Tamko la Padre Kitima na changamoto ya Korona dhidi ya Usalama wa Nchi: Tunakwenda wapi baada ya hapa?

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,477
1615232148104.png

Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Athuman Diwani (Kushoto) akiwa amesimama na Rais John Magufuli (Kulia)

Usuli

Tarehe 03 Machi 2021, akiwa anatekeleza majukumu yake kama Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima, aliitisha mkutano wa maripota kutoka vyomba kadhaa vya upashanaji habari hapa Tanzania na kutoa
tamko muhimu, ambalo lilibeba hoja kadhaa, hoja yake mojawapo ikiwa inaweza kufupishwa katika muundo wa kimantiki ufuatao:

1. Matokeo yanayofanana huwa na sababu zinazofanana.
2. Kati ya Desemba 2020 na Februari 2021 makuhani tumeshuhudia vifo vingi vilivyotokana na changamoto za upumuaji ambazo huko nyuma tuliona kuwa zilikuwa ni dalili za ugonjwa wa virusi vya korona, yaani UVIKO;
3. Kwa hiyo, huenda vifo hivyo vimetokana na UVIKO;
4. Njia ya uhakika zaidi ya kutuwezesha kujua ukweli juu ya chanzo cha vifo vinavyotokea sasa hivi ni kufanya upimaji wa kisayansi.
5. Na tayari tunavyo vifaa vya kisayansi kwa ajili ya kutambua maambukizi ya UVIKO, lakini serikali inatuzuia kufanya vipimo hivyo;
6. Hakuna sababu nzuri ya serikali kuendelea kuzuia vituo vyetu vya afya kuchukua vipimo vya UVIKO;
7. Kwa hiyo, kwa niaba ya TEC, na kupitia kwenu waandishi wa habari, natoa wito kwa serikali kuruhusu wataalam wa tiba kutekeleza kwa vitendo mchakato wa vipimo vya kisayansi kuhusisna na tatizo la UVIKO.

Kupitia tamko lake Padre Kitima aliufahamisha umma kwamba Kanisa Katoliki linamiliki na kuendesha vituo vya afya zaidi ya 500 ambavyo mapaka sasa vimezuiwa na serikali kufanya kazi ya kupima uwepo wa virusi vya ugonjwa wa korona, jambo ambalo ni sawa na kulizuia Kanisa kufanya kazi yake ya kitume kupitia huduma ya tiba za kisayansi.

Naandika kama raia ili kutoa maoni yangu juu ya tamko hili kwa kuonyesha sababu zenye kueleza kwa nini wito wa Padre Kitima haupaswi kupuuziwa na serikali.

Utangulizi

Tangu Machi 2020, ugonjwa wa virusi vya korona (UVIKO) ulipozuka, mjadala wa siku nyingi juu ya mahusiano yaliyopo kati ya sayansi na dini umefufuka upya.


Kihistoria, zimekuwepo kambi kuu nne. Kuna kambi ya watu wanaosema kuwa dini na sayansi ni maadui wasioweza kusalimiana. Hawa wanadai kwamba, kauli za upande mmoja zinapinga kauli za upande wa pili, kama ambavyo tofauti kati ya nadharia ya uumbaji wa viumbe hai na nadharia ya mvuvumko wa viumbe hai zinavyothibitisha. Hii ni nadharia inayosisitiza uhasama kati ya sayansi na dini.

Kuna kambi ya watu wanaosema kuwa dini na sayansi ni majirani wasio na mahusiano ya urafiki wala uadui. Hawa wanadai kwamba, kila kambi ni himaya inayojitegemea ambako mwingine hawezi na hapaswi kukanyaga, kama ambavyo tofauti zilizopo kati ya data zinazoonekana kwa njia ya milango mitano yafahamu na tunu za kimaadili zisizoonekana wala kugusika zinavyothibitisha. Hii ni nadharia inayosisitiza uhuru wa sayansi na dini, yaani kila kambi kujitegemea.

Kuna kambi ya watu wanaosema kuwa dini na sayansi ni majirani wanaokamilishana. Hawa wanadai kwamba, kila kambi ni himaya ambako jirani wa upande wa pili anaweza na anapaswa kukanyaga kwa ajili kubadilishana mawazo na mwenzake ili kutafuta mwafaka juu ya masuala muhimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hii ni nadharia inayosisitiza majadiliano endelevu kati ya dini na sayansi.

Na kuna kambi ya watu wanaosema kuwa dini na sayansi ni marafiki wanaweza kusalimiana. Hawa wanadai kwamba, kuna kauli za upande mmoja zinazosikilizana na kauli za upande wa pili. Hii ni nadharia inayosisitiza kuendeleza mwafaka uliopo kati ya sayansi na dini.

Mjadala bado unaendelea juu ya nafasi ya nadharia hizi nne katika jamii. Lakini, kwa hapa Tanzania, ujio wa uviko umeligawanya Taifa katika kambi kuu mbili. Kuna kambi ya kina Rais Magufuli inayosema kuwa sala, maombi na sakramenti ya kumunio ni mazindiko tosha dhidi ya maambukizi ya UVIKO. Hivyo, kwa sababu hii, serikali ilipiga marufuku vipimo vyote vya kisayansi katika maabara za serikali na sekta binafsi.

Na kwa upande mwingine, kuna kambi ya kina Padre Kitima wanaosema kuwa dini na sayansi ni majirani wanaokamilishana. Hawa wamekuwa wanahimiza wananchi kusali na kuzingatia maagizo yote ya wanasayansi. Pia wamekuwa wanahimiza serikali kuruhusu vipimo vya kisayansi kufanyika katika maabara zote nchini.

Kwa mujibu wa tamko la Padre Kitima, tangu Desemba 2020 hadi Machi 2021, tayari mapadre 25 na watawa 60 wamekufa kwa sababu ya changamoto za upumuaji, changamoto ambazo zilikuwa zinawasumbua sana waathirika wa virusi vya korona katika miezi ya Machi 2020.

Hivyo, Padre Kitimaalitoa wito wa kulikumbusha Taifa la Tanzania juu ya umuhimu, uharaka na ulazima wa kuienzi Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi kupitia huduma ya tiba za kisayansi.

Kwa ujumla, tamko la Padre Kitima liliongelea nafasi ya Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi katika kutatua matatizo ya jumuiya ambayo ni pamoja na ujinga, maradhi kama vile Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO), umaskini, rushwa na unyonyaji.

Hata hivyo, wito wa Padre Kitima haujapokelewa vema na baadhi ya Watanzania. Kuna waliokejeli hoja yake, wapo waliomkejeli yeye mleta hoja, na wapo waliojaribu kuhamisha mawazo ya wasikilizaji kutoka kwenye hoja iliyo mezani na kuwapeleka kwenye hoja mwanasesere, hasa hoja zenye kuamsha hisia na kudhoofisha urazini.

Naona kuwa zote hizi ni mbinu za makusudi kwa ajili ya kupotosha ukweli uletao uhuru dhidi ya ujinga. Ni upotoshaji wa ukweli unaofanywa kimakusudi kwa ajili ya kutafuta maslahi fulani ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kidini au vinginevyo, yaani, kwa neno moja, utapiahabari (disinformation).

Na kama tunavyojua, utapiahabari huleta ujinga, ujinga huleta magonjwa, magonjwa huleta umaskini, umaskini huleta unyonge, unyonge huleta vifo, vifo huleta mmomonyoko wa nguvukazi ya Taifa, mmomonyoko wa nguvukazi ya Taifa huleta kifo cha Taifa.

Kwa hiyo, utaona kuwa, katika miaka kadhaa iliyopita, na hasa tangu enzi za kashfa kubwa kubwa, tatizo la utapiahabari limekuwa tatizo lililoongezeka katika orodha ya maadui wakubwa wa maendeleo ya Taifa letu.

Yaani, ukitaka kuelewa kirahisi maana na ukubwa wa tatizo la utapiahabari hapa nchini kumbuka namna taarifa juu ya matukio yafuatazo zilivyochakachuliwa: Escrow, Lugumi, Epa, Nida, Richmond, Kiwira, Kagoda, Mkataba wa Buzwagi, Uuzwaji Nyumba za Serikali, Ununuzi wa Majengo Pacha ya Bot, Kashfa ya Loliondo, Chavda na Mashamba ya Mkonge, Pembe za Ndovu Kwenye Ndege ya Rais Wa China, Uuzwaji wa Fukwe za Bahari ya Hindi, Ununuzi wa Nyumba ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia, ununuzi wa BAE Radar, Deep Green Finance Company Limited, Ujenzi wa Maghorofa Pacha ya BoT, Mradi wa IPTL, Mgodi wa Mchuchuma, Vitalu vya Uwindaji, Kampuni ya Mwananchi Gold Ltd, Kampuni ya Meremeta Ltd, Mradi wa Quality Plaza, Kampuni ya Tangold Ltd, Kampuni ya Mwananchi Trust Co. Ltd, na Kampuni ya TICTS ya kule Bandarini Dar.

Sasa hivi tatizo hilo la utapiahabari limehamia kwenye sekta ya uhai wa binadamu kupitia ugonjwa wa virusi vya korona (UVIKO). Lakini, haki ya kuishi ni kikonyo cha haki zingine zote. Yaani, haki za binadamu ni haki za binadamu hai. Mwili wa marehemu ni mabaki ya mwili wa binadamu.

Kwa hiyo, tunapaswa kusanifu na kusambaza hoja za kukataa na kukataza itikadi ya utapiahabari kuhamishiwa kwenye sekta ya uhai wa bindamu. Hoja katika bandiko hili ni hoja mojawapo kati ya hoja nyingi zinazoweza kusanifiwa na watetezi wa uhai wa binadamu na uhai wa Taifa.

Tofauti kati ya sayansi na ushirikina

Lakini, ni maoni yangu kwamba, tatizo hili la utapiahabari katika kipengele cha UVIKO lisingekuwa kubwa zaidi kama serikali ingekuwa inaelewa na kuheshimu tofauti zilizopo kati ya sayansi na ushirikina.

Ninavyoelewa mimi, "
ushirikina ni tabia ya kuamini na kuaminisha watu baki kwamba tukio moja ni chimbuko la tukio jingine wakati ukweli ni kwamba hakuna uhusiano wa sababu na matokeo kati ya matukio hayo mawili."

Ndio kusema kuwa, mtu ambaye akili yake inaongozwa na imani ya kishirikina ni kama mtu aliyevaa miwani ya rangi nyekundu ambayo humfanya kuona kwamba kila kitu kilicho mbele yake kina rangi nyekundu wakati ukweli halisi hauko hivyo. Anakuwa amekumbwa na tatizo la
akili yake kuona maruweruwe kila anapojaribu kutambua sababu za vitu mbalimbali.

Yaani, ushirikina ni ulemavu wa akili kama ambavyo
tatizo la upofu wa kushindwa kuona baadhi ya rangi ni ulemavu wa macho unaomfanya mhusika kushindwa kabisa kutambua rangi kadhaa kwa kutumia macho.

Na kwa upande mwingine, naelewa kwamba, "
sayansi ni maarifa ya hakika juu ya vitu na sababu zake za kweli yaliyopatikana kutokana na uthibitisho dhahiri wa kirazini."

Kwa hiyo, mwanasyansi ni mtu ambaye anamini na kuaminisha watu baki kwamba tukio moja ni chimbuko la tukio jingine kwa sababu ukweli ni kwamba kuna uhusiano wa sababu na matokeo kati ya matukio hayo mawili, ambapo tukio la kwanza ni sababu ya tukio la pili.

Matukio mawili yanayoletana huwa na mahusiano ya sababu na matokeo na husemekana kuwa na mahusiano ya kietiolojia, kwa kuwa "etiolojia" ni sayansi inayochunguza mahusiano kati ya sababu na matokeo yake.

Katika mahusiano haya ya kietiolojia, tukio la kwanza huitwa sababu, chanzo, kiini, asili au chimbuko la tukio la pili. Na tukio la pili huitwa matokeo, hatima, tamati au fainali ya tukio la kwanza.

Na kwa ujumla, endapo tukio A na tukio B ni matukio mawili tofauti yanayowezekana, basi, matukio haya yanaletana endapo, na endapo tu, ikiwa tukio A linatokea ni lazima tukio B lifuate, na ikiwa tukio A halitokei ni lazima kwamba tukio B halitafuata.

Kwa ujumla, fasili hizi za maneno "sayansi," "sababu" na "matokeo" zinamaanisha kuwa mitaala yote ya chuo kikuu ni sayansi zinazotofautiana, sio kwa aina, bali kwa viwango tu.

Sayansi imekuwa na mchango mkubwa sana katika jamii. Kwanza, imekuwa kimiminika cha kuyeyusha punje za ushirikina. Imetusaidia kuachana na kasumba ya kauli ya bosi ni ukweli siku zote.

Kuna manufaa mengine mengi sana ya sayansi. Kwa ufupi, kutokana na kazi ya watu mashuhuri wa karne ya kumi na saba mtazamo mpya juu ya ulimwengu ulibuniwa, na ilikuwa mtazamo huu, sio hoja maalum, ambao ulisababisha kupuuzwa kwa imani kwamba kuna juju, uchawi, watu wanaopagawa kwa sababu ya mapepo, na kadhalika.

Kimsingi, kulikuwa na viambata vikuu vitatu katika mtazamo wa kisayansi wa karne ya kumi na nane ambavyo vilikuwa muhimu sana.

Kwanza, ni madai kwamba, taarifa za ukweli zinapaswa kutegemea uchunguzi, na kusikiliza sio kutoka kwa mamlaka isiyo na ushahidi thabiti mikononi.

Pili ni madai kwamba, ulimwengu wa vitu vinavyoonekana na kushikika ni mfumo wenye kujisimamia na kujiendesha binafsi, na ambamo mabadiliko yote huongozwa na kanuni za maumbile.

Na tatu ni madai kwamba, dunia sio kitovu cha ulimwengu wa sayari zote tunazozifahamu.


Mchakato wa tafiti zinazofanyika kisayansi

Tangu enzi za kina Isaac Newton, mchakato wa utafiti wa Kisayansi umevuvumka na kuhusisha hatua saba zifuatazo: “Kuona, Kuhoji, Kutuhumu, Kutafiti, Kutahini, Kuhukumu na Kutenda.” Kwa sababu hii, Kanuni ya utafiti wa Kisayansi tunaweza kuiita “Kanuni ya 7K.


1615325823074.png

Mwanasayansi Sir Isaac Newton (1642-1727)

Hatua saba za utafiti wa kisayansi ni: (1) Kutambua tukio (kuona) kwa msaada wa hisia za macho, masikio, mdomo, pua au ngozi; (2) Kuhoji sababu ya pengo linalojitokeza kati ya matarajio yako na uhalisia wa kitu ulichokiona; (3) Kutuhumu sababu ya ulichokiona kwa kupendekeza jawabu la awali; (4) Kukusanya taarifa za kiushahidi kwa ajili ya kuthibitisha au kukanusha tuhuma; (5) Kutahini ushahidi ulioukusanya kwa kupima kama unathibitisha au kukanusha tuhuma; (6) Kama tuhuma inathibitika, kufanya hukumu kwa kuandaa hitimisho la kinadharia kwa msingi wa ushahidi uliokusanywa na kutahiniwa; na (7) Kutangaza nadharia na kuiweka katika vitendo.

Mchoro ufuatao unaonyesha vizuri hatua zinazotumika kwenye mchakato wa utafiti unaofuata ustaarabu wa kisayansi:


1615832117719.png

Mchoro wenye kuonyesha Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi

Hebu sasa tutumie mfano wa kawaida kabisa kuonyesha jinsi ustaarabu wa kufanya utafiti wa kisayansi unavyofanyika.

Kwa sababu ya kutumia milango mitano ya fahamu, ni wazi kuwa, watu wengi tunatumia ustaarabu wa tafiti za kisayansi kila siku tunapotumia milango mitano ya fahamu, hata kama hatujui kwamba tunafanya hivyo. Kwa mfano, fikiria kuwa, unataka kuchaji simu yako.

KUONA: Umechomeka chaja kwente simu na kwenye soketi ya umeme ukutani. Matarajio yako ni kwamba utaona kioo cha simu kinapiga kope kuashiria kuwa simu inapokea moto. Lakini ukiangalia kioo hicho unaona kuwa hakuna dalili zozote zenye kuonyesha kwamba simu hiyo inapokea moto. Hapa kuna pengo kati ya matarajio na uhalisia, na pengo hili linahitaji maelezo.


KUHOJI: Hapa utajiuliza, kwa nini kioo cha simu ninayotaka kuichaji hakipigi kope kama ambavyo huwa kinafanya siku nyingine huko nyuma?

KUTUHUMU: Baada ya kujiuliza swali la "kwa nini" hatua inayofuata ni kujaribu kutabiri au kuotea sababu zake. Huenda TANESCO wamekata umeme; huenda umeme katika meta yako ya LUKU umekwisha; huenda soketi ya umeme ukutani imeharibika; huenda kitako cha simu unayojaribu kuchaji kimeharibika; au huenda simu yote imeharibika. Zote hizi ni tuhuma zinazowezekana, na kunahitajika namna ya kuzipangua moja baada ya nyingine ili hatimaye simu ipate chaji.

KUKUSANYA USHAHIDI: Unaweza kuchunguza kama nyumba ya jirani imeunganishwa kwenye umeme na kama TV yake inaongea ili kujua kama TANESCO wamekata umeme au hapana; unaweza kuchungulia kwenye LUKU ili kuona kama bado kuna yuniti za umeme au zimekwisha ili uweze kuongeza umeme; unaweza kudadidisi sebule kusudi uone kama kuna soketi ya pili, ili uweze kuhamishia chaja kwenye soketi nyingine na kuona kama simu itawaka; na unaweza kuona kama kuna mtu mwenye simu nyingine jirani yako kusudi uweze kuchomeka chaja ile ile kwenye simu nyingine na kuona kama simu hiyo itawaka.

KUTAHINI USHAHIDI: Katika hatua hii, kama umegundua kuwa nyumba ya jirani imeunganishwa kwenye umeme WA tanesco na kama TV yake inaongea ina maana TANESCO hawajakata umeme; kama LUKU haina yuniti za umeme unaweza kuongeza umeme ili upate kuchaji simu yako baada ya hapo; kama sebuleni kuna soketi ya pili unaweza kuhamishia chaja kwenye soketi nyingine na kuona kama simu itawaka; na kama kuna mtu mtu mwenye simu nyingine jirani yako unaweza kumwomba na kuchomeka chaja ile ile kwenye simu yake ili kuona kama simu hiyo itawaka.

KUHUKUMU: Katika hatua hii, kama TANESCO hawajakata umeme utahitimisha kuwa umeme wa TANESCO unafika kwenye nyumba yako ; kama LUKU ina yuniti za umeme utahitimisha kuwa umeme wa TANESCO unafika kwenye soketi ya ukutani; kama soketi ya pili haikuiwezesha simu kuwaka utahitimisha kwamba kitako cha simu kimeharibika; na kama simu nyingine ya jirani yako itawaka utahitimisha kuwa kitako cha simu kimeharibika. KIla hitimisho ni hukumu, kwa maana ya nadharia inayoelezea sababu ya pengo ulilolibaini kati ya matarajio na uhalisia wa kitu ulichokiona.

KUTENDA: Kila hitimisho lililofikiwa katika hatua inayofuata linamaanisha hatua fulani ichukuliwe. Kwa mfano, kama TANESCO hawajakata umeme na LUKU yako ina yuniti za umeme zero inataamua kuchaji simu yako kwa jirani. Na kama utahitimisha kuwa umeme wa TANESCO unafika kwenye soketi ya ukutani na simu nyingine ya jirani yako haiwaki kwa kutumia chaja ile ile utaamua kubadilisha chaja ili kuchaji simu yako.

Muhtasari wa hatua saba katika mchakato wa kutafiti kisayansi

Tulipokuwa wanafunzi wa shule ya sekondari mwalimu wetu wa sayansi alitufundisha kukumbuka Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi, kwa msaada wa neno OPHETTA.

Neno OPHETTA ni kifupi cha maneno haya: “Observation Making, Problem Definition, Hypothesis Formulation, Evidence Collection, Hypothesis Testing, Theory Formulation, Theory Application.

Yaani, kwa Kiswahili tunaweza kusema kwamba, Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi ni kanuni inayotuhimiza “Kuona, Kuhoji, Kutuhumu, Kutafiti, Kutahini, Kuhukumu na Kutenda.” Ndio maana nimeiita “Kanuni ya 7K.

Kanuni hii inayo matumizi mapana katika sekta zote za sayansi, zikiwemo sayansi asilia, sayansi za jamii, sayansi za kihistoria, sayansi za kifalsafa, na sayansi za kiteolojia. Sayansi hizi zinatofautishwa na jinsi hatua za "kukusanya ushahidi (evidence collection) na “kutahini ukweli wa tuhuma” (hypothesis testing) zinavyofanyika.

Tofauti kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayani

Kwa kutumia Kanuni za 7K iliyojadiliwa hapo juu, sasa tunaweza kutofautisha kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi. Tunajua kuwa, kila mshirikina sio mwanasayansi, lakini sio kila mtu asiye mwanasayansi ni mshirikina.

Hapa nataka kutofautisha kati ya watu ambao sio mwanasayansi na sio washirikina, kwa upande mmoja, na watu ambao sio mwanasayansi na ni washirikina, kwa upande mwingine, ili kwa njia hiyo, tuweze kuweka mikakati miwili.

Mosi ni mkakati wa kuwatoa maofisini watu ambao sio mwanasayansi na ni washirikina. Na pili ni mkakati wa kuwarudisha kwenye mstari watu ambao sio mwanasayansi na sio washirikina.

Napendekeza kwamba kuna tofauti kubwa sita kati ya mtu ambaye ni mwanasayansi na mtu ambaye sio mwanasayansi. Hatua saba (7) za mchakato wa utafiti wa kisayansi zinatoa mwanga muhimu hapa.

Kila mtu mwenye akili timamu anaweza kupokea taarifa na kutunza kumbukumbu ya matukio yanayoendelea katika mazingira yake. Kwa hiyo, katika hatua ya kwanza hakuna tofauti kati ya mtu ambaye ni mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi.

Kwa maneno mengine, tofauti ya kwanza kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi inajitokeza kwenye hatua ya pili, yaani uwezo wa kuona utata na hivyo kubaini tatizo kwa “kuhoji” sababu ya utata huo (problem definition).

Ukweli ni kwamba, sio kila mtu anayeweza “kuona” atachukua hatua ya pili ya “kuhoji.” Kimsingi, kuhoji ni hatua ya kujiuliza swali la “kwa nini jambo hili linatokea namna hii na sio vinginevyo?

Kwa mfano, Mwanasayansi Isaac Newton (1642-1727) alipokuwa ameketi chini ya mti na kuona tunda linadondoka kuelea kwenye uso wa dunia, na sio kupaa angani, alijiuliza swali, “kwa nini?

Watu wengi kabla yake walikuwa wanaona tukio hilo lakini ni wachache waliwahi kujiuliza swali hili.

Hivyo, tofauti ya kwanza kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kubaini tatizo kwa “kuhoji” (problem definition).


Tofauti ya pili kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kubuni tuhuma inayojaribu kujibu swali lilijitokeza hapo awali. Sio kila mtu anayejiuliza “kwa nini?” anasonga mabele na kujaribu kupendekeza jawabu kwa swali hilo.

Kwa mfano, baada ya Isaac Newton kujiuliza swali la “kwa nini tunda linadondoka kuelekea kwenye uso wa dunia na sio kinyume chake?” alipendekeza kwamba huenda kuna nguvu ya uvutano kati ya dunia na tunda, ambapo ukubwa wa nguvu hiyo unategemea uzito wa dunia, uzito wa tunda na umbali kati ya tunda na dunia.

Watu wengi kabla ya Newton walikuwa wanaona tukio la kudondoka kwa matunda na kujiuliza swali kama yeye, lakini ni wachache waliowahi kujaribu kupendekeza jawabu la makisio kama alivyofanya Newton.

Hivyo, tofauti ya pili kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa “kubuni tuhuma” (hypothesis formulation) ambayo ni jawabu la makisio tu.

Tofauti ya tatu kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kuandaa jaribio kwa ajili ya kukusanya ushahidi (evidence collection) unaoweza kutumika katika hatua ya kutahini ukweli wa tuhuma (hypothesis testing) iliyobuniwa hapo awali kama jawabu la makisio,.

Kwa mfano, baada ya Newton kupendekeza kwamba huenda kuna nguvu ya uvutano kati ya dunia na tunda, ambapo ukubwa wa nguvu hiyo unategemea uzito wa dunia, uzito wa tunda na umbali kati ya tunda na dunia, aliandaa jaribio la kimaabara na kukusanya taarifa muhimu kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma hii.

Watu wengi kabla ya Newton walikuwa wanaona matukio ya kudondoka kwa matunda, kujiuliza swali kama yeye, na kujaribu kupendekeza jawabu la makisio kama alivyofanya Newton. Lakini, ni wachache waliwahi kuchukua hatua ya ziada ya kubuni jaribio kwa ajili ya kukusanya taarifa zinazoweza kutumika katika kutahini ukweli wa tuhuma husika.

Hivyo, uwezo wa "kukusanya ushahidi kitafiti" (data collection) kwa ajili ya kutuwezesha “kutahini ukweli wa tuhuma” (hypothesis testing) ndio tofauti ya tatu kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi.

Maandalizi ya jaribio la kitafiti kwa ajili ya kukusanya taarifa zitakazotumika kutahini ukweli wa tuhuma hutegemea sekta ya sayansi inayohusika. Kuna sayansi asilia, sayansi za jamii, sayansi za kihistoria, sayansi za kifalsafa, na sayansi za kiteolojia.

Kwa mfano, wataalam wa sayansi asilia na sayansi za jamii hutumia majaribio pacha kukusanya ushahidi. Jaribio la kwanza huwa ni kwa ajili ya kutahini ukweli wa tuhuma chanya (positive hypothesis), na jaribio la pili ni kwa ajili ya kutahini ukweli wa tuhuma hasi (null hypothesis). Wanafalsafa na wanateolojia wanazo mbinu zao za ziada.

Tofauti ya nne kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kutumia ushahidi uliokusanywa “kutahini ukweli wa tuhuma” (hypothesis testing) iliyo mezani.

Yaani, kama ilivyo katika mtihani wowote, kazi ya kutahini ukweli wa tuhuma inatoa fursa kwa mtahiniwa (yaani mleta tuhuma) ama kufauli au kufeli. Hii ni hatua ya kujiuliza: Je ushahidi uliokusanywa unakubaliana na tuhuma au unapishana na tuhuma? KInachofanyika ni sawa na kazi ya mwalimu kusahihisha karatasi za mtihani kwa kutumia skimu ya uhakiki.

Kama majibu ya mwanafunzi yanakubaliana na majibu yaliyo katika skimu ya uhakiki, basi mwanafunzi anapewa alama, vinginevyo anapigwa mkasi. Vivyo hivyo, kama ushahidi uliokusanywa ukithibitisha tuhuma, basi mtahiniwa anakuwa amefaulu. Na kama ushahidi uliokusanywa ukishindwa kuthibitisha tuhuma, basi mtahiniwa anakuwa amefeli.

Tofauti ya tano kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kutoa hukumu (theory formulation) sahihi baada ya kukusanya na kutafsiri ushahidi wa kitafiti.

Kwa mfano, kama tunataka kujua kama dawa ya kwinini inatibu ugonjwa wa malaria, tutaandaa makundi mawili ya watu wenye vimelea vya malaria. Kundi la kwanza watapewa dozi ya kwinini na kundi la pili hawapewi dozi hiyo.

Baada ya muda vipimo vya damu vitachukuliwa kutoka kila kundi. Kama kundi lililopewa dozi ya kwinini litapona na kundi la pili kuendelea kuumwa malaria, tutahitimisha kuwa dawa ya kwinini inaweza kutibu malaria, ikiwa masharti kadhaa yatazingatiwa.

Hitimisho hili litakuwa ni hukumu ya mtafiti dhidi ya mtu aliyeleta tuhuma kwamba "huenda dawa ya kwinini inatibu ugonjwa wa malaria kama vidonge viwili viwili vikimezwa kwa siku tatu mfululizo."

Na hivyo, uwezo wa “kuhukumu” kwa usahihi, yaani uwezo wa kutafsiri taarifa za kitafiti kwa kuandika nadharia sahihi unatupa tofauti ya tano kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi.

Kuna tofauti ndogo sana kati ya kutahini ukweli wa tuhuma (hypothesis testing) na hatua ya kutoa kuhukumu (theory formulation). Njia rahisi ya kueleza ni kurejea walimu wanachofundishwa katika somo liitwalo "Measurement and Evaluation," maneno ambayo hapa nayatafsiri kama "Kutahini na Kuhukumu Maendeleo Mwanafunzi."

Kutahini uwezo wa mwanafunzi ni kutafuta alama za mwanafunzi katika jaribio fulani. Na kuhukumu uwezo wa mwanafunzi ni kutafsiri maana ya alama hizo ili kumweka katika kundi mojawapo la wanafunzi wenye uwezo unaofanana. Ni viyvom hivyo katika kutahini na kuhukumu ukweli wa tuhuma ya kisayansi (scientific hypothesis).

Ufafanuzi huu unaturuhusu kuona tofauti ya sita kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi. Tofauti ya sita, na ya mwisho, kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa kuweka nadharia katika vitendo (theory application).

Kwa mfano, kama nadharia ya kutibu malaria kwa kutumia kwinini inasema kuwa mgonjwa ameze vidonge viwili kila siku asubuhi, kwa siku tatu mfululizo, basi uwezo wa kusimamia utaratibu huu wa matibabu pia utamtofautisha mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi.

Hivyo, tofauti ya sita kati ya mwanasayansi na mtu asiye mwanasayansi ni uwezo wa “kutekeleza nadharia” kwa usahihi (theory application).

Mtazamo wa Kanisa Katoliki Kuhusu Sayansi

Tangu enzi za Galileo Galilei (1564–1642), Baba wa Taifa la Wanasayansi, Kanisa Katoliki limeendelea kuboresha mtazamo wake juu ya uhusiano kati ya Sayansi na Dini. Nitaeleza kwa ufupi.

