Tamaduni zetu za asili na zenyewe ni chanzo cha rushwa kutusumbua

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,487
13,612
Tamaduni za kiafrika ni zile ambazo kila mtu hutaka kumfurahisha na kuwa karibu na mfalme ( chifu, omwami na watu wa aina hiyo). Kwa miaka mingi sana jinsi waafrika tunavyoishi, tunafundishwa kwamba familia za machifu wetu, hutakiwa kuheshimiwa na kuonyeshwa upendo wa dhati.

Karibu makabila yote ya kiafrika huwa na tamaduni za kupeleka vitu vya thamani kwa familia za machifu, ikiwa ni kama alama ya kutoa shukrani na kuionyesha kujali, ile familia namba moja katika kabila aua ukoo fulani. Kwa wengine mwisho wa mwaka, hupeleka kwa machifu, yale majogoo makubwa kabisa, hupeleka mbuzi waliyonona, kondoo pamoja na ng'ombe wenye afya nzuri. Lengo ni lile lile ambalo limetokana na tamaduni zetu, yaani heshima kwa familia au nyumba (mji) ya chifu.

Ubaya ya mfumo wa aina hii wa maisha ni kwamba, hata baada ya wazungu kuondoka na kutuachia afrika yetu, bado hatujaweza kutambua kwamba machifu wa nyakati hizi ndio viongozi wa serikali ambao wamegeuka kuwa maadui wa wananchi kwa sababu ya ufisadi. Mfanyakazi wa shirika la kiserikali ambaye babu zake walifundishwa kupeleka kuku au Ng'ombe nyumbani kwa chifu, anajiona kama vile anao wajibu wa kumpendezesha mkurugenzi mkuu wa shirika. Kwenye harusi ya mtoto wa mkurugenzi wa shirika, atatafuta zawadi ya bei kubwa sana ili mradi aweze kupeleka kile kilichonona kwa chifu wake. Lakini chifu wake ambaye ni mkurugenzi na yeye anajiona ana haki ya kufanana na yule chifu wa miaka ya nyuma, huku akisahau kwamba kwa sasa yeye ni mtumishi wa umma.

Mazingira ya aina hii ndio yanaifanya rushwa iendelee kuwepo, ni mfumo wetu wa kimaisha ambao tunashindwa kutambua kuwa umeshaleta athari ndani ya mitazamo yetu ya maisha ya kila siku. Hawa ambao kwa sasa wanatumbuliwa majipu, ni watu ambao tamaduni zetu za maisha zimewafanya wakajiona kama vile wao ni warithi wa machifu na watemi wa miaka ya nyuma.

Maprofesa wa vyuo vikuu vyetu, wanayo kila sababu ya kufundisha wanafunzi wao, juu ya mabadiliko ya kimaisha, yaani namaanisha kuwafundisha watumishi wa baadae wa serikali, ule umuhimu wa kuondokana na hizi tamaduni zetu wakati wakiwa ni waajiriwa wa taifa. Ni kitu kinachowezekana, wala haina maana kwamba tumezidharau tamaduni zetu, bali ni katika kuwekana sawa, ili miaka kadhaa ijayo Tanzania iwe ni nchi itakayokuwa imesahau kuhusiana na uwepo wa majipu mapya.
 
Back
Top Bottom