Taifa linalotaka maendeleo, ni lazima lizingatie uadilifu

Elius W Ndabila

JF-Expert Member
Jul 17, 2019
322
645
TAIFA LINALOTAKA MAENDELEO, NI LAZIMA LIZINGATIE UADILIFU

Na Elius Ndabila
0768239284

Mjadala unotawala hivi sasa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii nchini, ni kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo imeibua mambo mengiambayo yanaonyesha kwamba baadhi ya watumishi wa umma siyo waaminifu.

Kumekuwepo na malalamiko mengi ambayo yamethibitishwa na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi mabaya ya fedha umma hususani kwenye Halmashauri zetu. Mara nyingi ubadhirifu juu umetokana na maamuzi mabaya ya Halmashauri zenyewe na mara nyingine kutokana na kutojali kwa watumishi wa Halmashauri zetu. Matokeo ya ubadhirifu huu yamekuwa yakidhoofisha Halmashauri husika; kudorora kwa huduma muhimu kwa wananchi na kupoteza imani ya wananchi kwa Serikali yao, na hivyo kususia wajibu wao wa kulipa kodi na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii.

Suala la uwajibikaji limekuwa linazungumzwa zaidi kuliko kutekelezwa. Fikra zilizotanda kwa walio wengi ni kwamba wanaopaswa kuwajibika kutokana na matokeo ya utendaji wao ni watumishi peke yao. Utaratibu wa viongozi kutoa taarifa kwa wapiga kura wao kuhusu utendaji wao ni jambo la nadra sana, na kwa wengi halipo kabisa. Pia si jambo la kawaida kuona kiongozi kwa hiari yake akikubali kuwajibika kwa maamuzi yake ambayo yameleta madhara makubwa kwa wananchi. Kinachoonekana zaidi ni utetezi usio na mwisho wala msingi wowote pindi wananchi wenyewe wanapoamua kuchukua hatua.

Ripoti za mara kwa mara za CAG zinaonyesha kuwa bado misingi ya utawala bora haijaimalika. Upotevu na uvujaji kiholela wa mali za umm ani kuomyesha kuwa kuna mahali kuna mianya ambayo wakwapuaji hao huitumia. Utawala bora ndiyo tiba ya kila jambo. Sifa ya utawala bora ni lazima kuwe na:-

Uwazi ni hali ya kuendesha shughuli za umma bila usiri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria. Uwazi unajumuisha, Wananchi kupata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo, kwa lugha rahisi na kwa wakati pia Wananchi kupewa taarifa za mapato na matumizi ya kila fedha inayotengwa na serikali.

Wananchi kufahamishwa huduma zinazotolewa bila malipo na huduma wanazopaswa kuchangia, na utaratibu wa kupata huduma hizo. Sambamba na hilo Wananchi kujulishwa mahali na wakati muafaka wa kupata taarifa wanazozihitaji na wazipate bila usumbufu kutoka kwa viongozi toka ngazi ya mtaa.

Kwenye utawala bora ni lazima kiongozi kuwa tiyari kuwajibika kwa masilahi mapana ya nchi. Uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa. Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa wananchi. Lakini je Wakurugenzi na Watendaji wanafanya hivyo?

Ili kuondokana na tabia za ufujaji wa mali za umm ani lazima kuzingatia nguzo ya usawa katika utawala bora. Usawa Ni hali ya kuwapatia wananchi wote fursa sawa katika kushiriki kwenye mambo yanayohusu jamii yao kama Kutoa huduma bila ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote,Kuendesha shughuli za umma bila ubaguzi ,Kuthamini watu wote bila kujali tofauti zao. Kutambua makundi yote katika jamii na kutoa fursa sawa kwa makundi yote katika kuboresha hali zao na Kumfanya kila mwanajamii kujiona kuwa yeye ni sehemu ya jamii na pia ana maslahi kwenye jamii yake.

Lazima kuzingatia ufanisi katika kufanya kazi. Ufanisi na tija ni hali ya utendaji inayozalisha matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu na kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali. Ufanisi na Tija unajumuisha mambo mengi kama vile Utendaji wenye matokeo yanayokidhi malengo na matarajio ya watu wote na pia Kutumia rasilimali kwa uangalifu na umakini (Matumizi bora ya rasilimali).

