Sungusungu wadaiwa kufanya ujambazi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
ASKARI wa Jadi (Sungusungu) watatu katika Mji Mdogo wa Sirari wilayani Tarime katika Mkoa wa Mara, wanashikiliwa na Polisi wakihusishwa na tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Costantyine Massawe, watuhumiwa hao ni George Omolo (27), Kibiche Nyangoye (25), na Joseph Sospeter (23).

Kamanda Massawe alisema watu hao wanatuhumiwa kufanya unyang’anyi wa kutumia bunduki aina ya gobore na kumpora Sh milioni sita mfanyabiashara wa duka la nguo, Lydia Paradiso mkazi wa Sirari.

Alisema tukio hilo lilitokea alfajiri ya Jumanne wiki hii wakati mfanyabiashara huyo alipokuwa akiwahi usafiri wa mabasi yaendayo Mwanza kwa ajili kununua mizigo ya biashara yake ya duka la nguo.

“Mfanyabiashara huyo alisindikizwa na vijana wake wawili wadogo kwenda kupanda basi,
walipofika eneo karibu na soko kuu la mji huo karibu na mabasi yanapoegeshwa walivamiwa na kundi la watu wakiwa wamevalia makoti meusi huku wakifunika nyuso zao na kuwaelekezea kitu kilichofanana na bunduki huku wakikikoki na kuwataka wakae chini na kusalimisha kile walichonacho.

"Walianza kuwapekua na kumkuta na fedha hizo za biashara na kumnyang'anya Sh milioni sita na kutoweka nazo ambapo mwanamama huyo alijaribu kupiga yowe ya kuomba msaada, lakini watuhumiwa hao walikimbia," alieleza Kamanda Massawe.

Alisema msako ulioendeshwa na Polisi kwa kusaidiana na Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni, Robert Nashon na wananchi, uliwabaini walinzi waliokuwa maeneo hayo na kukutwa mmoja wao, Omolo akiwa na chuma nyumbani kwake kilichotumiwa kama gobore wakati wa unyang'anyi huo.

“Tunawahoji walinzi hao ambao pia wengine ni wapiga debe wa stendi ya magari hapo Sirari kwa uchunguzi zaidi na wakibainika tutawafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema.
 
Back
Top Bottom