Tafakuri: Kwanini sisi Tusiweze Kuwachabanga kwa Kiswahili chetu?

Nietzsche

JF-Expert Member
Dec 5, 2014
206
391
Bunduki ni silaha nzuri sana. Toka igunduliwe, bunduki imewasaidia watu katika mambo mengi. Imewasaidia watu kwa kuwapatia kitoweo kama vile kwale – nakumbuka nilipokuwa mdogo, baba yangu alikuwa akinichukua porini kwenda kuwinda kwale. Bunduki pia imewasaidia watu katika kujilinda dhidi ya wanyama wakali wa mwituni kama mbwa-mwitu; na hata katika vita, mataifa yao yalipovamiwa na mataifa mengine. Kwa hakika, kuvumbuliwa kwa bunduki kumeyabadili maisha ya watu kwa namna yake.

Kwetu sisi Afrika, bunduki zilipoingia zilikuwa maalum kwa watawala, “watemi”. Akina Mirambo wa Unyamwezi na Béhanzin wa Dahomey, kwa mfano. Bunduki hizi zilitamba sana kiasi kwamba, ili waweze kuzimiliki, watawala walifikia hatua ya kuuza vito na amana zao nyingi – kama almasi, pembe za ndovu, na hata watu (watumwa). Amana hizi waliziuza kwa wageni walioleta bunduki kutoka Ulaya. Bunduki zikawa kama “status symbol” (alama ya hadhi) kwa watawala (The Cambridge History of Africa, Vol. 5, circa 1790-1870).

Hata hivyo, haikuwachukua muda mrefu wanadamu kugundua kwamba, pamoja na mazuri yake yote, kumbe bunduki nazo zilikuwa na madhara! Tena basi wakabaini kwamba, zikitumika vibaya madhara yake yanaweza yakawa na athari mbaya zaidi hata kwao wenyewe: bunduki zinaweza zikawaua!

Katika uhalisia wake, bunduki ziligunduliwa ziwatumikie watu. Lakini baada ya umaarufu wake kusambaa na kugeuka kuwa “status symbol”, fikra zikabadilika, na badala ya kuwatumikia watu, watu wakazitumikia na hata kuzisujudu bunduki. “Wenye hadhi” wakatembea nazo viunoni huku wakizifyatua ovyo kila walipojisikia “kujimwambafai”, walipoghadhabika, au walipolewa pombe. Na hapo ndipo madhara yake yaliposhamiri. Nyenzo hizi za kigeni zikawageukia watu. Ili kuondokana na madhara haya, ilibidi watu watahadharishwe, wasahihishwe, na kufundishwa kanuni sahihi za utumiaji wa bunduki (Parker, 1996, “The Military Revolution: Military Innovation and the Rise of the West”).

Sambamba na utumiaji wa bunduki, tawala zetu za Kiafrika pia zilitumia pinde, mishale na mikuki ya sumu. Japokuwa kuingia kwa bunduki ndani ya bara letu kulizuzua watu, ukweli ni kwamba silaha zetu za jadi nazo hazikuwa haba. Dr John Thornton, mwanahistoria kabambe wa Chuo Kikuu Cha Boston anasema “rekodi nzima inapochambuliwa, inaonyesha vikosi vya Ulaya vilivyokuwa na bunduki vilishindwa mara kadhaa kwa kushambuliwa na vikosi vya Kiafrika vilivyotumia mikuki au mishale ya sumu” (Thornton, 1999, “Warfare in Atlantic Africa”).

Hii inaonyesha kwamba, hata baada ya bunduki kufika, bado Waafrika walipigana kwa umahiri zaidi wakitumia silaha za jadi. Hili pia linathibitishwa na “Warugaruga”, askari machachari wa Mtemi Mirambo waliowatwanga Waarabu na bunduki zao kila walipopigana nao. Laiti kama teknolojia yetu ya silaha za jadi isingeelemewa na teknolojia ya silaha za kigeni, nafikiri sasa hivi tungekuwa tumeshaziendeleza, tukaziboresha, na kuziimarisha zaidi. Upinde kwa mfano, umekuja kuendelezwa na hao hao wageni waliotuzubaisha kwa silaha zao za kigeni, na sasa kuna pinde madhubuti za kisasa, rahisi kutumia, na zenye usahihi bora zaidi (better precision), wenyewe wakiziita “crossbows”.

