Taazia: prof. Immanuel Kilima Bavu hupigi goti kwake kusoma ila atakuacha na elimu ya kudumu

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,787
30,083
TAAZIA: PROF. IMMANUEL KILIMA BAVU HUPIGI GOTI KWAKE KUSOMA ILA ATAKUACHA NA ELIMU YA KUDUMU
Miaka mingi sasa imepita lakini mengi ya yale aliyonifunza Prof. Immanuel Kilima Bavu bado nayakumbuka.

Siku ya kwanza alipoingia darasani kukutana na sisi wanafunzi wake kwenye somo lake, ‘’Theories of Decision Making,’’ alituambia, ‘’Mimi nimesomesha kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu.’’

Prof. Bavu alikuwa mwalimu mwema ambae mwanafunzi lazima utampenda.

Alikuwa hatishi wanafunzi na akijaribu sana kuwafanya wanafunzi wake walipende somo analofundisha hasa kwa namna ya ufundishaji wake na zaidi jinsi alivyokuwa akitufunza kwa mifano halisi ya Tanzania ambayo alikuwa akituambia kuwa lazima tutakutananayo tutakapokwenda kushika nafasi za uongozi katika mashirika ya umma.

Prof. Bavu alikuwa hachoki kutusisitizia kuwa tuna jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa mashirika ya umma tunayaendesha ipasavyo kutokana na elimu tunayopata hapo chuoni.

Alikuwa anapenda kutuambia, ‘’Hapa mimi nitakufundisheni kila kitu katika vitabu kinachohusu kufanya maamuzi, ‘’rational decisions,’’ maamuzi ambayo yataleta tija katika ufanisi wa kazi lakini lazima mtambue kuwa yapo mengine itabidi mtumie akili zenu wenyewe ili mambo yaende sawa.’’

Prof. Bavu alikuwa na Kiingereza kizuri si mchezo, utapenda kumsikiliza na hapo yupo mbele darasani hana ‘’notes,’’mkononi kila kitu kinatoka kichwani na alikuwa na kawaida ya kutabasamu wakati wote.

‘’Ngojeni nikupeni mfano mdogo,’’ Prof. atasema.

‘’Uko ofisini unatengeneza ‘’board papers,’’ za Board Meeting kesho asubuhi saa tatu. Inafika karibu saa tisa hivi umeme umekatika ofisi haina ‘’generator,’’ mnasubiri umeme urudi hadi saa kumi inaingia umeme haujarudi. Haya niambie unafanya nini na kazi yako bado haijakamilika.’’

Hapa Prof. Bavu atanyamaza kusubiri jibu kutoka kwetu.
Darasa zima kimya.

Wanafunzi tunakuna vichwa na kukodoleana macho labda mwenzangu atatoa jibu.

Yawezekana swali hili Prof. kauliuliza mara chungu nzima na wanafunzi hawatoi jibu ila kukuna vichwa na kutumbua macho.

‘’Hamfungi ofisi na kwenda nyumbani kwani kazi bado haijakamilika na ikiwa mtaondoka kazi haijakamilika labda mkategemea kuwa kesho asubuhi na mapema mtawahi ofisni kukamilisha kazi ya jana mkitegema kuwa umeme utakuwapo, huo utakuwa uamuzi mbaya sana kwani kesho asubuhi yawezekana umeme ukawa bado haujarudi. Sasa ikiwa umeme haukurudi na ‘’Board Papers,’’ hazijawa tayari kwa ajili ya ‘’Board Meeting,’’ ukimwambia Mkurugenzi Mkuu kuwa makaratasi ya kikao hayajawa tayari kwa kuwa umeme ulikatika jana na wewe ukaona kuwa hiyo ni sababu ya maana, Mkurugenzi Mkuu yeye anajua atafukuzwa kazi siku hiyo hiyo sasa yeye kabla hajafukuzwa kazi ataanza kukufukuza kazi wewe.’’

Hapo tumejiinaamia tunachukua notes kama tuna wazimu vile, tunataka kila neno la Prof. Bavu tulihifadhi.

Prof. Bavu akatufunza ‘’concept,’’ ya ‘’Futuristic,’’ mimi neno hili kwa mara ya kwanza nimelisikia kwake na kanifunza mwalimu wangu Prof. Bavu.

