Taasisi ya Kukuza Maendeleo Vijijini (PRIDE Tanzania) ilivyotafunwa

Manyerere Jackton

JF-Expert Member
Dec 11, 2012
2,436
4,429
Pride Inakufa
JAMHURI, toleo Na. 337

Taasisi ya Kukuza Maendeleo Vijijini (PRIDE Tanzania) inachungulia kaburi.
Hali hiyo imesababishwa na kile kinachoelezwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha na ufisadi baada ya taasisi hiyo kuonekana kama haina mwenyewe.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, imeanza kuwachunguza viongozi wa PRIDE (Promotion of Rural Initiative and Development Enterprises Limited) wanaohusishwa kwenye ufisadi huo.

Uchunguzi huo unafanywa ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kutolewa kwa taarifa ya Mkaguzi wa Ndani iliyosheheni maelezo ya namna viongozi wakuu wa PRIDE Tanzania walivyochota fedha. Ukaguzi huo ni wa Januari hadi Novemba, mwaka jana na taarifa yake iliwasilishwa kwenye kikao cha Bodi ya PRIDE cha Februari, mwaka huu. Ukaguzi huo ulifanywa na Apolinary Mwijage (CPA).

Gazeti la JAMHURI limepata nakala ya Ripori ya Mkaguzi wa Ndani inayoonyesha kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, mwaka jana pekee, fedha zilizotumika na ambazo hazina maelezo ya kuridhisha ni Sh bilioni 1.481.

PRIDE tayari ina wanachama zaidi ya 100,000 katika matawi 72 nchini kote; na hii ina maana kuyumba kwake kunaashiria kuyumba kwa uchumi kwa maelfu ya Watanzania. Ilianzia katika mikoa mitatu ya Arusha, Tanga na Dar es Salaam. Makao Makuu yake yako Arusha.

Imebainika kuwa kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kikitolewa benki na kupelekwa kwenye ofisi ya malipo ambako baadaye kiliwafikia walengwa kwa kutumia nyaraka zilizoghushiwa na ambazo hazikuwa na viatambanisho kwa mujibu wa taratibu za fedha.

Malipo mengine yalifanywa kwa ‘mtu wa tatu’ kwa fedha taslimu badala ya hundi kama miongozo ya fedha ya PRIDE inavyoagiza. Pia imebainika kuwa malipo ya mamilioni ya fedha yamefanywa kwa kisingizio cha kuwalipa watoa huduma mbalimbali wa PRIDE, lakini mwishowe fedha hizo zikaingia kwenye akaunti za wakuu wa kampuni ya PRIDE.
Kwa mtiririko huo wa utoaji fedha unaodaiwa kutozingatia taratibu, imebainika kuwa Mkurugenzi Mkuu, Rashid Malima, kwa nyakati tofauti aliweza kuchota Sh milioni 334.84; na baadaye alitoa kwenye akauti kiasi cha Sh milioni 275.582 kwa kutumia kadi ya AMEX.

Fedha nyingine, Sh milioni 213. 048 zilitolewa na Meneja wa Fedha, Alfred Kasonka; Sh milioni 23.4 zilitolewa na Maltin Ndibaika; Sh milioni 338.204 zilitolewa kama malipo ya awali ya mishahara, lakini hakuna nyaraka za kuthibitisha hilo; Sh milioni 126.227 zililipwa kama marejesho ya mikopo lakini hakuna nyaraka; na kiasi kingine cha Sh milioni 170 hazijulikani zililipwa kwa shughuli gani.

Kwenye ukaguzi huo wa ndani imeelezwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kilichodaiwa kutumika kuwalipa watoa huduma wa PRIDE, lakini kikawa kinawekwa kwenye akaunti binafsi za Mkurugenzi Mkuu Malima. Baadhi ya waliodaiwa kutoa huduma na wakaandaliwa malipo yaliyoishia kwenye akaunti ya Malima ni Arusha Arts kwa ajili ya matengenezo ya magari ya PRIDE. Pia baadhi ya fedha anadaiwa kuzichukua kama malipo ya awali ya mishahara (salary advance), lakini baadaye kwenye mshahara wake akawa hakatwi. Kiasi kinachodaiwa kupotea kwa mtindo huo ni Sh milioni 338.204 ambacho ni cha kuanzia Januari hadi Novemba, 2017.

