Taarifa ya Msimamo wa CDM Juu ya Uteuzi wa Tume ya Mchakato wa Katiba Mpya

Ninashukuru kwa hili kwani naamini CDM kimeamua kutoa taarifa hii ili wadau watoe maoni yao. Maoni yazingatiwe wakati wa kutoa msimamo wa CDM. Maoni yangu nilishayatoa, ntarudia kuhusiana na wajumbe ninaowajua vizuri: JAJI WARIOBA, JAJI RAMADHANI, PROF. KABUDI, BUTIKU, na BALOZI SALIMU. Hawa ninawapinga kwa nguvu zote, na sababu zi wazi. Waheshimiwa hawa, mosi, wana misimamo yao binafsi inayopinga hoja za wananchi kutaka Katiba mpya. Kwa mfano moja ya madai ya wananchi kutaka Katiba mpya ni kurejeshwa TANGANYIKA: wanalipinga. WARIOBA ndo usiseme, ameandika mara kadhaa kwenye gazeti la RAIAMWEMA na kwingineko akipinga hoja ya kuwepo kwa TANGANYIKA. Sasa tazama hiyo hoja imeshindwa kabla ya mchakato wenyewe kuanza; na naomba mniweke katika kumbu2 zenu kuwa niliandika kwamba kwa TUME hii, 'futeni wazo la TANGANYIKA, haitarejeshwa'.

Pili, ni mgombea anayejitegemea. PROF MAGAMBA akiwa rafiki wa mahakama ktk kesi ya AG v Rev MTIKILA na JAJI RAMA, wanajua walicholifanyia suala hili: WALILIZIKA kabisa. KABUDI alipewa na RAMA kazi ya kufanya utafiti wa kisheria ili kupata hoja za kuhakikisha kwamba mgombea anayejitegemea haruhusiwi, ilikuwa kimyakimya. Baada ya KABUDI kupata hoja [kwamba (i) MAHAKAMA KUU TZ haina uwezo wa kutamka kuwa kipengele kimoja cha Katiba kinachopingana na kingine hakiko halali kikatiba - unconstitutional, na (ii) Bunge lina mamlaka ya kurekebisha kipengele chochote cha Katiba, yaani hakuna kip. kinacholindwa kwa (a) Katiba yenyewe kutamka kuwa Bunge halina mamlaka ya kurekebisha - entrenchment, au (b) vifungu visivyoweza kubadilika - basic structure] kupitia kesi za INDIA, Kabudi akamtonya RAMA. Ili wasijulikane walichopanga, RAMA akaiambia Serikali kuwa ktk uchaguzi mkuu 2010 mgombea anayejitegemea anaruhusiwa mpaka hukumu ya MAHAKAMA KUU itakapotenguliwa na MAHAK YA RUFAA. Serikali ikafufua kesi yake MAHAK YA RUFANI. RAMA akiitisha MAHAKAMA yote ya RUFANI (full bench) na kumualika KABUDI kama rafiki wa mahakama. HUKUMU yao, wote wakasema: MAHAKAMA KUU TZ haina uwezo wa kutamka kuwa kipengele kimoja cha Katiba kinachopingana na kingine hakiko halali kikatiba - unconstitutional; hivyo kipengele cha Katiba kinachoruhusu mgombea anayejitegemea (yaani ibara 21) na vile vinavyokataza (ibara 39, 47 na 67) ni halali, japo vinagongana. HILI HALIKUWA SUALA KTK KESI HIYO, BALI WAHESHIMIWA HAWA WALILIBUNI ili kuzuia. SWALI LILIKUWA JE, MGOMB ANAYEJITEGEMEA anaruhusiwa na Katiba au la? NDIYO, ndilo lilikuwa jibu.

TATU ni hoja ya kubadilisha kabisa mfumo wa utawala wa nchi hii kwa (1) kupunguza au kuondoa kabisa uteuzi wa RAIS, (2) kuweka majina na IDADI YA WIZARA kikatiba ili RAIS asiunde baraza la mawaziri 60 kwa nia ya kutoa fadhila kwa marafiki, (3) kufuta nafasi za wakuu wa Mikoa na Wilaya: nimefanyakazi na hawa waheshimiwa kwa miaka mingi, sijawahi kuona kazi yao mbali na kukimbiza mwenge na kupokea viongozi. Japo sina ushahidi wa hili ila naamini, hii nayo ni hoja inayopingwa na wateule hao wa RAIS, kwani wenyewe katika maisha yao wamefaidika sana na mamlaka hayo ya RAIS kuteua. Kwa mfano, SALIMU HAJAWAHI KUGOMBEA NAFASI yoyote HAPA NCHINI akachaguliwa. NAFASI zake zote ni za kuteuliwa. Haya ni baadhi tu ...


TAARIFA KWA UMMA


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea kuchambua wasifu wa wajumbe walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba.

CHADEMA kitatoa tamko juu ya uteuzi wa tume husika baada ya uchambuzi kukamilika wa kutafakari iwapo uteuzi husika umezingatia matakwa ya umma na dhamira ya kujenga muafaka wa kitaifa wa kuwa na katiba mpya na bora.


Pamoja na kutaja majina ya wajumbe wa tume, CHADEMA kilitarajia kwamba Rais Jakaya Kikwete angeeleza pia ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika hatua husika.


Katika muktadha huo, Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyoundwa tarehe 20 Novemba 2011 kwa ajili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011; itafanya kikao chake karibuni kupitia taarifa ya uchambuzi unaoendelea kufanywa juu ya uteuzi uliofanyika wa wajumbe wa tume na tamko litatolewa kwa umma kuhusu mchakato huu muhimu kwa maslahi ya taifa.

Itakumbukwa kwamba tarehe 27 na 28 Novemba 2011 Rais Kikwete alifanya mkutano wa siku mbili na viongozi wa CHADEMA kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na pande mbili kukubaliana kuhusu haja ya sheria husika kufanyiwa marekebisho kwa mashauriano na wadau mbalimbali kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa katiba mpya.

Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana tena na Rais tarehe 21 Januari 2012 Ikulu Dar es salaam ambapo kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ilitaarifiwa hatua ambayo ilifikiwa na serikali katika kuanza kuiboresha sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ili ikidhi mahitaji ya kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano na wadau mbalimbali.


Tarehe 22 Januari 2012 Kamati Kuu ilipokea na kujadili taarifa ya Kamati Maalum kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na kujulishwa hatua ambazo serikali ilifikia katika maandalizi ya kuifanyia marekebisho tajwa katika Mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajia kuanza tarehe 31 Januari 2012.

Kamati Kuu iliamua kwamba Kamati Maalum iendelee kufanya mawasiliano na mashauriano na Rais Kikwete na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inafanyiwa marekebisho ya msingi kabla ya mchakato wa kukusanya maoni kwa mujibu wa sheria husika haujaanza.

Kamati Maalum ilitakiwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio matatu ya Kamati Kuu yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu mchakato wa katiba mpya; maudhui ya maazimio hayo ni kama ifuatavyo:

Mosi; “kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki”.

Pili; “Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo”.

Tatu; “viongozi wote wa chama na wa kuchaguliwa katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi”

Imetolewa tarehe 07 Aprili 2012 na: John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
 
Back
Top Bottom