Tamko la kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM (M) Mtwara

mcndomba maprosoo

JF-Expert Member
Apr 8, 2013
225
94
Kamati kuu ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Mkoa iliyokutana tarehe 21/11/2013 katika Ofisi ya CCM Mkoa pamoja na mambo mengine ilipokea na kujadili taarifa ya ununuzi wa korosho na harakati za vijana za kupinga dhuluma dhidi ya wakulima.

1. Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa inaupongeza Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa kwa ujasili wao na moyo wa kuwapigania wakulima wa korosho.

2. Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Mkoa inaungana na umoja wa vijana wa CCM Mkoa, kukemea vitendo vyovyote vinavyofanywa na bodi ya korosho Tanzania vinavyopelekea kuleta mkanganyiko miongoni mwa wakulima na kupelekea kutokea mwanya unaowezesha walanguzi wa korosho kuwalaghai wakulima na kuwadhulumu kwa kununua korosho kwa bei pungufu ya bei dira.

3. Aidha kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM mkoa inaungana na Umoja wa vijana wa CCM Mkoa kuwataka wajumbe wa Bodi ya Korosho wajipime na kuchukua hatua za kuwajibika.

4. Sambamba na hatua za ufuatiliaji wa mianya iliyopo katika mfumo wa stakabadhi ghalani, chama mkoa kinawaagiza viongozi na wanachama wote wa CCM kutojishughulisha na biashara haramu ya " Kangomba", (korosho nje ya utaratibu). Iwapo kiongozi yeyote atabainika kufanya hivyo atawajibishwa na taratibu za chama dhidi ya vitendo hivyo vitafuatwa.

5. Kamati ya siasa mkoa pia imeielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuandaa kikosi kazi maalumu ili kushughulikia taarifa zilizopo zinazoonyesha kuwa kuna wafanyabiashara wengi wa korosho wanaonunua korosho nje ya utaratibu wa stakabadhi ghalani. Rekodi zitolewe na mamlaka zilizopo ziangalie upya ili kugundua udanganyifu.

Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, wakati ikiwapa muda wajumbe wa bodi ya korosho Tanzania wajipime na kutafakari, imeunda kamati ndogo ya kamati ya siasa itakayoongozwa na ndg Mohamed Sinani mwenyekiti wa CCM Mkoa itakayokwenda kuonana na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kumfikishia kilio cha wakulima wa zao la korosho na matatizo yanayoigubika tasnia nzima ya korosho Tanzania mapema iwezekanavyo.

Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Mkoa, inawaomba vijana kuendelea kuwapigania na kumsemea mkulima kwa umakini kwa hali ya juu hasa kwa kuzingatia hali ya Amani na Usalama katika mkoa wetu.

Mwisho, CCM Mkoa wa Mtwara itaendelea kushirikiana na vijana na jumuiya zingine katika kuendesha siasa bila ya kuathili au kuwa chanzo cha uvunjifu wa Amani, bila kutoa mwanya kwa watu ambao hawapendi amani kujiingiza na kuvuruga amani iliyopo.

Imetolewa na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Leo tarehe 25/11/2013 na kusainiwa na ndg


Haroun R. Maarifa
KATIBU WA SIASA NA UENEZI
MKOA WA MTWARA
 
Back
Top Bottom