Ufanisi wa kazi yoyote ile ni lazima iwe na maridhiano .Utawala bora unahimiza kukutanishwa kwa mawazo mbalimbali ili kupata suluhu au maamuzi ya pamoja ambayo yanazingatia matakwa ya jamii nzima. Zaidi ya yote ni uadilifu hali ya kuwa mwaminifu na kuwa na mwenendo mzuri katika utendaji kazi. Uadilifu unahusisha kujali watu, kujali muda, kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kuepuka vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, kuwa mkweli, kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Viongozi wengi wanapopata uongozi au nafasi za kuwasaidia viongozi basi uadilifu unapotea. Uadilifu unapopotea ndipo wanapoanza kutumia fedha za umma bila nidhamu kwa kuwa wanaamini kwenye kujirundikia mali na si katika kuleta jita na matokeo kwenye maeneo waliyoaminiwa. Taifa lolote duniani linalotaka kupiga hatua kubwa ya maendeleo ni lazima kuzingatia uadilifu. Uadilifu ndiyo msingi wa maendeleo.

Kwenye utawala bora ni lazima mifumo yote ya nchi ifanye kazi sawia. Mifumo ya nchi ni sawa na viungo vya binadamu kwenye mwili, kiungo kimoja kinapokosekana basi viungo vingine vyote haviwezi fanya kazi kisawa sawa. Mifumo ya nchi kwa upana wake inatawaliwa na mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.

Mhimili mmoja usipofanya kazi sawa sawa basi ni sawa na binadamu kupoteza macho na kushindwa kuona, kupoteza miguu na kushindwa kutembea au kupoteza masikio na kushindwa kusikia. Lakini viungo vyote vikiwa sawa sawa basi kiula jambo binadamu atalifanya kwa ufanisi.

Wakati mwingine wananchi wa kawaida ndio wamekuwa wanatengeneza nyufa hizi za ubadhilifu. Kwa mfano miradi mingi inayoonyeshwa kwenye ripoti ya CAG inatekelezwa kuanzia ngazi ya chini kabisa. Je kama ni madarasa wananchi waliona yanajengwa chini ya kiwango walitoa taarifa kwenye mamlaka za juu?

Jukumu la Mwananchi mwenye uzalendo wa kweli na anayeipenda nchi yake huwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa, bila woga wowote. Uzalendo ni kuitetea nchi hadi kujitoa kufa kwa ajili yake huku ukitetea haki, utamaduni, mali za nchi pamoja na mambo yote yanayowafanya kuwa wamoja katika taifa.

Bila kumnyooshea kidole mtu mwingine mwananchi unatakiwa kuchukua hatua pale unapoona mtu anavunja sheria, kwa kupokea rushwa au kwenda kinyume na maadili ya kazi. Katiba ya nchi Ibara ya 26 (2) “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya katiba na sheria za nchi”

Kuwa mzalendo ni zaidi ya kuifia nchi yako. Kwa sababu aidha kwa uzembe au kwa ujinga au kwa imani yake mtu aweza kufa lakini kumbe hakuipenda nchi ila kwa matakwa yake binafsi. Shinikizo la kuifia nchi ni lazima liwe tunda la uaminifu, upendo kujitoa, kuipigania na kuitetea nchi yako. Wako wazalendo ambao wameitetea nchi yao toka utotoni, ujanani na uzeeni na hawakuifia nchi.

Watu wasio wazalendo ni hawa hapa: watu wanaoihujumu nchi kwa kuiba, kutumia rasilimali za nchi viabaya, kuharibu miundo mbinu, kuweka pesa nje ya nchi, kuisema vibaya nchi na viongozi au watu wake, kushabikia wizi na ufisadi, kuvunja sheria za nchi, kuthamini vitu na mambo kutoka nje, nk.

Unaweza kweli ukawa Mzawa, mwaminifu, mkweli lakini unakuwa kimya watu wanapoiba na kutumia vibaya rasilimali za nchi, wewe pia sio mzalendo kwa mfano huo. Kila mtu kwa nafasi yake analojukumu kuwa la kutafsiri utawala bora kwa kutanguliza uzalendo.

Inasikitisha unapoona hata vijana wadogo walioaminiwa na mamlaka kuwa kwenye tuhuma za kuhisiwa kuto kuzitumia vizuri ofisi zao na kuwa harafu ya Rushwa. Ni ndoto kufikia mapinduzi makubwa ya kiviwanda kama tunaoaminiwa hata kwa nafasi ndogo na viongozi wetu tunakimbilia kuiba ili kujipa utajiri badala ya kuisaidia nchi kuwaletea wananchi maendeleo.
 
Back
Top Bottom