‘’Kuna mtu huu darasani anajua, ‘’Futuristic,’’ ni nini?

Hapo sasa macho yote yanakwenda kwa Mwingereza wa darasa jamaa mmoja, lakini kwa bahati mbaya na yeye hana moja ingawa pengine akili yake inamtuma kufukiria kuwa bila shaka hii, ‘’futuristic,’’ itahusu mambo ya baadae.

Yule jamaa kajipinda kajificha kwanza nyuma ya mgongo wa mwenzake aliyekaa mbele yake kisha kajibonyeza chini Prof. Bavu asimuone wenzake wanamuangalia akamsimamisha kujibu swali.

‘’Futuristic,’’ Prof. ataendelea baada ya kutambua kuwa hatuna tulijualo, kwani sisi ndiye wale ‘’sukmun bukmun humyun.’’

‘’Futuristic ni kuangalia mbele na kufikiria kinachoweza kutokea na ikawa umekiona kimetokea na wewe ukapanga mambo yako kwa ile hali ya kilichokuwapo. Hapa kilichokuwapo ni kuwa umeme hakuna. Kwa kuwa umeme hakuna na kazi lazima ikamilike siku hiyo basi unahamisha ofisi yako yote na kazi yako mnakwenda Kilimanjaro Hotel pale kuna Secretarial Bureau ‘’state of the art,’’ unakwenda kukamilisha kazi yako hata kama itabidi mkae hadi saa sita usiku na gharama katika hali kama hiyo zisikuzuie kukamilisha jukumu lako.’’

Hapa Prof. Bavu atamaliza mhadhara wake kwa kutuambia kuwa, ‘’Mkurugenzi Mkuu atakupongeza na ile gharama ya kupeleka kazi ‘’secretarial bureau,’’ wala haitamshughulisha ataidhinisha ilipwe haraka na pengine atatoa motisha kwa watumishi wote waliokamilisha kazi ile katika mazingira yale magumu.

Siku moja Prof. Bavu kaniona mitaa ya Administration Block nazubaa zubaa akanisalimia kumbe kilichomvutia ni yale makaratasi niliyokuwa nimebaba natembea huku nikayachakura.

Akaniuliza nini nimebeba nikamjibu kuwa ni mswada wa kitabu.
Unaandika kitabu?

Nikamjibu basi akaniomba aangalie.

Kwa haraka haraka nikaona vidole vyake vinatembea na kichwa kinaanza juu kuja chini ishara kuwa alikuwa anasoma kwa haraka.
Akaniuliza kitabu hiki kinahusu kitu gani.

Nikamjibu kuwa naandika maisha ya Abdulwahid Sykes.

Prof. Bavu alishtuka kidogo akaniangalia kisha akarejea kupitia karatasi zangu.

‘’Huyu Mohamed Mabosti ni nani?’’ Prof. akaniuliza.

Alikuwa amemsoma katika yale makaratasi, Mohamed Mabosti ambae katika miaka ya 1950 alipata kuwa President wa Young Africans Football Club.

Nikamfahamisha nikamwambia kuwa jina lake hasa lilikuwa Mohamed Sultan lakini hii, ‘’Mabosti,’’ ni lakabu, alipachikwa kwa ajili ya utanashati wake katika mavazi na akitembea kwa maringo wakati wa ujana wake.

Akatingisha kichwa kisha akanirejeshea makaratasi yangu.

Siku moja miaka imepita na Prof. Bavu katoka Chuo Kikuu nadhani alikwenda UNESCO, Paris.
Mtu akafungua mlango wa ofisi yangu namwangalia namwaona ni Prof. Bavu.

Haraka nikasimama nikatoka nyuma ya meza kwenda kumlaki na kumpokea mwalimu wangu kwa taadhima zote uzijuazo.

Alipomaliza kunieleza kilichomleta nikamwambia twende kwa Mkurugenzi Mkuu Athmani Janguo.

Tulipofika kwa Mzee Janguo mie nikamtambulisha Prof. Bavu kama mwalimu wangu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Mzee Janguo akacheka na Prof. Bavu pia akawa anacheka.

‘’Mohamed, wewe Prof. Bavu kakusomesha Chuo Kikuu, mimi kanisomesha shule ya msingi.’’
Hakika nilipigwa na butwaa.

Miaka michache iliyopita Prof. Bavu alikuja nyumbani kwangu kaongozana na Mzee Paul Sozigwa.
Katika mazungumzo nikamwambia Mzee Sozigwa kuwa itapendeza kama ataandika historia ya maisha yake kwani kaona mengi akiwa mwandishi wa Mwalimu Nyerere.

Prof. Bavu akaniambia, ‘’Mohamed, kazi hiyo ungeifanya wewe.’’

Iko siku mimi na mke wangu ambae sote alitusomesha tulikwenda kumtembelea nyumbani kwake.

Prof. alifurahi sana na kuna wakati aliniletea ujumbe nikamtembelee tuzungumze kuhusu makala fulani aliyosoma ambayo wandishi nilikuwa ni mimi.

Bahati mbaya sana kipindi hicho ndiyo Barabara ya Morogoro ilikuwa katika kujengwa na kufika kwake ilikuwa tabu sana.
Kwa ajili hii sikuwahi kwenda kwake.

Mara nyingi sana nimemkumbuka Prof. Bavu pale nilipokabiliwa nilipokuwa kazini nimekalia kiti changu na ikabidi mimi lazima kufanya maamuzi magumu.

Nikawa nakumbuka moja ya usemi wake, ‘’The buck stops here.’’

Kwangu ndiyo mwisho wa habari zote.

Sina wa kumtupia mzigo maamuzi lazima niyafanye mwenyewe.

Nikifika hapa nikawa namkumbuka Prof. Bavu kuwa alitufunza kutumia akili zetu kwani kuna mambo hayamo kwenye vitabu.

Naamini wanafunzi wake wengi waliozagaa kila mahali na kila pembe ya dunia kila mmoja wetu kuna alichorithi katika hazina kubwa ya Prof. Bavu ambayo na sisi kokote tulipo lazima tuwamegee wengine kwa heshima ya mwalimu wetu.

Pumzika kwa Amani mwalimu wangu Immanuel Kilima Bavu.

PICHA: Katikati ni Prof. Immanuel Kilima Bavu kulia ni Dr. Ibrahim Msabaha na kushoto ni Mwandishi.
Picha ya pili kushoto Prof. Immanuel Kilima Bavu, Mwandishi na Mzee Paul Sozigwa

PROF. BAVU.jpg
PROF. BAVU NA PAUL SOZIGWA.JPG
 
Dah...hongera sana Mkuu...historia nzuri....angalau safari Nyerere na Bakwata umewasitiri

Sent using Beretta ARX160
Rohombaya,
Kuna mtu aliniuliza kwa nini kila unapotaja historia ya TANU lazima umtaje na Abdul Sykes?

Mimi nikamjibu kwa kumuuliza swali.

Unaweza kuandika historia ya Azimio la Arusha bila kumtaja Nyerere?

Unaweza kuandika historia ya TANU bila ya kumtaja Abdul Sykes?

Watu wanatajwa kwa stahili zao.
Ikiwa unaona nakosea nifahamishe.

Nyerere na BAKWATA historia inawataja kwa stahili zinazowagusa.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nikajua tanzia

Sent using Jamii Forums mobile app
mfate...
Mimi zamani nikiandika, "tanzia."
Mshairi na Mtaalamu wa Kiswahili," Abdilatif Abdallah akanisahihisha akasema ni taazia kwa lahaja ya sisi watu wa Pwani.

Sasa hata ukiandika, "tanzia," ni sawa hujakosea.

Watu wanasema, "mapungufu," "masaa" au "lisaa."

Mimi siwezi kuzungumza hivyo kwangu ni "upungufu" na "saa."

Watu wanasema, "kidole cha kwanza," kwetu ni, "kidole cha shahada."

Mimi naweza kukuapia kuwa nikopeshe hela nitakulipa siku kadhaa na katika kuapa nikasema, "Baratuminnallah."

Au nikamwambia, "Nakushika kidevu cha Mtume."

Mswahili atakuwa kanielewa.

Tukizungumza namna hii utotoni lakini lugha inakua na mabadiliko katika semi huwezi kuyaepuka.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Sijui yuko wapo sasa, ila Bavu tulifundisha naye pale chuo kikuu cha Dar es Salaam. Kuna wakati alikuwa anakaa pale magorofa ya getini kutoka chuo cha maji karibu na akina Lwaitama.
 
13 Reactions
Reply
Back
Top Bottom