Tabia ya wazazi kuwapeleka Watoto Mijini kufanya kazi yapelekea DC Lushoto kuagiza Wahitimu wa Darasa la Saba kuripoti Shuleni kila wiki

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika ametoa agizo kwa wazazi wa wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba mwaka huu kuhakikisha wanafunzi hao kila siku ya Jumatano ya wiki wanaripoti katika shule zao za msingi walizosoma na kuitwa majina.

DC Lugangika ametoa agizo hilo lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi hao hawatoki nje ya wilaya au mkoa wa Tanga hadi hapo watakapochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Akizungumza na HabariLEO jana, mkuu huyo wa wilaya alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi ambao watoto wao wanapohitimu darasa la saba wengi huwapeleka katika miji mikubwa kufanya kazi jambo ambalo ni kinyume cha haki za watoto na wengi huwa hata wakichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza hawaripoti shule.

"Nimetoa agizo kwa walimu wakuu wa shule za msingi na maofisa elimu kata kuhakikisha wanasimamia hilo la mahudhurio ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu, wanahudhuria shule kila siku ya Jumatano na kuitwa majina hadi hapo watakapopangiwa shule za sekondari za kujiunga na kidato cha kwanza."

"Hii ni kutokana na tabia ya baadhi ya wazazi ambao wanawatoa watoto wao waliomaliza darasa la saba kwenda katika miji mikubwa kufanyishwa kazi matokeo yake wengine wakichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari hawaendi, hili ni agizo mzazi au mlezi yeyote atakayekwenda kinyume hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.

Wilaya ya Lushoto ina jumla ya shule za msingi 251, ambapo Halmashauri ya Bumbuli ina shule 83 na Halmshauri ya Wilaya ya Lushoto ina shule 168.

Kwa muda mrefu kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi na walezi katika wilaya hiyo watoto wao wakishahitimu elimu ya msingi huwaruhusu watoto wa kike kuchukuliwa na watu katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kazi za ndani.

Watoto wa kiume hupelekwa mijini kufanyishwa biashara ndogo ndogo na wengine huamua kujishughulisha na shughuli za kilimo.
 
Back
Top Bottom