Ujio wa bunduki kwetu Afrika unanikumbusha kitu kingine kilicholetwa na wageni – lugha! Lugha nyingi zinazotumika Afrika sasa hivi nazo zimeletwa na wageni kwa meli kama jinsi wageni hao walivyotuletea bunduki zao kwa meli. Kuanzia Kaskazini mpaka kusini mwa Afrika, Kiswahili tu ndiyo lugha halisi ya Kiafrika inayotumiwa kama “lugha rasmi” na nchi chache za ukanda wa Mashariki, zikiongozwa na Tanzania. Nchi nyingine barani Afrika zinatumia aidha Kiingereza (Ghana, Nigeria, Gambia, Zimbabwe, n.k.), Kifaransa (Kongo, Kameruni, Burkinafaso, n.k.), au Kiarabu (Misri, Sudan, Libya, Algeria, Moroko, n.k.).

Hili ni jambo linalofikirisha. Lakini kinachofikirisha zaidi ni kwamba, kama tu ambavyo silaha zote huundwa ili ziwatumikie wanadamu, lugha zote nazo huundwa ili ziwatumikie wanadamu. Na hivyo, kwa kutumia kurunzi hiyo hiyo ya “bunduki dhidi ya mishale”, ningependa kuirejesha tafakuri yangu hii katika suala la lugha, ili niutumie muktadha wake kulimulika songombingo la “Kiingereza dhidi ya Kiswahili” nchini Tanzania.

Kwangu mimi, Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kisukuma, Kinyamwezi na hata Kichina, vyote ni vitendea kazi. Hizi ni lugha tu. Na hata kama lugha moja itakuwa na thamani zaidi kuliko lugha nyingine, thamani yake haiwezi kuishinda thamani ya watumiaji wa lugha hiyo wanaojaribu kuitumia kwa shida, kama ambavyo thamani ya bunduki isivyoweza kuishinda thamani ya mtumiaji wake anayeitumia kwa shida, hata kama mtumiaji huyo ni askari aliyekubuhu katika medani ya vita na ambaye, kama angepewa upinde na mishale, angeweza kuwaokoa mateka wote kutoka mikononi mwa adui.

Sijui ni wangapi waliiona sinema maarufu ya “Rambo: First Blood” utotoni mwao. Humo, askari hodari, mkongwe wa vita vya Vietnam, John Rambo, anapigana na kikosi kizima cha maaskari wenye bunduki na helikopta, huku yeye akiwa na kisu na mawe tu, lakini anapambana nao na kuwachabanga vibaya! Hali kadhalika, Rambo anaonyesha kuwa na weledi katika maeneo mengine, kama vile “survival skills”, au mbinu za kuulinda uhai wake katika mazingira magumu. Simulizi hizi ziko nyingi. Na nyingi kati ya hizo ni tohozi (adaptations) za mambo ya kweli.

Lakini swali ni je, kama John Rambo angepewa bunduki na badala ya kuitumia bila matatizo akaitumia kwa kuhangaika na hivyo, baada ya kuona inamsumbua, akaamua kuiweka pembeni ili aendelee na kisu chake, hilo lingempungunzia “uhodari” wake katika maeneo mengine ya uaskari wake? Na je, angestahili kuchekwa na kudhihakiwa kwamba yeye ni mtu dhalili kwa kuwa tu hajui kutumia “silaha za kisasa”, au angestahili kukosolewa kiueledi? Kama askari aliye na weledi wa kutumia silaha zote za jadi ila bunduki, unafikiri Rambo angestahili kutendewaje katika muktadha huu?

Na katika muktadha huo huo, je ni sahihi kuwacheka na kuwadhihaki wale wanaokosea kuongea Kiingereza kwa kuwa tu hawayatoshelezi matakwa ya “usomi” ya wale wanaowadhihaki, ingawa wakipewa “upinde na mishale” wataweza kuyatosheleza matakwa ya jamii kushinda hata wale wanaoyatosheleza matakwa binafsi ya “usomi” ya wanaowadhihaki? Au na sisi tunataka kukifanya Kiingereza kuwa kama “status symbol” za “usomi” wetu, kama watemi wetu walivyozifanya bunduki kuwa kama “status symbol” za utemi wao?

