TAKUKURU yamkamata mtumishi wake Zainabu Mohamed Jabir kwa kuomba rushwa ya Tsh milioni 50

Unaweza kudhania ni hadithi, lakini ndio ukweli wa mambo.

-
AFISA WA TAKUKURU AKAMATWA KWA KUOMBA RUSHWA YA SHILINGI MILIONI 50

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo, napenda kuufahamisha umma kwamba, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imekuwa ikiendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini, kama yalivyotamkwa na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Kupitia majukumu haya, tumekuwa tukiuhabarisha umma juu ya mafanikio mbalimbali yanayotokana na utekelezaji wa majukumu haya ikiwa ni pamoja na kuwahabarisha juu ya watumishi wa umma wanaokamatwa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Kama mtakavyokumbuka, wiki iliyopita kupitia ofisi yetu ya TAKUKURU mkoa wa Arusha tumewakamata Askari Polisi 7 waliodaiwa kudai rushwa ya Shilingi Milioni 200 kutoka kwa Mfanyabiashara mmoja wa jijini Arusha na kupokea shilingi milioni 100, lakini pia kupitia ofisi yetu ya TAKUKURU mkoa wa Manyara, tulimkamata Mwendesha Mashitaka wa Mkoa wa Manyara kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa ya Shilingi Milioni 5 kutoka kwa watuhumiwa wa makosa ya Jinai.

Ndugu waandishi wa Habari,
Kupitia taarifa hii ya leo, tunaujulisha umma kuwa tumemkamata Mtumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU aitwaye ZAINAB MOHAMED JABIR, kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa – Kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Mtumishi huyu aliomba rushwa kiasi cha shilingi Milioni 50 kutoka kwa mtu mmoja (Jina limehifadhiwa) kwa madai ya kumsaidia mtu huyo katika tuhuma dhidi yake ambazo zinachunguzwa na TAKUKURU. Uchunguzi dhidi ya tuhuma hii unaendelea na utakapokamilika hatua stahiki zitachukuliwa.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Vilevile, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, napenda kuzungumzia kuhusu uwepo wa tabia ya baadhi ya watu wanaofanya UTAPELI kwa kujitambulisha kwa vyeo tofauti tofauti ikiwemo Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU.

Matapeli hawa wamekuwa wakipiga simu na kujitambulisha kuwa wao ni Maafisa wa TAKUKURU wakiwaeleza watu hao kwamba tuhuma zao zipo TAKUKURU na kwamba wanawaita TAKUKURU kwa ajili ya mahojiano.

TAKUKURU inawapongeza wale wote walioweza kubaini kuwa watu hawa ni MATAPELI na kutoa taarifa TAKUKURU mara moja. Hata hivyo, tunaendelea kusisitiza wananchi kutokubali kutapeliwa na mtu yeyote. Unapopokea simu ya aina hii tafadhali fika katika ofisi ya TAKUKURU iliyoko karibu nawe kwani TAKUKURU ina ofisi katika mikoa yote na Wilaya zote Tanzania Bara.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, tunaendelea kuwashukuru wananchi na wadau wengine wote ambao wamekuwa wakishirikiana nasi katika kufanikisha jukumu hili la kuzuia na kupambana na rushwa nchini kwa kutuletea taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.


IMETOLEWA NA:

DOREEN J. KAPWANI
AFISA UHUSIANO
KWA NIABA YA MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU

Huyu anawakilisha idadi kubwa sana ya wafanyakazi wa takukuru.
 
Back
Top Bottom