Taarifa ya Utekelezaji wa kazi wa TAKUKURU kwa Mwezi Oktoba hadi Desemba 2020

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
TAARIFA KWA UMMA

JANUARI 22, 2021
TAARIFA YA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU (M) ARUSHA KWA KIPINDI CHA MWEZI OKTOBA HADI DESEMBA 2020

Ndg. Wanahabari,
Kwa kuwa leo ndio mara ya kwanza kukutana nanyi tangu mwaka huu uanze, naomba kabla ya yote nitumie fursa hii kuwatakieni Kheri ya mwaka mpya wa 2021.

Tumewaita hapa ili kupitia kwenu, tuendelee kuujulisha umma kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Arusha, pamoja na mambo mengine, inaendelea na kampeni kabambe ya uokoaji wa mali zinazoporwa na watu wasio na maadili, zikiwemo mali za Serikali, Mashirika ya Umma na wananchi wanyonge wanaodhulumiwa haki zao, ikiwemo malipo ya fedha zao toka Vyama vya Ushirika, SACCOS, waajiri binafsi, wakopeshaji pamoja na mali nyingine kama vile viwanja, nyumba na vyombo vya usafiri.

Taasisi imekuwa ikitekeleza wajibu huu unaotokana na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 lakini pia maelekezo ya kuwasaidia wananchi wanyonge kutoka kwa Mhe. Daktari John Pombe Joseph Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo amekuwa akiyatoa kwa TAKUKURU na Watanzania wazalendo.


Ndg. Wanahabari,
Napenda umma ufahamu kwamba Operesheni ya ufuatiliaji na urejeshaji wa mali za Serikali na wananchi wanyonge ni zoezi endelevu ambalo linafanyika nchi nzima kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 na kwamba kupitia operesheni hii - kwa kipindi cha miezi mitatu - yaani kuanzia Oktoba 2020 hadi Desemba 2020, TAKUKURU Mkoa wa Arusha imefanikiwa kuokoa Fedha na Mali zenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Tano Sabini na Nane, Laki Tano Themanini Elfu, Mia Tatu Thelathini na Nne (Sh. 578,580,334/-) ambapo kati yake fedha taslim ni Shilingi Milioni mia Tatu Sitini na Tano, laki Tano Themanini elfu, Mia Tatu Thelathini na Nne (Sh. 365,580,334/-).

Fedha hizi ni kodi za serikali, madeni ya vyama vya ushirika na madai binafsi ya wananchi wanyonge yaliyokuwa kwenye hatari ya kupotea kutokana na ubadhirifu, dhuluma na utapeli uliofanywa na aidha watendaji wa serikali, viongozi/wanachama wa vyama vya ushirika, waajiri binafsi, wafanyabiashara au wananchi wasiowaaminifu. Fedha hizi zote, nyumba na magari viliishakabidhiwa kwa wahusika kwa nyakati tofauti.


Ndg. Wanahabari,

Mbali na kufanikisha uokoaji wa kodi ya Serikali, ulipwaji wa madeni ya Vyama vya Ushirika na ya watu binafsi, ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria kupitia Madawati ya Uchunguzi na Mashtaka, Uelimishaji Umma na Uzuiaji Rushwa kama ifuatavyo:-

  1. UCHUNGUZI NA MASHITAKA:
  2. TAARIFA ZILIZOPOKELEWA
Kwa kipindi tajwa jumla ya taarifa 474 zilipokelewa kutoka sekta mbalimbali. Taarifa hizi zilipelekea kufunguliwa kwa majalada 212 ya uchunguzi na majalada hayo yanaendelea kuchunguzwa na chunguzi zake zipo katika hatua mbalimbali.

Pia ushauri yakinifu ulitolewa kwa watoa taarifa kwa malalamiko 262 yaliyoonekana kutoangukia katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007.

B: KESI MAHAKAMANI
Kwa kipindi tajwa, TAKUKURU (M) Arusha imefungua Mashitaka mapya Matano (05) Mahakamani.
Pia Mashitaka Arobaini na Tano (45) yaliendelea Mahakamani yakiwa katika hatua mbalimbali za kimahakama. Aidha kwa kipindi hicho mashauri kumi na sita (16) yalitolewa uamuzi ambapo kati ya hayo, Jamhuri ilishinda mashauri kumi na tatu (13).

  1. ELIMU KWA UMMA:
TAKUKURU (M) Arusha imeendelea kufanya jitihada za kuelimisha Umma juu ya uelewa mpana wa dhana ya Rushwa na pia kuwakumbusha wananchi wajibu wao katika mapambano dhidi ya Rushwa. Uelimishaji huo ulifanyika kwa njia mbalimbali kama ifuatavyo:-

NaKAZI ILIYOFANYIKAIDADI
1SEMINA48
2MIKUTANO/MIJADALA 63
4KUFUNGUA KLABU03
5KUIMARISHA KLABU99
6UANDISHI WA MAKALA12
7MAONESHO03
8TAARIFA KWA UMMA04

  1. UZUIAJI RUSHWA
Katika kipindi cha mwezi Oktoba – Desemba, 2020 TAKUKURU mkoani Arusha imefanya uchambuzi wa mfumo katika uchaguzi mkuu na utendaji kazi wa NSSF ofisi ya mkoa wa Arusha ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo na kushauri namna sahihi ya kuiziba.

MIRADI YA MAENDELEO

TAKUKURU Mkoa wa Arusha imefika na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Katika kipindi tajwa jumla ya miradi ya maendeleo kumi na tatu (13) ikiwemo miradi inayotekelezwa kwa fedha za asilimia 10 ya makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imefikiwa na kukaguliwa.


  1. MIKAKATI YA TAKUKURU (M) ARUSHA KWA KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI, 202I
Ndg. Wanahabari,

TAKUKURU (M) wa Arusha imejiwekea mikakati madhubuti katika kuendelea na mapambano dhidi ya rushwa. Lengo la kuweka mikakati hii ni kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu ya Kuelimisha, Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ufasaha ili kuweza kufikia lengo la kuwa na Utawala Bora Nchini na kuitokomeza Rushwa.

Mikakati yetu inayotekelezwa ni kama ifuatayo;

  1. KUTOA ELIMU YA RUSHWA
TAKUKURU (M) Arusha itaendelea kutoa elimu ya rushwa kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa kuendesha semina, kufanya mikutano ya hadhara, kurusha vipindi vya Radio kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule na taasisi za elimu ya juu. Aidha TAKUKURU mkoa wa Arusha itaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya Rushwa

  1. UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
TAKUKURU (M) Arusha itaendelea kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa ili kuhakikisha kwamba fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali na wafadhili zinatumika kwa usahihi na miradi iliyokusudiwa inakamilika kwa wakati ili kuweza kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

  1. KUFANYA UCHUNGUZI WA TAARIFA ZA VITENDO VYA RUSHWA
TAKUKURU (M) Arusha itaendelea kupokea na kufanyia uchunguzi taarifa zote za vitendo vya rushwa zitakazopokelewa ofisini sanjari na kuhakikisha kwamba wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki. Kwa kipindi tajwa TAKUKURU Mkoa wa Arusha itajikita zaidi katika:



  1. Kufanya chunguzi zinazorejesha kodi ya serikali
  2. Kufanya chunguzi kuhusiana na matumizi sahihi ya fedha za ujenzi wa miradi ya serikali katika sekta za maji, afya, Barabara nk.
  3. Chunguzi zinazohusiana na urejeshaji wa fedha za vyama vya ushirika (SACCOS, AMCOS na vyama vya wafugaji)
  4. Chunguzi kuhusiana na Fedha na Mali za Wanyonge – ikiwemo dhuluma katika Mikopo Umiza
  5. Chunguzi kuhusiana na Rasilimali asilia za nchi kwenye sekta za Maliasili/Utalii na Madini
Kwa sasa ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha inaendelea na kazi ya kufuatilia na kusimamia urejeshwaji wa fedha katika maeneo yafuatayo:-

  1. Fedha za Mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF na PSSF), Fedha za NSSF zinazochunguzwa ni kiasi cha (Sh. 326,335,977/) ambayo ni makato ya watumishi katika sekta binafsi mbalimbali ambayo waajiri walikuwa hawayawasilishi NSSF kwa mujibu wa sheria na pia fedha za mfuko wa PSSF ambazo ni mikopo iliyotolewa kwa SACCOS za AICC (Sh. 435,754,790.46/-) na AUWSA (Sh. 498,111,609.22/-) na baadae SACCOS hizo (AICC, AUWSA) kushindwa kurejesha fedha hizo tajwa kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano. Fedha hizi zinatokana na michango ya wananchi wanyonge hivyo ni muhimu zirejeshwe.
  2. Fedha za pembejeo za kilimo kiasi cha Shilingi Milioni mia Nne Kumi na Nne, laki Tisa na moja, mia Mbili Sitini na Nne (Sh. 414, 901, 264/-) zinatakiwa kurejeshwa. Fedha hizi zilitokana na mkopo wa matreka uliotolewa na Mfuko wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo kwa wakulima kumi wa halmashauri za wilaya za Meru, Arusha na Monduli kati ya mwaka 2013 hadi 2016 na wakulima hao kushindwa kurejesha mkopo huo kwa muda waliokubaliana. Fedha hizi ni muhimu kurejeshwa ili zitumike kukopesha wakulima wengine kama lengo la serikali ya Awamu ya TANO kuwezesha wakulima wengi zaidi kujikomboa kiuchumi.
  3. Fedha za mikopo ya matrekta, hizi ni fedha zinazotokana na mkopo wa matrekta uliotolewa na Shirika la maendeleo la Taifa NDC kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuondokana na utumiaji wa jembe la mkono katika kilimo. Baadhi ya wakulima waliokopeshwa mkopo huo tangu mwaka 2018, hawakurejesha mkopo huo na imebainika kuwa ni kutokana na kuhamasishwa na walaghai kuwa mikopo ya serikali huwa hairejeshwi.
Natumia fursa hii kuwaasa wakulima wote mkoani Arusha waliopata mkopo huu wa matrekta, kupuuza upotoshaji huo na kurejesha fedha zote wanazodaiwa ili kufanikisha nia ya serikali ya Awamu ya TANO ya kuwawezesha wakulima wengi zaidi kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija.

