Tafrani polisi, raia

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,076
7,855
WANANCHI katika Kijiji cha Nyankende, wilayani Kahama, wamelishambulia gari la polisi kwa kulipiga mawe, kisha kumuua mtuhumiwa wa unyang'anyi wa kutumia silaha.

Wananchi hao walianza kulishambulia gari hilo baada ya polisi kugoma kuwashusha watuhumiwa hao, ili wawaadhibu kutokana na kuhusika katika matukio hayo ya ujambazi.

Wakati wananchi wakiendelea kulishambilia gari hilo, polisi walifyatua risasi 13 hewani, ili kuwatawanya wananchi hao.

Katika purukushani hiyo, mmoja wa watuhumiwa hao, Hamisi Shabu (23), aliruka kutoka kwenye gari na kukimbia.

Kutokana na kitendo hicho, wananchi hao walimkimbiza mtuhumiwa huyo hadi katika nyumba ya Magokelo Shabu, alikokimbilia.

Wananchi hao waliishambuliwa nyumba hiyo na kufanikiwa kumtoa nje mtuhumiwa huyo, ambapo walimpiga hadi kufariki dunia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanya, Isuto Mantage, alisema jana kuwa askari hao walikwenda kijijini hapo kuwachukua watuhumiwa hao ambao walikuwa wamehifadhiwa kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Nyankende.

Kamanda Mantage, alisema kutokana na hali hiyo, polisi hao waliondoka na kufanikiwa kuwanusuru Charles Monyanda (42), mkazi wa Nyautengero, Manonga Lukubanija (23) na Alex Shabu (31), wakazi wa Kijiji cha Nyankende.

Kamanda huyo wa Polisi alisema wananchi walikuwa wakiwatuhumu watu hao kuhusika katika tukio la uporaji wa kutumia bunduki Novemba 3, mwaka huu kijijini hapo.

Alisema polisi mkoani hapa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na baada ya kukamilika upelelezi, watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Hivi karibuni wananchi wilayani Chato, mkoani Kagera, walivamia kituo cha polisi na kisha kukichoma moto baada ya kupata taarifa kwamba polisi hao walikuwa na mpango wa kumwachia mtuhumiwa wa wizi.

Kabla ya tukio hilo, wananchi hao walifika kituoni hapo kwa lengo la kutaka mtuhumiwa huyo atolewe, ili wamwadabishe, lakini polisi waligoma ndipo ilipotokea tafrani hiyo.

Aidha, hivi karibuni wananchi walivamia kituo cha polisi mkoani Kagera na kukichoma moto, kwa madai kuwa kulikuwa na mahabusu ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kuwa na ngozi za watu.

Matukio ya aina hii yameonekana kushamiri katika jamii, kwani mbali na matukio hayo, mwezi uliopita wananchi wilayani Singida, walivamia Kituo Kidogo cha Polisi cha Ilongero, na kumpiga mtuhumiwa, Mohamed Nkindwa hadi kufa na kisha wakachoma moto kituo hicho.

Tukio hilo lilitokea baada ya kundi la wanakijiji kuvamia kituo cha polisi na kuwazidi nguvu askari 10 kutoka Singida mjini na wengine wafanyakazi wa kituo hicho, na kuanza kumpiga mtu mmoja ambaye alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kuwalawiti hadi kufa watoto wawili.

Wanakijiji hao walidai kuwa polisi hawataweza kumfikisha mahakamani kijana huyo, hivyo waliamua kuchukua sheria mkononi na kumuua.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
Novemba 19, 2007
Mwandishi: Shangwe Thani, Shinyanga
 
Hii ni kwa kuwa wananchi nao wameshapoteza imani na vyombo vyetu vya dola ndio maana wanajichukulia sheria mikononi.
 
Hii ni kwa kuwa wananchi nao wameshapoteza imani na vyombo vyetu vya dola ndio maana wanajichukulia sheria mikononi.

Unajua tatizo kubwa ni pale raia wanapoona wanawakabidhi watuhumiwa mikononi mwa polisi na baada ya siku kadhaa jamaa wanakuwa mtaani wakiendeleza kazi kama kawaida!

Hata ungekuwa wewe unaweza kujikuta unajichukulia sheria mkononi. Hali si nzuri mitaani, polisi wanatakiwa kuchukua hatua kali zaidi na si kuwapa ushirikiano wahalifu.

Ni hayo tu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom