Tanzania inawahitaji wawekezaji kuliko wawekezaji wanavyoihitaji Tanzania?

KalamuTena

JF-Expert Member
Jul 7, 2018
13,189
17,156
Niliposikia/niliposoma maneno hayo, tena toka kwa kiongozi wa nchi sikuamini kabisa nilichosikia au nilichokisoma!

Kiongozi kamwe hawezi kamwe kuwa na fikra za namna hii kuhusu suala hili.

Pengine labda tuseme alikuwa na maana ya wawekezaji, hasa wa ndani ya nchi, ikihusisha wananchi wenyewe katika kuwekeza katika maendeleo ya nchi yao?

Lakini kama maana yake ilikuwa ni kuwalenga wawekezaji wanaotoka nje ya nchi, naikataa na kuitupilia mbali dhana potofu kama hiyo.

Lengo hapa ni nini, kwamba tufanye kila liwezekanalo, hata yale tunayoona sio kwa manufaa ya nchi hii ili mradi tuwafurahishe wawekezaji walete miradi yao hapa? Hili wazo sikubaliani nalo kabisa. Haiwezekani hata siku moja kutegemea maendeleo ya nchi yetu yaletwe na uwekezaji toka nje ya nchi. Maendeleo yetu yanategemea juhudi zetu sote, wananchi wa nchi hii kuyaleta kutokana na shughuli mbalimbali tutakazokuwa tunajihusisha nazo. Serikali isiweke kipaumbele kupapatikia uwekezaji toka nje na kusahau kuweka mazingira ya kutuwezesha sisi kujiletea maendeleo hayo.

Sasa, naomba nieleweke, sijakataa umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya kuvuta uwekezaji kutoka nje ya nchi, lakini uwekezaji huo usiwe kwa gharama ya juhudi zetu wenyewe. Tusiweke mazingira ya wawekezaji kuja kuzoa mali hapa na kutuacha hohehahe. Ni lazima tuwelke masharti yatakayohakikisha uwekezaji huo unaleta tija kwa manufaa ya wananchi wetu.

Niache mfano mmoja hapa: China, pamoja na kutokuwa kwenye nchi zinazofahamika kuwa na mazingira mazuri zaidi kwenye uwekezaji (kufuatana na vipimo vya wakubwa - World Bank); lakini uwekezaji kwenye nchi hiyo upo juu kuliko nchi kama New Zealand, amabaye ni kinara, namba moja katika kuwa na vigezo vya uwekezaji.
China anaweka masharti, kama kampuni yako inataka kuwekeza nchini humo, ni lazima 'intelectual property' yako uiweke wazi na uitumie kuwezesha wachina na wao waweze kuitumia. Kama hutaki, baki huko huko, hupati soko la China! Hiki ni kikwazo kigumu sana kwa mashirika, lakini bado wapo tayari kwenda kuwekeza China.

Najuwa vyema sana, sisi siyo China, lakini pia nakataa kabisa kukubali kujiuza kwa bei rahisi kwa wawekezaji, eti kwa vile sisi tunawataka zaidi kuliko wao wanavyotuhitaji sisi.
Tanzania ina sifa na vivutio vingi sana vinavyohoitajiwa na wawekezaji. Tusijiuze kwa bei rahisi kwa kushindwa kwetu katika kuvitumia vyema vivutio hivyo.

Angalia kwa mfano ilipo Bagamoyo. Hii unaweza kuishindanisha kwa njia yoyote na sehemu nyingine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki?. Sasa tunataka kujirahisisha, tugawe raslimali tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kwa masharti ya kijinga kabisa, eti tusipofanya hivyo washindani wetu watachukuwa wawekezaji!

Kwenye utalii hapa tunashindana na nani katika eneo hili katika kuvutia wawekezaji! SAWA, gesi ile Mtwara, Msumbiji wapo, lakini hatushindani. Kwa nini tuuze gesi yetu kwa masharti yasiyoleta manufaa makubwa kwetu, eti tusipoweka mazingira mazingira ya kupora, wawekezaji hawataendeleza mradi huo! Kwani Tanzania itatoweka wakiikalia hiyo gesi kwa masharti tusiyoyataka?
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom