TANROADS: Kama JK hataki kuamka kwanini kumwamsha? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TANROADS: Kama JK hataki kuamka kwanini kumwamsha?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mzee Mwanakijiji, Jul 16, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jul 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Lula wa Ndali Mwananzela - Raia Mwema (Jumatano Julai 14, 2010)

  KUNA wakati mwingine ni lazima tuuite ukweli kwa jina lake. Kama mtu hataki kuamka wakati unamwambia nyumba inawaka moto utafanya nini? Kama unaweza kumbeba, basi, inabidi umbebe mzibemzibe na kuyaokoa maisha yake. Lakini itakuwa vipi kama anakuambia hataki kuamka kwa sababu kanogewa na usingizi?  Kama ni mtoto mdogo unamtia viboko viwili tu kumkurupusha au kumwagia maji azinduke, lakini kama ni mtu mzima njia pekee ni kumshawishi tu; maana hata ukimwagia maji anaweza kukugeukia na kukutwanga mangumi huku wote mko hatarini kuangamia.
  Vipi kama unawaambia watu kuwa kuna vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na watu hao wanakuona kama unapandikiza “chuki binafsi” na kuwa unafanya hivyo kwa sababu ya “wivu” au “umetumwa”? Njia pekee ni kuwaacha watawalane wenyewe kwa wenyewe.


  Bado sijaelewa kwanini najikuta naandika tena kuhusu suala la ajira ya Mkurugenzi wa TANROADS Bw. Ephraim Mrema. Sikutaka kulirudia jambo hili tena kwa sababu kurudia jambo lile lile, kwa watu wale wale likiwa na ujumbe ule ule na kutarajia matokeo tofauti, ni wazimu! Na sipendi kuwa na wazimu.
  Hata hivyo, kuna wakati inabidi kurudia tena kumwamsha mtawala ili hatimaye iwepo rekodi kuwa alijaribiwa kuamshwa hata kama hataki.
  Kinachoniudhi na kunikera mimi kwenye suala hili la TANROADS ni kufanana kusiko na utata wa jinsi gani Serikali ya CCM, chini ya Rais Kikwete, imekuwa ikishughulikia tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi au utendaji mbovu katika taasisi za umma.
  Mara zote tulipojaribu kuwaamsha kwa kutumia taarifa mbalimbali ambazo, kama vyombo vya habari na wachunguzi tuliweza kuzipata, mwitikio wao umekuwa wa kulegalega, uliojaa kusitasita na ukosefu wa uharaka wa kurejesha heshima na nidhamu katika maeneo hayo.  “Mhe. Rais, kuna tatizo katika akaunti ya EPA, Benki Kuu” - “Ni tuhuma zisizo na msingi”
  “Mhe. Rais, Gav. Ballali anahusika na ufisadi huo” - “Serikali ina imani na utendaji wa Gavana”. “Mhe. Rais, mabilioni yamechotwa na makampuni feki” - “Serikali iko mbioni kuanza mchakato”. “Mhe, Rais, mkataba wa Buzwagi umeingiwa visivyo” - “Serikali inaamini kabisa..”
  “Mhe, Rais, Richmond ni kampuni ya kitapeli” - “Serikali itafanya kila jitihada.”
  “Mhe, Rais, Dowans ni mtoto wa Richmond” - “Serikali itaanza mchakato mpya.”
  “Mhe, Rais, kuna tatizo ATCL ” - “Serikali itajihidi kwa uwezo wake wote..”
  “Mhe, Rais, ATCL wamenunua dege bovu” - “Serikali imepanga kuanza safari za moja kwa moja”. “Mhe, Rais, kampuni ya Meremeta ni ya kitapeli” - “Serikali imesema ni usalama wa taifa.”
  “Mhe, Rais, Chenge ameficha mabilioni UK” - “Chama cha Mapinduzi kina uongozi safi”.
  “Mhe, Rais, waziri wako katapeli, mng'oe” - “Tuna mpango wa kuongeza idadi ya wanawake”. “Mhe, Rais TANROADS kuna matatizo” - “Serikali inaamini kabisa.”
  “Mhe, Rais, mkataba wa Mrema haukuwa sahihi” - “Serikali yetu inazingatia utawala bora.”

  Sasa, kati ya sisi na wao nadhani tofauti ni mbingu na dunia. Haiwezekani turudie mambo yale yale kwa watu wale wale huku tukijua watatupa jawabu lile lile la kutupuuzia. Sielewi kwanini vyombo vya habari vimeshupalia suala hili la TANROADS wakati watawala hawaoni uzito wowote kwa miaka karibu mitatu sasa!


  Labda hakuna ubaya kukumbushia tu kwanini narudia kwa mara hii ya mwisho suala hili; kwani sitaki nionekane nina wazimu.


  Gazeti la Serikali la Habari Leo la Ijumaa ya tarehe 4 Julai 2008 liliandika kwa kirefu madai yaliyotolewa na Bw. Mporogomyi, mbunge wa Kasulu Magharibi kuhusu suala la mafao mbalimbali ambayo Mkurugenzi wa TANROADS, Bw. Mrema alikuwa anayapata. Gazeti hilo likimnukuu Bw. Mporogomyi lilielezea kuwa Mkurugenzi huyo wakati akianza ajira yake “alipewa posho ya kuanza (commencement allowance) dola za Marekani 9,000 kwa siku 60 (sawa na Sh milioni 10.8), mshahara wake kwa mwezi ni dola za Marekani 8,500 (Sh milioni 10.2), posho ya nyumba kwa mwezi ni dola 2,200 (Sh milioni 2.6), posho ya matibabu dola 400 kwa mwezi (Sh 480,000), posho ya usafiri dola 500 (Sh 600,000).
  Pia analipwa pensheni kwa mwaka kiasi cha dola za Marekani 10,200 (Sh milioni 12.4), akienda likizo analipwa dola 3,000 (Sh milioni 3.6), bonasi yake kwa mwaka analipwa dola 102,000 (Sh milioni 122.4) na mwisho wa mkataba wake analipwa dola 10,000 (Sh milioni 12) kama malipo ya kumaliza kazi.”


  Kiasi anacholipwa kwa mwezi kwa mahesabu hayo kinakaribia dola 25,000! kwa mwezi! Hapo bila hayo malipo mengine yanayotolewa kwa mwaka!


  Hapa ndipo wengine tulipoona utaratibu wao (CCM na Serikali) yake ulivyo wenye kuchochea ufisadi. Kwenye taifa la kimaskini kama la kwetu tunaweza vipi kumlipa mtu kiasi hiki wakati walalahoi tunawanyima hata nyongeza yenye maana?
  Lakini hilo la Mrema la malipo ni tatizo moja tu na kwa hakika si la kwake peke yake; kwani tunakumbuka lilivyokuja kujirudia kwenye ujenzi wa majumba ya Benki Kuu na malipo ya watu wengine kwenye utumishi wa umma. Nitaliacha hilo kwa leo.
  Lakini habari za awali kabisa mwaka 2008 zilivujishwa na kutuelezea jinsi gani Bw. Mrema alipata nafasi hiyo. Tulidokezwa na vyanzo vya kuaminika kuwa baada ya watu waliotafutwa kushika nafasi na kampuni iliyoajiriwa kufanya kazi hiyo (short listing firm) majina hayo yalipelekwa kwa wakubwa ili mojawapo liteuliwe kushika nafasi hiyo. Hata hivyo, majina yale yote yalikataliwa.  Baadaye kwa utaratibu mwingine ndipo Bw. Mrema akaingizwa kuomba nafasi hiyo na akaipata. Jinsi gani aliingia na kupata nafasi hiyo limebaki kuwa sehemu ya gumzo la kukisia lakini madai ya mahusiano ya karibu na baadhi ya viongozi fulani fulani yamedumu kwa muda mrefu sasa. Hadi hivi sasa haijachunguzwa kama alipewa upendeleo wa aina yoyote katika kupata kazi hiyo au la.


  Lakini huo ulikuwa ni mwanzo tu wa tatizo. Huko huko TANROADS chini ya Bw. Mrema zikagawiwa fedha za “asante” (shilingi milioni 40) kwa watumishi mbalimbali kwa kile kilichodaiwa kuwashukuru kwa kufanikisha kupitisha nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa TANROADS.  Sijafahamu binafsi watendaji wa umma wanaojilipa fedha kwa kuongeza mishahara ya watu wengine! Lakini ndivyo ilivyokuwa huko TANROADS na hadi sasa hakuna mtu kwenye Serikali ya Kikwete ambaye anaona hilo ni tatizo au ni ishara ya uwezekano wa tatizo kubwa zaidi kama mtindo huu huu utatumika kwenye taasisi nyingine za umma.
  Fikiria uwezekano wa kuwa ili mishahara ya wafanyakazi wengine iongezwe, ahadi inatolewa kuwa wakifanikiwa ikapitishwa basi na wenyewe wahusika watapata honoreri!
  Waliojigawia fedha hizo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Miundo Mbinu (ambaye ni mtendaji mkuu wa wizara na ambaye hajarudisha fedha hizo) na maofisa wengine kadhaa. Lakini kwa sisi tunaofuatia hili si geni kwani tumeliona likitokea ATCL ambapo wakurugenzi na watumishi kadhaa walijigawia fedha za kununulia magari mbalimbali kwa bei ya juu na hadi hivi sasa hakuna aliyewajibishwa kwa hilo hata kidogo; japo walifanya hivyo wakati ATCL inalalamika kuwa haina fedha! Na sisi bado tunajaribu kumwamsha mwenye nyumba.
  Lakini mojawapo ya mambo ambayo yamekuwa yakidaiwa ni pamoja na mtindo wa kutimua baadhi ya wakandarasi na kuwaingiza wengine kwa bei ya juu zaidi. Mfano mmoja ambao ulidokezwa wakati huo ni mradi wa barabara ya Kagoma-Lusahunga huko Kagera ambapo mkandarasi wa awali alikuwa anajenga barabara hiyo kilometa 150 kwa Shilingi bilioni 48 lakini Mrema akamtimua na kumpa mkandarasi mwingine ambaye alikuwa aijenge kwa bilioni 190.


  Mfano mwingine ni ile kesi ambayo TANROADS ilipoteza baada ya kushtakiwa katika sakata la kampuni ya Prismo-Badr, J. V ya Italia ambayo Mrema alifuta mkataba wake na kukamata vitu vyake. Suala hilo lilipelekwa kwa msuluhishi na kuonekana kuwa TANROADS ilifanya makosa kwa kuvunja mkataba huo wa Shilingi bilioni 23 na kuamriwa kuilipa kampuni hiyo bilioni 22 huku wakati huo huo TANROADS ikiingia mkataba mwingine wa bilioni 25 na kampuni nyingine kuhusu ujenzi wa barabara ile ile.  Hilo lilisababisha Mwanasheria Mkuu kuingilia kati baada ya TANROADS, chini ya Mrema, kutokata rufaa ya uamuzi huo na kutakiwa kuitii hukumu hiyo baada ya kuandikiwa na kampuni ya uwakili ya Mkono.  Katika barua ya Mwanasheria Mkuu kwenda Wizara ya Miundo Mbinu alijikuta anawashauri Wizara kufanya mazungumzo na kampuni ya Prismo nje ya mahakama; kwani madai hayo ni makubwa mno kulipwa na serikali. Lakini Mrema bado ameendelea kukingiwa kifua!
  Lakini ipo na mifano mingine kwa mfano ule wa kuvunjwa kwa mkataba wa Konoike na kupewa kampuni nyingine ambayo inadaiwa kulipwa zaidi ya bilioni 16 zaidi wakati kazi kubwa ya ujenzi ilikwishafanywa na kampuni ya Konoike. Nani anawalinda hawa kama siyo watawala wenyewe?  Kuna madai mengine mbalimbali ambayo yanafanana na yale ambayo serikali tayari imeshindwa na endapo yatafikia mahakamani kwa mtindo huo huo, serikali italipa karibu zaidi ya Shilingi bilioni 250! Hizo ni zaidi ya wizi wa akaundi ya EPA! Lakini hili hawalioni, hawataki kuliona na hawataki kulisikia.


  Lakini jambo ambalo hadi leo limeacha mwangwi huko TANROADS ni kitendo cha kibabe cha Mrema cha kuwatimua watu kwa utaratibu ambao haukubaliki katika utumishi wa umma. Bw. Mrema alitangaza kuwatimua Oktoba mwaka jana watendaji mbalimbali wa TANROADS wakiwemo Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara, Thomas Mosso, Mkurugenzi wa Mipango, Jason Rwiza na mameneja wa mikoa mitatu ya Dodoma, Gerson Lwenge; Morogoro, Charles Madinda na wa Ruvuma, Abraham Kissimbo. Vile vile alikuwepo mhandisi William Shilla.  Watumishi hao walikata rufaa wizarani na Wizara ikatengua maamuzi ya Mrema. Hiyo peke yake kwenye nchi nyingine ilitakiwa iwe sababu tosha ya kumtimua Mrema. Mrema kwa muda inadaiwa akaheshimu maamuzi hayo kwa kuwaandikia watumishi hao akiwataarifu kuwa “Napenda kuwajulisheni kwamba nimepata agizo la Serikali kwamba uteuzi wa wakurugenzi na viongozi wengine wa TANROADS umesitishwa”. Hiyo ilikuwa ni Novemba 6. Tukumbuke kuwa uamuzi wake wa kuwatimua kazi ulichukuliwa Oktoba 30.  Furaha ya hao watumishi haikudumu kwani siku tatu baadaye (Novemba 9) Mtendaji Mkuu wa TANROADS mwenye kulipwa mabilioni na serikali ya CCM, chini ya Kikwete, akaamua kugeuka tena. Akawaandikia na kudai “Nasikitika kuwajulisheni kwamba taarifa ya kusitisha utekelezaji wa waraka wa terehe 30 Oktoba 2009 ilitumwa kwenu kimakosa kabla ya kupata kibali cha mtendaji mkuu kwa hiyo waraka huu unafuta waraka wa kusitisha utekelezaji wa waraka wa Mtendaji Mkuu wa Novemba 6 na unawajulisha kwamba uteuzi wa uongozi uliotajwa Oktoba 30 umeanza kazi rasmi Novemba 1, 2009 na umepelekwa katika ngazi husika kupata baraka za mwisho.”


  Katika nchi zenye utawala bora huu ugeugeu ungekuwa ni sababu tosha ya kumuondoa mtu madarakani; kwani ni kuchezea madaraka, kusababisha mashaka kwa watendaji na kukosa umakini. Lakini chini ya watawala wetu, hili ni 'bahati mbaya' tu; ni tatizo la ‘kupitiwa’.
  Lakini haya yote siyo ya kubuni au kusingiziwa kwani Ofisi ya Waziri Mkuu mapema mwaka huu iliandikia barua ofisi ya Miundo Mbinu kuelezea kile ambacho kinaonekana tatizo la uongozi TANROADS. Barua hiyo ilikuwa inataka kupata maelezo kuhusiana na TANROADS kwani “Ni dhahiri kwamba kama hali ya utendaji kazi ndani ya Wakala wa Barabara kama ilivyoelezwa na uongozi wa Chama Cha Wafanyakazi haitarekebishwa, Taifa linaweza kupata hasara kubwa ikizingatiwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimetengwa kwa ajili ya shughuli za wakala huo”


  Sasa, naweza kuendelea na kwenda kuzama zaidi katika hili na kurudia ambayo tayari yameandikwa na kusemwa vya kutosha. Naweza na mimi kama niliyeshika Vuvuzela langu kuendelea kupaza sauti kwa nguvu nikiamini kuwa goli laweza kufungwa! Lakini yote ni bure. Watawala hawawezi kuamka.  Ni lazima kuna sababu. Ipo sababu kwanini Mrema hang'oki na hawezi kung'oka kabla ya Uchaguzi Mkuu. Na kama atang'oka ataondolewa kwa heshima zaidi na si kwa kashfa.
  Mrema alipelekwa pale kwa sababu, hadi hivi sasa sababu yake inaonekana ameitimiza kwa kiwango cha juu kabisa na sasa anasimama kama shujaa wa CCM na Serikali yake.
  Natamani Chadema na uongozi wake wangetuahidi kuwa wakiingia madarakani watawachunguza wote hawa na kuwakifisha mahakamani na kuahidi kufilisi mali zao zote ili liwe fundisho kutochezea fedha za umma au madaraka ya umma.
  Lakini na hili nalo liwe rekodi kwao kuwa siligusi tena suala hili la TANROADS; kwani wahenga waliasa vyema kabisa, “ukimwasha aliyelala...”


  Labda na sisi wananchi tuanzishe kikao cha “Kamati yetu Kuu” maana kwa mtindo huu bila Mkutano Mkuu hatutafika. Mkutano wa kuwang'oa watawala waoga, na wenye kulea ufisadi.
   
 2. C

  Chief JF-Expert Member

  #2
  Jul 16, 2010
  Joined: Jun 5, 2006
  Messages: 1,490
  Likes Received: 194
  Trophy Points: 160
  Hakutakuwa na mabadiliko mema nchi hii bila kuwa na China solution. Hii nchi imeoza kupitiliza.
   
 3. Shapu

  Shapu JF-Expert Member

  #3
  Jul 16, 2010
  Joined: Jan 17, 2008
  Messages: 1,922
  Likes Received: 245
  Trophy Points: 160
  Hii habari ukiisoma kabla hujaingia kwenye mkutano muhimu, unaweza jikuta unaharibu mkutano kwani mood yako itakuwa imeharibika sana.

  Hii nchi bwana.......
   
 4. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #4
  Jul 16, 2010
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Tatizo ni katiba, institutions problems na hata sera na taratibu zote ndio zinalisha mambo ya ajabu kama haya tanzania
   
 5. Utingo

  Utingo JF-Expert Member

  #5
  Jul 16, 2010
  Joined: Dec 15, 2009
  Messages: 7,121
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 160
  Hii hapa chini imenichefua hata habari yenyewe nimeshindwa kuisoma yote, mood yangu imeharibika kabisa.

   
Loading...