Tafakuri ndefu na ya kina kutoka Bungeni kuhusu kutorusha LIVE Mijadala ya Wabunge Bungeni.

S

S.N.Jilala

JF-Expert Member
540
500
Tafakuri ndefu na ya kina kutoka Bungeni.

Ni marufuku kurusha majadiliano ya Bunge moja kwa moja kwenye Luninga (Television).

Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Michezo na Sanaa Nape Nauye kwa mara ya kwanza iliwasilisha habari Bungeni kwa kusema kuwa katika kipindi hiki; Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halitarushwa moja kwa moja (LIVE). Sababu mojawapo alizozitoa ni pamoja na kueleza kuwa TBC wameona ni gharama mno kurusha matangazo moja kwa moja kwa hiyo basi watarekodi na kurusha muda wa saa nne usiku kila siku. Pili, kurusha LIVE kunawafanya wananchi na wengine kutopata muda mzuri wa kufuatilia Bunge kwa sababu huwa wako kazini. Nilivyofatilia taarifa hii kutoka serikalini niliosema sawa si vyombo vya habari kama Azam TV, Star TV, Channel Ten, ITV n.k watarusha na wananchi watapata taarifa za wawakilishi wao namna wanavyojadili mambo yanayowahusu wao moja kwa moja wakati huo serikali ikiangalia upya swala hili.

Jambo la pili na lililonishutua ni la taarifa ya pili, kupitia kwa Waziri huyo huyo akisema kuwa; vyombo vya habari binafsi havitaruhusiwa kurusha vikao vya Bunge moja kwa moja (LIVE), na badala yake Bunge linaandaa TV yake ambayo itakuwa inarusha baadhi ya matukio muhimu na vyombo binafsi vitakuwa vinapata taarifa kutoka katika Television ya Bunge. Hapa kwa wale tunaopenda kufuatilia maswala ya Kitaifa lazima waanze kujiuliza maswali mengi sana; mojawapo ni;

a) Kwa nini mambo haya yanatokea katika serikali ambayo inahubiri kuwa lazima kuwe na uwazi katika mambo yote?
b) Kwa nini maswala ya wananchi yanajadiliwa kwa usiri hivi wakati wa awamu hii kwani kuna jambo gani la siri?
c) Je, Bunge limewajibika kwa namna gani kuzuia hili au limekubali kupokwa Uhuru huu?, Kwa nini kipindi cha maswali na majibu tu kirushwe na tukijua maswali hayo ilishaulizwa serikali muda mrefu na majibu yake lazima yajadiliwe na wanaweka zuio.
d) Je, haki za wananchi ziko wapi katika Uhuru wa habari ambazo zimetajwa hata kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977?.

Mimi naona kuzuia vyombo vya habari kutorusha Mijadala ya Bunge, serikali imepora Haki za Bunge na Wananchi wameporwa haki zao. Vilevile haki ya kupata habari tena zinazowahusu wananchi zimeporwa na serikali pasipo na sababu za msingi. Naona pia kuna uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 kama nitakavyoonyesha hapa chini.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hii hii ya (1977) ambayo inapigiwa kelele na wadau wengi wa maendeleo kwa sababu ya kuonekana kuwa mosi, iko kimfumo wa chama kimoja katika sehemu nyingi na pia imetengenezwa bila kushikiriskisha wananchi wa Jamhuri ya Muungano, katika kipengele cha 62 (1) kimeainishwa vyema kabisa kuwa;

Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo litakuwa na sehemu mbili; yaani;

a) Rais na,
b) Bunge.

Sehemu ya pili ya Bunge ndicho chombo Kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, KJMT 1977 kifungu cha 62 (2)).

Mimi naiona Taasisi ya Urais ndani ya Bunge na si ya Bunge katika maamuzi. Kwa sababu taasisi hii kupitia kwa Waziri wa Habari, Michezo na Sanaa ndio wamezuia kurusha matangazo ya moja kwa moja na si Bunge kujadili na kukubaliana kwa sababu za msingi bali imetoka amri kutoka kwa Waziri kwa kisingizio cha gharama, mara tena vyombo binafsi navyo vikapigwa marufuku kurusha matangazo.

Lakini ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaonyesha wazi kuwa; Bunge ndicho chombo Kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, KJMT 1977 kifungu cha 62 (2)).

Kwa mujibu wa KJMT 62 (3), kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza;

(a) Kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;
b) Kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;
c) Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
d) Kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;
e) Kujadili na uridhiria mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.

Ukiangalia madhumuni ya Bunge ya utekelezaji wa madaraka yake utagundua na kujiuliza maswali mengi; kwa mfano, kwa nini warushe kipindi cha maswali na majibu na wasirushe wajibu mwingine au maeneo mengine kama nilivyoiorozesha hapo juu?; yaani b,c,d,e hili ndo swali ambalo linakinzana na linaibua maswala mengi sana.

Kwa mfano, chombo ambacho huwa ni mwiba kwa wanaotumia ovyo Mali za umma ni Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa serikali. Na hili pia Umma hautaona ni namna gani Bunge lina wawajibishwe wale waliotumia ovyo Mali za umma. Pia, cha kusikitisha zaidi ni kuwa haya mambo hayatajadiliwa kwa uwazi ili wananchi waone yanayoendelea. Kwa mfano, Halmashauri nyingi hazitekelezi maoni ya CAG na za Kamati za Bunge haya maswala tungetoa kuwa kuyaona wananchi namna yanavyojadiliwa.

Natambua sana serikali hii inapambana na rushwa na mengi tunaisifia serikali hii, lakini tuwe wazuri wa kuishauri ikikosea na tusiogope na kuona kuwa serikali hii haikosei katika maamuzi yake, ili ijirudi na ijitafakari kuwa imekosea. Na Bunge nalo hasa wale ambao wako kimya katika jambo hili au wanaounga mkono jambo hili naona hawajui madhara yake. Watanzania wamekuwa makini sana miaka yote kufatilia sera na mijadala inayowahusu wao, lakini kwa sasa hawajui kinachoendelea na vyombo vya habari kama magazeti, TV, n.k navyo vinakosa taarifa za ndani kutoka ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.

HAKI YA UHURU WA MAWAZO.

Katika sehemu ya Haki ya Uhuru wa Mawazo. KJMT, (1977), kifungu cha 18(d), kimeandikwa kuwa, kila mtu; anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia wa kuhusu masuala muhimu kwa jamii. Katika hili, ukiangalia kitendo cha kuzuia urushaji wa matangazo ya moja kwa moja cha Bunge ni kuwanyima haki wananchi kupata taarifa.

Psychology said "Guilty is coward - Mwovu ni mwoga "

Katika kipengele cha Uhuru wa Habari serikali nyingi hujitahidi kuminya UPATIKANAJI wa habari kadri ya uwezo wao. Serikali ya awamu hii nayo isipojitathimini vyema katika swala hili la Bunge yaani kunyima bunge lisirushwe moja kwa moja mpaka taarifa zichujwe, hakika, serikali hii itaonyesha uoga wa wazi kabisa katika sehemu hii ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja.

Nini kifanyike?

1. Wafikirie vyema serikali katika jambo hili na Bunge likiongozwa na Spika wa Bunge lijitathimini vyema katika jambo hili;

2. Kama wataona wao kupitia chombo cha wananchi TBC ambao ndio walipa kodi na kodi yao ikiwa inatumika katika kukiendesha chombo hiki, basi waachie vyombo binafsi virushe matangazo moja kwa moja;

3. Kama wanavyodai kuwa. Bunge litakuwa na TV yake na itarusha moja kwa moja, basi wana wajibu wa kurusha kupitia TV Bunge ili wananchi waone na kujifunza mengi kuhusu maisha yao.

Simon Jilala
26/4/2016
 

Forum statistics


Threads
1,425,226

Messages
35,085,100

Members
538,249
Top Bottom