TAKUKURU kuwaburuza Mahakamani Vigogo wa Halmashauri ya Shinyanga

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, inatarajia kuwafikisha mahakamani watumishi wa halmashauri, kwa tuhuma za kugushi nyaraka za manunuzi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Francis Luena, ametoa taarifa hiyo leo kwa vyombo vya habari mkoani hapa, ambayo ni ya kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 kuanzia Januari hadi Machi.

Luena, amemtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni Godfrey Mwagairo, ambaye alikuwa Mkuu wa Kitendo cha Manunuzi Manispaa ya Shinyanga, kuwa aligushi nyaraka za uongo, na kusababisha bodi ya zabuni kutoa kazi kwa Kampuni ya EMC System, ya kuweka mfumo wa mtandao kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo bila ya ushindani na kujipatia Sh. milioni 43.2.

Amemtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Edward Maduhu, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kuwa ana kabiliwa na kesi ya kumdanganya mwajiri wake juu ya usambazaji wa Pembejeo za Kilimo na kujipatia Sh.milioni 3.4.

"Kesi ya mtuhumiwa wa kwanza aliyekuwa mkuu wa kitengo cha manunuzi Manispaa ya Shinyanga bwana Godfrey Mwagairo, atashitakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi," amesema Luena.

"Mtuhumiwa wa pili Edward Maduhu, atashitakiwa kwa kosa la Jinai, ambapo huyu yupo na wenzake watatu ambao ni wafanyabiashara walioshirikiana naye kugushi nyaraka za kusambaza Pembejeo kwa wakulima katika kijiji cha Ibubu na Mwabundala,"aliongeza.

Aidha amewataja wafanyabiashara hao, ambao walishirikiana na Maduhu kugushi nyaraka hizo za usambazaji wa Pembejeo, kuwa ni Emmanuel Ipandu, Adam Kilimbi, na Wang Wei ambaye ni Raia wa China, na kubainisha wote watafikishwa mahakamani na sasa wapo chini ya ulinzi.

Katika hatua Nyingine Luena, amesema, kwa kipindi hicho cha kuanzia Januari hadi Machi, walipokea taarifa 41 za masuala ya Rushwa, ambapo baadhi zimekamilika na nyingine bado zipo kwenye uchunguzi, huku akitaja Serikali za mitaa ndio kinara kwa taarifa hizo.

Chanzo: IPP MEDIA
 
Back
Top Bottom