Mchanguo wa baadhi ya fedha zilizochukuliwa na Malima ni kama ifuatavyo: Januari 26, 2017 zilichukuliwa Sh milioni 15 kupotia vocha Na. 166 kwa ajili ya malipo za matengenezo ya gari kwa Arusha Art, lakini vocha ikasainiwa na Malima.

Februari 1, 2017 Malima alichukua Sh milioni 27 zikiwa ni malipo ya awali ya mshahara kupitia hundi Na. 364571. Vocha ya malipo haikusainiwa, lakini malipo hayo yaliingia kwenye akaunti iliyoko Benki ya BOA.

Februari 17, 2017 Malima alichukua Sh milioni 10 kwa vocha ya malipo Na.341 kwenda kwa Arush Art kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa matengenezo ya gari la ofisi. Fedha hizo zikawekwa kwenye akaunti yenye jina lake katika Benki ya BOA.

Machi 10, 2017 zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 20 kwenda kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi. Hati ya malipo iidhinishwa na Malima, na fedha taslimu zikaingizwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Benki ya Stanbic.
Machi 16, 2017 ilitolewa hundi yenye Na. 364659 kwa ajili ya usafiri. Imebainika kuwa malipo hayo hayakuidhinishwa na Meneja wa Fedha.

Tarehe hiyo hiyo zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 15 kwenda kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi kwa hati ya malipo Na. 542. Hakuna invoisi wala stakabadhi iliyotolewa na mtoa huduma kuhalalisha malipo hayo.

Machi 17, 2017 inaonyesha kuwa zilitolewa fedha taslimu Sh milioni 15 kwa Antelope Safaris Ltd kugharimia safari za viongozi wa PRIDE. Muidhinishaji malipo alikuwa Malima lakini hakuna invoisi wala risiti kutoka kwa mtoa huduma huyo.

Machi 27, kiasi kingine cha Sh milioni 17 kiliidhinishwa na Malima kwa kampuni hiyo hiyo ya Antelope kwa ajili ya safari ya viongozi wa menejimenti, lakini pia hakuna stakabadhi kutoka kwa mtoa huduma.

Machi 24, 2017 Sh milioni 5 ziliidhinishwa na Malima kwa ajili ya safari huku kumbukumbu zikionyesha kuwa Meneja wa Fedha hakuidhinisha malipo hayo.
Machi 24 vocha Na. 596 ilitumika kutoa Sh milioni 15 kwa ajili ya malipo ya matengenezo ya gari la ofisi kwa Arusha Art huku kukiwa hakuna risiti ya malipo hayo kutoka kwa mtoa huduma.

Aprili 12, 2017 Sh milioni 16 zinadaiwa kulipwa kwa Antelope Safaris Ltd kwa ajili ya safari za viongozi wa PRIDE, lakini hakuna risiti ya malipo kutoka kwa mtoa huduma. Badala yake, fedha hizo zikaingia kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Benki ya BOA.

Aprili 24, 2017 Sh milioni 26.5 zilitolewa kupitia hundi Na. 157621 kwenda kwa Essence International Ltd kugharimia mafunzo. Vocha ya malipo haikusainiwa na mtoa huduma, na badala yake fedha hizo zikawekwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima iliyoko benki ya BOA.

Aprili 28, 2017 zilitolewa Sh milioni 2 kwa Arusha Art kwa matengenezo ya gari la ofisi. Malipo yaliidhinishwa na Malima na hakuna risiti kutoka kwa mtoa huduma huyo. Mei 21, 2017 Sh milioni 5 zinadaiwa kupelekwa Arusha Art kwa matengenezo, lakini kama ilivyokuwa nyuma hakuna risiti ya mtoa huduma.

Juni 5, 2017 Malima alilipwa Sh milioni 10 kupitia hundi Na. 157736 kama ‘salary advance’, lakini kiasi hicho hakikukatwa kwenye mshahara wake wa mwezi huo kama sera ya PRIDE inavyoagiza. Hati ya malipo ilisainiwa naye mwenyewe.

