TANGA: Watu watano wafariki kwenye ajali ya Scania na Semi trela

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Watu watano wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 21, 2020, mara baada ya malori mawili kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Kitumbi mkoani Tanga, huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uzembe wa kutokuzingatia sheria za usalama barabarani.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, hii leo Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga ACP Blasius Chatanda, amesema kuwa malori hayo moja lilikuwa likitokea jijini Dar es Salaam likiwa na vifaa vya dukani likielekea mkoani Tanga, na lingine lilikuwa limebeba saruji kuelekea mkoani Dodoma.

"Gari mbili zimewaka moto ni wazi kwamba magari yote haya mawili yalikuwa kwenye mwendokasi, kwa mujibu wa mashuhuda gari moja ilihama kutoka upande wake na ku-overtake gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kugongana, hiyo miili ilivyo ni ngumu hata kufanya utambuzi kwa sababu wameungua vibaya na miili yote imehifadhiwa kwenye kituo cha afya Mkata", amesema ACP Chatanda.

Aidha ACP Chatanda, akatoa rai kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, kwa sababu huo ni mwarobaini wa ajali zote za barabarani.
 
Madreva wengine wanaendesha huku wamelewa ama pombe au bangi. Kuna kipindi traffic walikuwa wanapima kiwango cha ulevi!
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilitokea juzi majira ya saa 5:00 usiku na kuhusisha gari lenye namba za usajili T988 na tela lenye namba T 757 CGC aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na Seleman Muya (32), mkazi wa Tanga.

Alisema gari hilo lilikuwa limepakia saruji kutoka Tanga kwenda Dodoma likiwa na abiria wawili ambao ni Bakari Tendwa mkazi wa Tanga na abiria mwingine ambaye hajafahamika majina yake.

Alisema gari lenye namba za usajili T 895 DMD aina ya Canter lililokuwa linaendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Rashid, akitokea Dar es Salaam kwenda Tanga akiwa na utingo wawili ambao wote wamefariki dunia.

Kamanda Chatanda alisema utingo hao waliofahamika kwa jina moja moja la Mujibu (28) na Dominic (20) wote ni wakazi wa Lushoto.

"Baada ya magari kugongana yote mawili yaliwaka na kuteketea kwa moto na kusababisha vifo vya dereva na utingo wote waliokuwa kwenye canter pia kusababisha vifo kwa dereva wa semi na abiria mmoja ambaye hajafahamika. Majeruhi Bakari Tendwa ambaye ameungua moto kidogo maeneo ya kichwani na kuvunjika mguu wa kushoto,” alisema.

Kamanda Chatanda alisema majeruhi amelazwa Kituo cha Afya Mkata, huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi wa daktari.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Canter kutaka kulipita gari lingine, wakati eneo hilo halifai kwa kupishana, hivyo kugongana na lori.


©IppMedia
 
Back
Top Bottom