzania wengi, lakini ipo elimu kutoka kwao ambayo nimeikusudia. Ni ile hali ya kuguswa na vifo vya ndugu zao na shauku ya kulipa kisasi.

Ulikuwa ujumbe kuwa Wajerumani ukitaka uwachezee basi mguse raia mwenzao. Ndicho ambacho natamani kuona Watanzania wakiwa na hamasa ya kulindana na isemwe kwamba ukitaka kuwavuruga basi jeruhi au katisha maisha ya Mtanzania mwenzao. Naitamani Tanzania yenye wananchi wenye kuhoji kuhusu usalama wao na
wanaoguswa na jambo lolote lenye kuwafika wenzao. Nione Watanzania wakipaza sauti na kushinikiza maelezo pale wanapoona jambo lisilo la kawaida, hususan linapohusiana na uhai wa Mtanzania mwenzao. Kipindi hiki ambacho miili ya watu inakutwa mara kwa mara fukwe za Bahari ya Hindi, taharuki ingepaswa kuwa kubwa.

Msukumo wa wananchi kuhoji ili kupata maelezo ya chanzo cha watu hao kukutwa wamekufa na ukweli wa uhusika wao, ungepaswa kuwa mkubwa. Msingi wa kuhoji ni kuthibitisha kuwa Watanzania wapo makini sana na usalama wa watu wao. Vilevile ni kuonyesha kuwa Tanzania si rahisi kufanya jambo baya halafu iwe kimya. Lazima kuwepo na ujumbe wenye nguvu unaojulisha kuwa Tanzania ni nchi ya watu makini. Tanzania ninayoitamani si ile ambayo watu wanaripotiwa kuokotwa ufukweni, lakini wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kama vile hakuna kilichotokea. Watu wanajadili kuokotwa miili ya watu kama gumzo jepesi tu kwenye daladala utadhani zilizookotwa ni samaki. Ndani ya mawazo yangu na mguso wa moyoni kuhusu Tanzania yangu ni kwamba nchi nisiyoitaka ni hii ambayo watu wakiwa baa ndiyo wanajadili masuala nyeti.

Wanazungumza vifo vya watu wenye kuokotwa ufukweni Bahari ya Hindi kusindikizia bia, nyama choma na michemsho. Naitamani Tanzania yenye wananchi ambao mmoja anajiona kuwa uhuru, amani na usalama wake vipo ndani ya Mtanzania mwenzake. Watanzania wenye hamasa kuwa akiguswa mmoja wameguswa wote. Siyo hii ya sasa mtu anashambuliwa, majirani wanajificha kwamba hayawahusu, eti mpaka
yawafike kwao. Tanzania inayoudhi Watu waovu kuiona Tanzania ni nchi nyepesi kufanya uhalifu halafu iwe kimya. Septemba 7, mwaka huu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 32 na zaidi ya tano zilipenya mwilini.

Athari ya shambulio la Tundu Lissu ni kubwa na haielezeki kwa maneno ikatosha. Kada wa Chadema, Ben Saanane anafikisha mwaka mmoja tangu alipotoweka. Imekuwa kimya mpaka leo. Haijulikani Ben bado mzima au la! Kinachoudhi ni kuona watu walio nyuma ya matukio hayo wanaidharau Tanzania kuwa ni nchi nyepesi kutenda waliyoyatenda. Tukio la Lissu kushambuliwa na mazingira yake yaliyokosa woga na yenye ishara ya kujiamini hadi kupitiliza kwa waliotenda unyama huo, kupotea kwa Ben na matukio mengine ya
utekaji, kwa pamoja yalipaswa kuwaunganisha Watanzania, kuwaleta pamoja kuitafakari nchi yao. Tanzania yenye watu ambao wanagawanyika mpaka suala hatari lenye kuhusu maisha ya Mtanzania mwenzao, upande moja wakiwatuhumu wenzao kuhusika, wengine wakikejeli utafikiri mjadala ni kuchomwa moto bendera za chama cha siasa, hii inaudhi sana.

Matokeo ya malumbano ya Watanzania yanaonyesha kuwa utu ndani ya mioyo yao haupo. Wanasiasa wameingiza ganzi kwenye nyoyo zao, matokeo yake wanajadili siasa na vyama vyao kuliko utanzania wao. Wanatuhumiana, kuchekana na kukejeliana kwa matukio ya shambulio la risasi na kupotea mtu. Hayo ndiyo mambo ambayo yanawafanya watu waovu waione Tanzania ni nchi nyepesi kwao kutekeleza uharamia. Baada ya matukio huwa hawaungani kuutetea Utanzania wao, bali hugawanyika na kuzungumza kama mambo madogo, kuanzia Ben mpaka Kibiti na Lissu. Watu wanavunjiwa nyumba zao na kugeuka wasio na makazi, upande wa pili Watanzania wenzao wanashangilia wengine wanalalamika.

Tanzania yenye watu ambao si faraja kwa wenzao nyakati za matatizo, yenye kuendekeza ushabiki kwenye masuala yenye kugusa hisia na maisha ya watu, ni yenye kuudhi. Tanzania ninayoishangaa Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu juzi alitangaza kujivua vyeo vyake vyote ndani ya CCM na kujivua uanachama kisha kuomba kujiunga na Chadema. Uamuzi huo ukavuta mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari hasa kwenye mitandao ya kijamii. Nyalandu akasababisha masuala mengine yote yasimame, yasijadiliwe na yalipojadiliwa yakawa na mvuto mdogo. Nyalandu ni mbunge tangu mwaka 2000 akiwa CCM, amekuwa naibu waziri kisha Waziri wa Maliasili na Utalii katika miaka miwili ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne, hivyo suala lake la kuhama chama halipaswi kuwa na mvuto mdogo.

Suala la Nyalandu kuhama chama, kuacha ubunge na sababu alizotoa, jumlisha na hatua hiyo kufuata baada ya kujishughulisha kwa ukaribu na tukio la kushambuliwa Lissu na kuumizwa sana kwa risasi, kwa pamoja inaleta tafakuri. Hata hivyo, mshangao ni kuona kuwa watu wanagawanyika, wengine wanapongeza, wapo wanaoponda na kumshambulia Nyalandu. Mitandao ya kijamii inajaa Nyalandu kwa pongezi na mashambulizi. Hali hiyo ukiipima na mazingira ambayo nchi inapita, inabidi tu ushangae. Mjadala wa Nyalandu sawa lakini inashangaza kuona nguvu inayotumika kumjadili ni kubwa mno, laiti msukumo huo kwa robo yake, ungetumika kujadili matukio ya watu kukutwa wamekufa Bahari ya Hindi, ingesaidia kuidhihirishia dunia kwamba Watanzania wapo makini mno na maisha yao pamoja na ya ndugu zao.

Tanzania haitakiwi kuwa kama Rwanda, miili ya makumi ya watu ilikutwa inaelea Ziwa Rukombe kwenye mpaka wa Burundi na Rwanda, Serikali ya Burundi ilishituka, Rwanda kimya. Lazima nchi ijiwekee viwango vya usalama wa raia, Taifa lazima lisimame kama ambavyo Wajerumani walivyomlia kiapo Mkwawa kwa sababu ya vifo vya Wajerumani 40.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom