Tamko la LEAT juu ya Ripoti ya Kamati Maalum ya Rais kuhusu Mchanganyiko wa Madini katika Makontena

Rugemeleza

JF-Expert Member
Oct 26, 2009
668
136
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) imetoa tamko juu ya Ripoti ya Kamati Maalumu ya Raisi Juu ya Mchanganyiko wa Madini (Makinikia) katika Makontena yaliyozuiliwa bandarini. Tamko hilo limeambatanishwa hapa.

Kwa ufupi LEAT haishangazwi na kile kilichobainika kwani ni kile ilichokuwa inakisema miaka yote tokea mwaka 2001. LEAT inataka mabadiliko makubwa katika sekta za mafuta, gesi na madini kwani sheria zinazoziongoza zinaruhusu kuporwa kwa rasilimali hizi muhimu za nchi yetu.

Asanteni

Dr. Rugemeleza Nshala
Mkurugenzi Mtendaji
LEAT


========

TAMKO LA TIMU YA WANASHERIA WATETEZI WA MAZINGIRA KWA VITENDO (LEAT) JUU YA TAARIFA YA KAMATI MAALUMU YA RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO YA TANZANIA JUU YA UCHUNGUZI WA KIWANGO CHA MADINI
KATIKA MAKONTENA YA MCHANGA (MAKINIKIA) LEO TAREHE 24 MEI 2016

Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT) imepokea bila mshangao Ripoti ya Kamati Maalumu ya Rais iliyoundwa kuchunguza kiwango cha madini mbalimbali katika makontena yenye mchanga wa madini (Makinikia). Kutoshanganzwa kwetu kunatokana na ukweli kuwa yale ambayo Kamati imeyabaini ni mambo ambayo LEAT ilikuwa ikiyasema kwa sauti kubwa lakini yalipokelewa kwa kejeli kubwa na uongozi wa serikali za awamu ya tatu na ya nne. Pia kampuni za madini, zikiongozwa na Acacia ambayo kwa muda mrefu ilijulikana kwa jina la (Barrick Gold), zilitupinga na kutugeuza kuwa ni wanaharakati wenye ajenda ya siri dhidi ya wawekezaji.

Upingaji wetu hakuishia hapo ulipinga mfumo mzima wa kitaasisi na kisheria wa madini kwani unaruhusu kuporwa kwa rasilimali zetu na sisi kuendelea kuwa masikini wa kupindukia. Licha ya kuwa taasisi yetu inajulikana serikalini kuwa ina utaalamu mkubwa katika sheria za madini na mafuta, taasisi hii imetengwa na utaalamu wake haukubaliki serikalini kwani haukuendana na “mawazo nyonywaji” ya watendaji serikalini ambao wamehakikisha kuwa hatupewi hata nafasi ya kutoa maoni yetu kwake.

Hata pale taasisi yetu ilipofungua kesi kupitia kwa mwanachama wake juu ya mikataba yote ya madini, Serikali yetu kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iliweka pingamizi juu ya kesi hiyo na kusababisha kutupiliwa mbali kwake. Jitihada za kukata rufaa hadi hivi sasa hazijazaa matunda. Ni kesi iliyolenga kupigania masilahi ya nchi yetu lakini watendaji wanaolinda “mfumo nyonywaji” walipinga, na Mahakama Kuu (ya Juu) kwa kutojua kilicho mbele yake, ikabariki.

LEAT inapenda kusema kibaya sana ni kuona viongozi na watumishi serikalini hawaoni umuhimu wa kuhakikisha kuwa nchi yetu ndiyoi nakuwa mnufaika mkubwa na wa kwanza wa madini, mafuta, na gesi yake. Wamekuwa wakisisitiza “mwekezaji lazima apate faida” na “liwa ili ule”. Hawakuishia hapo wanaamini kuwa mfumo wa sasa wa kisheria na kitaasisi ni mfumo mzuri ambao mwisho wa siku utatunufaisha! Mfumo gani huu ambao unaruhusu kampuni hizi kushiriki katika udanganyifu wa bei “transfer pricing” na kuwa na urari mkubwa wa denimtaji (debt-equity ratio), mfumo mbaya wa ukaguzi wa madini (assaying), na mfumo mbovu wa kujadili mikataba ya madini (mineral development agreements (MDAs)) pamoja na mikataba ya ushiriki katika uzalishaji mafuta na gesi (production sharing agreements (PSAs))?

Kwa kipindi chote hiki, tokea mwaka 2001, LEAT imesema wazi kuwa Tanzania imegawa madini yake bure, na kibaya zaidi inawalipa wachukuaji (sio “wawekezaji” kwani huwezi ukawekeza katika madini) kuchukua madini yetu. Nchi yetu inawalipa wachukuaji hawa kwa njia ya misamaha ya kodi, vivutio vya uwekezaji (uchukuaji), na marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani. Tume ya Jaji Bomani ilionyesha wazi kuwa nchi yetu inaibiwa, matokeo yake ilikuwa ni kutungwa kwa sheria dhaifu sana ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Kinachouma ni kuwa sheria hii na kama ile iliyofutwa ya Madini ya Mwaka 1998 zilitungwa kwa mkopo na shinikizo la Benki ya Dunia.

Ni ukweli usiokwepeka kuwa mfumo mzima tulionao wa sheria za madini katika nchi zote za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara unatokana na Mkakati wa Madini wa Afrika wa Mwaka (Africa Mining Strategy) ya mwaka 1992 uliotaka serikali za nchi zote za Afrika kubinafsisha sekta ya madini, na kutoa vivutio na motisha za uwekezaji kwa kampuni hizo binafsi. Nchi za Afrika zilitakiwa kujikita katika kukusanya kodi na kutunga sera na sheria za sekta hiyo. Lakini zilitakiwa kuwa na uvumilivu kwani “uwekezaji” huu huchukua muda mrefu kutoa faida.

Aidha, Mkakati huu ulizitaka zising’ang’anie kujenga mitambo ya uchechuaji (processing and smelting) bali ziruhusu kampuni hizi kupeleka madini-ghafi katika mchanga kuchenjuliwa katika vinu vyao vya uchenjuaji nje ya nchi. Ndivyo walivyosema miaka ya 1960 na miaka ya 70 kwa Jamaica na Zambia. Nchi za Zambia na Jamaica hazikuwakubalia. Kwa hapa Tanzania tuliambiwa na kuaminishwai kuwa mchanga wa madini yetu hauwezi kuchenjuliwa kwani una kiwango kidogo cha madini na kuwa umeme wetu hauaminiki. Katazo hili lililenga kuyawezesha makampuni haya kutunyonya hadi wakia (ounce) na tani ya mwisho ya madini yetu.

Kutungwa kwa Sheria ya Madini ya 1998 kulifuatia ziara 17 za Wataalamu wa Benki ya Dunia kuanzia mwaka 1994 hadi 1997. Na sheria yetu iliandikwa kutokana na ile ya Zambia ambayo kampuni ya uwakili ya Clifford Chance iliiandika kwa kandarasi ya Benki ya Dunia. Ni kampuni hii, kwa kushirikiana na Kampuni moja ya uwakili hapa nchini, ndiyo iligeuza sheria hiyo ya Zambia kuwa sheria yetu ya Madini ya Mwaka 1998!

Baada ya malalamiko yetu na wadau wengine pamoja na Tume ya Jaji Bomani, Benki ya Dunia iliikopesha nchi yetu, mnamo mwaka 2009, dola milioni 56 kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya 1998 na kuandikwa kile kilichoitwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na “kuimarisha” taasisi za madini. Matokeo yake ni taasisi tulizonazo ikiwa ni pamoja na TMAA, ambayo kiongozi wake wa muda mrefu wa kwanza alikuwa ni yule yule Kamishina wa Madini aliyeondolewa hivi karibuni, ilifumbia macho uporwaji wa madini yetu. Sheria hiyo ya mwaka 2010 haina tofauti yoyote kubwa na ile ya Mwaka 1998 isipokuwa kuanzishwa kwa Bodi ya Ushauri ya Madini kwa Waziri kuchukua nafasi ya Kamati ya Ushauri! Kwa hiyo nchi yetu ilikopeshwa dola milioni 56 kutunga sheria nyingine mbovu ambayo imeendeleza kunyonywa kwake!

LEAT inasema kile Kamati Maalumu ya Raisi ilichobaini ni chembe ndogo sana ya ukweli, Tanzania imefukarishwa na kampuni hizi za madini na madini yake yamechukuliwa bure. Kibaya zaidi ni kuwa Tanzania, ambayo ni mzalishaji pekee wa Tanzanite, hainufaiki na madini haya. Mnufaikaji mkubwa ni Kampuni ya Tiffany ya Marekani ambayo mapato yake kila mwaka hayapungui dola za kimarekani milioni 600, huku nchi yetu ikiambulia dola za kimarekani milioni 13-16!

Haishangazi hata kidogo kampuni hizi zinapokuwa zimekomba madini yote huishia kutukabidhi mashimo kwa kisingizio cha kutupatia sehemu ya wanafunzi wetu wa madini kujifunza utaalamu, kuyajaza mashimo hayo maji na kuanzisha na kusema kuwa mashimo hayo yatakuwa mazalio ya samaki. Ndivyo ilivyofanya kampuni ya Resolute katika mgodi wa Lusu Nzega kwa kukikabidhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mgodi huo na kuyajaza mashimo maji ya mto eti watu wa Nzega wajipatie chanzo kipya cha mapato. Hawakuchukua hatua za kuyafukia mashimo hayo kama itakiwavyo kimazingira. Kampuni ya Acacia iliamua kuukabidhi mgodi wa Tulawaka kwa STAMICO baada ya kukomba madini yote na kuacha mabaki!

Ni kwa minajili hiyo LEAT inamtaka Rais na Serikali yake kufanya mambo yafuatayo:

1. Kuamuru kusimamisha na kujadiliwa upya kwa mikataba yote ya madini, gesi, na mafuta kwani ilijadiliwa na watendaji wasiojua au wasiojali thamani ya madini hayo na ina masharti mabovu sana kwa nchi yetu.

2. Kuundwa kwa Idara Madhubuti ya Wanasheria ndani ya serikali wanaohusika na masuala ya gesi, petroli na madini. Wanasheria hawa wafunzwe kanuni zote za sheria za mikataba, uwekezaji na majadiliano ya mikataba, madini, mafuta na gesi. Nchini Tanzania hakuna hata chuo kikuu kimoja kinachotoa mafunzo ya majadiliano (Negotiation). Ni wanasheria hawa wasio na utaalamu wa majadiliano ndio ambao tunawategemea kushiriki katika majadiliano ya mikataba au kutoa ushauri-elekezi kwa serikali juu ya mikataba na migogoro ya uwekezaji. Wenzao wa nchi za magharibi wanapokea mafunzo haya. Vyuo vikuu kama Harvard, Columbia, Yale, Berkeley, Georgetown vya Marekani hutoa mafunzo haya kwa wanasheria wao na ndio hao hujadili na wanasheria wetu wenye uelewa finyu wa masuala haya.

3. Serikali iunde Kamati Bobezi ya Wataalamu kuipitia mikataba yote ya madini na kuona udhaifu wake. Wataalamu wanaounda Kamati hii watoke ndani na nje ya serikali kwa kuiga mfumo wa Kamati ya Sera ya Uchimbaji Madini ya Botswana (Mining Policy Committee) na wawe watu wenye mapenzi na uaminifu usiotiliwa mashaka kwa nchi yetu. Kamati hii ndiyo iwe inajadili mikataba yote ya madini. Kamati hii iundwe na wachumi, wataalamu wa uwekezaji, kodi, madini, wanamazingira, na wanasheria wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara za Madini na Fedha. Kamati hii iwe ya kudumu kama ile ya Botswana na iwe na haki ya kutafuta ushauri wa kitaalamu ikiwa ni pamoja na kushirikisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.

4. Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na mabadiliko yake ya mwaka 2015 ipitiwe upya kwani ni sheria inayohalalisha uporwaji wa madini ya nchi yetu. Ni sheria ambayo ilipitishwa kwa shinikizo la Benki ya Dunia na kampuni hizi za kinyonyaji na ilikuwa na lengo la kupunguza malalamiko ya wanaharakati na taasisi kama LEAT zilizokuwa zinasema kuwa madini yetu yameporwa. Upitiaji wa sheria hii ujumuishe taasisi na wadau wote wa ndani ya nchi yetu na iandikwe na Watanzania wenyewe. Serikali ikatae “msaada” wowote ule wa mchakato wa uandikaji wa muswada wa sheria hii kutoka Benki ya Dunia au mataifa ya kibeberu kwani ajenda yao katika sekta hii ni kuwa kampuni za nje ndizo zenye haki ya kuchimba na kunufaika na madini yetu.

5. Uchimbaji na uchechuaji wa Tanzanite pamoja na utengenezaji wa bidhaa za mwisho za madini hayo lazima ufanyike Tanzania. Kampuni kama Tiffany ziambiwe kuwa ni lazima waanzishe viwanda vya utengenezaji vito na mapambo yatokanayo na Tanzanite nchini. Hivyo nchi yetu ndiyo iwe duka la bidhaa za Tanzanite na si Marekani kama ilivyo sasa.

6. Serikali izidai kampuni zote za madini zinazofanya shughuli zake nchini kulipa malimbikizo ya kodi na mrahaba wa madini ambayo hazikuyasema na kuyataja katika taarifa zao tokea zilipoanza kuchimba madini hapa nchini. Kampuni hizi zikishindwa basi ifute leseni zao mara moja.

7. Serikali ifute leseni za uchimbaji wa kwa kampuni zote za madini ambazo zimeshiriki katika udanganyifu huu. Hili kuondoa tuhuma ya kibaguzi serikali ifanye uchunguzi wa makontena yote ya madini kutoka katika makampuni yote ya madini ili kuweza kujua kiwango cha udanganyifu wao.

8. Serikali ifute nafuu zote za “uwekezaji” za uchimbaji madini zilizo katika Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali za Fedha ya Namba 27 ya Mwaka 1997, Sheria ya Mauzo ya Mwaka 1976 kama ilivyorekebishwa na nyinginezo nyingi. Sheria hizi zimebariki kuporwa kwa madini ya nchi yetu.

9. Serikali ipitie upya sheria za mafuta, Umuduji wa mapato ya mafuta na ile ya Tume ya Uwazi katika sekta ya Mafuta za mwaka 2015 ambazo zilipitishwa na Bunge la 9 bila hata ya kuwepo koramu (akidi) mwezi Julai 2015. Sheria hizi hazikujadiliwa kikamilifu na zilipitishwa kwa haraka na serikali iliyokuwa inamaliza muda wake na kukomoa wale waliokuwa wanaipinga.

10. Sheria ya Kodi irekebishwe na kuweka vifungu madhubuti vya kuzuia udanganyifu wa bei. Kampuni zote zitakazoruhusiwa kuchimba madini, mafuta na gesi lazima zitaje kampuni zao zote tanzu. Adhabu kwa kushiriki katika udanganyifu wa bei ni kufutiwa leseni ya uchimbaji na kulipwa kwa kiwango cha mara nne cha mapato yote yaliyotokana na madini hayo.

11. Serikali ishiriki katika uchimbaji wa madini kupitia kampuni zake na iwe na hisa katika kampuni mama zote zinazochimba madini. Serikali iige mfano wa Botswana wa kutoridhika na kuwa na hisa katika kampuni ya ubia kati yake na De Beers (Debswana) bali kuwa na asilimia 15 katika kampuni ya De Beers yenyewe. Hii imeiwezesha kuwa na taarifa sahihi za mapato ya De Beers na kuweza kudai kodi stahiki.

12. Migogoro yote inayohusiana na uchimbaji madini kati ya serikali na kampuni za nje za madini itatuliwa na mahakama zetu na sio mabaraza ya usuluhishi kama yale ya International Centre for Settlement of Investment Disputes(ICSID), International Chamber for Commerce (ICC) na London Court of International Arbitration (LCIA), kwani haya ni mabaraza yaliyoanzishwa kulinda masilahi ya kampuni za kigeni na si ya nchi yetu. Waamuzi wa migogoro hii hutokana na mawakili wa kampuni za nchi za Magharibi ambao hudai pesa nyingi kuamua migogoro hii. Nchi yetu isimamie kwa nguvu zote Kanuni ya Umiliki wa Milele wa Maliasili yake ambayo ni Azimio Namba 1803 la Mwaka 1962 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Azimio Namba 3281 la 1974 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Haki na Majukumu ya Kiuchumi ya Mataifa. Yote haya yanatamka bila shaka yoyote ile juu ya mamlaka ya nchi kuweka mfumo wa kuondoa unyonyaji katika maliasili na kuamua migogoro juu ya maliasili ikiwemo madini, gesi na mafuta.

13. Tanzania ijitoe katika Mikataba ya Usuluhishi ya Migogoro ya Kimataifa ikianzia na ule wa ICSID kwani unapingana na Maazimio Namba 1803 ya Mwaka 1962 na Namba 3281 ya Mwaka 1974. Nchi yetu lazima ipiganie, kulinda, na kutetea umiliki wake wa milele wa rasilimali zake. Aidha idai
kujadiliwa kwa mikataba yote ya pande mbili ya uwekezaji iliyosaini na mataifa yote ya (bilateral investment treaties) ambazo zinatoa haki kwa kampuni au raia wa nchi zilizosaini mikataba kufungua mashitaka katika mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya kimataifa kama ICSID, ICC, na LCIA.

14. Katiba ya Nchi yetu ifanyiwe marekebisho na kutamka wazi kuwa Tanzania ndiyo mmiki wa milele wa rasilimali zake zote za asili na kuwa uchimbaji wowote ule lazima ufanyike kukiwa na hakikisho la wazi kuwa Tanzania ndiyo itakayofaidika kwanza na uchimbaji huo.

Mwisho:
LEAT inatoa pongezi kwa Raisi Dk. John P.J. Magufuli kwa kuamuru kufanyika kwa uchunguzi huu. Aidha, inatoa pongezi kwa Kamati Maalumu ya I kwa kuonyesha kiwango cha udanganyifu. LEAT inaahidi kutoa ushirikiano wake pamoja na utaalamu wake katika masuala ya madini ikiwa pamoja na njia zitumiwazo na kampuni hizi kudanganya na kuziibia nchi zinazoendelea.

Pindi pale jitihada hizi za serikali zitakapopingwa na hata kusababisha kushitakiwa katika mabaraza ya migogoro ya usuluhishi wa mikataba LEAT itatoa ushirikiano hata kuweza kupata wanasheria wabobevu kutoka nje ya nchi kupambana na kampuni hizi. Wanasheria hao tunawajua na tunaweza kuwapata katika vyuo vyenye kuheshimika duniani kuweza kuitetea nchi yetu.

Tunachoirai serikali ni kuwa hatua zote za kisheria za kuvunja mikataba zifuatwe kwani uzoefu wetu katika Kesi ya City Water unatuasa kufuata kwa umakini wote taratibu za kuvunja au kusitisha mikataba.

Imesainiwa mjini Dar es Salaam leo tarehe 24 Mei 2017.
 

Attachments

  • TAMKO LA LEAT JUU YA RIPOTI YA KAMATI MAALUMU YA RAISI.pdf
    251.6 KB · Views: 75
[HASHTAG]#Serikali[/HASHTAG] ya [HASHTAG]#CCM[/HASHTAG] haistahili kuwepo madarakani..
Wametufikisha hapa tulipo kwa kupitisha miswada ya sheria za zima moto kupitia hati za dharura
 
Back
Top Bottom