Tanzania, Hungary kushirikiana kielimu, Hungary yaongeza ufadhili wa masomo

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,441
7,780
TANZANIA na Hungary zimesaini mkataba wa miaka mitatu wa ushirikiano katika sekta ya elimu, huku Hungary ikiongeza nafasi za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kutoka kumi hadi 30.

Hafla ya kusainiwa kwa mkataba huo ilifanyika mwishoni mwa wiki huko Budapest, Hungary ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakati Hungary iliwakilishwa na Waziri wake wa Uwezeshaji, Dk Laszolo Palskovics. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya elimu, mkataba huo utaanza rasmi Januari Mosi, 2018 na kwa kuanzia, Watanzania 30 watapata fursa ya udhamini wa masomo kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2020.

Udhamini huo utahusisha nafasi kumi za wanafunzi wa shahada ya kwanza katika kilimo, uchumi, sayansi na uhandisi. “Kutakuwa pia na nafasi 15 za Shahada ya Uzamili katika kilimo, uhandisi, uchumi na sayansi na pia kutakuwa na nafasi tano za wasomi wa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika maeneo yatakayopendekezwa na Serikali ya Tanzania,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Tanzania itapokea wanafunzi wa shahada ya uzamili kutoka Hungary, watakaokuja katika vyuo vya Tanzania kwa muda wa mwezi mmoja. Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Ndalichako aliishukuru Serikali ya Hungary kwa ushirikiano huo na pia alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za Rais, John Magufuli kwa serikali ya Hungary ambayo imeongeza nafasi za udhamini kwa Tanzania kutoka kumi hadi 30 kuanzia mwakani. Alitembelea pia vyuo vikuu vitatu na chuo kimoja cha ufundi kwa lengo la kujifunza zaidi.
 
Back
Top Bottom