Tabitha Siwale: Waziri wa kwanza mwanamke Tanzania

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Saturday, 26 May 2012 21:59
tabithasiwale.jpg


Mrs. Tabitha Siwale

Na Florence Majani

NILIPOFIKA nyumbani kwake maeneo ya Kawe kwa Warioba, nilidhani nitamkuta ndani.

Wakati nabisha hodi, ninamuona akivuka barabara kuja nilipo.

Mwanamke mweusi, aliyevalia vazi la kitenge anasimama mbele yangu, pamoja na umri wake wa miaka 75, lakini sura yake bado imebeba uzuri wake wa ujana.
Huyu ni Tabitha Ijumba Siwale, Waziri wa kwanza mwanamke, nchini Tanzania.

Siwale ambaye kwa sasa amejikita zaidi katika shughuli za kanisa, na usimamizi wa Taasisi ya Jinsia na Makazi ya WAT-Human Settlement, anasema kufika hapo alipo kumetokana na jitihada.

Anasema, alianza kupenda siasa tangu akiwa kinda."Wakati ule bado hatujapata uhuru, nilikuwa najipenyeza katika mikutano ya TANU ili nipate kusikia wanayozungumza," anasema

Anasema, baba yake alimkataza kujihusisha na siasa na kumtaka asome kwanza lakini yeye aliipenda sana siasa.

"Sikupenda siasa pekee, bali hata shughuli za mahakama, baba yangu alikuwa mtu wa mahakamani kwa hiyo nilivutiwa zaidi na kazi hizo," anasema Mama Siwale.

Mama Siwale kitaaluma ni Mwalimu. Anasema, alipata mafunzo ya Maarifa ya Jamii katika Shule ya Wasichana ya Geita kabla ya kupata taaluma ya ualimu huko Mpwapwa na baadaye alikwenda kujinoa zaidi katika Chuo Kikuu cha Nairobi kwa miaka mitatu.

"Nilianza kufundisha mwaka 1961, hata siku tuliyopata uhuru, nilikuwa tayari ni Mwalimu," anasema

Anaitaja shule yake ya kwanza kufundisha kuwa ni shule ya wasichana ya Bwiru.

Hata hivyo, katika kipindi chake chote cha ualimu, alikuwa akitunukiwa vyeo vya kuwa mkuu wa shule tu, na si mwalimu wa kawaida.

"Niliweza kuzisimamia shule zile na zikawa imara, kwa mfano, Korogwe Girls wakati ule ilikuwa ndiyo inafaulisha wanafunzi wengi waliokwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam," anasema

Anawataja baadhi ya wanafunzi wake ambao anajivunia kwa kuwa walipita mikononi mwake ni Naibu Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Mataifa,(UN) Dk. Asha -Rose Migiro na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu,(HLRC)Helen Kijobisimba.

Wakati huo huo, Siwale anasema, walimu wakuu wote waliitwa kwenda kupata mafunzo katika Chuo cha Siasa cha Kivukoni.

"Huo ulikuwa ni mpango wa taifa wa kuwafanya Watanzania waijue siasa ya Tanzania, ndiyo maana walimu wakuu tulipelekwa Kivukoni ili tuisafirishe taaluma hiyo kwa wanafunzi," anasimulia.

Anaitwa na Nyerere Ikulu
Siku moja,akiwa bado mafunzoni Kivukoni, alipata mgeni. Ingawa mgeni yule alikuwa ni rafiki yake, lakini ujumbe wake ulimtisha.

"Alikuja Peruzi Butiku, mke wa Joseph Nyerere, aliniambia hayati Mwalimu Julius Nyerere, amemtuma aje anichukue na kunipeleka Ikulu," anasema

Anasema, aliogopa, kwani hakuwahi kutegema mtu mkubwa, Rais wa nchi kumwita.

"Baada ya Peruzi kusisitiza, ilinibidi niende hivyo hivyo, nikaonana na Rais," anasema

Anaongeza: " Mwalimu aliniambia kuwa, ameniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu vya Rais."

Anasema, alikubali ingawa hakujua ni kwa nini Mwalimu Nyerere alimteua yeye.

Usiku huo huo, Redio Tanzania ilitangaza majina ya wabunge wanawake wa Viti Maalumu wapatao kumi, akiwemo.

Baada ya wiki moja, aliitwa tena Ikulu, lakini safari hii hakushtuka.
"Nilipofika, Rais alinipa mshtuko mwingine ambao sikuutegemea.

Aliniambia amenichagua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini," anasema.

Anasema, alikubali wajibu huo mzito, akiwa ni mwanamke wa kwanza Tanzania kushika cheo cha uwaziri.

"Niliingia Ikulu nikiwa na amani, lakini nilitoka nikiwa nimechanganyikiwa kwa kile nilichoambiwa," anasema Mama Siwale akicheka.

Mama Siwale aliishika nafasi hiyo tangu mwishoni mwa mwaka 1975 hadi 1982 alipohamishiwa Wizara ya Elimu.

Anasema: "Lakini mwaka 1984, nilipelekwa Wizara ya Elimu,"
Mwaka 1984, aliachia uwaziri na kubaki na ubunge hadi mwaka 2000 alipostaafu.

"Nilikaa ndani ya Bunge kwa miaka 20, nilifurahia sana nafasi yangu kwa sababu niliipenda siasa," anasema.

Anasema, akiwa bungeni alipenda kupigania mambo mawili, nafasi ya mwanamke katika jamii na umiliki wa ardhi na makazi.

