Tanesco wanaendesha mitambo ya IPTL kwa tsh bilioni 15 kwa siku

Mabilioni ya IPTL yanyemelewa BoT

Mwandishi Wetu
Raia Mwema
Mei 18, 2011
bul2.gif
Wizara yajikanganya matumizi ya mafuta

VITENDO vya ufisadi katika ununuzi wa mafuta ya mitambo ya kufua umeme wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ni mwanzo tu wa mpango unaolenga kuchota fedha za IPTL zilizoko kwenye akaunti maalumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambazo zimefikia Sh. bilioni 215.

Fedha hizo Sh 215,224,967,877.12 zimekuwa zikinyemelewa na wanasiasa na wakubwa serikalini kwa zaidi ya miaka miwili sasa wakati zikisubiri uamuzi wa kisheria wa mashauri yanayoendelea kuhusu IPTL na washirika wake.
Miaka miwili iliyopita, Mei 2009, fedha hizo zikiwa zimefikia Sh bilioni 137 (137, 769, 763, 052.84) Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, alikataa kuidhinisha uhamishwaji wa fedha hizo kutoka udhibiti wa benki hiyo kwenda IPTL, akiungwa mkono na Bunge.

Fedha hizo ambazo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo maalumu ndani ya BoT, zinatokana na malipo yaliyokuwa yalipwe kwa kampuni ya IPTL kutokana na kuliuzia umeme Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kabla ya kubainika kuwapo udanganyifu uliofanywa na kampuni hiyo tata kuhusiana na gharama halisi za uwekezaji.

Mpango huo umekuwapo kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni fedha hizo ‘kuzubaa' BoT baada ya mali za IPTL kuwekwa chini ya mfilisi, ambaye ni Wakala wa Usajili, Vizazi na Vifo (RITA) bila kujumuisha fedha hizo.

Baada ya kukwama kwa juhudi za kuhamisha fedha hizo mwaka 2009, wanasiasa na watendaji kadhaa wamekuwa wakihaha kutafuta njia za kuchota fedha hizo ikiwa ni pamoja na kuvuruga uongozi wa RITA na wote ambao wameonekana kuwa kikwazo kwa uchotaji huo.

Wakati kukiwa na mkakati wa kuhamisha fedha hizo kumekuwapo Azimio la Bunge linalotaka mgogoro wa IPTL kumalizwa haraka nje ya Mahakama ili fedha hizo zitumike katika kumaliza madeni ya TANESCO na kuichukua mitambo ya IPTL ili ibadilishwe na kutumia gesi na hivyo kupunguza makali ya bei na uhaba wa umeme nchini.

Mmoja wa watu waliowahi kupinga moja kwa moja kuchotwa kwa fedha hizo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, ambaye kamati yake ndiyo iliyowasilisha mapendekezo yaliyotoa azimio hilo, ambaye amewahi kusema "uamuzi wowote utakaofikiwa kuhusiana na IPTL unapaswa kuzingatia azimio la Bunge."

Akizungumza na Raia Mwema jana Jumanne, Zitto amesema hadi sasa azimio la Bunge linazuia kutolewa kwa fedha hizo na ameipongeza BoT na vyombo vingine kwa kuzingatia maslahi na hivyo kuzuia kutolewa kwa fedha hizo. Zitto amesema uamuzi wowote wa kutoa fedha hizo itakuwa ni kuingilia uhuru wa Bunge.

Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) azimio ambalo linahusu IPTL lilitolewa Aprili 29, 2000 likiwa na maelezo ya kuitaka Serikali na wadau wengine wa suala hilo kuzingatia zaidi maslahi ya Taifa katika maamuzi yao.

Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikijikanganya kwa kutoa taarifa kuhusiana na ununuzi wa mafuta ikidai kwamba zilizotumika katika ununuzi wa mafuta ni Sh bilioni 28 na si bilioni 46 alizosema Waziri wa wizara hiyo, William Ngeleja, alipokuwa akijibu maswali bungeni.

Katika taarifa yake, wizara kupitia msemaji wake, Aloyce Tesha, ilieleza kwamba malipo yaliyofanyika kati ya Novemba 15, 2010 hadi Aprili 13 2011 ni Sh. bilioni 28.5, huku taarifa hiyo ikishindwa kufafanua sababu za Ngeleja kuzungumzia bilioni 46 Aprili 6, mwaka huu akiwa anarejea matumizi ya mafuta hadi Februari 14 mwaka huu, miezi miwili baada ya mafuta hayo kutumika na wahusika kulipwa.

Mwezi uliopita akiwa kiongozi wa juu kabisa wa Wizara ambaye ana mamlaka ya kupata takwimu zote za wakati huo huo kutoka IPTL na wizarani kwake, Ngeleja alisema; "Kiasi cha shilingi bilioni 46.4 au wastani wa shilingi bilioni 15.6 kwa kila mwezi zilihitajika kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa tani 36,800 za mafuta mazito kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia 15 Novemba, 2010 hadi 14 Februari, 2011 sawa na tani 400 kwa siku.

Ofisa mmoja wa Wizara ya Nishati na Madini, aliliambia Raia Mwema jana Jumanne kwamba tamko la wizara limezidi kuibua maswali mengi zaidi kuliko majibu kutokana na Waziri kuzungumza bungeni akitaja takwimu za juu (46bn/-) katika kipindi ambacho wahusika walikwisha kulipwa fedha hizo, na baadaye wizara kutoa takwimu za chini (28.5b/-).

"Waziri wetu hapo ameukwaa mkenge na sasa anajaribu kufunika. Bora wangetulia kwanza hata kama wamefundishwa na Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi kwa mambo yanayowahusu," anasema ofisa huyo wa Wizara, ambaye yuko karibu sana na masuala ya umeme na mafuta.

Akiwa bungeni Ngeleja alishindwa pia kujibu swali la nyongeza la Zitto kuhusiana na zinakotoka fedha za kununua mafuta na badala yake alimtaka wazungumze baada ya kikao akisema;
"Nimuombe Zitto Kabwe kama anavyofahamu vizuri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge suala hili ni la takwimu tunayo ofisi inayosimamia mambo yote ya Fedha, chini ya Wizara ya Fedha mimi na yeye tukutane baada ya kikao hiki ili tupeane taarifa kupitia Wizara ya Fedha."

Katika swali lake Zitto alihoji akianza kwa kusema; "Ni dhahiri kwamba shilingi bilioni 15 kwa mwezi ni fedha nyingi sana. Wakati tunapitisha bajeti ya Serikali mwaka 2010/2011 hapakuwa na provision yoyote ya bajeti kwa ajili ya mafuta kwa mitambo hii. Waziri alithibitishie Bunge ni katika vote gani na kama ni ya Wizara yake au Wizara nyingine yoyote ambayo tunapata fedha (mabilioni) haya kwa ajili ya kulipia mafuta haya?""Kumekuwa na malalamiko na maombi na hoja mbalimbali za kutaka mitambo hii igeuzwe kuwa gas na imilikiwe na Serikali. Lakini mpaka sasa hakuna lolote ambalo limefanyika. Waziri haoni kwamba kuendelea mitambo hii kutumia mafuta kama hivi na bila utaratibu ambao labda mitambo hii imilikiwa na Serikali ni kuwa ni mradi wa watu wachache ambao wanafaidika na mafuta haya?"

Kwa mujibu wa takwimu hizo ambazo Raia Mwema ilizochapisha wiki iliyopita, kwa Novemba mafuta yaliyotumika IPTL ni meta za ujazo 3,670.09 ambazo ni sawa na lita za ujazo 3,670,090 ambazo kwa mauzo ya fedha za kigeni wakati huo yanaweza kufikia gharama ya shilingi 3,934,336,480 (Tsh. bilioni 3.9).Takwimu zinaonyesha pia kwamba kutokana na mgao kuwa mkali sana Desemba mwaka jana, IPTL ilizalisha zaidi umeme na hivyo kutumia mafuta mengi zaidi yaliyofikia meta za ujazo 8,146.80 sawa na lita 8,146,800 zenye gharama ya shilingi 8,733,369,600 (sh. bilioni 8.7).

Matumizi ya Januari 2011 hayakuwa makubwa sana na takwimu zinaonyesha kwamba mafuta yaliyotumika IPTL yalikuwa ya meta za ujazo 2,021.43 sawa na lita 2,021,430 ambazo gharama yake iliyoko katika nyaraka ni karibu shilingi 2,166,972,960 (Sh.bilioni 2.1).

Huku mgao ukiendelea kupungua na sababu nyingine, ikiwamo ya Meneja mgeni Magesvaran Subramaniam kuzima mitambo katikati ya mgao ili kushinikiza apewe mkataba mpya baada ya mkataba wake wa awali kwisha (alikwishakuandika notisi ya miezi mitatu ya kuacha kazi) uzalishaji mwezi Februari ulishuka, IPTL ikiwa imetumia mafuta ya meta za ujazo 1,876.94 ambayo ni sawa na lita 1,876,940 kwa gharama ya shilingi karibu 2,012,079,680 (Sh.bilioni 2.0).

Kwa Machi, IPTL ilitumia mafuta ya meta za ujazo 4,368.08 ambazo ni sawa na lita 4,368,000 zenye gharama ya shilingi 4,642,496,000 (Sh.bilioni 4.6) wakati kwa Aprili, mafuta yaliyotumika IPTL ni meta za ujazo 2,818.20 ambazo ni sawa na lita 2,818,200 zenye gharama ya shilingi 3,021,110,400 (Sh.bilioni 3.0).

Ukiongeza gharama hizo za Machi na Aprili katika jumla ya miezi mitatu ya mwanzo hesabu ya miezi yote inafika shilingi bilioni 24,510,365,120 ambayo dhahiri ni pungufu chini ya nusu kwa hesabu aliyotoa Waziri Ngeleja katika Bunge.

Habari zinaeleza hata kuwapo wa Magesvaran Subramaniam, ambaye sasa ni Kaimu Meneja Mkuu wa IPTL ambaye amekuwa mwakilishi wa Standard Chartered Bank ya Hong Kong iliyoishitaki Serikali ya Tanzania una usiri na uhalifu kwa kuwa kibali chake cha kuishi nchini, cha daraja la B, kiliisha tangu Februari 19, 2011 lakini amekuwa akiendelea kuwapo kwa nguvu ya wakubwa wanaonufaika na kuwapo kwake.

Taarifa zinasema hata mkataba wake wa kufanya kazi IPTL ulikwisha Januari 31, 2011 na kwa karibu miezi mitatu, mpaka alipopewa mkataba mpya na RITA alikuwa hafanyi kazi kutokana na notisi yake ya miezi mitatu ya Novemba mwaka jana ambayo ingemfikisha katika kuacha kazi Februari 2011.
Imeelezwa kwamba baada ya kumpa mkataba, sasa RITA inamtafutia kibali cha kuishi nchini kupitia Kituo cha Uwekzaji (TIC), huku kukiwa na taarifa kwamba uwapo wake una siri nzito kutokana na kulinda maslahi ya alikotoka zaidi kuliko maslahi na usalama wa Tanzania.

Mbali ya kuendesha biashara ya mgahawa bila kuzingatia sheria inayomzuia kufanya hivyo nchini, Subramaniam ni kati ya wahasibu wanaolipwa vizuri sana nchini pamoja na kuwa kuna pingamizi dhidi ya ajira yake kutoka kwa baadhi ya watendaji serikalini. Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kuwa mpango wa ulaji mkubwa kiasi hicho, unaoweza kuingiza fedha nyingi kiasi hicho katika mifuko binafsi unaweza tu kufanikishwa na ushiriki mkubwa wa wakubwa, tena katika ngazi ya watendaji wakuu au makatibu wakuu na tayari baadhi wanaelezwa kununua mahekalu ama kuwanunulia watu wa karibu nao.
Sekta ya nishati nchini imeendelea kugubikwa na kashfa na baada ya IPTL iliibuka kashfa nyingine katika miradi kama hiyo ikihusisha kampuni za Richmond Development LLC na Dowans Holding Limited, kashfa ambazo ziliwagharimu wanasiasa kadhaa akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, ambao wote waliwahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini.
hs3.gif
 
leo ndio nimejionea kwa nini viongozi wa ccm wanaipenda IPTL,nimekuta malori ya super star yenye tenda ya kupeleka mafuta mazito iptl yakishusha uchochoroni manzese hayo mafuta yaliyokua yapelekwe iptl!hivyo tanesco serikali wanatuibia wananchi kwa kulipa bili ya mafuta ambayo IPTL haikuyatumia kuzalisha umeme!
 
umetoa taarifa polisi na pccb? tafadhali fanya hivyo.

Hawatachukua hatua kwani wanajua wezi ni maboss wao.Tuvumilie hadi 2015 tufanye kweli kwenye sanduku la kura na tulinde kura au la tuharakishe mchakato wa katiba au tume huru vinginevyo tutaendelea kuumia hadi tuzeeke.Kwa sasa CCM ni wepesi kuwatoa hata bila tume huru.Tutatumia nguvu ya umma, hawana pa kujificha
 
leo ndio nimejionea kwa nini viongozi wa ccm wanaipenda IPTL,nimekuta malori ya super star yenye tenda ya kupeleka mafuta mazito iptl yakishusha uchochoroni manzese hayo mafuta yaliyokua yapelekwe iptl!hivyo tanesco serikali wanatuibia wananchi kwa kulipa bili ya mafuta ambayo IPTL haikuyatumia kuzalisha umeme!

kesho yavizie kisha yapige picha tubandike hapa jamvini pamoja na hizo namba za gari, kisha hatua nyingine ndefu zaidi zitafuata.
 
Back
Top Bottom