Juni 9, 2017 akachukua tena ‘salary advance’ ya Sh milioni 6 na hazikukatwa kwenye mshahara wake. Julai 18, 2017 zilichukuliwa Sh milioni 5 kwa ajili ya kuwalipa Essence International Ltd kwa kile kilichodaiwa kuwa ni gharama za mafunzo. Mkaguzi wa Ndani hakuonyeshwa risiti wala hati ya malipo kutoka kwa mtoa huduma.

Agosti 17, 2017 Malima alichukua dola 6,500 (Sh milioni 15) kwa hundi Na. 158148. Siku iliyofuata, alichukua dola 3,500 (Sh milioni 8.05) kama ‘advance salary’ yake lakini hakuna nyaraka za kuhalalisha malipo hayo.

Agosti 23, 2017 alichukua Sh milioni 8 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa kutumia hundi Na. 158185 lakini baadaye ikabainika kuwa Sh milioni 3.005 aliziweka kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima katika Bank M; na Sh milioni 1.985 akaziweka kwenye akaunti yenye jina la Abdallah Malima iliyoko katika benki hiyo hiyo.

Agosti 31, 2017 alijiidhinishia malipo ya Sh milioni 52 kupitia hundi yenye Na. 158193 na kwenda kuziweka zote kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima iliyoko katika Benki ya Stanbic.

Septemba 7, 2017 alichukua Sh milioni 10 ambazo ziliwekwa kwenye akaunti yake ya M-Pesa iliyosomeka kwa jina la Rashid Malima. Septemba 19, 2017 alichukua dola 2,000 ambazo hazina maelezo. Novemba 14, 2017 kiasi kingine cha Sh milioni 3.5 kiliingizwa kwenye akaunti yenye jina la Rashid Malima, katika benki ya Stanbic.

Kwenye ukaguzi huo, inadaiwa kuwa Malima, kwa kutumia kadi ya AMEX (American Express) inayomwezesha kuingia kwenye akaunti ya PRIDE moja kwa moja. Malipo kwa kadi hiyo mwa mwaka ni dola 2,500 (shilingi zaidi ya milioni 10). Kwa kuitumia AMEX aliweza kuondoa Sh milioni 275.582 kwa mchanganuo ufuatao:

Februari 3, 2017 alichukua Sh milioni 80.521 kutoka Bank M; Aprili 3, 2017 alichukua Sh milioni 52.744; Mei 3, 2017 alichukua Sh milioni 35.549 kutoka Tawi la Magomeni; Juni 2, 2017 alichukua Sh milioni 37.42; Julai 13 alichukua Sh milioni 22.5; Julai 14, 2017 alichukua Sh milioni 14.7; na Septemba 4, 2017 Sh milioni 32.146 zilitolewa kwa utaratibu huo.

Pia kiasi kingine cha Sh 126 kinaonekana kutumika kulipa deni la mkopo binafsi wa Malima kati ya Januari-Novemba, mwaka jana lakini nyaraka za kuthibitisha malipo hayo hazikuweza kuonekana wakati wa ukaguzi wa ndani.

Mkaguzi anahoji kuwa kama kiasi hicho cha fedha kimepotea kwa mwaka mmoja wakati PRIDE ikiwa taabani kifedha, je ni kiasi gani kilichopotea wakati ilipokuwa kwenye hali nzuri? Anapendekeza ukaguzi wa kina ufanywe, ikiwezekana kwa miaka minne yote ya nyuma na kuwabaini waliohusika.

Anapendekeza malipo yote yanayokwenda kwa ‘mtu wa tatu’ yafanywe kwa hundi badala ya utaratibu wa sasa wa malipo taslimu ambayo wakati mwingine yanafanywa kupitia akaunti za vigogo wa PRIDE.

PRIDE ni mali ya nani?

Kumekuwapo utata wa umiliki wa PRIDE, lakini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anasema kampuni hiyo ni mali halali ya Serikali.

Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 iliyowasilishwa kwa Rais John Magufuli, Machi 27, mwaka jana ilieleza bayana hali na umiliki wa kampuni hiyo.

Hoja za Ukaguzi na Mapendekezo
Taasisi ya PRIDE Tanzania Limited ilianzishwa Mei 5, 1993 chini ya Sheria ya Makampuni (CAP 212) kwa dhamana. Madhumuni ya kuanzishwa kwa chombo hiki ni kutoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali. Taarifa ya Msajili wa Hazina ilionyesha uwekezaji wa Serikali katika kampuni hii.

Mkahuzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anasema, “Kufikia tarehe 30 Juni, 2008 ilionyesha kuwa hisa zote za PRIDE zinamilikiwa na Serikali. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hazina inayoishia tarehe 30 Juni, 2012, Shirika hili liliondolewa katika orodha ya Mashirika ya Umma. Uhalali na sababu za kuondolewa kwa Shirika hili katika orodha ya Msajili wa Hazina haukuweza kubainika.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, kila Shirika la Umma linatakiwa kupeleka hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha. Hata hivyo, hesabu za PRIDE Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwenye Ofisi yangu kama inavyotakiwa na sheria.

“Pamoja na majibu ya Serikali kuwa kampuni imeacha kupata fedha kutoka Serikali ya Kifalme ya Norway na Tanzania mwaka 2005, haijawekwa wazi jinsi hisa za kampuni hii zilivyohamishwa kwenda kwa wamiliki binafsi. Hivyo basi, ninaendelea kusisitiza kuwa Msajili wa Hazina anapaswa kufuatilia kwa karibu juu ya umiliki wa kisheria wa hisa za PRIDE Tanzania zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali na baadaye kuhamishiwa kwa wamiliki binafsi.”

Majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anaweka bayana majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali ambayo yanaeleza kuwa: “PRIDE Tanzania ilisajiliwa kama kampuni yenye umiliki kwa dhamana na sio umiliki kwa hisa, hivyo Serikali haikuwa na hisa.
“Hata hivyo, Serikali ipo kwenye mchakato wa kuibadilisha PRIDE Tanzania kutoka kampuni yenye umiliki wa dhamana na kuwa kampuni yenye umiliki wa hisa chini ya Msajili wa Hazina ambaye atakuwa na umiliki wa kampuni kwa asilimia 100.”

Maoni ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu

“Nasisitiza kuwa, bado haijawekwa wazi ni kwa jinsi gani umiliki wa Serikali katika shirika ulivyohamishwa kwenda kwa wamiliki binafsi. Hivyo basi, ninaendelea kusisitiza kuwa Msajili wa Hazina anapaswa kufuatilia kwa karibu juu ya umiliki wa kisheria wa hisa/dhamana za PRIDE Tanzania zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali na baadaye kuhamishiwa kwa wamiliki binafsi.”

Mvutano mkubwa
Mei, 2016, aliyekuwa Msajili wa Hazina, lawrance Mafuru, alisema PRIDE si mali ya Serikali, akitumia kigecha cha kwamba taasisi hiyo haipo mahali popote kwenye kumbukumbu za ofisi hiyo. Alisema anachojua ni kuwa Pride ni asasi isiyo ya serikali (NGO).

Hata hivyo, ripoti zote za CAG zimekuwa zikionyesha kuwa uanzishwaji wa PRIDE ulifanywa kwa fedha za Serikali ya Tanzania na ya Norway kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali kiuchumi

Msimamo wa Mafuru unashabihiana na wa Malima ambaye anasema PRIDE iliandikishwa mwaka 1999 chini ya sheria ya makampuni ikiwa ni kampuni iliyo chini ya wadhamini isiyokuwa na hisa.

Malima anasema mwaka 2008 PRIDE ilikuwa taasisi ya Serikali, lakini mwaka 2010 iliondolewa, na kwamba CAG hana taarifa hiyo na ndiyo maana hajui kwanini haikaguliwi na ofisi yake.

Machi 30, 2015, akijibu swali bungeni, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, aliongeza utata wa umiliki wa taasisi hiyo baada ya kusema si mali ya Serikali.
Alisema Pride Tanzania ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa kama kampuni Mei 5, 1993 chini ya wadhamini wasio na hisa (Company Guarantee, Not Having Share Capital) kulingana na Sheria ua Makampuni. Malima alikuwa akijibu swali la Amina Mwidau aliyetaka kujua sababu za PRIDE kupotea kwenye orodha ya taasisi za Serikali ambayo ndiyo iliyoiwekea dhamana wakati ikianzishwa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa baadhi ya viongozi, kwa niaba ya Serikali walioshiriki kuanzisha PRIDE ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Salmon Odunga; na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Damas Daudi.

