Tamko Rasmi kuhusu “mgogoro wa ardhi” wa Mivumoni, Kata ya Madale, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
705
Tamko Rasmi kuhusu “mgogoro wa ardhi” wa Mivumoni, Kata ya Madale, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam

MWANA HAKI

Mnamo Aprili 5, 2011, tukio la kustaajabisha na kusikitisha lilitokea kwenye kitongoji cha Mivumoni, kilichopo kwenye Kata ya Madale, Tarafa ya Kunduchi, Wilaya ya Kindononi, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo inadaiwa takriban watu watano, wakiwa ni walinzi wa kukodiwa, kati ya takriban walinzi hamsini, waliuwawa na wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo la Mivumoni.

Binafsi, sitaki kuingilia katika kile kinachoitwa “mgogoro wa ardhi” kwani matukio ya aina hii yamekwishatokea mara nyingi hapo awali, pasi na wahusika kuchukua hatua zozote zile za kuwalinda na kuwatetea wanyonge. Ninachotaka kuzungumzia, kama mtetezi wa haki za wanyonge ni kama ifuatavyo:

  1. Ni mara nyingi sana tumeshuhudia, vyombo vya habari vikiarifu, kuwapo kwa ubomoaji wa nyumba na kampuni za Madalali wa Mahakama, wanaopewa amri na ruhusa ya Mahakama, kutekeleza “ukaziaji” wa hukumu, pale ambapo inapoamriwa kuwa, ama waliopo ndani ya nyumba husika, bila kujali iwapo wanayo haki au hawana haki ya kuwapo huko, kutakiwa kuondoka kabisa na kuhama ndani ya nyumba hiyo, si kwa hiari yao, bali kwa lazima kabisa.
  2. Ni mara nyingi sana tumeshuhudia kwamba, watu hao wanapopewa amri hiyo ya kuondolewa kwenye nyumba zao, ambazo wengi wao walizaliwa na kukulia humo ndani, huwa hawapewi muda wa kutosha kujiandaa kuhama, kwa hiyo inakuwa ni tafrani kubwa kwao. Wanapofika maofisa kutoka kampuni za Udalali wa Mahakama, huwa wanafika na karatasi zao kutoka Mahakamani, wakiambatana na walinzi (wenyewe wanawaita “mabaunsa”) pamoja pia na askari polisi, ambao wanakuwa ni tishio kubwa kabisa, kiasi kwamba, wanaokutwa nyumbani hao, mara nyingi wakiwa ni watoto wadogo kabisa na wasaidizi wao – mara nyingi wakiwa ni wa kike – ambao huwa hawana uwezo wala nafasi ya kujitetea, hivyo, huwa ni jambo rahisi kutekeleza “Amri” hiyo ya Mahakama.
  3. Kuna ule usemi wa, penye safari ya mamba na kenge nao wamo; mara nyingi, kunapotokea zoezi kama hili, wahusika huwaita vijana wanaokaa vijiweni, ambao mara nyingi huwa hawana shughuli maalum ya kujipatia ujira, jamii huwa inawaita “masela” au “vibaka”, kwani mara nyingi, vijana hawa huwa hujipatia chochote kwa kuwakaba raia wasio na nguvu, haswa wanawake na wasichana, wanapopita “kwenye anga zao” nyakati za jioni au usiku. Vijana hawa huwa wanaitwa “kuja kusaidia” kuhamisha mali za wanaotolewa ndani ya nyumba zao, kabla ya nyumba hizo kubomolewa, na mara nyingi, vijana hao huwa pia wanatumia fursa hiyo kujitwalia chochote kile wanachoona kina manufaa kwao, bila kujali kwamba vitendo hivyo ni WIZI, tena WIZI WA MCHANA KWEUPE!


Binafsi nimesikitishwa, aidha, nimehuzunishwa na kile kinachoitwa kuwa “mgogoro wa ardhi”, kwani, bila ya kuingilia undani wa suala hili, hapa hakuna jambo kama hilo! Hakuna “mgogoro” wa aina yoyote ile. Hapa kuna uporaji wa ardhi wa mchana kweupe, tena bila ya soni, ambapo matajiri wanatumia fursa zao, kwa njia isiyo halali, rushwa, kujitwalia ardhi kwa kuwahonga watumishi wasio waadilifu, kwenye Mahakama, kujipatia “amri halali” kwa “mlango wa nyuma”, hivyo kuweza kutimiza matakwa yao YA KIFISADI KABISA!

