Tabora: Watumishi 653 wamepandishwa vyeo

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,458
Halmashauri ya Manispaa Tabora imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja watumishi wake 653 wa kada mbalimbali katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake.

Pongezi hizo zimetolewa Aprili 4, 2022 na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Ramadhan Kapela ambaye pia ni Diwani wa Kata ya lsevya katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa watumishi wote waliopandishwa vyeo pia wamebadilishiwa mishahara jambo ambalo limewapa ari mpya ya utendaji hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao walikaa muda mrefu sana bila kupandishwa vyeo.

Alibainisha kuwa licha ya watumishi hao kuendelea kuchapa kazi, hatua hiyo italeta tija kubwa katika kutekeleza majukumu yao, hii ni motisha kubwa kwa mtumishi wa umma.

“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kujali watumishi wake walioko katika sekta mbalimbali, tunamwahidi kuwa tutaendelea kumuunga mkono katika kila hatua ya utendaji wake,” alisema.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Dkt Peter Nyanja alisema Serikali ya awamu ya 6 imetenga jumla ya sh bil 2.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo katika mwaka huu wa fedha.

Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Februari mwaka huu halmashauri imepata jumla ya sh bil 30.9 ambazo ni sawa na asilimia 66 ya lengo lake, kati ya fedha hizo sh bil 3.2 zimetokana na makusanyo ya ndani, sh bil 17.1 ni ruzuku ya mishahara kutoka serikali kuu, sh bil 2.4 ni ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka serikali kuu na sh bil 8.2 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo kutoka serikali kuu.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia halmashauri hiyo imetoa mikopo ya jumla ya sh mil 662.5 kwa vikundi 129 vya wanawake vijana na wa tu wenye ulemavu.

Aidha, jumla ya wanachama 1,119 wamenufaika na mikopo hiyo na kujikwamua kiuchumi ambapo kati ya fedha hizo sh mil 311.9 ni kutokana na mapato ya ndani na sh mil 350.5 ni marejesho ya mikopo.

Dkt Nyanja alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mambo makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa utawala wake, ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara kwa wajasiriamali wadogo na kuongoza nchi kwa amani, usawa na utulivu.

Chanzo: Majira
 
Hizi ndio habari njema familia zinazidi kubadilisha mboga

Sio ile Awamu ya roho mbaya.
 
Back
Top Bottom