Kujivunia “usomi”, na hasa kwa kumdhihaki binadamu mwenzetu pale anaposhindwa kuvifikia viwango vyetu vya usomi tulivyojijengea, ni kuutumikia usomi wetu badala ya kuuacha usomi wetu ukatutumikia sisi. Majivuno si mazuri. Yanachusha. Lakini kuna kujivuna na kujivuna; kuna kujivuna kubaya na kuna kujivuna kuzuri. Kujivunia nchi yetu au kujivunia lugha yetu kwa mfano, siyo kitu kibaya. Lakini kujivunia “hadhi” yetu kwa kuwanyanyapaa wale wasiokuwemo katika kundi la “wenye hadhi”, hiyo siyo siha njema.

Hivyo, mimi nafikiri tukiwacheka au kuwadhihaki watu wasiojua Kiingereza tutakuwa tunapotoka. Kwa mfano, ni sawa kumkosoa Mwalimu Ndalichako, lakini siyo sawa kumcheka. Kama John Rambo, Ndalichako ni mmoja wa “askari” wetu wazoefu aliye na weledi katika maeneo mengi kama vile takwimu na hisabati. Tusiusahau “uaskari” wake wote kwa kukumbatia kipengele kimoja cha uaskari huo – “bunduki”. Badala yake tumsaidie kwa kuiboresha “mishale” yake, yaani Kiswahili, na kwa kumwelekeza kiungwana aitumie “bunduki” yake sawasawa. Hizi ni silaha tu; zinapaswa zitutumikie sisi watu badala ya kusujudiwa na jamii na kisha kutumiwa kuwadhihaki watu.

Lakini muhimu zaidi ni kwamba, tunapaswa turudi nyuma kidogo tuliangalie suala hili kihistoria zaidi na kwa upana wake, kisha tufanye maamuzi magumu. Je, tukiendeleze Kiswahili chetu au tukiendeleze Kiingereza chao? Tunaweza tukakiendeleza Kiswahili chetu na bado tukajifunza Kiingereza chao – kwa faida yetu, siyo kwa faida yao – kama alivyofanya Vladmir Putin. Inawezekana. Lakini ningeshauri, “emphasis” au msisitizo uwe kwenye Kiswahili chetu. Tusisahau kuienzi bahati tuliyotunukiwa, ya kuwa “waasisi” (pioneers) wa lugha halisi ya Kiafrika iliyoweza kuvuka mipaka na kutumika katika hadhira na vyuo vikuu vikubwa takribani vyote duniani (Oxford, Cambridge, Glasgow, SOAS, n.k.).

Kama vile utumiaji wa bunduki katika tawala zetu ulivyoupiku utumiaji wa silaha za jadi na hivyo kuutuamisha ukuaji wa silaha hizo, ndivyo utumiaji wa lugha za kigeni utakavyoupiku utumiaji wa lugha za Kiafrika na hivyo kuutuamisha ukuaji wa lugha hizo. Historia ya Mirambo imebeba falsafa nzito na mafundisho mengi. Historia hiyo inatuachia tafakuri hii tunduizi: kama Warugaruga waliweza kuwachabanga Waarabu na bunduki zao kwa mishale yao, na kama Wachina wanawachabanga Wamarekani na Kimarekani chao kwa Kichina chao, kwanini sisi tusiweze kuwachabanga Waingereza na Kiingereza chao kwa Kiswahili chetu?
 
Nimejaribu kukusoma mwanzo nikawa sijakuelewa. Ila hapo mwisho ndio nimeelewa 'target' yako ni nini hasa.

Waingereza wana msemo wao kuwa 'The end always justifies the means'.

Watu makini duniani kote wanapambana kuifanya dunia iwe mahala pazuri zaidi pa kuishi, hivyo hatua yoyote inayofanywa inapaswa kuwa na lengo hilo.

Kwanini unataka watu waendelee kutumia baiskeli za miti ( eti kwa kuwa ndio inaelekea kwenye ukuaji kiteknolojia ) wakati tayari kuna ugunduzi mkubwa ushafanywa kuelekea ambako na wewe huenda unaelekea ?

Tatizo Waafrika tumeshindwa vibaya sana kwenye 'Succession'

Ndio maana hata umasikini hautaisha.

Suala la lugha na maarifa liachwe huru na kila mmoja apewe fursa ya kujifunza kadri ya uwezo wake !

Huwezi Kucompromise Hatma ya watanzania zaidi ya milioni 50 ili kuridhisha nafsi au kufunika dhaifu la mwanasiasa mmoja.

Yaani unataka kiingereza kionekane si lolote si chochote kwasababu Magufuli kinampiga chenga, ili watu wote wafanane nae, kweli ?
 
Back
Top Bottom