1615322961998.png


Padre Charles Kitima, Katibu Mkuu wa TEC, akiwa amebeba kitabu chenye jina la "Ibada ya Misa Takatifu"

Kwa mfano, Papa Yonae Paul II, katika "
Waraka juu ya Makutano ya Imani na Urazini (1998)," anasema kuwa kanuni ya OPHETTA ni kanuni inayomtofautisha mwanasayansi na mshirikina.

Alipoandika alikuwa waraka huu anataka kuwakumbusha makuhani katoliki juu ya umuhimu wa kutumia kanuni ya OPHETTA katika uinjilishaji.

Papa alisema kwamba, Misahafu sio marejeo pekee ya Kanisa, kwani, Kanuni ya imani yake inatokana na umoja uliopo katika vyanzo vikuu vitatu, yaani, Mapokeo , Misahafu na Urazini wa kisayansi na kifalsafa uliothbitishwa na vyombo vya kitafiti vinavyomilikiwa na Mamlaka Kuu ya Kanisa.

Alifafanua kwamba, vyanzo hivi vitati vina hadhi sawa, kwa maana kwamba hakuna hata chanzo kimoja kati yake, kinachoweza kujitosheleza bila kukamilishwa na vyanzo vingine viwili (ibara ya 55).

Kwa njia hii, Papa aliwahimiza makuhani kubalansi hoja zao kwa kutumia ushahidi uliokusanywa kutokana na Mapokeo, Misahafu, na Urazini wa Majisteria ya Kanisa. Urazini huo unarejea maarifa ya Sayansi na Filosofia kama yanavyotafsiriwa na Majisteria ya Kanisa, baada ya kushauriana na
Taasisi zipatazo 10 za Kisayansi na Kifalsafa zinazoongozwa na Papa.

Taasisi hizo za Kipapa ni pamoja na: Akademia ya Sayansi Asilia; Akademia ya Sayansi za Jamii; Akademia ya Uhai; Akademia ya Mt. Thomas Aquinas; na Akademia ya Teolojia ya Kipapa.

Baada ya kusikiliza tamko la Kuhani Charles Kitima, ni hitimisho langu kwamba, yeye ni mwanafunzi mzuri wa Papa Yohanne Paul II na mtu mwenye uelewa mkubwa kuhusu nafasi ya Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi katika maisha ya watu.

Pia ni mwanafunzi mzuri wa kina Galileo Galilei, JOhannes Kepler, Isaac Newton na Albert Eistein. Kauli yake ifuatayo ni ushahidi tosha:

''Ukweli huwaweka watu huru, kama mafundisho ya Biblia yanavyosema, lakini Tanzania tunaambiwa (na serikali kwamba) utaleta hofu. (Kanisa Katoliki linasisitiza kwamba) ukweli utapatikana kwa njia ya tafiti huru (za kisayansi)."

Padre Kitima pia alisisitiza kwamba kutegemea sala pekee hakuwezi kuondosha tatizo la ugonjwa wa korona nchini.

''Mungu si hirizi. Anataka binadamu tuwajibike. Korona ipo. Unaambiwa chukua tahadhari unasema umekwisha sali... Mungu wetu anataka tuwajibike. Yaani tutende majukumu yetu kwa karama na utashi tuliopewa," anafafanua Padre Kitima.

Ni kwa sababu ya imani hii thabiti katika ustaaarabu wa tafiti za kisayansi, hatimaye Padre Kitima aliwaalika wataalam wa tiba, watafiti na wanasayansi kufanya utafiti ili kubaini chanzo cha vifo vya watu wanaokufa kwa sababu changamoto za upumuaji.

1615699204272.png

Baba wa Taifa la Wanasayansi, Galileo Galilei
Hitimisho na mapendekezo muhimu

Tumeona tofauti kati ya sayansi na ushirikina kwa kusisitiza kwamba sayansi ni zaidi ya sayansi asilia, na kwamba sayansi ni maarifa yaliyothibitishwa kirazini kwa kutumia njia mahsusi kulingana na sekta ya sayansi inayohusika. Baada ya kusema haya, napenda kumalizia andiko langu kwa kupendekeza mambo matano.

1615323923310.png

Padre Charles Kitima, Rais Magufuli, Askofu Nyaisonga na Askofu mwingine mmoja wakiwa wanajadiliana juu ya Maendeleo ya Taifa la Tanzania

Kwanza, nawaalika wanazuoni wote wa Tanzania kuienzi kanuni ya OPHETTA kwa kuifanya kaulimbiu yao ya kila siku.

Ni kanuni inayowahusu wanasiasa, wachumi, wanasosiolojia, watumishi wa umma, wanasheria, wanateolojia, na waandishi wa habari.

Pili, na kwa namna ya pekee, nawaalika Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kuienzi kanuni ya OPHETTA kila wakati, kila mahali na kwa kila mtendaji.

Nimewahi kuambiwa kwamba, taarifa kadhaa zinazoandaliwa na baadhi ya Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa zinakiuka kanuni ya OPHETTA, na hasa katika hatua ya kukusanya ushahidi kwa ajili ya kutahini ukweli wa tuhuma (hypothesis testing).

Hivyo, kama tatizo hili bado lipo, namwaalika Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Diwani Athuman, kuchukua hatua stahiki za kuwajengea uwezo maafisa wake wanaopwaya.

Afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa asiyejua tofauti kati ya tuhuma na hukumu atakuwa anakiuka kanuni ya OPHETTA kila siku, na hivyo kuhatarisha Usalama wa Taifa anaopaswa kuulinda.

Na ninaona kuwa huenda kina Cyprian Musiba ni miongoni mwa watu wa aina hii.

Wito wangu ni kwamba, Idara ya Usalama wa Taifa inapaswa kulisaidia Taifa kusogea karibu na sayansi na kuwa mbali na ushirikina ambao ni moja ya vitisho vikubwa dhidi ya usalama wa nchi.

Naamini kuwa, Kanuni ya Utafiti wa Kisayansi inayo nafasi kubwa katika Maendeleo ya Taifa letu, na hasa katika kukabiliana na ushirikina unaoambatana na changamoto za upumuaji zilizoligubika Taifa.

Tatu, kwa sababu hizi zote, ni maoni yangu kuwa, tunakopaswa kwenda baada ya hapa ni kwenye maabara zinazotumia kanuni ya OPHETTA. Wataalam wa tiba tulio nao wapewe nafasi ya kuamsha vipaji vyao.

Taarifa kwamba kuna vituo vya afya zaidi ya 500 vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki ambavyo vimezuiwa kupima ugonjwa wa virusi vya korona ni kashfa inayoliweka Taifa letu karibu na ukweli wa kishirikina na kulisogeza mbali na ukweli wa kisayansi.

Nasisitiza kuwa, ushirikina ni moja ya vitisho vikuu dhidi ya usalama wa nchi sehemu zote duniani. Hivyo, serikali yetu inapaswa kubadilisha mtazamo wake kuanzia sasa kwa kuruhusu upimaji wa kisayansi katika vituo vyote vya afya vilivyopo nchini.

Nne, napendekeza kwamba, siku zote tukumbuke kuwa tunalo jukumu la kukata mnyororo wa sababu na matokeo (etiological connections) unaotengenezwa na muungano wa maadui wakubwa dhidi ya usalama wa nchi yetu.

Mnyororo huo ni kama ifuatavyo: Ushirikina na utapiahabari (disinformation) huleta ujinga, ujinga huleta magonjwa, magonjwa huleta umaskini, umaskini huleta unyonge, unyonge huleta vifo, vifo huleta mmomonyoko wa nguvukazi ya Taifa, mmomonyoko wa nguvukazi ya Taifa huleta kifo cha Taifa.

Hivyo, kila mtanzania anaalikwa kulinda Usalama wa Taifa letu kwa kuukata huu mnyororo wa kietiolojia ili kuliweka huru Taifa letu dhidi ya kifo. Njia nzuri ya kuua nyoka ni kugonga kichwa. Na kichwa cha mnyororo huu wa kietiolojia ni "Ushirikina na utapiahabari."

Tuanzie hapo na yeyote atakayejaribu kukwamisha kazi hii anapaswa kuwekwa pembeni kistaarabu. nchi yoyote dunia, na Tanzan ia ikiwemo, ni kubwa kuliko serikali yake. Aidha, nchi yoyote dunia, na Tanzan ia ikiwemo, ni kubwa kuliko mkuu wake wa nchi.

Na tano, ni wito kwa wanateolojia kuhusu mafundisho ya kidini yanayohamasisha ushirikina miongoni mwa waumini wake. Nitatumia mfano wa mvutano kati ya Rais Magufuli na baadhi ya viongozi wa dini.


Tamko la Padre Kitima lenye kuilalamikia uamuzi wa serikali wa kulikataza Kanisa kuchukua vipimo vya ugonjwa wa virusi vya korona kupitia vituo vyake vya afya, limekuja wakati ambapo Rais Magufuli anawatuhumu baadhi ya vioongozi wa dini kufanya maamuzi yanayopingana na imani wanayomfundisha yeye kama muumini wao.

Rais John Magufuli ni muumini wa Kanisa Katoliki. Anasema kuwa, viongozi wake wa dini wamekuwa wanafundisha kwamba, wakati wa mageuzi, mkate na divai hugeuka mwili na damu ya Yesu kiuhalisia; kwamba Yesu ni Mungu; na kwamba Mungu anaweza kufanya kila kitu.

Kwa hiyo, kwa mtazamo wa Rais Magufuli, kila muumini anayekula mwili na kunywa damu ya Yesu, hapaswi kuogopa ugonjwa wa virusi vya korona, kwani ndani ya maumbo ya mkate na divai kunapaswa kuwepo na kinga ya kimungu inayoweza kuua virusi vya korona. Hii maana yake ni kwamba, hakuna haja ya waumini wenye maisha mazuri ya kisakramenti kuvaa barakoa wala kutumia sanitaiza.

Lakini, kilichomshangaza Rais Magufuli ni kwamba, changamoto ya ugonjwa wa virusi vya korona imesababisha waumini wengi wenye maisha mazuri ya sakramenti kufa na kuwasukuma baadhi ya viongozi wa Kanisa Katoliki kufunga makanisa yao kwa muda.

Kwa hiyo, kuna mambi mawili yanawezekana. Ama wakati wa mageuzi (consecration) Yesu haingii katika maumbo ya mkate na divai tofauti na viongozi wa dini wanavyofundisha. Au wakati wa mageuzi (consecration) Yesu huingia katika maumbo ya mkate na divai kama viongozi wa dini wanavyofundisha, lakini huyo Yesu hana nguvu ya kufanya kila kitu kama viongozi wa dini wanavyofundisha. Ndio kusema kwamba, Yesu anayeingia katika maumbo ya mkate na divai anazo nguvu dhaifu kuliko nguvu za virusi vya korona.

Mpaka Padre Kitima anatoa tamko lake, bado Rais Magufuli alikuwa anaendelea kusisitiza kwamba, kuvaa barakoa ni dalili ya imani haba juu ya Mungu anayeweza kufanya kila kitu. Bila shaka, hii ndiyo sababu iliyomsukuma kuzuia vituo vya afya nchini kuchukua virusi vya korona.

Lakini, Padre Kitima anasema hapana. Hata kama viongozi wa dini wanafundisha kwamba Mungu anaweza kufanya kila kitu, bado kuna haja ya kuchukua vipimo vya kisayansi. Hili ndilo chimbuko la mgogoro kati ya Kanisa Katoliki na serikali inayoongozwa na Rais Magufuli.

Hivyo, natoa wito kwa wanateolojia. Kuna kila dalili kwamba, baadhi ya mafundisho ya kidini yanachochea ushirikina ambao unamfanya hata mkuu wa nchi kugeuka kituko. Kwa mfano, wakati wa ujenzi wa Kanisa kila altare ya Kanisa Katoliki inawekewa mifupa ya watakatifu. Nilimsikia Askofu aliyehubiri siku ya kuhamisha mwili wa Kardinali Rugambwa kuupeleka Kanisani alikozikwa akijigamba, "hata sisi huo ndio uchawi wetu."

Kuna maji ya mabaraka, chumvi ya baraka, kupunga pepo, sala ya mageuzi (consecration) ambako tunafundishwa kwamba Yesu anaingia katika maumbo ya mkate na divai kifiziolojia, na mambo kama haya.

