Tafakuri yangu ya leo; tafadhali Kikwete kigawe chama ili UVCCM igawike Mapema

KAMBOTA

Senior Member
Mar 21, 2011
176
103
WASQ.jpg
5.jpg

“ kama ilivyo tofauti ya milima na mabonde ndivyo yapaswa kuwa uadui kati ya waadilifu na mafisadi”


Sijakosea msomaji wangu nayosema ndiyo haswa namaanisha kutoka moyoni yaani naomba usiku na mchana mwenyekiti wa CCM Luteni Jakaya Kikwete akigawe chama chake cha Mapinduzi ili aharakishe pia kugawanyika kwa Umoja wa Vijana wa Chama hiko maarufu kama UVCCM kabla mambo hayajawa mabaya zaidi, nitaeleza kwa hoja kwanini natamani hili litokee haraka?

Kwanza ukiangalia nini kimeifikisha CCM hapo ilipo ? jibu lake ni rahisi tu nalo ni “kuleana” kulikojengwa kwa misingi ya “kujuana” kwa mfumo wa “huyu mwenzetu” na “yule siyo mwenzetu”.

Mfumo huu umeendelea kuitesa CCM tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa maana nyingine mfumo huu ambao nathubutu kuuita wa kihafidhina ndiyo umeivuruga CCM kiasi kwamba kuna sauti za watabiri zishaanza kusikika kuwa CCM iko mbioni kugeuka chama cha upinzani.


Watanzania wanashangazwa na tabia ya chama hiko kushindwa kujipambanua kwenye mambo ya msingi kiasi kwamba kinalazimika kulea makundi yasiyo na maslahi ndani ya chama mwishowe chama kinazidi kudhoofika.

Mifano iko mingi sana ya tabia hii ambayo bilashaka inalelewa na uongozi wa juu wa chama hiko tawala nchini, imefika sehemu uongozi wa CCM umekuwa bubu kwenye maswala ya msingi.

Sasa kila mwenye ushawishi ana kundi lake ndani ya chama hiko kwa maana nyingine ni mantiki kusema kuwa kwa nje CCM inaonekana ina mwenyekiti mmoja tu lakini kwa ndani ina wenyeviti wengi tu kila mtu akiwa na kakundi kake na mtandao wake.


Bila kupindisha maneno naomba niulize swali moja kwa uongozi wa CCM, hivi CCM inadhani mtanzania gani asiyefahamu kuwa kuna hali ya kusigana kati ya Samwel Sitta na Harrison Mwakyembe kwa upande mmoja dhidi ya Edward Lowassa na Rostam Aziz kwa upande mwingine?

Nani asiyefahamu kuwa kuna vuta nikuvute kati ya Samwel Sitta na Andrew Chenge? nani hakumbuki zile kauli zenye utata zilizotolewa na Andrew Chenge dhidi ya Sitta wakati ule wa kinyang’anyiro cha uspika? Sasa katika migawanyiko ya namna hii CCM inasimama wapi? Inavunja vipi minyukano hii?


Sasa kwa chama makini kilipaswa kijipambanue lakini sivyo kwa CCM , unajua hata magwiji wa siasa duniani wanashangazwa na tabia hii ya CCM ya kutaka kuwapatanisha watu waliotofautiana “kimtazamo” na pengine “kiitikadi” kwa maana itikadi ya ujamaa na kujitegemea inazungumzwa tu midomoni.

Kuna wachache sana wanaifuata, viongozi wa CCM wanataka kutuaminisha kuwa kinachoendelea ndani ya CCM ni tatizo la kimaadili tu, huu ni uongo mkubwa kabisa tena waache mara moja kudanganya kwani wakiendelea na propaganda ya namna hii hakuna shaka kuwa watazidi kuyaongeza makundi na mitandao na wenyewe wanafahamu madhara ya mitandao.

Ukweli ni kuwa ndani ya CCM kuna mpasuko wa kimtazamo na kiitikadi miongoni mwa wanachama wake kiasi kwamba chama kinazidi kuyumba.


Chukulia mfano falsafa ya kujivua gamba ilivyoonyesha dhahiri tofauti ya kimtazamo ndani ya chama hiko, hivi unadhani kwa hatua ya baadhi ya wana CCM wakongwe tena wastaafu wa serikali kupinga hadharani kuwashughulikia watu watatu tu kama ilivyoenezwa yaani Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz ni ya kishabiki?

Hivi kwanini waziri mkuu mstaafu Cleopa Msuya na Balozi Paul Ndobho wamepinga hatua hiyo? CCM wanataka tuamini na hawa ni mafisadi? Huu ni uzushi mkubwa hakuna mtanzania atakayeamini upuuzi wa namna hii wa kudai na hawa viongozi wawili wastaafu ni watetezi wa ufisadi, ni nini basi? Huu ndiyo sasa unaitwa mpasuko wa kimtazamo ndani ya chama hiko hakuna haja kupindisha maneno hapa.


Mpaka sasa mpasuko wa kimtazamo unaendelea kukitafuna chama hiko, ona sasa makundi yanavyozidi kuzaliwa, kwa haraka haraka ni kuwa kwa sasa CCM ina makundi si chini ya saba na kuendelea ambayo ni matokeo ya kulea tofauti za kimitazamo ndani ya chama hiko kama ifuatavyo;


Kundi la kwanza ni lile linaloamini kuwa Kikwete aendelee kuongoza chama na serikali tena anafaa sana huku kundi lingine likiamini kuwa Kikwete avuliwe kofia moja hawa wanataka Kikwete aongoze serikali lakini kuwe na mwenyekiti mwingine wa CCM.


Kundi la pili ni lile linaloamini kuwa falsafa ya kujivua gamba ilipaswa iondoe mfumo wote wa ubabaishaji lakini kwa upande mwingine kuna lile linaloamini kuwa tatizo siyo mfumo bali watu hivyo ni lazima hao watu watemwe.


Kundi la tatu ni lile linaloamini kuwa Makamba ameshinikizwa kujiuzulu hivyo ameonewa na mwenyekiti huku kundi lingine likiamini kuwa uamuzi ule wa Makamba kujiuzulu ulikuwa ni muhimu sana huku hawa wakijipa matumaini kuwa Nape anafanyakazi vizuri sana lakini wenzao wanasema Nape ni mropokaji tena bado mchanga kisiasa.


Kundi la nne ni lile linaloamini kuwa kushindwa kwa CCM kwenye baadhi ya majimbo ni matokeo ya mipasuko ndani ya chama hiko lakini kundi lingine linaamini kuwa kushindwa huko ni matokeo ya chama kung’ang’ania wazee.

Kundi hili linaundwa na vijana wengi hawa wanatoa mifano kwenye jimbo la Ubungo ambapo wanadai iwapo CCM ingemsimamisha Nape basi wangeshinda pia wanasema jimbo la Kawe kama angesimamishwa mtoto wa Warioba basi wangelitwa jimbo hilo.


Lakini haya tisa kumi ni kundi jipya lililoibuka ndani ya CCM lililojipachika jina la “VISION 2015” ambalo limeundwa na baadhi ya waliokuwa maswahiba wa Kikwete mwaka 2005 , hawa wanadai ni lazima wakamate dola mwaka 2015 tena wanasisitiza kwa sauti moja “ ni zamu yetu baada ya Kikwete”, sasa katika haya yote iko wapi nafasi ya Kikwete kama mwenyekiti?

Ndiyo maana namtaka Kikwete akigawe chama mapema wasioamini kuwa CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi basi wajiengue, wasioaminui kuwa ufisadi hauna nafasi ndani ya chama hiko wajiengue pia.

Wasioamini kuwa ni wananchi watakaomchagua rais wa 2015 watoke kabisa, pia wasioamini kuwa uamuzi wa Dodoma ulikuwa sahihi waachie ngazi pia. Au iwapo Kikwete ataamua kusimamia kinyume cha haya pia basi wale wanaoamini CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi wakae pembeni.

Wale wasioamini katika ufisadi nao wajiengue, na wale wasioamini kuwa ni mitandao ndiyo itamweka madarakani rais ajaye basi watoke. Halikadhalika wale wanaounga mkono uamuzi wa Dodoma watoke ndani ya CCM.


Njia hii ya kukigawa chama ndiyo pekee itaokoa CCM, Kikwete inabidi aamue yuko upande gani ili wasioafiki wajiengue mapema, mwendelezo ni huu hata kwenye uchaguzi ujao wa UVCCM pia mwenyekiti ajaye na yeye ahakikishe anawagawa vijana katika makundi makuu mawili ili abaki na moja.

Iwapo ataamua kuwa upande wa vijana wanaotumiwa na mafisadi basi ahakikishe wale wanaopinga ufisadi watoke kwenye umoja huo na iwapo ataungana na wale wanaopinga ufisadi basi ahakikishe wale wanaotumiwa na mafisadi watoke mara moja.


Nasema tena imefika wakati Kikwete aigawe CCM ili na UVCCM nayo igawike mapema , HUU NDIYO MWAROBAINI WA MATATIZO YA CCM. Kinyume na hili ni kukiua chama, juhudi zozote za kuwaleta meza moja watu wenye mitazamo tofauti na itikadi mbalimbali ndani ya chama hicho hakuna ubishi kuwa CCM itakuwa imejichagulia “kaburi” badala “giza” ingawaje hata kwenye kaburi kuna giza pia..

Tafakari!



Kitendawili si deni ukishindwa nipe mji,
Wenye upungufu wa akili hupenda kuweka kikomo cha Uhuru,
Kwa wanataaluma kutofautiana kimawazo si kosa bali ni uhai wa jamii husika,
Nova Kambota Mwanaharakati,
Nipigie; 0717-709618 (Ndani yaTanzania) au +255717-709618 (Nje ya Tanzania)
Niandikie; novakambota@gmail.com
Kwa habari zaidi za uchambuzi nitembelee; www.novatzdream.blogspot.com
Tanzania, East Africa,
Jumapili 15, May 2011.
 
Back
Top Bottom