Tafakuri Yangu Ya Leo; Katiba Mpya Tunamaanisha Kweli Au Tunacheza Makida makida? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tafakuri Yangu Ya Leo; Katiba Mpya Tunamaanisha Kweli Au Tunacheza Makida makida?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by KAMBOTA, Apr 14, 2011.

 1. K

  KAMBOTA Senior Member

  #1
  Apr 14, 2011
  Joined: Mar 21, 2011
  Messages: 176
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  pinda and kikwete.jpg
  “He who knows not and knows not that he knows not is a fool”

  Hii ni nukuu katika kitabu cha mwandishi nguli wa Nigeria Chinua Achebe inayopatikana kwenye kitabu chake kiitwacho A Man Of The People, katika ukurasa wa 294 kwenye kitabu hiko. Tunapoendelea na kile tunachoita mchakato wa kupata katiba mpya naona nguvu za wanasiasa zinavyotupeleka puta kiasi kwamba tunaonekana tunacheza mchezo maarufu wa watoto uitwao makida makida huku vijana wetu wanaonunuliwa kwa bei rahisi kwenda kutukana watu wakidhani wanajua kumbe hawajui kwamba hawajui kwa maana nyingine ni wapumbavu.
  Ndiyo tunacheza makida makida, kama tungekuwa hatuchezi makida kwanini kuna minyukano na misigano ya kukomoana kwenye mchakato huu? Nashindwa kuelewa kwanini watoto wa sekondari za kata wanasombwa kwa wingi na kupelekwa kwenda kuzomea? Rejea gazeti la Mwanahalisi la jana ukurasa wa 5 kwenye makala ya Abel Ndekirwa yenye kichwa cha habari Ya Tambwe, Makamba na janga la CCM, ambapo mwandishi anatueleza jinsi kaimu katibu kitengo cha propaganda na uenezi CCM Bw Hizza Tambwe alivyokusanya vijana wadogo na kuwajaza Karimjee kwa lengo la kuzomea wasemaji wote ambao sio CCM na kweli inadaiwa vijana hao waliifanya kazi yao vizuri ya kuzomea wasio wana CCM na kuwashangilia wana CCM pia katika gazeti hilo ukurasa wa 13 katiba habari yenye kichwa cha habari Mjadala wa katiba kama usanii, ambapo mwandishi anatueleza jinsi vijana wadogo walivyosombwa na kiongozi wa UVCCM wa Buguruni kwa ujira wa shilingi 2,000 kwenda Karimjee kwa kazi ya kuzomea wasio CCM na kushangilia wana CCM.
  Kwa matukio haya machache ni ushahidi kuwa tunacheza makida makida ndio maana hata vijana wale waliosombwa hawajui hata tofauti ya muswada na sheria, inatia huzuni kwamba hawafahamu hata muswada ni nini? sio jambo la kuchekesha hata kidogo ndio maana vijana wale hata walipofika pale Karimjee baada ya kuchoka kushangilia na kuzomea wakaanza kulala ovyo, inauma sana!
  Cha kusikitisha zaidi inaelezwa kuwa vijana hao baadhi yao ni kutoka shule zetu za kata na wengine ni vijana wa vijiweni wasio na ajira, Mungu atuepushie dhambi hii yaani kweli mwanasiasa wa chama Fulani anathubutu kusomba vijana hawa masikini kwenda kuzomea na kushangilia? Kama kweli anaweza angechukua watoto wa vibopa walioko kwenye shule za saint hizo za kimataifa akawapeleka pale Karimjee lakini kwa hili la kusomba vijana hao masikini kwa ujira wa shilingi 2,000 halikubaliki hata kidogo!
  Ndio maana nasisitiza na nitaendelea kusema kuwa hoja ya katiba mpya ni ya watanzania masikini walala hoi lakini kuna mdudu ameingia katikati , angalia mapungufu ndani ya hiyo rasimu ya marejeo ya katiba ndio utashangaa iwapo walioandaa muswada huo ni wanasheria kweli? na wanafahamu matatizo ya watanzania? Au tuseme wao wameshushwa kutoka mbinguni kiasi kwamba hawafamu yanayowasibu watanzania ndio maana wameandaa muswada wa aina hiyo wenye mapungufu kibao tena ya wazi? Tusemaje basi au watu hao walikuwa wanajipendekeza au waliandaa kutukomesha masikini wan chi hii? au wameandaa kuwaziba midomo Dr Slaa, Mabere Marando, Julius Mtatiro na Dr Kitila Mkumbo? Watwambie waziwazi vinginevyo tuwahoji wakishindwa kutoa majibu yanayoeleweka tuukatae.
  Hivi nani asiyefahamu kuwa wazanzibar walichana muswada huo mbele ya Samwel Sitta? Wasitufanye watoto , tena aliyechana ni kiongozi wa dini, na alichana kwa madai kuwa hauna faida kwa wazanzibar na mwingine aliuita ni ‘utumbo’ nani asiyefahamu kuwa wazanzibar walibeba mabango yaliyomtaka mbunge wa mji mkongwe Sanya kurudi Zanzibar ili wadai talaka kwa watanganyika? Haya si siri nani asiyefahamu pale viwanja vya shule ya Haile Sellasie Unguja kuna bango lilisomeka ‘Muungano hatuutaki jamani’ au kuna haja gani ya kuficha kuwa wazanzibar wanadai kuwa wanataka wapige kura ya maoni iwapo wanautaka muungano au la? Haya yalisemwa na mabango yalibebwa Zanzibar sio mambo ya siri tena.
  Sasa kwa mambo haya yote ya uhafidhina wa kina Hizza Tambwe, vijana kulala kwenye mijadala ya katiba, madai ya wazanzibar na mapungufu chungu nzima ya muswada wenyewe sasa nahoji maswali mawili , la kwanza ni je kuna haja gani ya kina Pindi Chana kuendelea kutumia fedha za umma kwa kazi ambayo dalili zinaonyesha kuwa haitofanikiwa? Kuna haja gani kuhoji wananchi wachache kwenye miji michache? Na pia kama mpaka wasomi wa pale chuo kikuu Dodoma waliwekewa ngumu kuingia ndani je wao hawaruhusiwi kutoa maoni yao kwenye huu muswada? Swali la pili ni kwa mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi hali ya mambo ilivyo hivi ni kweli katiba mpya tunamaanisha au tunacheza makida makida tu?


  Kitendawili si deni ukishindwa nipe mji,
  Kwa wasomi kutofautiana kimawazo si kosa bali ndio uhai wa jamii husika,
  Nova Kambota mwanaharakati,
  0717-709618 au 0766-730256,
  novakambota@gmail.com
  www.novatzdream.blogspot.com
  Tanzania, East Africa,
  Alhamisi 14 April, 2011.
   
Loading...