Ni kwa sababu hizi, na sababu zinazofanana na hizi, baadhi ya waumini kama vile Rais Magufuli wanasema kwamba hostia takatifu na maombi ni silaha tosha dhidi ya korona. Wanateolojia wetu wanasemaje kuhusu changamoto hii, na wanatoa mwogozo gani kwa watu walioathiriwa na mafundisho ya Kanisa kwa kiwango hiki?

Naomba kuwasilisha hoja, na wote karibuni "Simbawanga" Primary School ninakofundisha.

MAREJEO MUHIMU YALIYOTUMIKA

  1. Bertrand Russel, The Impact of Science in Society (New York: AMS Press, 1968
  2. Helena Matute, et al, Scientific thinking and Illusions of causality: How they bias our everyday thinking and how they could be reduced, Journal of Frontiers in Psychology 2015, vol. 6 (July), p. 1-14.7.
  3. John Hagen, "Science and the Church." The Catholic Encyclopedia. Vol. 13. New York: Robert Appleton Company, 1912. (Accessed on 09 Mar. 2021).
  4. Pope John Paul II, Fides et Ratio (1998)
  5. Wikipedia, Magical thinking (Accessed on 09 March 2021).
  6. Wikipedia, Color blindness (Accessed on 09 Marh 2021).
  7. J. Dmitri Gallow (2017), Seminar Notes for Causality (Accessed on 09 March 2021).
  8. Ian G. Barbour, Religion in Age of Science (Harper Collins e-Books, 1991). (ATTACHED BELOW)
  9. Keith Ward, God, Faith and the New Millennium: Christian Belief in an Age of Science (Oxford: One World Publications, 2002). (ATTACHED BELOW)
  10. Caleb W. Lack, Jacques Rousseau, Critical Thinking, Science, and Pseudoscience: Why We Can’t Trust Our Brains (Springer Publishing Company, 2016). (ATTACHED BELOW)

    Mama Amon,
    Shule ya Msingi 'Simbawanga',
    Mkoa wa 'Simbawanga',
    Andiko la: 09 March 2021.
    Maboresho ya hivi karibuni: 14 March 2021.

 

Attachments

  • Religion in an Age of Science by Ian G. Barbour (z-lib.org).pdf
    2.8 MB · Views: 11
  • God, Faith, and the New Millennium Christian Belief in an Age of Science by Keith Ward (z-lib....pdf
    7.7 MB · Views: 11
  • Critical Thinking, Science, and Pseudoscience Why We Can’t Trust Our Brains by Caleb W. Lack, ...pdf
    5.3 MB · Views: 12
Padre alikiuka muongozo wa nchi kuhusu itifaki ya utoaji taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO. Tiini mamlaka za nchi kwa maana nazo zimetoka kwa MUNGU WA MBINGUNI
 
Nashangaa inakuwaje mwalimu wa shule ya msingi uko nondo hivi, hao watoto wetu huko darasani si unawapasua vichwa?

Nyaway, akili yangu imegota hapa hasa ukizingatia kama mwanasayansi mzuri ni yule anayeenda hatua moja zaidi mbele kujiuliza kwanini jambo fulani limetokea, hapo anaingia maabara kufanya tafiti ili kuja na jibu kamili zaidi.

Sasa inakuwa vipi kwa upande wa Corona ambayo mpaka leo bado tunaambiwa haina dawa, huoni mpaka kufikia hapo hii hypothesis nayo inakuwa ni null? means imefeli? sasa kama inatokea hivi kuna sababu yoyote ya kumpinga yeyote atakaekuja na njia yake ya kujitibu? nasema hivi kwasababu naona njia nyingi zinazokuwa applied now ni za kujikinga zaidi (barakoa, nyungu etc).

Pia nimejifunza kitu kumbe teolojia nayo ni sayansi, nilidhani inahusu mambo ya Mungu pekee, basi teolojia tukiita sayansi ya Mungu tutakuwa tumekosea? hapa ina maana kwamba inaruhusiwa wakati unamuomba Mungu kwenye jambo lako, lakini pia usisahau ku-apply njia za kujikinga nalo ambazo zimethibitishwa na wanasayansi, na hiki ndicho alichokifanya Father Kitima, Katibu Mkuu wa TEC.

Mwisho kabisa umetoa ushauri wako kwa TISS hapo sijui kama wanaweza kuufanyia kazi, kwasababu namna wanavyokuwa recruited siku hizi ni kama wanaokotwa tu, wanapeana kazi kwa kuangaliana huyu ni wa chama gani badala ya kuangalia IQ ya mtu, hili linasababisha hata kazi wanazofanya hao vijana ziwe nyepesi tu, sio za kuumiza vichwa vyao coz uwezo wa kufikiri hawana.
 
Padre alikiuka muongozo wa nchi kuhusu itifaki ya utoaji taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO. Tiini mamlaka za nchi kwa maana nazo zimetoka kwa MUNGU WA MBINGUNI
Ajabu!! Kutii mamlaka hata ikiwa OVU inalielekeza taifa kwenye shimo la mauti. Weka akili yako kichwani, vinginevyo kichwa chako na boga au tikiti vitakuwa na tofauti ndogo sana.
 
Asante sana kwa bandiko elimishi. Nadhani sasa hivi adui mkubwa wa Watanzania ni ushabiki wa kipuuzi ambao mtu anaweza kuibuka saa sita mchana na kutaka kutusadikisha kuwa huo ni usiku wa manane. Kuna ushabiki wa kisiasa ambao umefikia viwango vya upofu, tena upofu mbaya.

Haingii akilini baadhi ya wanasiasa na watendaji serikalini kukazania kuwa tatizo halipo ilhali kila uchao watu wanakufa kwa jinsi isiyo ya kawaida.

Hali hiyo imepelekea kuibuka kwa lile kundi lililoamua kushangilia hayo yatokeapo kama njia ya kujibu mapigo kwa wakana-ukweli. Hapo ndipo tulipofika Watanzania, inasikitisha sana.
 
Umeandika maelezo mazuri sana ya namna utafiti unavyofanyika kuanzia satage ya mwanzo kabisa inayohusiana na kitu ambacho huwa kina-trigger uwepo wa hypothesis (kuona). Hata hivyo umesahau kuandika chochote kuhusiana na "heading" au kichwa cha habari cha bandiko lako. Very good short notice on "scientific reaseach approach"
 
Back
Top Bottom