Mama Siwale anajisikia fahari, si yeye pekee bali hata na wanawake waliokuwa bungeni kipindi kile, kwa kutetea hoja hadi kufanikiwa kuundwa kwa Sheria ya Ardhi na Jinsia ya mwaka 1999 .

"Sheria ile inatumika hadi leo, inasema, mwanamke ana haki ya kumiliki, kuuza na kutumia ardhi kama ilivyo kwa mwanaume,"anasema.

Anachowaasa wanawake

Mama Siwale anasema, hakuwahi kupata changamoto za kutisha wakati alipokuwa mwanasiasa kwa kuwa hakuwa mwoga.

"Neno sijui, siwezi … kwangu ni mwiko. Nikiambiwa nifanye kazi hii, naifanya kwa nguvu zote na lazima ionekane," anasema

Anawaasa wanawake na kuwaambia, wawe na jitihada na wadhamirie makubwa.
"Chochote unachofanya sasa, fanya vizuri kana kwamba hutopata nafasi ya kukirudia. Ili watu wakiiingalia kazi yako, wakukubali," Anasema.

Mwanasiasa huyu mkongwe, aliwahi kutunukiwa Tuzo ya Mwanamke Mahiri wa Karne ya 21 mnamo mwaka 2000 na Taasisi ya Kimarekani.

Aidha, mwaka 2008, alipata Tuzo ya Mwanamke wa mwaka kutoka taasisi hiyo hiyo.

Amewahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwemo uenyekiti wa Kampuni ya Uvunaji wa Maziwa (DAFCO) na Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wakati huo, likiitwa (NPF)

Hivi sasa ni Mlezi wa Taasisi ya Wanawake na Makazi ya WAT-Human Settlement.

Mama Siwale ni mke wa mwalimu mstaafu, Edmund Siwale. Ana watoto wanne, wawili kati yao ni marehemu, na amebarikiwa wajukuu watatu.
Alizaliwa wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
 
Hawa ndio Mawaziri wanafanya kazi Malipo yao ni Jasho lao kazini, Wanakumbuka Fahari za Kazi zao na Matokeo ya hizo.

fahari kama alimfundisha Naibu Secretary General wa UN Asha Rose Migiro (Mtengeti) Anaishi Kawe, hakuwa FISADI

Hawa ndio wachapakazi taifa letu sasa hivi linawahitaji sababu ya Mali tulizo nazo sasa.
 
Nilimjua kwa jina tu lakini sikujua kuwa alikuwa mrembo namna hiyo kwa vile sikuwahi kumwona physically. Kweli katika kipindi cha nusu ya pili ya miaka ya 70, ni shule tatu tu zilizokuwa zinachachafya Tanzania kwa kutoa Division I: Weruweru, Korogwe Girls na Kibaha.
 
Hawa ndio Mawaziri wanafanya kazi Malipo yao ni Jasho lao kazini, Wanakumbuka Fahari za Kazi zao na Matokeo ya hizo

fahari kama alimfundisha Naibu Secretary General wa UN Asha Rose Migiro (Mtengeti) Anaishi Kawe, hakuwa FISADI

Hawa ndio wachapakazi taifa letu sasa hivi linawahitaji sababu ya Mali tulizo nazo sasa.
Ni huyu mama hakuwa fisadi, ila kuishi kwake kawe hakumaanishi that is the only land aliyonayo!. Yeye ndiye mmiliki wa kile kiwanja chenye maduka na appartments ile kona ya Msasani kwa Mwalimu, opposite na BP Petrol ststition!
 
Haya mambo ya mwanamke wa kwanza, mwafrika wa kwanza, mtanzania wa kwanza, mweusi wa kwanza ndio yanayoendelea kudumisha uhaba wa usawa. Hatujui tu
 
Haya mambo ya mwanamke wa kwanza, mwafrika wa kwanza, mtanzania wa kwanza, mweusi wa kwanza ndio yanayoendelea kudumisha uhaba wa usawa. Hatujui tu

Kweli kabisa mpendwa,

Hata mimi yananikera sana, basi tu sijui nifanye nini kuyakomesha!!

Unajua hata mimi ni mwanamke wa kwanza kupata shahada ya chuo kikuu nyumbani kwetu, sasa sijui kama hii nayo ni ishu? akili zetu zimekaa kikekike na kiumeume, lini akili zetu zitakaa kibinadamu zaidi? mimi hata ungenipa urais leo, siwezi kuunda wizara ya wanawake, jisia sijui na nini, nitaunda wizara ya maendeleio ya jamii tu na hili jina linajitosheleza kabisa!

Kweli safari bado ndefu!!

Mbarikiwe sana

Glory to God!
 
Ni huyu mama hakuwa fisadi, ila kuishi kwake kawe hakumaanishi that is the only land aliyonayo!. Yeye ndiye mmiliki wa kile kiwanja chenye maduka na appartments ile kona ya Msasani kwa Mwalimu, opposite na BP Petrol ststition!.
.....................Wizara ya Ardhi pia kapitia !
 
Kile kiwanja pale kona ya msasani,nafikiri alikipata wakati ule kukiwa pori na maji yanajaa maana miaka ya 90 mwanzoni bado palikuwa kibanda kimoja tu. Akaanza kuendeleza taratibu sana hadi leo unaona vile. Angekuwa fisadi ukute alikuwa viwanja 30 vya beach
 
Back
Top Bottom