Tanesco: Bajeti ya Sh499 bil., haitalipa deni la mabilioni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanesco: Bajeti ya Sh499 bil., haitalipa deni la mabilioni

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Jun 23, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 23, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,612
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  Baadhi ya maofisa wakitembelea mitambo ya Songas jijini Dar es salaam

  Na Matern Kayera
  WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi nchini kwa mwaka 2011 na Mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13 Bungeni, Mjini Dodoma, amesema, ukame ulioikumba taifa mwaka, umechangia kuwapo kwa matatizo ya umeme nchini.


  Amesema, kukosekana kwa nishati ya kutosha na ya uhakika ya umeme, kumeathiri shughuli za uzalishaji viwandani na maeneo mengine.


  Ameeleza kwamba mwaka 2011, sekta ndogo ya umeme wa gesi ilikua kwa asilimia 1.5 tofauti na asilimia 10.2 ya mwaka 2010.


  Wasira amefafanua kuwa ukame ulisababisha kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya Mtera na Kihansi. Mambo mengine yaliyochangia ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya umeme, ukarabati wa mitambo ya Songas ambayo yalisababisha kusimama kwa uzalishaji wa wa umeme wa gesi kwa muda.


  Kutokana na matatizo ya mgawo wa umeme unaojirudia kila mwaka, na kuathiri shughuli za uzalishaji viwandani na maeneo mengine, Wasira amesema tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya umeme.


  Amesema, fedha hizo zitahusu miradi ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Miradi mingine ni ya kujenga mitambo ya kufua umeme Kinyerezi ambayo itasaidia kuzalisha megawati 150 na megawati 240.


  Amebainisha kwamba katika upande wa usambazaji, fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi na kuimarisha njia za umeme wa msongo wa 220Kv North-West Grid; Kv 400 Iringa mpaka Shinyanga na Kv 132 Makambako mpaka Songea.


  Suala la kusambaza umeme vijijini, anasema fedha kwa ajili ya kazi hiyo zimetengwa ili kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo ya vijijini.


  Wasira amesema kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 5.5 mwaka 2010, mpaka kufikia asilimia 12.7 (2011), kumechangia kupanda kwa bei ya umeme, gesi, na bidhaa zingine kama vile mchele, sukari na mafuta ya kupikia.


  Kimsingi, tatizo la umeme nchini, linaonekana kutopata ufumbuzi wa uhakika tangu mwaka 2006, baada ya sakata la Richmond kuibuka. Licha ya mipango mingi na mizuri ya Serikali katika kushughulikia tatizo hilo, bado uchumi unaathiriwa kwa kuwa upatikanaji wa nishati hiyo umekuwa ukisua sua.


  Julai mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, William Ngeleja, alinukuliwa na vyombo vya habari akioredhesha miradi kadhaa ya umeme wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake Bungeni, Mjini Dodoma.


  Kwa mujibu wa Ngeleja, miradi hiyo ililenga kumaliza matatizo ya nishati ya umeme nchini. Anasema, Serikali imekusudia kuimarisha na kuboresha sekta ya nishati ili kuongeza fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine.


  Ili kufikia azma hiyo, Ngeleja aliorodhesha miradi 16 ambayo Serikali ingeitekeleza kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua na kuboresha njia za umeme, pamoja na kupanua miundombinu ya gesi asilia.


  Miradi hiyo ni pamoja na ule wa kufua umeme wa megawati 100 uliopo Dar es Salaam. Miradi mingine ni ule wa megawati 60 (Mwanza), megawati 240 (Kinyerezi- Dar es Salaam), megawati 300 (Mnazi Bay-Mtwara), megawati 230 (Somanga Fungu -Kilwa), makaa ya mawe megawati 200 (Kiwira), megawati 400 (Ngaka), megawati 600 (Mchuchuma).


  Miradi mingine ni ule wa megawati 16 (Murongo/Kikagati- Kagera), megawati 63 ( Rusumo-Kagera), Stiegler’s Gorge megawati 2,100 (Pwani), megawati 165 (Mpanga), megawati 222 (Rumakali).


