TAKUKURU yaimulika bodi ya mikopo kwa kujilipa shilingi Bilioni 15 kama posho za 'ukarimu'

kirerenya

JF-Expert Member
Aug 27, 2013
1,696
2,252
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inafanya uchunguzi dhidi ya vigogo na maofisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wanaotuhumiwa kutafuna mabilioni ya shilingi kutokana na mbinu mbalimbali ikiwamo ya kujilipa posho ya ukarimu, imefahamika.

Agosti 31, mwaka jana, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikipitia taarifa za fedha za bodi hiyo kwa mwaka 2014/15, ilibainika imetumia Sh. bilioni 15 kwa shughuli za uendeshaji huku kiasi kikubwa kikiwa posho.

Kutokana na 'madudu' hayo, kamati hiyo iliitaka bodi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha ulipaji wa posho
unazingatia sheria na miongozo ya serikali.

Kabla ya kupitiwa kwa taarifa za fedha za bodi hiyo na PAC Februari 16, mwaka jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.
Joyce Ndalichako, alitangaza kusitisha mkataba wa ajira wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega, pamoja na kuwasimamisha kazi wakurugenzi watatu kutokana na kile alichokieleza siku hiyo kuwa matatizo ya kiutendaji na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanyika ndani ya bodi hiyo.

Prof. Ndalichako alisema taasisi hiyo imeonyesha utendaji usioridhisha kiasi kwamba kumekuwa na matatizo mengi na yanayojirudiarudia kwa wateja wao.

“Mikopo kwa wanafunzi imekuwa ikichelewa kuwafikia bila sababu za msingi kiasi kwamba imejengeka taswira kwa wanafunzi kwamba hadi walalamike wizarani ndipo matatizo yao yashughulikiwe, hivyo tatizo si ukosefu wa fedha bali ni uzembe wa watendaji katika kuwapatia wanafunzi mikopo yao kwa wakati," Prof. Ndalichako alisema.

Watumishi wa bodi hiyo waliosimamishwa kazi siku hiyo ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusuph Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.

Prof. Ndalichako alizitaja baadhi ya sababu za kufukuzwa na kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kuwa ni kufanya malipo yasiyo sahihi kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma ndani na nje ya nchi pamoja na udhaifu uliobainika katika mifuko ya fedha.

Wakati Prof. Ndalichako akichukua hatua hiyo, Takukuru nayo imekiri inaichunguza taasisi hiyo yenye jukumu la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kusimamia urejeshaji wa mikopo hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Nipashe ilimtafuta jijini Dar es Salaam Ofisa Uhusiano na Habari wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, ambaye alikiri kuwa wanaichunguza taasisi hiyo kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa na ufisadi zinazowakabili vigogo na maofisa wake.

"Si hilo tu (la posho za mabilioni ya shilingi), tuna mambo mengi ambayo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu tunaichunguza. Wana tuhuma nyingi ambazo tunazifanyia kazi ili wahusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa," alisema Misalaba.

Hata hivyo, Misalaba hakuwa tayari kuziweka wazi tuhuma zingine ambazo vigogo na maofisa wa HESLB wanachunguzwa nazo.

Lakini habari za uhakika ambazo Nipashe inazo, Takukuru inachunguza pia HESLB kwa malipo ya mikopo kwa wanafunzi hewa na ulipaji wa mikopo mpaka minne kwa mwanafunzi mmoja.

POSHO YA UKARIMU

Agosti 31, mwaka jana, wakati PAC ikipitia hesabu za HESLB kwa mwaka 2014/15, ilibaini ulaji kupitia matumizi ya bodi hiyo yanaofikia Sh. bilioni 15 kupitia mbinu mbalimbali ikiwamo ya kulipana posho kufuru, mojawapo ikipewa jina la 'posho ya ukarimu'.

Kutokana na matumizi hayo, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walihoji kwa nini bodi hiyo isivunjwe na majukumu yake kutekelezwa na moja ya benki nchini.

Katika kikao cha kupitia hesabu za HESLB, baadhi ya wajumbe walionekana kuwa wakali wakisema wakati wananchi wanaumia kulipia kusomesha watoto wao, bodi hiyo ambayo kipindi hicho ilikuwa na watumishi 144 pekee, inatumia mabilioni ya shilingi kufanya mambo yasiyo ya msingi.

Baadhi ya posho zilizowakera wabunge hao ni pamoja na ile iliyopewa jina la posho nyinginezo (other payroll allowance) ambayo mwaka 2014/15 ilikuwa Sh. milioni 999.45 kutoka Sh. milioni 762.96 mwaka 2013/14.

Posho nyingine inayoitwa posho maalum (special allowance) kwa mwaka 2014/15 ilikuwa Sh. milioni 582.05 kutoka Sh. milioni 463.96 mwaka uliotangulia.

Kwa upande wa safari za ndani ya nchi, kwa mwaka 2014/15 Sh. milioni 979.5 zilitumiwa wakati mwaka 2013/14 zilitumika Sh. milioni 665.09.

Safari za nje ya nchi kwa mwaka 2014/15 zilitumia Sh. 697.38 na mwaka 2013/14 zilitumia Sh. milioni 564.22.

