Tanzania na China zasisitiza kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya utamaduni na michezo

Ojuolegbha

JF-Expert Member
Sep 6, 2020
662
429
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika uendelezaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo hapa nchini.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo Machi 29, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania, Suo Peng akieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika kuendeleza Sekta ya Utamaduni na Michezo hapa nchini, kubadilishana uzoefu wa Wataalam wanaoweza kutoa ujuzi kwenye Sekta hizo.

“Tumekutana leo kuona namna tunavyoweza kuja na ubunifu na kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania na China kwenye sekta zetu hususani maeneo ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutambua kuwa China ina utajiri mwingi kwenye sekta hizi” Amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.

Amesema Tanzania na China zimekua na ushirikiano mkubwa katika masuala mbalimbali tangu uhuru ambapo Viongozi waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Tse Tung wa China walianzisha ushirikiano huo kwa manufaa ya Wananchi wa pande zote akiongeza kuwa China imekua ikitoa misaada mingi kwenye maeneo mbalimbali.

Waziri Balozi Pindi Chana ameeleza kuwa Tanzania na China zimeshaingia na kusaini makubaliano ya uendelezaji wa masuala mbalimbali ambayo pia Marais wa nchi hizo wamekua wakiyaeleza hivyo ni wakati muafaka wa kuendelea kuyatekeleza.

Aidha, amemueleza mwakilishi huyo wa Balozi kuwa eneo la Utamaduni, Sanaa na Michezo ni muhimu sana katika kuimarisha Amani, Umoja na maelewano miongoni mwa jamii, hivyo ni muhimu lipewe kipaumbele akibainisha kuwa Wizara yake imeanzisha programu za michezo ya Mtaa kwa Mtaa kuhakikisha kuwa michezo inapewa nafasi kwenye nchi “China ni Tajiri kwenye eneo la lugha, tunataka hata sisi Lugha yetu ya Kiswahili iweze kutumika Kimataifa”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi wa China Suo Peng amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China zimekua na ushirikiano mkubwa tangu miaka ya 1960 akisisitiza kuwa Marais nchi hizo Dkt. Samia Suluhu Hassana na Xi Jinping wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika kuendeleza maeneo mbalimbali yakiwemo ya Utamaduni na Michezo.

“ Sisi China na Tanzania tunayo mambo mengi ya kujivunia katika ushirikiano na tunaendelea kuweka mazingira ya kuwa na ushirikiano katika maadhimisho na matukio ya pamoja yatakayojumuisha masuala ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Tunahitaji tujipange vizuri na tuainishe maeneo ambayo tunaweza kuongeza ushirikiano zaidi” Amesema Peng.

IMG-20230329-WA0055.jpg
IMG-20230329-WA0054.jpg
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom