Taftai ya Eid El Fitr nyumbani kwa marehemu Shariff Abdallah Attas 1990

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,841
30,168
1118760

Leo siku ya Eid El Fitr asubuhi nimejiinamia na mengi katika maisha yangu ya utoto yakanijia nikikumbuka ilivyokuwa asubuhi ya Eid wakati wetu.

Nimemkumbuka kinyozi wetu jina lake Muingereza ambae ''saluni,'' yake ilikuwa chini ya mkwaju Mtaa wa Sikukuu na Kirk Street.

Asubuhi kama hii ya leo siku ya Eid kuna foleni ndefu ya watoto wanasuburi kunyolewa na Muingereza kashika mkasi wake akiwanyoa mmoja baada ya mwingine mkasi ule ukitoa sauti kama nyimbo tata tatatata kwa haraka sana.

Siku hizo vinyozi waliokuwa ndani ya nyumba na kunyoa kwa mashine ukiwataka sharti uwafate Uhindini na bei zao zilikuwa juu na takriban wote walikuwa Wahindi.

Ilipokuwa saluni ya Muingeraza hivi sasa kuna jengo la ofisi ya CCM Gerezani.

Hapo ilipokuwa saluni ya Muingereza kuna historia kubwa sana ya TANU na uhuru wa Tanganyika katika kichwa cha kinyozi Muingereza.

Kuna historia kubwa kwa sababu mbele tu na hii saluni yake ndipo ilipokuwa nyumba ya Bi. Mruguru bint Mussa mama yake Abdul Sykes.

Hapa chini ya mkwaju wa saluni ya Muingereza ilikuwa baraza ya TANU wenyewe wakikutana hapo kupeana taarifa za mambo yalivyokuwa yakienda dhidi ya mkoloni.

Muingereza kamuona Mwalimu Nyerere akifuatana na Abdul Sykes siku za mwanzo za TANU 1954/55 wakienda nyumbani kwa Bi. Mruguru na wakipita hapo watasalalimiana.

In Shaa Allah iko siku nitaeleza historia ya barza hii na muhusika wake mkuu Kinyozi Muingereza.

Leo nataka nikuhadithieni habari za chai niliyokunywa na radiki yangu marehemu Kleist Sykes nyumbani kwa Shariff Abdallah Atttas siku ya Eid kama hii takriban miaka 30 iliyopita.

Sie wengine tumekuja kumjua Shariff Abdallah Attas katika utu uzima wake akikaa Mtaa wa Twiga na Sikukuu nyumba yake mkabala na Msikiti wa Shadhili Dar es Salaam.

Katika miaka ya 1950 Shariff Attas alikuwa akifanyakazi Soko la Karikaoo Market kama Collector wa ushuru wa mnada wa nafaka.

Market Master yaani Mkuu wa Soko akiwa Abdulwahid Sykes.
Abdul Sykes alichukua nafasi hii kutoka kwa Mwingereza Brian Hodges.

Sifa kubwa ya Shariff Attas nimeelezwa ni ubingwa wake katika hesabu.

Yeye alikuwa na uwezo wa kukokotoa hesabu ndefu kichwani bila ya kutumia ‘’calculator.’’

Kisa chake hiki ninachokieleza nimekisikia kwa masikio yangu mwenyewe miaka kadhaa nyuma takriban zaidi ya 25 hivi sasa..

Ilikuwa siku ya Eid El Fitr mimi na Kleist, mtoto wa Abdul Sykes tumekwenda kusali Eid Msikiti wa Kitumbini.

Kleist ana uhusiano mkubwa sana na msikiti huu kwani hapo katika miaka ya 1930 babu yake alikuwa akienda kuswali hapo huku kafatana wa wanae Abdul, Ali na Abbas.

Habari hii kanihadithia Ali Mwinyi Tambwe.

Mzee Ali Mwinyi alikuwa kaniita nyumbani kwake Kinondoni Block 41 ili asahihishe baadhi ya mambo ambayo alikuwa kasoma katika mswada wa kitabu cha Abdul Sykes, mswada ambao mwane mmoja Abdulrahman Mbamba alikuwa kamwonyesha.

Kabla ya kuanza mazungumzo yetu akanambia, ‘’Mimi Abdul hanipati kabisa mimi nikimuona akija kuswali na baba yake pale Kitumbini mtoto mdogo kashikwa mkono. Si huu msikiti unaouna hii leo, msikiti ule wa zamani.’’

Msikiti huu ndipo baba yake Kleist, Abdulwahid Sykes alipofanyiwa sala ya jeneza kabla hajakwenda kuzikwa Makaburi ya Kisutu.

Kwa hiyo sikushangaa Kleist aliponiambia tukasali Eid Kitumbini.

Nakumbuka wakati ule Kleist alikuwa na Mercedes Benz nyekundu, gari ya kupendeza sana.

Nami nikawa sishi kumtia tashtiti kuwa kafuata nyayo za baba yake kwa kuwa baba yake amekufa gari yake ikiwa Mercedes Benz 280 SE.

Nikimpiga vijembe hivi yeye kazi ilikuwa kucheka tu.

Baada ya kumaliza kuswali na kupena mikono na wazee wetu, Kleist hapo yeye ndipo alikuwa anakutana na rafiki wa marehemu baba yake na sasa ni watu wazima sana yeye akawa kila akitoa mkono anaufumba anamwachia kitu mzee wake.

Tulipomaliza akanambia, ‘’Mohamed sasa twende kwa Shariff Attas.’’

Tulipofika kwa Shariff Attas tukakuta veranda yake imejaa ‘’who’s who’’ katika wazee maarufu wa Dar es Salaam, mmoja wapo marehemu Bwana Hamida Tuli, muungwana wa Kizaramo kutoka Masaki.

Bwana Tuli akiishi Mtaa wa Matumbi hapo jirani.

Mikeka ya rangi nzuri nzuri imetandikwa na udi unatoa riha nzuri,

Sinia zimejaa maakuli - kaimati, maandazi, visheti, vitumbua, tambi, katlesi, kababu, sambusa nk.

Tumewakuta wazee wetu wanafuturu.
Shariff kumuona Kleist kafurahi sana kupita kiasi anamwashiria aje akae ubavuni kwake.

Mara tumeletewa sahani na vikombe tunakaribishwa chai.

Mara Bwana Hamida Tuli kasimama anaomba ruksa kwa niaba ya wenzake anasema, ‘’Shariff tunaomba ruksa tuondoke kwa kuwa tumelikwa chai Ikulu kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.’’

Basi ikapigwa fatha ikaombwa dua wazee wakapeana mikono na Shariff Attas hao wakatimka kwenda Ikulu kunywa chai na Rais.

Ukumbi ukabaki mtupu tuko sie watatu tu - Shariff Attas, Klesit na mimi.

Kleist akaangua kicheko kile cha kejeli.

Shariff Attas yeye ni babu yake anamtania na kumuogelea atakavyo.

Hizi ndizo mila zetu watu wa pwani.

‘’Duu, Shariff wenzako wote wanaalikwa Ikulu kwa rais, wewe uko hapa huna akujuaye!’’

Kleist anaangua kicheko.

Shariff Attas hakuwa mdogo hivyo ni mtu maarufu kwa watu maarufu wa mjini na wenye majina ya kutajika.

Shariff Attas yuko kimya kaegemea ukuta anamtazama kwa jicho la deko hasemi kitu.

Kleist kamaliza kumcheka Shariff mkono unakwenda kwenye sambusa, kababu, kaimati.

‘’Kleist sikiza bwana.

Mimi kama kuingia Ikulu ningeliingia enzi za Nyerere yeye ndiye alikuwa mwenzangu.

Mimi Mwinyi atanijulia wapi?’’ Shariff Attas akaanza.

Mimi masikio yangu yashakuwa walu namtazama Shariff usoni.

Picha ninayoiona siyo ile ya dakika mbili zilizopita.

Namuona Shariff ghafla amebadilika anaacha maskhara anataka kusema jambo.

‘’Sikiza Kleist, hiyo ni 1955 Nyerere anakaa kwa baba yako pale Stanley ndiyo TANU inakuja juu.

Nyerere kesha acha ualimu.

Anakuja ofisini kwa baba yako pale Kariakoo Market.

Ikifika mchana Abdul ananiita ananiambia nifatane na Nyerere nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana.

Mimi na Nyerere mguu kwa mguu, tunaingia Swahili, Narung’ombe, Gogo, Mchikichi, Sikukuu hadi Stanley kwa mama yako Mama Daisy.

Njia nzima mimi na Nyerere tunazungumza.

Wakati ule hakuna anaemjua.

Tunafika nyumbani kwa mama yako chakula kipo mezani tunakula tukimaliza tunarudi ofisini pale kwa baba yako pale sokoni.

Yeye alikuwa hatoki anaendelea na kazi.

Nyerere alikuwa mwenzangu na mzungumzaji wangu sana wakati ule.

Basi miaka ikenda hadi tukapata uhuru na Nyerere akawa Waziri Mkuu.

Siku hiyo mimi niko ofisi ya TANU ghafla Nyerere anaingia watu hamkani wamesimama na Nyerere anaanza kupeana mikono na watu walioko pale hadi akafika kwangu nami nikampa mkono.

Nyerere akanitazama nami nikamtazama tukawa sote tunatazamana usoni. akasema,‘’Mzee tumepata kukutana?’’

Mimi nikamjibu, ‘’Hapana hatufahamiani.’’

Basi akapita kusalimiana na watu wengine.

Sasa Kleist mimi ilikuwa niingie Ikulu enzi za Nyerere rafiki yangu lakini bahati mbaya kanisahau.’’

Shariff Attas alikuwa mtu wa tasnifa sana.

Akajinyoosha kaegemea ukuta anamtazama Kleist kwa mtazamo wa jicho la pemebeni huku uso umejaa tabasamu kama vile anamwambia mjukuu wake Kleist, ‘’Nimekukomesha kwa kutaka kwako kunicheka ati sijaalikwa Ikulu.''

Mimi nilishusha pumzi kwani nilikuwa nimechoka kwa kisa kile kilichokuwa kimetokea kwa wakati ule zaidi ya miaka arobaini nyuma.

Kleist akaomba ruksa na Shariff akaturuhusu baada ya kupiga fatha.

Kleist wakati tunatoka akaingia jikoni kwa mke wa Shariff Attas kwenda kuaga.

Tulipokuwa sasa tunatoka nje Shariff Attas akampigia kelele Kleist, ‘’Kleist bibi yako umempa shilingi ngapi?’’

Kleist akacheka akamjibu Shairff, ‘’Nenda kamuulize mwenyewe.’’

Shariff akawa anacheka kwa ndani ya nyumba na sisi tunacheka hapo nje.

Picha hapo juu ni Shariff Abdallah Attas akiwa kijana na hiyo nyingine hapo chini ni mimi na Kleist Msikiti wa Kipata.

1118761
 
Mzee Mohamed Said shikamo! Kijana wako nikuombe kitu. Kama unaijua historia ya Shariff bin Ahmad wa Lamu naomba siku ukipata wasaa utuwekee. Ahsante.
 
Mzee Mohamed Said shikamo! Kijana wako nikuombe kitu. Kama unaijua historia ya Shariff bin Ahmad wa Lamu naomba siku ukipata wasaa utuwekee. Ahsante.
Beberu...
Hapana siijui lakini nitakuwekea kitu ambacho nimeandika kuhusu
Lamu.

Bahati mbaya nimeandikwa kwa Kiingereza.

 
Mimi nimependa hapo ulipokuwa ukitaja hayo maakuli katika njia ya madaha na utuvu wa hali ya juu Wallah.

Binafsi nilijua inaitwa Kalimati kumbe ni Kaimati.

Nashkuru sana kwa kuniongezea msamiati, ndio faida ya kuwa na wazee kama nyinyi Wallah.

Shukran sana.
 
Asante kwa ujumbe mzuri mambo mengi nisiyoyafahamu lakini naamini siku zote wazee wa Pwani ndio wameleta Uhuru wa Tanganyika lakini historia iliwageuka ikawasahau wamekuwa kama bulllodozer na roller zinatengeneza barabara ikipendeza hubebebwa zisiharibu barabara
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom