Taifa Lilivyotamalaki Dodoma!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,473
39,986
ZIMEPITA wiki kadhaa sasa tangu matukio muhimu yatokee kule Dodoma yaliyosababisha kutetemeka kwa wenye nguvu na kudondoka kwa walio mahiri.

Matendo yale makuu yatakayobakia kusimuliwa kwenye historia yetu hayana budi kutungiwa tenzi na nyimbo na kupambwa kwa ngoma zirindimazo. Na miye mzee wenu kama kawaida naliacha jambo lipite kidogo ili niweze kulitolea maoni yasiyo ya kihisia.

Ndugu zangu, kilichotokea Dodoma siku ile Waziri Mkuu, Edward Ngoyai Lowassa, alipojiuzulu, ni kitu ninachoweza kusema ni kutamalaki kwa taifa letu.

Ndiyo. Taifa letu lilitamalaki Dodoma na wengi wetu tulifurahia kwa shangwe. Taifa liliinuliwa juu zaidi ya chama cha kisiasa, majina ya watu, na kwa hakika juu ya majigambo ya wanasiasa na wapambe wao.

Wako wapi basi leo hii wale mashujaa waliotamba bungeni! Ati kwamba wanafaa kwa nini hatuwaoni? Wale waliosema ni mahiri na ya kuwa ni mahodari? Wamedondoka, wamepinduka, wamejikwaa na kutua chini pwaa! Taifa limetamalaki, wananchi na tufanye shangwe.

Niacheni leo niimbe sifa za taifa langu, niacheni nitambe kwa ajili ya heshima ya watu wangu, niacheni nitunge na tenzi kuisifia Tanzania. Na ijulikane kwa watu wote wa kizazi chetu na kile kijacho, walio karibu na walio mbali, waliokwisha zaliwa na wale wajao; kwamba kashfa ya Richmond ilituonyesha kwa mara ya kwanza kwamba Watanzania tukitaka tunaweza.

Suala la Richmond lingeweza kuisha kimya kimya kama wananchi wangekubali maelezo ya wanamazingaombwe wa serikali. Kama tungekubali Richmond ifanye itakavyo na tusiwahoji na hivyo kuwakubalia ufisadi, leo wangeendelea kutamba na kutanua, wangeendelea kula na kutafuna kama mchwa. Lakini tuliwakatalia - Tukawahoji, tukawauliza, na tukawaandama kwa maswali yenye kuliza. Wakatupuuza wakadhani tutasalimu amri na kuweka manyanga chini kwa woga!

Hatukukubali na wala kupiga magoti na kuwaomba radhi watawala wetu. Tukawafuatilia na kuzidi kuwahoji. Na hatimaye ‘kilipoiva’ wakajikuta hawana jinsi isipokuwa kuungana na Watanzania wengine kuhoji suala la Richmond. Mizengwe ikaletwa, tarehe zikapigwa na mikwara ikarushwa “msiijadili Richmond” lakini siku ya kufa nyani miti yote huteleza!

Na ikaundwa Kamati ikiongozwa na mwana wa Tanzania na mzalendo Dk. Harrison Mwakyembe na timu nzima ya wabunge mahiri kina Lucas Selelii, Mhandisi Stella Manyanya, Mohamed Habib Mnyaa na James Mntangi wakasimama kinyume na nguvu zote zisimamazo! Wakaliinua taifa lao na bila woga wakaenda kule ambako wengi wanaogopa kwenda; kama vile msitu wa ‘Usiku wa Balaa’ na kama vile waliotumwa kwenye kuleta ‘Salamu toka Kuzimu’ walikwenda wakijua wanakwenda kukutana na ‘Malaika wa Shetani’. Hawakuogopa wakaenda kufanya walichotumwa na taifa lao.

Sijui ni vitisho gani walivipokea wakati wa uchunguzi na hasa baada ya uchunguzi, lakini kwa vyovyote vile sidhani kama walipata simu za pongezi tu na mikono ya heri. Siwezi kushangaa kuwa walipewa hata ‘ofa’ za nguvu za kubadilisha ripoti. Watanzania hawa waliokula kiapo kufanya kazi yao kwa uadilifu hawakugwaya. Wakasimama na kujiandaa na makombora yote wakiweka nafsi na roho zao mikononi mwa yule aliyejuu sana! Wakafanya kazi zao.

Hata siku zilipokaribia mchecheto ulianza kuwakumba wahusika; wakajitahidi watu kuitafuta ripoti hiyo waone kilichomo; wakadhani wameipata; wakafurahia kuwa ndani yake hakuna kitu wakajipongeza kuwa “hakuna jipya”.

Na siku ya siku ikafika. Ndipo ripoti yenyewe ikaonekana! Lahaula la kuwata! Kumbe waliyokuwa nayo mikononi ni geresha tu, ripoti yenyewe ilitunzwa kiaminifu na Spika!

Ndiyo miguu yao ikanyong’onyea na midomo yao ikakauka huku ngozi zao zikisinyaa kwa ubaridi wa hofu wakajua “mjini shule”. Wakaweweseka na kuanza kulalamika hasa baada ya Dk. Mwakyembe kuisoma ripoti ile kwa “mbwembwe”. Kikawauma, kikawakaba shingoni, kikawaudhi na kuwekera lakini maji yalishazidi unga. Taifa la Tanzania likatamalaki.

Wakaangalia pa kutokea hakuna; Wakatafuta njia “mbadala” za kujitetea wakakwama; wakatafuta maneno matamu ya kujibu mashambulizi wakashikwa na kigugumizi siyo cha ndimi tu bali pia ubongo! Midomo ikabakia wazi, na mioyo yao ikidunda kama wale waliofumaniwa.

Wakaamua kuzira. Wakaamua kuweka manyanga chini na kudai wameonewa. Niliwahi kuandika huko nyuma kuhusu “viongozi wasiokosea na Taifa la wasiokasirika”. Hakuna kati yao hata mmoja aliyekubali makosa. Wote wanalalamika kuwa wameonewa na ati wanawajibika kutokana makosa ya “walio chini yao”. Huku ni kuwajibika kihuni. Ndiyo maana leo naimba sifa za Taifa letu kutamalaki; kuwa Tanzania ni kubwa zaidi ya jina la kiongozi na ni kubwa sana kuliko vibendera vipepeavyo na ving’ora vimulikavyo!

Leo hii wako wapi waliokuwa wakipigiwa saluti na kutetemekewa kila wapitapo? Wako wapi leo waliodhani kwamba bila wao Tanzania haiendi? Na hili basi liwe somo kwa watawala wetu na wale wanaoota njozi za kututawala. Mamlaka ya kutawala inatoka na inabakia kwa watu siku zote, wasisahau hilo.

Hivyo wale waliokuwa na mbwembwe za maneno huko nyuma wakaishiwa kauli; kama vile mjusi anavyotoa macho anapobanwa na mlango, ndivyo hivyo wao pia wakatoa macho ya hasira na wakakunja ngumi za kisasi. Wakajiandaa kujibu mashambulizi; wakajiandaa kujibu mapigo.

Hilo nalo likawaharibikia kwani fisadi hawi shujaa hata akipokewa kwa mbwembwe. Ndipo tukaiona ile ndege iliyombeba yule “kiongozi mahiri, shujaa, hodari aliyetamba bungeni” kumbe ni kijidege tu kidogo dogo tu.

Ni hapo ndipo tulipogundua kuwa taifa ni kubwa kuliko cheo cha mtu na ni kubwa kuliko majigambo yake. Na hili liwe funzo kwa wale ambao leo hii wanapepewa vibendera na kupigiwa saluti kila waendapo; wale waitwao “waheshimiwa” na ambao wanafikiri kutokana na vyeo vyao basi wako juu ya nchi yao. Watambue leo kuwa Taifa la Tanzania ni kubwa kuliko mtu yeyote, na liko juu mno kuliko chama chochote kile.

Na hivyo basi tunapofurahia kutamalaki kwa taifa letu Dodoma wiki chache zilizopita, hatuna budi kudhamiria wazi kabisa kuwa hatutawapa vibali watawala wetu kutupeleka tusikotaka taka kwenda na kutubebesha mizigo tusiyochutama kuibeba. Hatuko tayari kuingizwa kwenye Ubuzwagi mwingine au Urichmond mwingine.

Niliandika mwishoni mwa mwaka jana kwamba mwaka huu tutaendelea kuwamulika na kuwaangalia kwa ukaribu na kuwaumbua mafisadi wote. Mwaka huu ni mwaka ambao tunataka watakapokaa chini kutia saini mkataba wowote ule kwa niaba ya jamhuri yetu wafikirie mara mbili. Tena wasidhanie hata kidogo kuingia mkataba kwenye kihoteli huko majuu, kwa maana leo macho ya Watanzania yanamulika kila kona.

Wasidhanie wanaweza tena kufanya mambo yao kwa siri kwani mwaka huu si tu tutajua wamefanya nini tutajua wamefanya wapi, lini na nani. Na Watanzania ambao leo hii wametokea kuona fahari sana ya Taifa lao watapewa nafasi ya kujua. Hivyo ni wito kwa watumishi wote wa umma kuwa waaminifu.

Ndugu zangu, taifa letu limesimama kwenye njia panda ya uadilifu na ufisadi na miguu yetu imesimama kwenye makutano ya ukweli na uongo, na kwa hakika sisi kama taifa tunajikuta tumepiga kambi kwenye kona ya mafanikio na maendeleo. Tusikubali watu wachache hata kama wanapepewa na vibendera elfu kujifanya wako juu ya taifa letu.

Tutawaheshimu wale wanaotumikia nchi yetu kwa uaminifu, tutawaunga mkono wanaokubali makosa yao na kujisahihisha, lakini wenye kiburi na waliolewa ugimbi wa madaraka ambao wamejiambia kuwa wao ni wadogo wa malaika wa mbinguni na ya kwamba wametumwa kutuongoza kuelekea nchi ya ahadi na hivyo tusiwahoji; hawa watambue kuwa tutawafuata kila waendako na kuhakikisha kuwapigia kelele za kuwaamsha.

Yawezekana wanatamani ndani ya mioyo yao kuona Tanzania ya waoga inarudi na ile nchi ya wanyamazao inazaliwa tena. Nina habari mbaya kwao. Tanzania iliyoamka ndiyo imefika na kwa hakika haitarudi tulikotoka; kizazi kilichooambiwa ni taifa la kesho hatimaye kimefika na sasa kinadai taifa lake.

Taifa limetamalaki Dodoma. Kwa mara ya kwanza katika miaka ya karibuni Watanzania walijihisi kuthaminiwa na kujiona kuwa na wenyewe wana sauti. Ile Kamati Teule ya Bunge ilichofanya si kusababisha kuiangusha serikali ya Lowassa lakini kwa hakika kuliinua taifa letu juu kuliko utawala wa kisiasa. Walichofanya ni kuturudishia heshima na kutufanya na sisi tetembee kifua mbele!

Walichofanya ni kusema kuwa Tanzania inaweza kufuata utawala wa demokrasia endapo tu itakuwa tayari kulipa gharama yake. Mojawapo ya gharama yake ndiyo hiyo ya viongozi kuwajibishwa au kulazimishwa kuwajibika. Kwenye nchi ya wababe na yenye utawala wa kiimla lililotokea Dodoma huwa halitokei kwelikweli; linabakia ni la simulizi kama lile la ‘Alfu Lela Ulela au Siku Elfu na Moja’.

Wako wapi mashujaa, wale waliojigamba!
Walodai wanafaa, na tenzi wakaziimba,
Mbona sasa washangaa, wamebakia wayumba?
Nchi imetamalaki, Tanzania iko juu.

Walidhani wanapaa, sasa leo wametua,
Tuliopigwa butwaa, mbona ndio twakenua,
Walituona vichaa, hoja tulipopangua,
Nchi imetamalaki, Tanzania iko juu.


Na sasa twawashangaa, wadaipo kuonewa,
Walikamatwa dagaa, mapapa wakaachiwa,
Kila kitu kina saa, ya kwao ilifikiwa,
Nchi imetamalaki, Tanzania iko juu.

Ndiyo. Tanzania iko juu na tutaendelea kuiinua kuliko mtu yeyote, tutaendelea kuilinda kuliko tunu yoyote, na kwa hakika tutawapinga bila woga wale wote ambao wanajikweza kinyume cha Taifa letu.

Tutaendelea kushindana nao wale wote ambao wanafikiri hii nchi ni ya kwao peke yao. Hadi pale kila aliye kwenye utumishi wa umma atakapotambua kuwa hapendwi mtu, haogopwi mtu, na haonewi mtu, Ni Tanzania na watu wake ndiyo tunayoijali! Na yeyote anayefikiri kuwa anaweza kufanya lolote na kusababisha Taifa letu kuwa duni na watu wake kujihisi wanaishi kwa kuhamia mtu huyo ni adui yetu na kuumbuliwa ataumbuliwa.

Na tusonge mbele wana na mabinti wa taifa hili; tusilaze damu tena. Tusikubali wafanye watakalo bila kuulizwa; tusiwafumbie macho na tusikubali kuzugwa tena. Na mahali pa kuanzia ni kutaka wale wote waliohusika na wizi wa fedha zetu Benki Kuu wafikishwe mahakamani na wasionewe huruma ili liwe fundisho kwa wengine wote. Tusonge mbele, kwani nchi hii ni yetu sote.
 
Hivi wewe una matatizo gani? unafurahia kudondoka kwa wenzako? Na siku na wewe yakikukuta na wewe utaimbwa nyimbo na kutungiwa na tenzi.

Mnajua mlichokifanya dhidi ya Lowassa ni kitendo kibaya na ambacho hakikuwa cha haki, halafu mnakaa chini kuimba nyimbo za "kutamalaki".

Na wewe zamu yako inakuja, si umesikia mnatembelewa tangu karibu wiki mbili sasa? Nilikuonya.
 
EL alikula kasungura peke yake kamempalia kooni.
 
Hivi wewe una matatizo gani? unafurahia kudondoka kwa wenzako? Na siku na wewe yakikukuta na wewe utaimbwa nyimbo na kutungiwa na tenzi.

Mnajua mlichokifanya dhidi ya Lowassa ni kitendo kibaya na ambacho hakikuwa cha haki, halafu mnakaa chini kuimba nyimbo za "kutamalaki".

Na wewe zamu yako inakuja, si umesikia mnatembelewa tangu karibu wiki mbili sasa? Nilikuonya.
Bi senti Hamsini, kumbe yaliyotokea Dodoma kwako hayajaleta furaha? Mbona hiyo ndio furaha ya wengi? Si kwa maana ya kudondoka kwa mtu mmoja mmoja lahasha, bali kwa ujumbe kufika kwa wale waliopewa dhamana ya kutuongoza. Ujumbe ni kuwa Tanzania ina wenyewe,na wenyewe ni wale waliojazana vijijini bila huduma bora za afya wala barabara,waliomjini bila ajira nk. na wote wanaoumia kwa mikataba mibovu isiyo na tija bali kujaa ufisadi wa aibu kabisa.Mkjj kasema kweli,na huu ni mwanzo tu,furaha itakuwa kubwa pale fagio litakapo safisha WOTE waliobaki ambao ni wachafu.
 
Hivi wewe una matatizo gani? unafurahia kudondoka kwa wenzako? Na siku na wewe yakikukuta na wewe utaimbwa nyimbo na kutungiwa na tenzi.

Mnajua mlichokifanya dhidi ya Lowassa ni kitendo kibaya na ambacho hakikuwa cha haki, halafu mnakaa chini kuimba nyimbo za "kutamalaki".

Na wewe zamu yako inakuja, si umesikia mnatembelewa tangu karibu wiki mbili sasa? Nilikuonya.

Kaazi kweli2!
 
yote maisha , ila cha maana hii ni nchi yetu sote na ninaimani safari hii haitaishia hapo ila itafagia kotekote hasa migodini na wale magaidi wetu wa EPA. ASANTE SANA MWANAKIJIJI.
 
Mimi nilifikiri yaliyojiri Dodoma yangewapandisha chati wapinzani, cha kushangaza nikaona wameshindwa kutumia fursa na matokeo yake wakagaragazwa Kiteto.

Yaliyojiri Dodoma yamempandisha chati JK. Ni Rais wa kwanza Tanzania kuonyesha ujasiri wa kutomvumilia yeyote asiyetekeleza majukumu yake kama ipasavyo. Wengine wakae mkao wa kula, biriani inaandaliwa.
 
Ujasiri ndio huu Wauaji wanaachiwa na mahakama,waandishi wa habari wanapigwa bakora. Walioleta ngebe Kiteto walikiona cha mtema kuni. MAFISADI wanaendelea kutunisha matumbo yao kwa pesa ya walipakodi.

EL, Karamagi wanapeta tu lakini wezi wa kuku Tandika na Manzese wako Keko.
 
Mimi nilifikiri yaliyojiri Dodoma yangewapandisha chati wapinzani, cha kushangaza nikaona wameshindwa kutumia fursa na matokeo yake wakagaragazwa Kiteto.

Yaliyojiri Dodoma yamempandisha chati JK. Ni Rais wa kwanza Tanzania kuonyesha ujasiri wa kutomvumilia yeyote asiyetekeleza majukumu yake kama ipasavyo. Wengine wakae mkao wa kula, biriani inaandaliwa.

DSM,
JK chati yake haikupanda bali imeshuka tena vibaya sana. Na pia Deep Green na akina Meremeta zitakapoibuka vizuri, sio ajabu zikamuweka pabaya zaidi. JK hajamuwajibisha mtu yeyote mpaka alipopewa shinikizo na either wafadhili au wabunge, hata Bilali alimuongezea wasaidizi badala ya kumfukuza kazi ingawa alishaonekana wazi kuwa ni kipanga. JK is a huge disappointment to many.

Wapinzani nao wametuangusha kwa kushindwa kujiimarisha kwa kutumia huku kuanguka kwa umaarufu wa JK na timu yake. Lakini nafikiri mwelekeo wao sio mbaya ila itawachukua muda kupata mafanikio tunayoyahitaji.
 
nakubali taifa lilitamalaki dodoma
na wanaopinga ndio waliotamalaki kabla ya taifa kutamalaki
 
Ni kweli lakini ushindi bado uko mbaliiiiii!!!!!

The following issues hazijawa resolved

1. Balali

2. Deep green, Meremeta, Tangold na hata Kagoda

3. Richmond yenyewe

4. Kiwira coal power

5. Takukuru

6. AG Mwanyika

7. Hosea

8. Chenge

9. TICTS

10. Ujenzi BOT

11. Dito

12. Rada

13. Ndege ya Raisi

14. Helicopter za jeshi na magari

15. etc etc!!!! the list goes on!!!!!!!!!!!!!
 
Unachosema Nyambala hapa ni kuwa serikali haijashughjulikiwa. Kazi ndo imeanza hivyo, watu wana usongo na nchi yao.
 
Ni kweli lakini ushindi bado uko mbaliiiiii!!!!!

The following issues hazijawa resolved

1. Balali

2. Deep green, Meremeta, Tangold na hata Kagoda

3. Richmond yenyewe

4. Kiwira coal power

5. Takukuru

6. AG Mwanyika

7. Hosea

8. Chenge

9. TICTS

10. Ujenzi BOT

11. Dito

12. Rada

13. Ndege ya Raisi

14. Helicopter za jeshi na magari

15. etc etc!!!! the list goes on!!!!!!!!!!!!!

Duh! Nyambala yaani nikajikuta nimeanza kupatwa na "upako" wa uzalendo hasa baada ya kuanza kusoma Maandiko Matakatifu ya Mafisadi - imekaa kama vitabu vya kifisadi kwenye maandiko hayo!!
 
Back
Top Bottom