TAMWA-Zanzibar yataka mabadiliko ya haraka sheria za habari Zanzibar

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
ZANZIBAR

CHAMA cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimesema kuna haja ya taasisi husika za mabadiliko ya sheria kuweka kipaumbele kufanyiwa marekebisho yanayoendana na matakwa ya wadau katika sheria za habari Zanzibar ili zitoe mazingira ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao.

Mkurugenzi wa Chama hicho Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa akizungumza na wandishi wa habari katika mkutano wa kuwasilisha ripoti ya sheria za habari Zanzibar zilizofanyiwa mapitio na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la INTERNEWS Tanzania ambazo zinakinza uhuru wa habari pamoja na uhuru wa kujieleza vyombo vya habari alisema uhuru wa habari ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa.

Alisema uhuru wa habari ni nguzo muhimu inayoweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ukuzaji wa maendeleo kwenye Nchi hivyo inapotokea sheria ya tasnia hiyo kubana ni sawa na kuchelewesha maendeleo ambayo yanahitajika na kila mtu.

Alieleza, “lazima tufahamu kwamba uhuru wa habari kwenye Nchi yoyote ni nguzo muhimu inayoweza kusaidia maendeleo na ndio maana enzi za uhai wake Nelson Mandela alipigania uhuru wa habari katika muda wake wote hususani vyombo binafsi (Private media).’’

Akitolea mfano changamoto za sheria hiyo alisema ni pamoja na Sheria namba nane, (27) (i) ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu ambacho kinaeleza afisa yoyote wa Jeshi la Polisi anaweza kuzuia au kukamata gazeti lolote lile lisichapishwe iwapo atashuku linakwenda kinyume jambo ambalo linakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza.

“Tuna kila sababu ya kuona kwamba Sheria zetu, Sera na matendo yaendane na mikataba ya kimataifa kuhusu uhuru wa habari ili iweze kuleta maslahi kwa makundi yote,” alieleza Dkt. Mzuri Issa.

Aliongeza “tumepitia sheria kumi za habari na katika kufanya mapitio hayo tunasukumwa zaidi na mambo matatu. kama Zanzibar na Tanzania tunapaswa kwendana na mikataba ya kimataifa.”

Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo akifafanua zaidi alionesha kusikitishwa kwake na mamlaka mengine ya sheria ambayo inampa uwezo waziri wa habari kufungia chombo chochote cha habari iwapo ataona inakwenda kinyume na matakwa yake.

Alieleza kuwa hatua ya kufungia chombo ni jambo kubwa amabalo lisingepaswa kufanywa na waziri badala yake lilipaswa kufanywa na mamlaka nyingine ikiwemo Mahkama.

Mapema akiwasilisha ripoti ya mapitio ya sharia za habari, Shifaa Said alisema licha ya juhudi kubwa kuchukuliwa na wadau wa habari kutoa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbalimbali lakini bado utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.

“Sisi kama wadau tumeshatoa mapendekezo yetu ya kuhitaji mabadiliko ya sheria mbalimbali za habari ikiwemo Sheria ya tume ya utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 na tunaendelea kufanya ushawishi ili tuweze kupata sharia bora zitakazotoa nafasi kwa wandishi na vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake kwa uhuru,” ’Shifaa Said Hassan, mdau wa habari.

Hivyo aliwataka wandishi wa habari kuendelea kufanya ushawishi wa mabadiliko ya sharia kwa kuandika mapungufu yaliyopo katika sharia hizo ili ziweze kufanyiwa marekebisho kwa haraka.

Alieleza, “sisi wandishi wa habari tuipigie chapuo sheria za habari zilizofanyiwa mapitio ambazo zinakinza uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa kufanya ushawishi kupitia vyombo vya habari ili hizi sheria ambazo tunahisi zinatatiza uhuru wa habaroi ziweze kufanyiwa marekebisho.”

Akichangia ripoti hiyo mwandishi wa habari mwandamizi Zanzibar, Jabiri Idrissa alisema waandishi wa habari Zanzibar wanakabiliwa na mazingira magumu ya kufanya kazi iwapo siku sheria zilizopo zitafanyiwa kazi ipasavyo.

Akitolea mfano kupitia Sheria ya Kinga na Madaraka ya Baraza la Wawakilishi no. 4 ya 2017, Spika anaweza kumuita raia yoyote wa Zanzibar kuhojiwa kwenye kamati za Baraza hilo iwapo ataona amefanya kosa ambalo limekinzana na sheria za Baraza, huku sheria hiyo ikimzuia alieitwa kwenda na wakili wake wakati wa kuhojiwa. Tunaona kuwa kufanya hivyo ni kumyima haki muhimu ya mtu kujitetea pamoja na kuwa jambo la kuitwa na kuhojiwa lilipaswa kufanywa na Mahkama na sio taasisi nyengine yoyote ile.

Nae Khadija Rashid kutoka Redio Jamii Mkoani Pemba alisema kuna haja ya kuongezwa uhamaishaji zaidi kwa wanahabri juu ya ushawishi wa mabadiliko ya sharia hizo ili kuweka mazingira salama kwa tasnia hiyo.

Alisema, “kinachosikitisha zaidi ni kuona idadi kubwa ya wananchi hawajui sheria zinazowahusu wao wenyewe na kuongezea kuna haja kazi kubwa zaidi kuendelea kufanyika.

Nae Berema Sleiman Nassor alisema wakati wa uchaguzi wanahabari wengi hukutana na mazingira mgumu licha ya kufanya kazi zao kwa misingi yote ya sheria za tume.

Alisema, “mazingira niliokutana nayo sitaweza kusahau maisha yangu yote nilitolewa kituo cha kupigia kura kama sikua na kazi maalumu ya kukusanya habari kwa maslahi ya umma’’alisema.

Mkutano huu wa kuwasilisha ripoti ya sheria za habari Zanzibar unakuja kufuatia kufanyika kwa mapitio ya sheria mbalimbali za habari ambayo yamefanywa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la INTERNEWS Tanzania pamoja na wadau wengine wa habari Tanzania.

WhatsApp Image 2023-01-18 at 15.35.01.jpeg
 
Back
Top Bottom