TANROADS: Pembetatu ya ufisadi hulinda maslahi yake! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TANROADS: Pembetatu ya ufisadi hulinda maslahi yake!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Halisi, Jun 17, 2010.

 1. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #1
  Jun 17, 2010
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Yamesemwa mengi kuhusiana na Tanroads lakini hili ndilo lina ukweli mkubwa na kwa kweli Tanroads na Mrema ni taswira ya tatizo kubwa zaidi katika nchi yetu. MUNGU ATUNUSURU.

  Pembetatu ya ufisadi hulinda maslahi yake!


  Lula wa Ndali-Mwananzela
  Juni 16, 2010

  KWA nini iliwachukua muda mrefu kuweza kumwajibisha yeyote kule Benki Kuu (BOT) licha ya tuhuma za vitendo vya kifisadi kudumu kwa muda mrefu? Kwa nini imewachukua muda mrefu kusafisha TANESCO na ATCL?

  Kwa nini imekuwa mbinde kufanya mabadiliko madhubuti hapo TANROADS na kwenye ofisi nyingine za serikali ambako tuhuma za uzembe, ukuwadi wa ufisadi na maamuzi mabovu zimekuwa zikitolewa siku hadi siku? Kwa nini, kwa mfano, pamoja na ‘madudu’ yote ambayo yamefanywa mbele ya Rais Kikwete kule Ikulu na wakati mwingine na vyombo vya usalama, hakuna mtu aliyewajibishwa zaidi ya kutafuta udhuru wa kufafanua nini kilichotokea? Jibu la maswali hayo siyo gumu kulipata.

  Hata hivyo, inategemea nani anayeulizwa. Tukiwauliza wao (watawala) ni kwa nini wanalea watendaji wabovu wenye kutia hasara taifa na taasisi wanazoziongoza, jibu lao linatoka kwenye kitabu chao cha utetezi wa ufisadi.

  Wanatuambia: “Hatuwezi kuchukua hatua bila kufuata taratibu za uajiri”, na tukiwabana sana wanatuambia; “tukimchukulia mtu hatua halafu akifungua kesi mahakamani tukishindwa serikali itapata hasara”!

  Na kama tukiamua kuwang’ang’ania, watatuambia, kwa kutufokea kama mbayuwayu; “nchi hii inafuata utawala wa sheria, tuhuma tu hazitoshi kumwajibisha mtu, vinginevyo tutawawajibisha wangapi?”.

  Kitu pekee ambacho hawatuambii ni kuwa wao ndio watunga taratibu za uajiri na ndio wao wenye uwezo (wakipenda) wa kutengeneza mazingira ambapo mtendaji mbovu hawezi kukaa zaidi ya siku moja kwenye kiti chake.

  Ukiangalia kwa karibu utaona kuwa kuna sababu kubwa zaidi ya kwa nini wamekuwa goigoi na wa mwendo wa kudemadema linapokuja suala la kuwajibishana. Wamekuwa wakitafuta visingizio vingi hadi tunaweza kujaza juzuu ya vitabu!

  Tatizo kubwa ambalo lipo ni kuwa kwa kadri ya kwamba watendaji wabovu wanaendelea kubebwa na kuvumiliwa, ndivyo hasara kwa taifa inavyozidi kuwa kubwa. Na ninapozungumzia “hasara” sizungumzii hasara ya fedha tu; bali hasara katika vipimo vyake vingine mbalimbali kama utamaduni wa uzembe kuendelea na tabia ya kuvumiliana kuendelezwa.

  Hili tumeliona kwa kiasi kikubwa kwenye asasi mbili kubwa ambazo nimezitaja hapo juu. Kwanza tumeona Benki Kuu ambapo mambo ambayo yamefanyika pale yangeweza kufanyika huko Uchina baadhi ya watendaji wake wangepangwa mstari mahali fulani na kuuawa kwa risasi!

  Na asasi nyingine ATCL ambako nako uongozi mbovu umelelewa na kuendekezwa kwa miaka nenda rudi; huku watu wakilalamika kuwa kinachohitajika ni “fedha zaidi” na watawala pasipo kufikiria wamemwaga mamilioni pale.

  Lakini, swali bado linabakia ni kwa nini watendaji wabovu wanavumiliwa kwa muda mrefu na kuendelea kulitia hasara taifa, kuendelea kulimbikiza manung’uniko na kuendelea kutawala kana kwamba bila ya wao shirika, idara au kampuni, haiendi?

