RUCCI
JF-Expert Member
- Oct 6, 2011
- 1,701
- 1,714
Tai mkubwa aliyezuiliwa nchini Lebanon akituhumiwa kuwa jasusi wa Israel ameachiliwa huru baada ya walinda usalama wa Umoja wa Mataifa kuingilia kati, maafisa wa Israel wamesema.
Ndege huyo, mwenye mabawa ya urefu wa mita 1.9, alipaa kutoka hifadhi ya wanyama ya Israel na kuingia Lebanon ambapo alikamatwa na kuzuiliwa na wanakijiji.
Walianza kumshuku baada ya kugundua kwamba alikuwa na kifaa cha kutumiwa kufuatilia anakoenda.
Maafisa wa kulinda wanyamapori wanasema tai huyo alitoka Uhispania mwaka uliopita na aliachiliwa huru mbugani mwezi mmoja uliopita katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyama ya Gamla, eneo laGolan Heightsambalo linathibitiwa na Israel.
Maafisa wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv kilichohusika katika kufuatilia anakoenda ndege huyo, pamoja na kifaa chake cha GPS, wanasema tai huyo alikuwa amebandikwa jina kwenye mabawa yake na alikuwa amefungwa pete ya chuma iliyoandikwa: "Tel Aviv Univ Israel".
Maafisa wa Israel waligundua ndege huyo alikuwa amekamatwa baada ya picha, zilizoonyesha ndege huyo akiwa amefungwa, kuanza kusambaa mtandaoni.
“Kupitia operesheni makinifu pamoja na maafisa wa Lebanon na kwa usaidizi mkubwa kutoka kwa walinda usalama wa Umoja wa Mataifa, Mamlaka ya Viumbe na Mbuga za Wanyama Israel imeweza kumrejesha tai ambaye alikuwa amekamatwa siku chache zilizopita na wakazi wa Bint Jbeil, Lebanon," taarifa ya Israel iliyotolewa Ijumaa inasema.
Vyombo vya habari Lebanon vinasema wanakijiji walikubali kumwachilia ndege huyo baada ya kubainika kwamba hakuwa akitumiwa kupeleleza.
Ndege huyo sasa anatibiwa majeraha madogo.
Hii si mara ya kwanza kwa tai kukamatwa Mashariki ya Kati akidhaniwa kuwa ‘jasusi’ kutoka shirika la Mossad.
Saudi Arabia ilikamata ndege kama huyo mjini Hyaal mwaka 2011.
Chanzo: BBC