Baadhi ya wadhamini wa awali ni ni Idi Simba, Dk. Abdallah Kigoda (marehemu), George Kahama (marehemu), Christoina Nsekela, na Mama Lubambe aliyekuwa akiiwakilisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

JAMHURI limeambiwa kuwa kuna wakati aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, aliagiza Sh milioni 900 ziwekwe PRIDE kwa ajili ya kusaidia juhudi zake za kuwakomboa wajasiriamali.

“Unaweza kusema wakati wa uenyekiti wa Idi Simba hali ilikuwa nzuri tofauti. Ilivyo sasa ni kama Bodi haina meno kabisa. Wadhamini wa sasa ndiyo wanahisa hao hao, unaweza kujiuliza kama shirika hili ni la watu binafsi kwanini wanaliibia?” Kimehoji chanzo chetu.

Baadhi ya Wajumbe wa Bodi wa sasa ni Rashid Malima, James Obama, Salman Odunga na Dk. Edmund Mndolwa, aliyejiuzulu baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baadhi ya wateja waliozungumza na JAMHURI jijini Arusha wamesema taasisi hiyo inakabiliwa na wakati mgumu kifedha, na wengi wao wanajiandaa kuiacha. Hadi mwaka juzi, ilikuwa ikidaiwa Sh bilioni 5.5 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).

Vyanzo vya habari ndani ya PRIDE vimesema malipo ya wafanyakazi ya NSSF hayajafanywa tangu mwaka 2016. Deni hilo linakadiliwa kuwa Sh bilioni 2.7. Pia wafanyakazi wake hawajalipwa mishahara kuanzia Januari, mwaka huu. Aidha, malipo ya PAYE yanayokadiliwa kufikia Sh bilioni 3 hayajalipwa.

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi, amezungumza na JAMHURI ofisini kwake mwishoni mwa wiki na kuthibitisha kuwa taasisi hiyo imeanza uchunguzi ndani ya Pride.

“Tuna wiki sasa tunafanya uchunguzi, hilo naweza kulithibitisha, lakini tunachunguza nini hilo siwezi kukueleza maana linaweza kuathiri kazi yote tunayoifanya,” amesema.
Ameulizwa kama ameshamhoji Malima, na kusema, “Bado hatujazungumza naye (kumhoji), tunazungumza naye kulingana na mwelekeo wa kile tunachokichunguza.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Malima, alizungumza na JAMHURI kwa simu na kuahidi kuzungumza kwa masharti ya kuonana na mwandishi.

“Hili jambo siwezi kulizungumza kwenye simu, nadhani ni vizuri tuonane ili nami nione hayo uliyonayo. Ofisi zetu ziko Arusha,” alisema.

Lakini alipoulizwa kuhusu ripoti ya Mkaguzi wa Ndani, akasema kuwa hata yeye hajaiona ingawa taarifa za uhakika zinathibitisha kuwa ripoti hiyo iliwasilishwa kwenye kikao cha Bodi kilichoketi Februari, mwaka huu.

“Kuna vitu viwili hapo, hilo la ripoti siyo langu, ni la Mwenyekiti wa Bodi. Mtafute huyo, lakini hata sijaiona kwa hiyo siwezi kusema lolote. Siwezi kuongea kwa sasa bila kuiona kwanza,” alisema.

Mwandishi wa JAMHURI alifika Arusha ili kuzungumza na Malima, lakini akajibiwa ofisini kuwa yuko safarini Dar es Salaam. Alipotafutwa kwa simu hakupokea na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi (sms) hakujibu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Pride, Profesa William Lywakurwa, hakupatikana katika simu zake za hapa nchini na zile alizosajili nje ya nchi. Hata alipoandikiwa ujumbe kupitia barua pepe hakujibu. Taarifa zilizopatikana mwishoni kwa wiki zilisema mwenyekiti huyo anatumia muda mrefu kufanya kazi za ushauri wa kitaalamu mjini Abidjan, Côte d'Ivoire.

.tamati…
 
Familia ya malima imeishi kama ya kifalme za kiarabu, bata tu na huyo Abdalah Malima ni mtoto wake yeye anaishi maisha ya starehe sana tangu chuo USIU Nairobi fedha wamezitafuna sana hawa.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom