Tafsiri ya Kiswahili: Ripoti ya CAG kuhusu "kupotea" Trilioni 1.5 iliyoibua "kupotea" Trilioni 2.4

Evarist Chahali

Verified Member
Dec 12, 2007
797
1,000
Habari inayotikisa kwenye anga za habari za Tanzania hivi sasa ni kuhusu ziara ya Tundu Lissu huku nchi za Magharibi. CCM wakishirikiana na MATAGA na vijana wa Lumumba wanafanya kila bidii mjadala huo uendelee kuvuma, wakielewa fika udhaifu wa Watanzania: kuendeshwa na matukio huku wanasahaulishwa ISSUES nyingine muhimu kwa mustakabali wa taifa lao.

Haimaanishi kuwa ziara za Lissu zipuuzwe. Wala haimaanishi kuwa CCM /MATAGA/Lumumba wakiandika utumbo wao kuhusu Lissu wasijibiwe. Hapana. Hayo yafanyike lakini kwa kwenda mbele zaidi ya hapo. What if kila mtetezi wa Lissu atajaribu japo kidogo kuwa kama nguli huyo wa utetezi wa maslahi ya Tanzania yetu? What if badala ya kumtetea tu mitandaoni, kila anayeitakia mema Tanzania yetu atakwenda mbali zaidi na kufanya yale ambayo Lissu angeyafanya laiti angekuwepo leo huko Tanzania?

Naam, Lissu asingekubali suala la "upotevu" wa shilingi Trilioni 1.5 lizimwe kienyeji kama ilivyofanyika majuzi. Na asingekalia kimya "ufisadi mpya" wa shilingi trilioni 2.4 ulioibuliwa na ripoti ya uchunguzi ya CAG,ambayo Bunge limekataa isiwekwe hadharani.

Bahati nzuri, jarida la mtandaoni la African Arguments lilichapisha ripoti hiyo kamili, sambamba na kuifanyia uchambuzi. Hata hivyo, uchambuzi huo ulikuwa kwa Kiingereza. Hakuna gazeti lililojihangaisha kuchapisha habari hiyo kwa sababu zinazoeleweka. Nikalazimika kufanya tafsiri ya makala hiyo ndefu, kwa minajili ya kila mmoja wenu kuisoma


Unaweza kusoma na ku-download tafsiri hiyo HAPA


Au waweza kuisoma yote hapa hapa

Machi mwaka jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mussa Assad aliwasilisha ripoti yake ya mwaka wa fedha 2016/2017. Ilikuwa na mengo yasiyopendeza. Ilionyesha kuwa taasisi mbalimbali zilivyotumia fedha kwenye shughuli hewa huku kanuni za bajeti zikikiukwa.

Kilichogusa hisia za wengi ni sintofahamu ya mapato ya shilingi trilioni 25.3 na jumla ya shilingi trilioni 23.8 zilizotolewa na Hazina kwa ajili ya matumizi ya serikali. Je shilingi trilioni 1.5 ( tofauti kati ya mapato ya sh trilioni 25.3 na matumizi ya shilingi trilioni 23.8) zilienda wapi?

Serikali ilitoa maelezo kadhaa kuhusu tofauti hiyo huku sintofahamu hiyo ikisambaa kutoka bungeni hadi kwenye mitandao ya kijamii. Kisha, katika hafla moja Ikulu, Rais Magufuli alimuuliza CAG Assad, akisema, "CAG yupo hapa...Unaweza kusimama na kutuambia kama kuna fedha yoyote imeibiwa?" Assad alijibu "hapana mheshimiwa, hakuna fedha iliyoibiwa!"

Hata hivyo, hatimaye Bunge lilimwagiza CAG kufanya uchunguzi wa sintofahamu hiyo ya shilingi trilioni 1.5, kazi iliyokamilishwa mwezi uliopita na kuwasilishwa.

Hatua ya pili ilipaswa kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia ripoti hiyo. Hatua hiyo iliingiliwa kati baada ya Spika Job Ndugai kumuita CAG bungeni "kujibu tuhuma za utovu wa nidhamu," katika hatua ya kushangaza na inayodaiwa kukiuka katiba. Ndugai pia alisimamisha kwa muda kazi kamati zote za Bunge ikiwa ni pamoja na PAC.

Licha ya hatua hizo, PAC ilimudu kupitia ripoti hiyo ya CAG na, mapema mwezi huu, ikawasilisha ripoti yake yenyewe. Ripoti hiyo, hata hivyo, kwa kiasi kikubwa "ilipuuza" matokeo ya uchunguzi wa CAG, kama ambavyo Mwenyekiti wa Kamati alivyohitimisha, "hakuna upotevu wala wizi."

Wabunge wa Upinzani walipatwa na mshangao.

Mbunge (wa Chadema) Catherine Ruge, mhasibu kitaaluma na mjumbe wa PAC aliishutumu ripoti hiyo ya Kamati ya Bunge. Alieleza kuwa kwa hakika kuna kasoro ya shilingi Trilioni 2.4 iliyoibuliwa na CAG. Naibu Spika alimshurutisha kuondoa kauli hiyo baada ya pingamizi kutoka kwa waziri mmoja.
Kisha Mbunge mwingine wa Upinzani, Zitto Kabwe, aliibua hoja kuhusu shilingi bilioni 976.97 ambazo ripoti ya CAG inaonyesha kuwa zilitumika bila kufuata taratibu za kisheria.


Mwisho, Mbunge (wa Chadema) Halima Mdee alitoa rai ripoti ya CAG iwekwe hadharani ili wabunge wote waweze kuisoma sambamba na ripoti ya PAC. Rai yake ilikataliwa.

Wanahabari na wananchi wengine walihoji kwanini ripoti hizo zifanywe siri wakati mara zote zimekuwa zikiwekwa wazi.Kadhalika, ni utaratibu unaotambulika kimataifa – kupitia matamko kama Azimio la Lima – kwamba ripoti kama hizo shurti ziwekwe hadharani kwa minajili ya udadisi, mijadala na uwazi.

Ndio maana African Argumens inaweka ripoti hiyo hadharani.

Mkanganyiko wa hali ya juu

Ukisoma ripoti ya CAG utabaini vitu kadhaa.

Kwanza, madai ya Mwenyekiti wa PAC kuwa ripoti ya CAG haikukuta ushahidi wowote wa upotevu au wizi, kwa kiasi flani si sawia; inaeleza ndivyo sivyo kuhusu kazi aliyopewa CAG. Uchunguzi wa CAG haukulenga kubaini wizi au ushahidi wa wizi au kumnasa mwizi. Kama ilivyoelezwa kwenye hadidu za rejea, lengo la uchunguzi huo lilikuwa kubaini tofauti ya shilingi Trilioni moja unusu iliyojitokeza.

Hii ilihusisha kwanza kufanya mapitio ya mapato na matumizi ili kuangalia kama kuna mwafaka. Kisha, iliangalia iwapo utoaji fedha ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kuangalia kama kuna malipo yaliyofanyika bila kuidhinishwa.

Kwa hakika ripoti ya CAG ilibaini kasoro kadhaa, zinazotosha kuumiza kichwa. Japo hakuna ishara za ujambazi wa kupora benki lakini tunaona kitu kama fedha kutoka kwenye sehemu ya kuhifadhia fedha ikitapakaa sakafuni katika hali inayokanganya kabisa.

Mwanzoni kabisa mwa ripoti hiyo kuna kauli inayogusa hisia kuhusu mwelekeo wa uchunguzi huo. Yapaswa kufanya nukuu kamili: " Uhakiki wetu ulikwazwa na ukosefu wa nyaraka stahili na maelezo yasiyojitosheleza kutoka kwa Utawala (wa Wizara ya Fedha), vitu ambavyo vilikuwa muhimu kupata usahihi na ukweli wa viwango husika. Kwa mfano, Wizara haikuweza kutoa nyaraka kama vile "Cash Book for Consolidated Funds" na "Bank Reconciliation Statements" ambazo hutoa taarifa za msingi kuhusu fedha husika. Taarifa zilizotolewa zilikuwa zimetapakaa katika vipengele kadhaa na zilikuwa zimefanyiwa marekebisho mengi wakati wa uhakiki.

