Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,735
- 40,858
Sina tatizo la watu mbalimbali ambao wanakosoa serikali au utendaji wa Magufuli - iwe ni staili yake au vitu vyenyewe anavyovifanya. Demokrasia inajengwa katika kupinga na katika kukosoa; mahali ambapo hakuna ukosoaji wa viongozi au kuwapinga viongozi hakuna demokrasia. Bila ya shaka hapa nazungumzia wananchi kupinga au kukosoa watawala wao.
Kuna mambo ambayo yamefanywa na Magufuli mwenyewe au na serikali yake ambayo wapo ambao hawayakubali na wanaona kama ni geresha 'ile ile' na wana haki ya kusema hivyo bila kubezwa.
Swali langu hata hivyo ni hili; kwa wale ambao wanaona kuwa Magufuli amekosea au anakosea sana katika hili la kutumbua majipu na kujaribu kuleta nidhamu kwa watumishi wa umma (wajibu aliopewa Kikatiba) sasa wao wangependa angefanya nini kwanza? Kwamba ni jambo gani labda angeshughulikia kwanza kabla ya kuanza kutumbua majipu, kusimamisha watu kazi, kufukuza au kufikisha watu mbalimbali mahakamani na kuendelea kuchunguza. Yaani, badala ya kufanya zile ziara za kushtukiza na matokeo yake Magufuli na Waziri wake Mkuu wangefanya jambo jingine; ni lipi hilo?
Nasikia wengi wanasema "angejenga mfumo" au "ashughulikie mfumo" kwanza. Hili linasikika masikioni vizuri lakini angeanza kwa kufanya nini ili kuujenga huu mfumo? Wengine wanaweza kusema "angechukua Katiba ya Warioba"? Sawa kwa vipi? Kwamba, atangaze tu kama alivyofanya JK au angeanza moja na kufuta yote yaliyotokea kwenye Bunge la Katiba n.k? au angefanyaje?
Au mambo ya kukamata makontena yale, wakwepa kodi, n.k wote hawa wangesubiriwa kidogo - kwa muda gani? Ili Rais afanye kwanza hilo jambo jingine ni lipi na lina umuhimu gani mkubwa kwa kuendesha serikali kulinganisha na yale ambayo aliamua kuanza nayo?
Wengine wanasema angeingilia suala la Zanzibar kwanza; sawa. Angeingilia kwa vipi? Angesema Shein ajiuzulu ampishe Seif au angesema Jecha tangaza matokeo yote usifute au angefanya vipi hasa?
Na wakati anafanya hayo mengine yote haya yaliyotumbuliwa yangekuwa kwenye orodha ya ngapi ili yafikiwe? Mfumo ungeweza kujengwa kwa haraka kiasi gani ili wananchi waone matokeo?
Bila ya shaka wengine katika kutaka kukosoa labda wanaweza wasijiulize maswali mengine ya ndani hivi kiasi kwamba wanajikuta wanalazimika kukosoa kwa sababu wasipokosoa wanaweza kudhaniwa wanaunga mkono.
Binafsi, hadi hivi sasa nimesoma wengi wanaokosoa; ukiondoa wale ambao wanazungumzia staili sijaona bado ni nini hasa ambacho Magufuli angeweza kukifanya kwanza badala ya hivi anavyovifanya. Niko tayari kueleweshwa kwa wenye uwezo wa kufanya hivyo.