TAMWA: Vyombo vya ulinzi viwachukulie hatua kali watuhumiwa wa vitendo vya mauaji ya Wanawake na Watoto

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
TAMWA, Zanzibar yaviomba vyombo vya ulinzi kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria watuhumiwa wa vitendo vya mauaji ya wanawake na watoto

Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kinaviomba vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinawakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa waliohusika na vitendo vya upigaji na uuaji wa wanawake na watoto vilivyotokea hivi karibuni, hapa Zanzibar.

Hivi karibuni msichana wa miaka 23 Sumaiya Mohammed Said mkaazi wa Jambiani Kikadini mkoa wa kusini Unguja amedaiwa kuuwawa kwa kupigwa mapanga na Imani Abdallah Abdallah umaarufu Kichele (38).

Tukio jengine la ukatili dhidi ya wanawake lilitokea huko Fuoni nyumba moja mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ambapo bi Raya Khamis Mgeni (45) alidaiwa pia kushambuliwa kwa mapanga yeye na mtoto wake aliye chini ya mwaka mmoja.

Mashambulizi hayo yalipelekea kifo cha mtoto huyo asiye na hatia na kumjeruhi vibaya Bi Raya ambaye amelazwa katika hospitali ya Mnazi mmoja tokea tarehe ya tukio, 30/8/2021.

Kwa mujibu wa rikodi za TAMWA ZNZ tangu mwaka 2016, matukio 19 ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa (wanawake 15 na watoto wanne) ambapo ni matukio machache tu ndiyo yaliyofikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar yakiwemo ya Wasila Mussa (21) na Hajra Abdallah Abdallah (21).

Hivyo, TAMWA-ZNZ inaviomba sana vyombo vya ulinzi kukomesha vitendo hivi kwa kuwatafuta wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili wapewe adhabu inayowastahiki.

Hali ya kuvamiwa wanawake na watoto na kupigwa inavunja haki ya msingi ya wanawake ya kuishi kwa amani na pia inawatia hofu katika kuendeleza shughuli zao muhimu za kimaendeleo.
 
Back
Top Bottom