Ikiendelea, ripoti hiyo ilibaini kwamba kiwango cha fedha za mapato na matumizi kilikuwa juu zaidi ya ilivyoripotiwa wali, japo ni muhimu kuzingatia kwamba sio kutokana na sababu zilizotolewa serikali April 2018. Tofauti na kiwango cha awali, inaonekana kuwa fedha za matumizi zilizidi fedha za mapato kwa shilingi bilioni 290.67, japo inatahadharisha kwamba "uthibitisho wa salio kutoka benki kuu hauendani na kiwango hicho."

Kisha uchambuzi katika ripoti hiyo unaangalia kwa kina udhaifu wa mfumo wa usimamizi wa fedha. Ripoti inaeleza kufeli kwa Hazina, na Katibu Mkuu wa Hazina (Mlipaji Mkuu wa Serikali) katika ufuatiliaji mahesabu kwenye akaunti mbalimbali. Pia inakosoa "akaunti zilizotapakaa ovyo na salio lisiloendana na ushahidi kiuhasibu", na kufanya ripoti hiyo kutanabaisha kwamba "utimilifu, uwepo na usahihi wa salio kwenye akaunti husika hauwezi kuthibitishwa."

Shilingi trilioni 2.4 "zimepotea"?

Katika uchambuzi wa fedha zilizotolewa, mapungufu mengi zaidi ya kiusimamizi na kasma yanajidhihirisha. Miongoni mwao ni shilingi bilioni 976.96 zilizotolewa bila idhibi stahili. Wizara kadhaa ziliathirika; hata hivyo, katika kikao na PAC, CAG alieleza kuwa Hazina haikuweza kutoa uthibitisho kuhushu kutolewa kwa fedha hizo, na badala yake Katibu Mkuu wa Hazina alidai kuwa fedha hizo zilipelekwa Ikulu. Ni muhimu kufahamu kuwa Ikulu haikaguliwi na CAG.

Maelezo haya yanapaswa kufuatiliwa na kuthibitishwa, lakini kwa namna yoyote ile, suala la shilingi bilioni 976.96 linaacha alama ya kuuliza, na ripoti inatanabaisha "utoaji wa fedha usiozingatia kanuni unaashiria kuhitajika kwa maboresho katika usambazaji wa fedha za bajeti."

Suala jingine muhimu kuzingatiwa ni kwamba ingawa usimamizi mbovu wa fedha unaweza kufanya majukumu na mamlaka ya CAG kikatiba kuwa magumu, vipi kuhusu zilipo shilingi trilioni moja unusu?

Katika hitimisho, ripoti hiyo inaondoa kiasi hicho cha fedha (shilingi trilioni moja unusu) lakini inazua kiwango kingine kikubwa zaidi cha shilingi triliioni 2.4

Hiki ndicho kiasi ambacho Mbunge (wa Chadema) Ruge alikieleza. Ni jumla ya kasoro za kifedha zilizoonyeshwa kwenye ripoti ya CAG ambazo ni
Shilingi bilioni 976.96 zilizotolewa bila kuidhinishwa (ukurasa 19-23)
Shilingi bilioni 656.6 ambazo ni tofauti kati ya "Exchequer Issues Warrant" na "Exchequer Release Report" (ukurasa wa 29)
Shilingi bilioni 290.67 za "overdraft" isiyo na maelezo (ukurasa wa 3)
Shilingi bilioni 234.12 za "Exchequer Issues Warrants" zilizotolewa bila maelezo ya kueleweka (ukurasa wa 23-4)
Shilingi bilioni 189.99 zilizochotwa bila idhini kutoka "Consolidated Fund" (ukurasa wa 19)
Shilingi bilioni 3.45 zinazounganishwa isivyo sahihi na kufutwa kwa "Exchequer Issue Warrants" (ukurasa wa 26)
Shilingi bilioni 3.26 ambazo ni Exchequer Issue Warrants isivyo halali (ukurasa wa 24)


Mustakabali wa fedha za umma Tanzania ukoje?

Mbunge Ruge anadai kwamba kuna haja ya kufanyia uhakiki kamili, lakini hilo linaonekana kuwa jambo lisilowezekana katika mazingira ya siasa za Tanzania kwa sasa. Ripoti ya CAG inaibua maswali kadhaa, hususan kuhusu Katibu Mkuu wa Hazina, Doto James, anayedaiwa kuwa mpwa wa Rais Magufuli. James alikuwa TANROAD wakati mjomba wake Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi. Baadaye alijiunga na timu ya kampeni ya Magufuli, ambaye baada ya kuwa Rais alimteua mpwae huyo kuwa Naibu Katibu Mkuu Hazina, na mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Katibu Mkuu kamili akichukua nafasi ya mtu ambaye alikuwepo Hazina kitambo.

Kuhusu mustakabali wa fedha za umma Tanzania, tutarajie hali kama hii iliyopo sasa au pengine mbaya zaidi.

Katika kikao cha Bunge kilichoisha hivi karibuni, taarifa zaidi zimejitokeza hadharani kuhusu utetezi usiokubalika kuhusu fedha zilizotengwa kwa matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Kwa mfano, iliripotiwa kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha, jumla ya shilingi bilioni 8.3 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi zilikuwa mara saba zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zilizotengwa. Kiwango hicho kilichotolewa kinaweza kuwa kikubwa zaidi, hasa kwa vile ilibainika kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitengewa shilingi bilioni 12.4 mwezi Septemba 2018 kwa ajili ya chaguzi ndogo tatu.
Ripoti ya CAG inaonyesha jinsi usimamizi wa fedha za umma nchini Tanzania ulivyo na mushkeli. Kwa bahati mbaya, uchaguzi mkuu ukiwa takriban mwaka mmoja tu kutoka hivi sasa, kuna kila sababu ya kuamini kuwa hali itakuwa mbaya zaidi.


Kukabiliana na hali hii kunapaswa kuanzia na uwazi, na ndio sababu ya kuchapishwa ripoti hii ya CAG hapa chini. Kiu ya wananchi kujua ukweli sambamba na mijadala vinaweza kusaidia kuleta mwanga kuhusu ripoti hii ya CAG, na pengine kutoa ufuatialiaji usiofungamana na upande wowote kuhusu kazi za Bunge na CAG.

Ripoti kamili ya CAG ni hii hapa

 

MsemajiUkweli

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
12,225
2,000
Eti upotevu wa 2.4T kwenye nchi yenye bajeti ya 30T

Cha kushangaza hizi ni hoja zinazotolewa na watu wanaojiita "wachumi"

Bilioni 300 tu za Tegeta Escrow account zilisababisha mpaka wahisani wakakata misaada halafu leo Lissu azunguke huko duniani bila kuulizwa na hao wahisani kuhusu upotevu wa 2.4T unaodaiwa "ulioibuliwa na CAG"

Hizi hoja kujua niza uwongo hazihitaji uwe mtaalam wa sayansi ya rocket bali uwe na akili za kawaida ( common sense)


Sent from my iPhone using JamiiForums
 

KWADWO ABIMBOLA

JF-Expert Member
Jan 8, 2019
763
1,000
Hiyo ya CAG inawezekana kupatiwa tafsiri? Kama haiwezekani basi angalau tupate tafsiri ya hiyo Executive Summary.
 

KWADWO ABIMBOLA

JF-Expert Member
Jan 8, 2019
763
1,000
Eti upotevu wa 2.4T kwenye nchi yenye bajeti ya 30T

Cha kushangaza hizi ni hoja zinazotolewa na watu wanaojiita "wachumi"

Bilioni 300 tu za Tegeta Escrow account zilisababisha mpaka wahisani wakakata misaada halafu leo Lissu azunguke huko duniani bila kuulizwa na hao wahisani kuhusu upotevu wa 2.4T unaodaiwa "ulioibuliwa na CAG"

Hizi hoja kujua niza uwongo hazihitaji uwe mtaalam wa sayansi ya rocket bali uwe na akili za kawaida ( common sense)


Sent from my iPhone using JamiiForums
Siyo upotevu. Ni matumizi yasiyoidhinishwa na bunge. Watu wanachota tu na kutumia wanavyotaka bila ruhusa wala maelezo ya kina yanayoonyesha zilikotumika.
 

KWADWO ABIMBOLA

JF-Expert Member
Jan 8, 2019
763
1,000
uzalendo wa magufuri sijui uko wapi, kumuweka mtoto wa dada hazina tayari unatia doa uadilifu wa magufuri.
Kuwa mzalendo ni pamoja na kuheshimu na kufuata sheria na taratibu.

Kwa maneno, matendo na mawazo ya Magufuli, ni wazi kuwa hana uzalendo.

Mzalendo hawezi kutoa matamko na makatazo yanayovunja haki za binadamu na haki za kikatiba za raia.

Mzalendo hawezi kuendesha nchi kwa msingi wa ubaguzi wa kikanda, kikabila na uchama(kuwachukulia vyama vingine kama wahaini).

Mzalendo hataona ufahari kuheshimu sheria na taratibu za matumizi ya fedha za uma (rejea kukosekana maelezo ya matumizi ya 2.4T).

Mzalendo wa kweli kwa nchi hii ya kidemokrasia hataona ufahari kulinda haki za raia na uhuru wao kujieleza, kufanya mikutano, kukosoa, nk.

Mzalendo wa nchi hii angetambua umuhimu wa kuwa na katiba bora na taasisi imara za kuitelekeza hiyo katiba bila kujali ni rais yupi aliyepo madarakani.

Mzalendo hawezi kujiona kuwa akiondoka yeye hakuna atakayeweza kuongoza nchi. Atawaona viongozi wenzake kuwa nguzo muhimu ya kulinda rasilimali za nchi....

Yapo mengi sana yanayotufanya tuamini kuwa huyu siyo mzalendo. Anatulasimisha tu tuamini kuwa ni mzalendo, lakini ni kinyume chake. Ana kiu iliyopitiliza ya madaraka mpaka anaona fahari kuua raia ili aonekane kuwa ni yeye tu anayefaa.
 

MENGELENI KWETU

JF-Expert Member
Oct 23, 2013
8,945
2,000
Nimekusoma mwanzo hadi mwisho Mkuu..
Uchambuzi mzuri sana, Asante.

Hazina ya Tanzania hali ni mbaya sana..

Jamaa anafanya kila ya uhuni kwenye matumizi ya fedha za Tanzania sababu tu muidhinishaji ni mtoto wa Dada..

Hatari sana.
 

number41

JF-Expert Member
Jul 11, 2015
2,009
2,000
Ngumu kumeza watanzania wa kijani wale wale walioiga kelele na kuungana kwa pamoja bungeni kupinga ufisadi kipindi cha kikwete na ndo watanzania wale wale wa kijani leo wanatetea ufisadi sijui wanaupenda utawala huu kuliko utawala ule tuna tatizo mahali tutalia siku moja vibaya ngoja wafumbie macho haya yanayotokea


Sent from my iPhone using JamiiForums
 

Laki Si Pesa

JF-Expert Member
Dec 20, 2018
3,303
2,000
wewe si ulishaukana uraia wa Tanzania ukakimbilia kwa wazungu huko finland? kwa kifupi wewe mkimbizi huna mamlaka ya kuzungumzia mambo ya tanzania tuletee habari za huko ukimbizini finland maana hata rais wa finland hatumjui ni nani?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar threads

Top Bottom