SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limewasilisha katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) maombi ya kushusha bei ya umeme kwa asilimia 1.1 pamoja na kuondoa kabisa gharama za maombi ya awali ya wateja wapya na gharama za huduma kwa wateja wa majumbani.
Gharama za maombi hayo ya awali ambayo pia yanajulikana kama gharama za fomu ni Sh 5,900 na gharama za huduma (service charges) ni Sh 5,520 kwa mwezi kwa wateja wa majumbani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanseco,* Felichesmi Mramba alisema kuwa kisheria maombi hayo yanatakiwa kujibiwa ndani ya siku 24 ambapo wanaamini kuwa watapata majibu mazuri.
Mramba alisema gharama za huduma zimekuwa zikiathiri sana watumiaji wa umeme wa majumbani tofauti na wanaotumia viwandani.
Mramba alisema kuwa maombi hayo yamewasilishwa baada ya Tanesco kufanya tathimini ya kina kimahesabu pamoja na kubuni namna ambayo wateja wao wataweza kupata ahueni ya gharama kwa kuzingatia mazingira ya sasa.
Alisema punguzo hilo la asilimia 1.1 ni kwa mwaka wa kwanza na matarajio ni kwamba mwaka wa pili, watapunguza kwa asilimia 7.9.
“Baadhi ya vyombo vya habari viitunukuu vibaya,hatuna mpango wa kupandisha bei ya umeme na wala serikali haijatulazimisha kushusha bei. Tunawahakikishia wananchi kuwa maombi yaliyotumwa Ewura ni kuondoa usumbufu wanaoupata watumiaji wa umeme wa majumbani,’’ alisema Mramba.
Alisema kwa mujibu wa sheria, Tanesco inapotaka kubadilisha bei, iwe ni kushusha au kupandisha ni lazima iwasilishe maombi hayo Ewura kwani ndiyo yenye mamlaka ya kisheria ya kubadilisha bei hizo.
Alifafanua kuwa Tanseco huwasilisha maombi yake pamoja na takwimu halisi zinazoshawishi mantiki ya kubadilishwa kwa bei hizo na kwamba maombi yaliyowasilishwa Ewura hivi sasa, ndio ilivyotakiwa.
Aliongeza kuwa baadhi ya mambo yanayoendana na mazingira ya sasa, ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa gesi, tofauti na ilivyokuwa hapo kabla. Pia alisema kuongezeka kwa ujazo wa maji katika mabwawa makubwa hasa Mtera, kunachangia Tanesco kushusha bei hizo.
Akizungumzia madeni ya Tanesco, Mramba alisema kuwa kiasi cha madeni yaliyotajwa na vyombo vya habari sio sahihi.
Alifafanua kwamba madeni hayo yamezingatiwa kikamilifu katika mapendekezo ya kushusha bei hivyo na si kweli kwamba kushuka kwa bei kutasababisha Tanesco kufilisika.
“Sio sahihi kusema kwamba serikali imeilazimisha Tanesco kushusha bei ya umeme na kwamba kwa kufanya hivyo shirika litafilisika. Tathimini tulioifanya ni ya kitaalamu na pia kwa mujibu wa sheria ya Ewura itafanya tathimini yake kabla ya kuidhinisha bei mpya,’’ alifafanua.