  Miradi ya dharura ilijumuisha Symbion (megawati 112.5), Aggreko (megawati 100), pamoja na ununuzi wa mitambo ya kufua megawati 70 ambayo ingefungwa Majani Mapana Tanga, na ule wa gesi wa IPTL, uliopo Tegeta-Dar es Salaam.


  Pamoja na kuwapo kwa matatizo ya umeme ya mara kwa mara, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud, amesema kiasi cha bajeti cha Sh 498.9 bilioni iliyotengwa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha, kinatosha kutatua matatizo ya umeme nchini.


  Akianisha matumizi ya fedha hizo Bungeni, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, alisema kiasi hicho cha fedha kitaelekezwa katika shughuli za uzalishaji, usafirishaji pamoja na usambaji wa nishati ya umeme nchini.


  Badra amesema, ingawa hawezi kusema mahitaji halisi ya umeme nchini ni kiasi gani, lakini anaamini kuwa kiasi hicho kitakidhi mahitaji katika uzalishaji, usafrishaji na usambazaji wa umeme kwenye maeneo mbali mbali ya nchi.
  “Unajua hakuna mahitaji halisi ya umeme, mahitaji ya umeme yanabadilika mara kwa mara, kwa hiyo kusema mahitaji halisi ya umeme ni kiasi fulani, siyo rahisi,”amesema Badra Masoud.


  Pia mefafanua kuwa kiasi cha Sh 498.9 bilioni kilichotengwa na Serikali kwa bajeti ya mwaka huu, hakitatumika katika kulipia deni ambalo Tanesco inadaiwa. Amesema fedha hizo zitaelekezwa kutatua matatizo ya umeme yaliyokusudiwa.


  Badra amesema, hivi sasa Tanesco inadaiwa Sh 300 bilioni ilizokopa kutoka taasisi za kifedha nchini. Amesema Tanesco imeanza kulipa deni hilo, na hakuna deni lingine lolote wanalodaiwa.


  Kuhusu uboreshaji wa huduma ya umeme, Meneja huyo amesema hivi sasa mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 100 umekamilika. Amesema mtambo huo umefungwa Ubungo na utazinduliwa muda wowote kuanzia sasa.


  Amesema mradi mwingine unaotarajiwa kukamilika mwaka huu, utazalisha megawati 60 uliopo Nyakato, Jijini Mwanza.


  Badra amesemahivi sasa wanaboresha miundombinu ya usafirishaji umeme maeneo mbali mbali nchini.
  Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na njia ya umeme ya Iringa-Shinyanga mpaka Makambako.


  Amesema Tanesco pia wanaendelea na shughuli za usambazaji umeme maeneo tofauti tofauti kama vile ilivyo katika Wilaya ya Temeke hivi sasa.


  Ametaja matatizo mengine ambayo Tanesco linakabiliana nayo ni uharibifu wa miundombinu ya umeme. Amesema kumekuwa na wizi wa mara kwa mara wa nyaya za umeme na mafuta ya transfoma.


  Amesema nia ya Tanesco ni kutoa huduma ya umeme wa uhakika kwa wananchi. “Sisi kazi yetu siyo kuzima umeme, na wala hatupendi kuzima umeme, lakini matatizo haya ya wizi wa nyaya na mafuta ya transfoma yanatulazimisha mara nyingie kufanya hivyo. wananchi wanapaswa kulijua hilo; wanatakiwa kutusaidia katika kulinda miundo mbinu hii,”anasema.


  Akijibu maswali Bungeni wiki hii, Naibu Waziri wa Nishati , George Simbachawene amesema, Tanzania ni nchi pekee Afrika Mashariki inayozalisha umeme kwa gharama kubwa na kuuza kwa bei ya chini.
  http://www.mwananchi.co.tz/makala/31-uchumi/24090-tanesco-bajeti-ya-sh499-bil-haitalipa-deni-la-mabilioni
   
Loading...