  Baada ya kufikiri (kwa muda mfupi) nimepata jawabu ambalo nina uhakika wa asilimia 100 mtakubaliana nami. Ni jawabu ambalo linapuuzia maelezo ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara kuelezea kwa nini watendaji wabovu bado wapo licha ya kuonyesha kuwa ni wabovu.

  Watendaji wenye mwelekeo wa kifisadi na ambao wamekuwa wakitia hasara idara, makampuni, mashirika na hasa taifa, ni muhimu kwa wanasiasa.

  Wanasiasa walio katika madaraka serikalini ambao, kwa mujibu wa sheria, ndio huwateua baadhi ya watendaji wakuu wa idara, mashirika na makampuni mbalimbali ya umma wakizingatia mambo mengi ya kawaida lakini nyuma ya baadhi ya teuzi hizi ni maslahi yao wanasiasa, jamaa zao na washirika wao mbalimbali.

  Kinachotokea ni kama pembetatu ya ufisadi; yaani watendaji + wanasiasa + wafanyabiashara wasio wasafi. Mtandao wa ufisadi nchini unafanya kazi kwa kuzingatia vitu hivyo vitatu.

  Watendaji (hapa nazungumzia hasa wale wa ngazi za juu kabisa kama wakurugenzi) na wanasiasa (hapa nazungumzia wale walio katika madaraka serikalini kama mawaziri) na wafanyabiashara wachafu (hapa nazungumzia wafanyabiashara wamiliki wakubwa), ndio hufanya kazi kwa kushirikiana katika kuhakikisha maslahi ya kila mmoja yanalindwa.

  Tuone: Mwanasiasa anamteua mtu fulani kuwa mkurugenzi wa shirika au kampuni au idara fulani. Ili kuhakikisha kuwa mkurugenzi huyo anakubali nafasi hiyo na atakuwa tayari kutumiwa, basi, anasainishwa mkataba “mnono” ambao unamhakikishia mshahara mzuri, marupurupu kibao ikiwemo nyumba, watumishi, magari, nyumba ya wageni, posho ya kutembea, posho ya kusimama, posho ya kukaa – inaitwa ya vikao!

  Posho zote hizo zinamuweka katika hali ya kuwa mtumishi mzuri wa wanasiasa. Mtu huyo akiishaingia kwenye nafasi hiyo atasimama na kudai yote aliyopewa ni kwa sababu “anastahili”. Hasikii uchungu hata kidogo kusainishwa mkataba wa namna hiyo katika nchi maskini kama ya kwetu, tena atatetewa na waziri au mwasiasa aliyemteua.

  Na mkibisha sana atakimbilia kuwaonyesha “mkataba” – hata kama makubaliano yalikuwa mengine na mkataba mwingine!

  Mtendaji anapoanza kazi yake pale anapata taarifa mbalimbali za ndani za kampuni, idara au shirika. Katika utendaji kazi wake na kwa vile yeye ndiye “bosi”, basi, anaweza kuitisha taarifa fulani ambazo zinaweza kutumika katika kujua wapi kuna upenyo wa fedha, wapi kuna mahali pa kuweza “kuwekeza” na wapi kuna uwezekano wa kuingia “ushirikiano” na sekta binafsi.

  Akishajua kinachoendelea kwenye idara yake (wakati mwingine kwa kudokezwa na watendaji wengine walio katika mtandao), mtumishi wetu huyu anakuwa katika nafasi ya kuanzisha mradi au kuja na mpango fulani ambao anajua utahitaji fedha serikalini au utahitaji ushirikiano na sekta binafsi.

  Na wakati mwingine wazo la mradi au mpango huu linatolewa na sekta binafsi au na mwanasiasa, na yeye mtendaji kutakiwa kulitekeleza.

  Wafanyabiashara wachafu wanaoshinda katika shughuli mbalimbali na wanasiasa na watendaji hawa wakuu hubadilishana mawazo katika milo ya jioni au katika sehemu za kupata kinywaji na burudani. Katika “kubadilishana mawazo” huko ndipo taarifa nyeti za idara na mashirika hupitishwa na huambiana ni kitu gani kinahitajika.

  Chukulia kwa mfano suala la vocha za pembejeo. Ukisoma vitabuni ni mradi uliobuniwa vizuri sana. Tatizo lake ni kuwa walioubuni walijifanya hawajui uwepo wa pembetatu hii ya ufisadi. Matokeo yake wanasiasa, watendaji na wafanyabiashara kwenye maeneo kadhaa nchini wakala njama ya kutumia vocha hizo kujilipa wenyewe na kusababisha upotevu wa mabilioni ya shilingi. Ni mtindo huu huu umetumika kwenye EPA na kashfa nyingine kadhaa ambazo zimezoeleka kama kibwagizo cha “Mbagala”.

  Hii ina maana gani? Kwa kifupi ni kuwa hakuna ufisadi unaofanyika kwenye taasisi ya umma ambapo hakuna wanasiasa wanaonufaika nyuma yake au wafanyabiashara wachafu ambao hawataki kufanya biashara katika mazingira ya haki. Nikinyanyambua zaidi ni kuwa ufisadi nchini katika nafasi zake zote umefungamana na kushikamana na maslahi ya makundi hayo matatu.

  Hii ina maana gani? Maana yake ni kwamba Mtanzania anapopiga kura kumchagua mwanasiasa na kumuweka madarakani ni lazima ajue kuwa anachagua zaidi ya mtu mmoja au chama kimoja.

  Ni muhimu kujua kuwa unapomchagua mtu kuwa rais usidhanie atakuwa ni “rais tu”; bali atakuwa ni mbia katika shughuli mbalimbali ambazo nyingine (kama siyo nyingi) zitamnufaisha yeye, familia yake na washirika wake mbalimbali.

  Hii ni kweli sana; kwani tumeiona kwenye utawala wa Mzee Mwinyi, tukaona ikikolezwa kwenye utawala wa Mzee Mkapa, na sasa hivi tunaiona ikiwa imepangwa kama “formation” ya kabumbu katika utawala huu wa sasa wa awamu ya nne wa Dokta Kikwete! Wote wanafuata kitabu kile kile.

  Bila shaka unajiuliza kwa nini nimeandika kifalsafa kidogo. Nimefanya hivi ili kuweza kuelewa kinachoendelea kwenye Wakala wa Ujenzi nchini; yaani TANROADS.

  Makala yangu ya wiki iliyopita imenifanya nipokee barua pepe kadhaa ambazo kuna watu waliona kuwa nimeandika kama namuonea mtu, nimetumwa au nimeombwa kuandika ili kumchafua mtu.

  Na wengine hawakutaka hata kujibu hoja zinazoibuliwa juu ya kile kinachoendelea. Na wengine wamenipatia data zaidi ambazo hakuna chombo chochote kingine cha habari kinazo. Data ambazo zinaonesha ni kwanini Mrema bado yupo hapo!

  Kutokana na hilo nikaamua kujitolea tu kusema kile ambacho naamini kinajulikana. Mrema ni mtendaji katika TANROADS mwenye madaraka makubwa tu. Nyuma yake ni lazima wapo wafanyabiashara na wanasiasa ambao wananufaika kwa namna moja au nyingine na yeye kuendelea kuwepo pale.

  Kwa vile kwa miaka kadhaa sasa inaonekana imekuwa vigumu kufanya mabadiliko yanayohitajika au yanayolazimika ili kuhakikisha mtendaji wa chombo cha serikali hatakiwi kuzungukwa na wingu la tuhuma, ni wazi kabisa mtu anayenufaika na uwepo wa Mrema pale hawezi kuwa mtu mdogo!

  Nilidokeza wiki iliyopita kuwa tatizo si Mrema wa TANROADS; kwani yeye ni dalili tu ya tatizo. Nikasema tatizo litakuwa liko Ikulu. Swali ambalo tuna budi kubakia nalo ni je, mtu mwenye kunufaika na Mrema TANROADS yuko Ikulu? Kama ndiyo ni nani? Mimi najua jawabu. Wewe je?


  Barua-pepe: lulawanzela@yahoo.co.uk

  SOURCE: Pembetatu ya ufisadi hulinda maslahi yake!
   
 2. D

  DoubleOSeven JF-Expert Member

  #2
  Jun 17, 2010
  Joined: Jul 5, 2008
  Messages: 661
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  ...Kutokana na hilo nikaamua kujitolea tu kusema kile ambacho naamini kinajulikana. Mrema ni mtendaji katika TANROADS mwenye madaraka makubwa tu. Nyuma yake ni lazima wapo wafanyabiashara na wanasiasa ambao wananufaika kwa namna moja au nyingine na yeye kuendelea kuwepo pale.....

  ROADS! ROADS! Zisizojengwa, zinazojengwa chini ya viwango at inflated costs...Pesa ya ROAD FUND!!! Nyingi sana hii!! Contracts anazopewa COWI na jamaa wengine... PESA ! PESA! Tazama kundi lile utawaona tu. Inno upo?
   
Loading...