Posho nyingine iliyowashatua wabunge hao ni ile ya ‘uhusiano na ukarimu’ (relationship and hospitality allowance) ambayo kwa mwaka 2014/15 ilikuwa Sh. milioni 296.77 kutoka Sh. milioni 243.64 mwaka 2013/14.

Walihoji pia sababu za ada ya ukaguzi kupanda kutoka Sh. milioni 61.7 mwaka 2013/14 mpaka Sh. milioni 330.56 mwaka uliofuata.

Jambo lingine lililowashatua wabunge hao ni matumizi makubwa ya bodi ya wakurugenzi ya HESLB, ambayo kwa mwaka 2013/14 ilikuwa Sh. bilioni 1.16 na mwaka uliofuata ikawa Sh. milioni 832.52.

Pia kitabu cha hesabu za bodi hiyo kilionyesha fedha kwa ajili ya likizo kwa mwaka 2014/15 ni Sh. milioni 294.21 na mwaka 2013/14 Sh. milioni 311.35.

Kwa upande wa fedha za maziko na rambirambi kwa wafanyakazi na watu wao wa karibu, kwa mwaka 2014/15 zilikuwa Sh. milioni 45.2 kutoka Sh. milioni 54.46 mwaka 2013/14.

Wabunge hao pia walihoji matumizi ya kawaida ya menejimenti ya bodi kuwa Sh. milioni 526.71 mwaka 2014/15 na kwa mwaka 2013/14 Sh. milioni 684.3.

Vilevile walihoji sababu ya matumizi ya jumla ya bodi hiyo kupanda kutoka Sh. bilioni 1.06 mpaka Sh. bilioni 1.15 mwaka 2014/15 ambalo ni ongezeko la takribani Sh. milioni 90.

Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM), alisema matumizi hayo ya bodi ya wakurugenzi ni ya kutisha ikizingatiwa ina wafanyakazi 144 lakini wanatumia kiasi hicho cha fedha wakati Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (wakati huo) yenye zaidi ya watumishi 3,000 kwa mwaka matumizi yake yasiyo ya maendeleo ni Sh. bilioni 12 pekee.

“Kwa mfano, bodi hii ingekuwa ndiyo Wizara ya Kilimo, fedha kwa ajili ya matumizi mengineyo pekee ingepaswa kuwa Sh. bilioni 200," alisema.

Kakunda ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), alishangaa pia bodi hiyo kutumia mabilioni ya shilingi ilhali ukusanyaji wake wa madeni kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu umeshindwa kuleta ufanisi na badala yake hasara.

Katika kikao hicho, Mbunge wa Viti Maalum, Sally Raymond (CCM), alisema ni lazima Rais John Magufuli apewe taarifa na ajue matumizi hayo mabaya ya fedha yanayofanywa na bodi hiyo huku watoto wa maskini wakiumia.

“Ukiangalia hayo matumizi ya misiba na nini, yaani tu kweli kununua majeneza na zile kadi za 'Rest in Peace' ndiyo pesa zote hizo mnatumia na idadi hiyo ya wafanyakazi mliyonayo?” alihoji.

Katika majibu yake kwa PAC siku hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema wameona kuna matumizi yasiyo ya lazima na tayari kuna baadhi ya posho wamezisimamisha.

Alisema wataendelea kupitia posho wanazolipa kwa watumishi wao ili kuona ni nani anapaswa kulipa kiasi gani na kwa kazi gani.

“Ukijaribu kuangalia tu kwenye matumizi makubwa hivi unajua kuna shida. Sasa tutaendelea kuangalia mfumo wa bodi yetu ulivyo kama unafaa au kuna cha kubadilisha, pia kuangalia baadhi ya vitengo tutaviunganisha ili kuleta ufanisi na kupunguza matumizi,” alisema.

TRILIONI 2.6/- WADAIWA SUGU
Baada ya kamati hiyo kujadili taarifa ya HESLB, Mbunge wa Vwawa, Japheth Hasunga, ambaye siku hiyo alikuwa mwenyekiti wa kikao, alitangaza maazimio matatu ya kamati yake ikiwa ni pamoja na kuitaka bodi hiyo kupuunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha ulipaji wa posho unazingatia sheria na miongozo ya serikali.

Pia aliagiza kuwe na mipango endelevu ya ukusanyaji mikopo ambayo inatolewa kwa wanafunzi na kwamba deni la Sh. trilioni 2.6 ambalo bodi inadai kwa wanufaika mbalimbali wa mikopo lichanganuliwe kwa umri wake.

Hasunga ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema azimio la tatu ni bodi hiyo kuhakikisha inaandaa utaratibu wa kuwatambua wadaiwa wake na kujua sababu za wao kutolipa madeni yao.

Chanzo: Nipashe
 
Jamani eeeh! kesi au matukio mengine huishia wapi? Bodi hii na kero zake haikutakiwa kuachiwa tu!
 
Hua nacheka sana nisikiapo kamati ya bunge inakerwa na "posho", wakati huohuo wao kama wabunge ukigusia tu posho zao basi ni vita.
 
Back
Top Bottom