TANROADS: Ujenzi ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani, unaendelea vizuri

Naipendatz

JF-Expert Member
Jul 27, 2011
5,080
8,219
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), umesema ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani, unaendelea vizuri na utakamilika kama ulivyopangwa.

Pia, umesema kuwa mpaka sasa mradi huo ambao utakwenda kupunguza tatizo la msongamano wa magari, umekamilika kwa asilimia 94, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kujengea matofali pembezoni mwa barabara.

Mkurugenzi mtendaji wa Tanroads, Rogatus Mativila, amelieleza Mwananchi kuwa kwa sasa wameomba nyongeza ya fedha kutokana na ongezeko la kazi ambazo hazikuwapo kwenye bajeti ya awali.

“Kwa sababu kuna kazi nyingi zilijitokeza wakati ujenzi ukiendelea, hivyo kuna ongezeko la kazi na moja wapo ni kujengea matofali pembeni upande wa kulia na kushoto,”alisema.

Kuhusu mapipa yaliyowekwa kwenye barabara hiyo, amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali hasa katika njia za katikati ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

“Hayo (mapipa) ya katikati hayajatolewa kwa sababu ukiyatoa ndiyo utasababisha ajali zaidi, kwani barabara itakuwa ni pana, itakuwa free (huru). Kwa kuwa zitakuwa ni barabara nane zote, hakuna namna ya kusema mtu anaweza kupata sehemu ya relief (unafuu) ya kusimama.

“Hata kwa magari yenyewe unajua kuna ku-overtake na nini. Hapo katikati ni kwa ajili ya BRT, lakini tunataka tutenganishe kwa kujenga hizo ‘cab stone’.

“Sasa ili kukamilisha hizo ‘cab stone’ tumeomba fedha wizarani kwa sababu bajeti yake haikuwepo kwenye kazi ya awali. Vipo vitu kadhaa ambavyo tumeviombea ambavyo havikuwamo awali. Kwa mfano, hata pale Mbezi, kuna tatizo la foleni pale ukiwa unakwenda Mbezi Beach kwa hiyo kazi hizo zitakamilika,” amesema Mativila.

Alhamisi Septemba 30, 2021, ndani ya gazeti la Mwananchi, tovuti na mitandao ya gazeti hilo, iliripotiwa kimakosa kuwa Mativila alisema kuwa ujenzi huo ulikwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Ukweli ni kwamba Tanroads iliomba fedha za nyongeza kukamilisha sehemu chache kwenye mradi huo, hasa maeneo ambayo awali hayakuingizwa kwenye mradi huo.

Source: Mwananchi
 
Back
Top Bottom