Watu waliovamiwa na mafisadi, ambao walikuwa na nia zote za kuwaondoa kwenye nyumba zao, kinyume na sheria, walikuwa na uhuru na haki zote za kujitetea, na kabla ya kutumia haki hiyo iliyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni Haki ya Kuishi. Kila Mtanzania anayo haki ya kuishi mahali popote pale anapotaka, nchini Tanzania, ili mradi tu asivunje sheria zilizoainishwa na kuhakikiwa na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Siku moja, ninaambiwa, kabla ya tukio hili, kuna tukio lingine ambalo halikufanikiwa, ambao mafisadi hawa walijaribu kuvamia eneo hilo, lakini hawakufanikiwa, siku moja kabla, yaani, Aprili 4, 2011. Waliporudia utendaji wao, Aprili 5, 2011, walijikuta wakiingia – kama wanavyosema – “choo cha kike”, kwani wakazi wa eneo hilo walikuwa wamejipanga vizuri kukabiliana na shambulizi hilo.

Polisi wa Kituo cha Wazo walipigiwa simu, kuja kuhakikisha usalama na kuwapo kwa amani, kwani wavamizi hao walikuja wakiwa na silaha za moto, hivyo nia ya hata kuua watu wasiokuwa na hatia ilikuwapo. Kiingereza, kisheria, jambo hili linaitwa “premeditated homicide”.

Binafsi ninapinga hatua zote zile za uporaji nyumba na ardhi, kwani zinawaweka wale wote wasio na uwezo wa “kuingia mlango wa nyuma” wa Mahakama na kujipatia uwezo na haki ya kufanya wanayoyataka kwa njia zisizo halali, katika wakati mgumu sana. Unapokuwa umeishi kwenye nyumba “yenu”, na anapofariki mzazi, mlezi mkuu, baba mwenye nyumba, unaweza kujikuta kwenye wakati mgumu pale ambapo, baba mdogo au baba mkubwa, anayekuwa ameinyemelea nyumba ile miaka nenda, miaka rudi, anapoamua kujitwalia nyumba hiyo, kujipa haki ya kuwa msimamizi wa mirathi, bila kuteuliwa na familia, kwa kutumia fedha zake kujitwalia haki hiyo, na kuamua kuiuza nyumba bila kushirikisha familia, unajiuliza: “Nitaenda wapi mimi? Kufa kwa baba ndiko kumeleta yote haya?”

Napenda kuhitimisha tamko hili kama ifuatavyo:

  1. Wananchi wamechoka na manyanyaso ya muda mrefu, ambapo Mahakama imeendelea kutumika kuwapendelea wale wenye uwezo, dhidi ya wasio na uwezo. Wananchi wameamua kuchukua hatua, za kulinda mali na maisha yao. Wasilaumiwe kwa hilo, wanatimiza haki yao iliyoanishwa kikatiba.
  2. Wale ambao wanadhani kwamba wataendelea kutumia Mahakama ili kujipatia haki kinyume cha sheria bila ukomo. Ukomo umewadia, na sasa, popote watakapoenda na matingatinga yao na wababe wao, wananchi watakuwa tayari kukabiliana nao, MTAA MZIMA. Harakati za kimapinduzi zimeanzia Mivumoni, Madale, lakini sasa ni nchi nzima. Ufisadi UTAKOMESHWA!
  3. Hii sio migogoro ya ardhi. Hapa ni kuidai na kuilinda haki yetu ya Kuishi. Watakaojaribu, na ubabe wao, kutuondoa ndani ya nyumba zetu, kana kwamba hatuna haki nazo, watatambua kwamba sisi ni Watanzania, wenye kutambua haki zetu. Kwani mtatuua NCHI NZIMA? Mtabaki na nani?

>>> MWISHO <<<
 
  • Thanks
Reactions: Paw
He who comes to equity must come with clean hands.Taarifa zipo kuwa mnaojiita wanyonge ndio mliovamia eneo hilo na sasa mnatumia wingi wenu kutaka kuhalalisha uvamizi huo.Mbona huelezi namna mlivyopata eneo hilo,lini na nani aliwapa?Unatumia hapa kutafuta public sympathy.Inajulikana miongoni mwenu ni wanahabari ambao mnawatumia kupotosha ukweli kwamba nyie ni wavamizi.Lazima tujenge tabia ya kuheshimu sheria na kuogopa mali za watu badala ya kunyanyasa wengine kwa kuwapachika majina ya ufisadi nk.
Hamna haki hapo.Nyie ndo mlijiandaa kuua na kweli mliua.Toka lini baunsa akatumia silaha kama si uongo wa wazi?Nani miongoni mwenu aliuawa zaidi ya mabaunsa tu?
 
Back
Top Bottom