The Khoisan
JF-Expert Member
- Jun 5, 2007
- 14,645
- 11,806
Awamu ya Mzee Mwinyi iliongoza kwa kunyonga
2008-01-30 17:28:15
Na Job Ndomba, Dodoma
SOURCE: Alasiri
2008-01-30 17:28:15
Na Job Ndomba, Dodoma
Serikali ya awamu ya pili iliyokuwa ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi almaarufu kama Mzee Ruksa ndiyo inayoongoza kwa kutekeleza adhabu ya kunyonga watu.
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Bw. Mathias Chikawe ameliambia Bunge mapema leo asubuhi kuwa watu tangu nchi hii ipate uhuru jumla ya watu 82 wamenyongwa.
Amesema kati ya watu hao, kumi walinyongwa katika kipindi cha awamu ya kwanza, iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akasema watu 72 walinyongwa awamu ya pili ya Mzee Ruksa, huku katika awamu ya tatu na ya nne hakuna mtu aliyenyongwa hadi sasa.
Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa adhabu ya kifo kwa Tanzania bado ni adhabu halali na inaendelea kutumika.
Hata hivyo amesema Serikali imepanua wigo wa maoni ya wananchi kwa kuiagiza Tume ya kurekebisha sheria kuanza mchakato na hatimaye kupata maoni ya wananchi kama adhabu hiyo inastahili kuendelea kuwepo kwenye vitabu vya sheria vya Tanzania ama la.
Amesema mchakato huo ukikamilika na kupata maoni ya wananchi, Serikali iko tayari kusikia maoni hayo na hata kuleta muswada bungeni wa kuiondoa sheria hiyo.
Bw. Chikawe ametoa maelezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve Mheshimiwa Richard Ndasa, CCM, aliyetaka kujua idadi ya watu waliokwishanyongwa chini ya adhabu hiyo na awamu ipi ya Serikali iliyotekeleza ipasavyo adhabu hiyo.
SOURCE: Alasiri