4. Kodi ya serikali zilizo kwepwa na wafanyabiashara wasio waaminifu, uchunguzi huu unahusu kodi kiasi cha Shilingi Bilioni Tisini na Nane, Milioni mia Sita na Mbili, laki Saba Thelathini na Nne, Mia Tisa Thelathini na Sita na Senti Tisini na Sita (Sh. 98,602,734,936.96) zilizopaswa kulipwa kwa mamlaka ya serikali hivyo zinafuatiliwa ili kurejeshwa na kuiwezesha serikali kutekeleza malengo muhimu ya afya, elimu, maji, afya nk.

Kazi hizi zinafanyika kwa kushirikiana na Taasisi na wizara za serikali kama vile NDC, TRA, NSSF, PSSSF na Wizara ya Kilimo. Aidha TAKUKURU Mkoa wa Arusha itaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali katika kurejesha fedha na mali za Serikali na za wananchi wanyonge zilizofujwa au kudhulumiwa.

  1. USIKILIZAJI WA KERO ZA WANANCHI
Ndg. Wanahabari,

Kwa kutambua umuhimu wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, na kwa nia thabiti ya TAKUKURU kuhakikisha kuwa vita dhidi ya rushwa inafanikiwa, TAKUKURU Mkoa wa Arusha imetenga siku ya Jumatano ya mwisho ya kila mwezi, saa moja na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu mchana kuwa siku ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya vitendo vya rushwa. Siku hii ni kwa ofisi zote za TAKUKURU Mkoa wa Arusha (Arusha, Arumeru, Monduli ,Longido, Karatu na Ngorongoro).


Kwa mwezi huu wa Januari 2021, Jumatano ya mwisho itakuwa tarehe 27.01.2021. Usikilizaji huu wa kero za wananchi utafanyika kwa maafisa wa TAKUKURU kutembelea maeneo mbalimbali katika ngazi ya kata na vijiji kupokea kero hizo ambazo zitafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na mrejesho kutolewa kwa wahusika. Hii itakuwa kampeni endelevu ijulikanayo kama ‘TAKUKURU inayotembea’ yenye lengo la kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kusikiliza kero zao. Naomba kutumia fursa hii kuwaasa wananchi wote wa mkoa wa Arusha kufika katika vituo vitakavyokuwa vimepangwa katika maeneo yao na kutoa malalamiko yao kwa maafisa wa TAKUKURU.

Natumia nafasi hii kuviomba vyombo vya habari na wananchi wote wa mkoa wa Arusha wanaonisikiliza, kufikisha ujumbe huu kwa wananchi wengine wa mkoa wa Arusha ili waitumie siku hii maalum kuwasilisha malalamiko yao TAKUKURU na tunawahakikishia malalamiko yote yatakayopokelewa yatafanyiwa kazi kwa wakati na kupewa mrejesho. Ni rai yangu kwamba tutoe taarifa ya vitendo vya rushwa kwa kufika ofisi ya TAKUKURU iliyopo karibu nawe au piga simu kwa namba ya bure 113 taarifa yako itapokelewa na kufanyiwa kazi.

  1. WITO
Ndg. Wanahabari,

Tunatoa WITO kwa jamii na wadau wetu wote kuendelea kutuletea taarifa za wanaojihusisha na vitendo vya Rushwa ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa, kutapeliwa na kunyimwa haki zao.

TAKUKURU tutazipokea na tutazifanyia kazi kwa haraka ili wahusika katika ubadhirifu waweze kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.


KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LANGU.

Imetolewa na:


James G. Ruge – 0738 150 063

MKUU WA TAKUKURU (M) ARUSHA
 
Back
Top Bottom