Tanzania: Gharama, Faida na Thamani ya Demokrasia

Aug 18, 2010
65
22
...Inawezekana wengine wakadhani ni fikra za mwendawazimu kudhani kwamba "demokrasia ni gharama." Na inawezekana pia wengine wakaona kwamba tuna wajibu wa kutumia rasilimali nyingi katika kukuza demokrasia...acha watu waamue; kwa kuwa watu ndio wenye sauti, siyo?! Ndio; hata wengine wanadiriki kusema kwamba, "chaguo la watu ni chaguo la Mungu." Huku tunakwenda mbali sana!

Tunambebesha Mwenyezi Mungu "mzigo" wa dhana ambayo si stahili yake kwa kuwa sisi (msisitizo, sisi) tunataka, siyo?! Tunataka demokrasia kwa gharama yoyote...na zaidi ni gharama ya nani hasa? Je, tumefanya tathmini ni gharama ya nani kwa demokrasia isiyokuwa na faida (thamani) kwa wananchi? Tazama, kura moja inayopigwa inagharimu kiashi gani cha "thamani ya fedha" na rasilimali nyingine ndani yake? Nadhani si busara tukaacha hali hii iendelee kwa kuwa inaligharimu taifa na zaidi inalitia taifa umasikini wa kujitakia. Gharama za demokrasia ni kubwa na thamani yake ni "ndogo" kwa vile utashi wa watu (wanaopiga kura) haupimiki kwenye mizani ya thamani ya fedha (value for money = VfM).

Sisemi kwamba ni ujinga kushiriki kwenye uchaguzi wa kidemokrasia; hasha! Isipokuwa tunapotumia fedha nyingi kwenye kuandaa uchaguzi na badala ya wananchi wenye haki ya kupiga kura kujitokeza kutumia nafasi yao, zaidi ya nusu (50%) ya wapiga kura hawajitokezi kupiga kura na sehemu ya rasilimlai zilizotumika kwenye kuandaa uchaguzi zimekwenda bure buleshi! Huu ni upuuzi (au uzezeta) wetu? Tunahitaji majibu; si majibu rahisi, bali majibu yaliyokwenda shule. Ilikuwa hivi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, 2010 na hata kwenye chaguzi ndogo zinazoendelea (kupita na kupituka) kwa vile demokrasia inachukua nafasi yake na wananchi sasa wanaitaka kweli! Kama kweli tunataka demokrasia yenye thamani ya fedha (VfM) tuna wajibu kama watu huru na wenye akili ya upembuzi wa "gharama" dhidi ya "faida [thamani]" juu ya demokrasia tuna wajibu wa kukokotoa thamani ya demokrasia kwa ghrama tunazotumia kwenye harakati na uchakataji wa demokrasia yenyewe.

Hivi; ni nani anayelipa gharama hizo? Tazama, uchaguzi na au chaguzi zote zinapofanywa kuna gharama aina tatu kubwa zinazoingizwa kwake (hapa ni mifano yake):

  1. Gharama za kuandaa uchaguzi husika ambazo hupangwa kutoka kwa 'fuko" la serikali kwa matumizi yake yanayotokana na fedha za walipa kodi na fedha nyingine za wafadhili (kama zipo);
  2. Gharama zinazotumiwa na vyama vinavyoshiriki kwenye mchakato ambazo sehemu ni kodi za wananchi wanazopewa vyama kama "ruzuku" na sehemu nyingine ni michango ya wanachama, wafadhili, wahisani wa vyama na vyanzo vingine vya vyama; na
  3. Gharama zinazolipwa moja kwa moja na wapiga kura ambazo ukokotozi wake unatokana na aidha kwa wananchi kupoteza muda wao kwenye harakati na michakato ya demokrasia ya uchaguzi kama vile kuhudhuria kwenye mikutano ya kampeni na kuacha shughuli nyingine (opportunity cost) au hata kufanya kazi za vyama vya siasa.

Kwa muktadha wa nukta hizi tatu (kama zilivyoainishwa hapa) tunaweza kupata mlolongo wa gharama ndogondogo na kubwa kwa jinsi tunavyoweza kuzisanifu na kuzikokotoa katika kutafuta "thamani ya demokrasia". Kwa ujumla, thamani ya demokrasia inayotakiwa ni ile inayoweza kumpa mwananchi uhuru, haki na usawa wake ndani ya nchi yake katika kufikia utashi wa maendeleo endelevu kwa kupata uwakilishi na au uongozi wenye mtazamo wa kuona na kuelekeza watu kuelekea kwenye njia ya maendeleo. Kuna masuala hapa juu yake: je, mara zote tunapotumia gharama za fedha (chache, ambazo zingeweza kuleta thamani kubwa) huwa tunapima thamani ya fedha (VfM) tuliyotumia? Je, kuna wakati tumefanya tathmini ya kupima thamani hiyo (kwa mtazamo wa kiakili)? Au, tunakwenda kama watu tusiyefikiri na kuona hatma yetu?

Huu ni ukumbusho kwa watu wenye "akili" ya utambuzi na wanaojitambua! Isiwe tunasherehekea "chereko" cha demokrasia ilhali gharama zilizotumika ni kubwa kuliko faida iliyopatikana. Utakuwa ni ujinga na au wendawazimu wa kichaa kuona jalala na kisha kuanza kuchekelea vioaja vya vyakula vilivyotupwa na au kuoza; kama vile, "ganda la muwa la jana chungu kuona kivuno!" Huu ni mtazamo tu; mara zote kwa watu wenye akili timamu wana wajibu kupima gharama na faida itokanayo kwenye mchakato wowote ili kupima ufanisi (efficiency) ya matumizi ya fedha. Isichukuliwe sababu kwamba, "Alaa, mbona fedha zinazotumika ni ruzuku toka serikalini!" Na mwisho, demokrasia ionekane kama mchezo wa kutafuna fedha ya umma kwa maslahi ya mfumo tu (na sio faida inayodhamiriwa ya demokrasia). Ni wajibu wetu kutafuta thamani ya demokrasia kwa gharama tunayotumia; tusifanye kwa mazowea peke yake...tuna wajibu wa kuthamini kiasi cha fedha tunachoingiza kwenye demokrasia na kwa jinsi hiyo lazima wananchi wapate thamani ya fedha hiyo kwa uongozi bora!
 
Back
Top Bottom