TANESCO Morogoro mbona kila siku umeme hakuna kwa muda mrefu?

BARUA YA WAZI KWA WAZIRI WA NISHATI WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

UTANGULIZI
Ndugu, Mhe, Waziri tunakusalimu kwa jina la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania......(Kazi iendeleee...). Baada ya salamu hiyo iliyohasisiwa na Rais wetu mpendwa Mama SSH, nikupongeze kwa kazi unayoendelea nayo ya kuwaletea watanzania maendeleo hasa umeme kweli unastahili kupongezwa sana maana nchi nzima sasa ni furaha na vifijo hasa baada ya tamko lako Kwenye bunge la bageti kuwa umeme ni elfu ishirini na saba (27,000/=) kwakweli kupitia wizara yako tunaipongeza serikali ya JMWT chini Mama yetu Rais SSH, Kwa kazi nzuri sana na iliyotukuka.

Mhe, Waziri sisi ni wananchi wa mtaa wa KAMBI TANO mtaa huu upo katika kata ya LUKOBE katika Manispaa ya Morogoro, mtaa huu ulipimwa viwanja na kuuzwa na Manispaa kwa wananchi 2008/2009 ambapo takwimu za hesabu ya kaya ya mwaka 2018 iliyofanywa na serikali ya mtaa wakati huo mtaa huu ulikuwa na kaya 1,700 (Ofisi ya serikali ya mtaa kwa rejea) ingawa kutokana kwamba ni mtaa unakua kwa kasi mpaka sasa 2021 kunaweza kuwa na ongezeko zaidi. Kijiografia mtaa huu upande wa magharibi unapakana na mtaa wa Lukobe Juu/Mikoroshini, kusini unapakana na Mtaa wa Mgudeni/Tushikamane, upande mashariki unapakana na Azimio/Mkundi na kasikazini ni mlima unaotenganisha Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Mvomero.

DHAMIRA LENGWA
Lengo la barua hii ni kilio cha umeme kilichogubikwa kwa wananchi wa mtaa huu kutokana na dhana kwamba toka mwaka 2008/2009 wananchi walipotangaziwa viwanja na Manispaa ya Morogoro nakununua viwanja hivyo mpaka leo 2021 bado mtaa hupo kizani hakuna umeme.

NINI KIMEFANYIKA
Mhe, Waziri, Kutokana na kwamba suala la umeme ni hitaji la muhimu sana kwa wananchi baada ya kuvumilia sana huku tukiwa tumechoka ahadi za viongozi kuwa wapo Kwenye mkakati wa kutatua tatizo hilo mwaka 2017/18 tulianza kufuatilia wenyewe katika ofisi za TANESCO MKOA kwa pamoja kukawa na majibu mengi na maelezo yasiyo na Tija kutokana na kwamba hayakutatua Kero yetu. Baada ya mvutano wa takribani mwaka mmoja Mwaka 2018/19 ndipo upande mmoja wa mtaa eneo la mashariki zililetwa nguzo 14 (HT) na nguzo ndogo 36 zikasambazwa kwa wananchi waliokuwa karibu na barabara zikaisha ambapo kulingana na uhitaji hata asilimia 5% hawakufikiwa. Zoezi la kuendeleza kuomba umeme ofisi za TANESCO ziliendelea kwa kasi lakini majibu yaliyotoka ilikuwa ni ufinyu wa bajeti, kila tulipokwenda tatizo ni bajeti pamoja na nguzo lakini wakati wanatuambia hakuna nguzo sisi kila siku tunapita Kwenye kalakana Msamvu Terminal tunaona nguzo zimerundikwa na zinashushwa na kuongezeka mara kwa mara, na tukinukuu kauli yako bungeni ulisema tuna ziada ya nguzo milioni mbili kwa dhana hii haiingii akilini meneja wa TANESCO anapotupa majibu kuwa hakuna nguzo.

NINI KIMESABABISHA TUKWAME
Mhe, Waziri; kilichosababisha TUKWAME Sisi wananchi tunapambana sana lakini ofisi ya TANESCO haitupi ushirikiano wa vitendo.

NINI TUNAOMBA KWAKO
• Mhe, Waziri; Kwakuwa tatizo la umeme limekuwa la muda sana katika mtaa wetu kama jitihada tumefanya za kutosha kwa viongozi wako wa chini kuanzia ofisi ya meneja wa mkoa miaka minne sasa toka tuanze jitihada za kuwafikia walengwa yaani Meneja mkoa, ofisi ya mkuu wa wilaya na ofisi ya mkuu wa mkoa lakini hatuoni majibu, sasa tumeona tukuombe wewe ambayo ni mamlaka ya juu Kwenye swala la umeme ili nasisi tuweze kuwa sehemu ya watanzania hasa waishio mjini maana tunachekwa na kufedheheshwa na ndugu zetu wanaotoka vijijini kuja kutusalimia maana wao wana umeme sisi Manispaa hatuna umeme kweli ni kero.
• Mhe, Waziri; Tunakuomba wewe uweze kuwasisitiza TANESCO watuletee umeme hili na sisi wananchi wa KAMBI TANO tuwe sehemu ya kulipa kodi ya majengo kwa maendeleo ya Taifa letu.
• Mhe, Waziri; Tunakuomba wewe HILI na sisi wananchi wa Kambi Tano tuwe sehemu ya mchango wa pato la Taifa kutokana na ulipaji wa bili za umeme na gharama nyingine zinazoambatana na matumizi ya umeme.
• Mhe, Waziri; Tunakuomba wewe HILI na sisi wananchi wa Kambi Tano tuweze kujiajili kutokana na uwepo wa Nishati ya umeme na hivyo kuisaidia serikali kuongeza pato la taifa.

MAPENDEKEZO
1. Mhe, Waziri; Kama bajeti ya serikali ni finyu sisi tupo tayari kujigharamia tununue nguzo watuletee umeme
2. Mhe, Waziri; Tunaomba TANESCO waje tukae pamoja Kwenye kikao watueleze kwa nini wanakataa kutuletea umeme HILI kama kuna tatizo tuone namna ya kulitatua maana kwasababu hiyo wanafanya mtaa wetu wote ushindwe kulipa kodi ya majengo na hivyo kukwamisha ulipaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

HITIMISHO
Mhe, Waziri; Tuendelee kukupongeza kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Taifa unaendelea kufanya chini ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwakweli sisi wananchi itoshe kusema kuwa TUMEWAELEWA! TUMALIZIE KWA KUKUSALIMU TENA KWA JINA LA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA...!

Nakala;
Mwenyekiti Mtaa Kambi Tano
Diwani Kata ya Lukobe - Fowarded
Meneja TANESCO (M) - Fowarded
Mbunge Morogoro (M) - Fowarded
M/Wilaya Morogoro - Fowarded
M/Mkoa Morogoro - Fowarded
 
Back
Top Bottom